Tuesday, 3 May 2016

[wanabidii] Kama JPM anatafuta sifa ni heri iwe hivyo

GAZETI moja la kila siku, hivi karibuni lilimkariri Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Vincent Mashinji, akidai kwamba kinachofanywa na Rais John Magufuli pamoja na timu yake, kwa maana ya mawaziri aliowateua baada ya kuingia madarakani, ni kutafuta sifa kwa wananchi.

Hiyo haikuwa mara yangu ya kwanza kusikia viongozi wa chama hicho kikubwa cha upinzani nchini wakitoa kauli kama hizo. Kuna wakati wanasema tunachokiona wananchi kikifanywa na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ni nguvu ya soda au msisimko wa muda. Lakini hili, kwamba kinachofanywa na Rais Magufuli na timu yake ni kutafuta sifa kwa Watanzania ndilo limekuwa likisemwa sana.

Liliwahi pia kusemwa na mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, na hata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Kwa mfano, Lissu alikaririwa wakati fulani akihojiwa na kituo fulani cha TV akimfananisha na Magufuli na Augustine Mrema kwamba eti anachotafuta ni kuandikwa vizuri na vyombo vya habari. Kauli ya nguvu za soda huwa pia siielewi vyema msingi wake kwani imejengwa katika dhana zaidi na wala haionekani kuuombea uongozi wa sasa wa nchi yetu heri, ili hatua zinazochukuliwa sasa ziwe endelevu.

Imekaa kama kejeli. Kinachonifikisha kukuna kichwa zaidi na kauli za viongozi wa Chadema ni ukweli kwamba mengi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni yale ambayo chama hicho huko nyuma kilikuwa kinayapigia kelele sana. Hayo yaliyokuwa yakipigiwa kelele na Chadema kwa muda mrefu ni pamoja na uwajibikaji uliotukuka kutoweka katika sekta ya umma, matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma, ufisadi, rushwa, wizi wa mali ya umma, ubadhirifu na kadhalika.

Niliwahi kuandika kwamba kama akina Mbowe wangekuwa waungwana kweli kweli wangekuwa wakimsifu Magufuli na siyo kumbeza, lakini pengine hizo ndizo aina ya siasa za Afrika! Kuna wakati nimekuwa ninajiuliza kwamba wanaosema kinachofanywa na JPM na timu yake ni kwa ajili ya kusaka sifa wanamwambia nani hasa? Ninasema hivyo kwa sababu hayo unaweza kuwaambiwa watu wasiomjua Magufuli vyema historia na utendaji wake wa huko nyuma wakakuamini.

Anayeweza kuamini kwamba JPM na timu yake wanachokifanya ni kutafuta sifa, kama si mtu ambaye ana chuki binafsi tu na serikali ya sasa, basi atakuwa ni ambaye hakufuatilia pia kampeni za Magufuli wakati anausaka urais wa nchi yetu mwishoni mwa mwaka jana au ambaye hajasoma Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuona inataka nini. Yaani akina Lissu na Dk Mashinji wanataka kusema kwamba hatua ya kubana matumizi kwa maana ya fedha zinazookolewa na kisha kupelekwa kwenye matumizi mengine muhimu zaidi, hakuna tija yoyote isipokuwa kinacholengwa ni kupata sifa?

Kwamba kupambana na mianya ya kupotea kwa fedha za umma katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa mfano, bandari ambayo tukiisimamia vyema ni 'mgodi' mkubwa kabisa wa kutuingizia fedha ni kusaka kuandikwa vizuri na waandishi wa habari? Kwamba kutumbua majipu, kwa maana ya kuwaondoa ofisini viongozi walio katika sekta ya umma ambao ni wabadhirifu na wameshindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo nako ni kutafuta sifa?

Kwamba kusimamia kwa dhati tatizo sugu la wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakitoboa mapato ya serikali nako ni kutafuta sifa? Kwamba kutengua uteuzi wa mkuu wa mkoa kwa sababu amesema uongo juu ya wafanyakazi hewa katika suala nyeti kama hilo ambalo Magufuli ameamua kulitafutia suluhu ya kudumu nako ni kutafuta sifa? Basi kama huko ndiko ambako kunatafsiriwa na akina Mashinji na Lissu kwamba ni kutafuta sifa, basi kwetu wananchi ni jambo jema na tunawataka na kuwaombea sana waendelee 'kutafuta sifa'.

Kinachofahamika ni kwamba uongozi uliotukuka ni kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, kutimiza wajibu na kutenda haki na kikubwa zaidi ni kufanya kile ambacho wananchi wako wanakitegemea kutoka kwako. Ni kwa maana hiyo, kiongozi unapotimiza majukumu yake, na hususani kufanya yale ambayo wananchi wanayataka, ni lazima utapata sifa tofauti na unapofanya kinyume na matarajio ya wananchi.

Ninataka kusema kwamba ipo tofauti kidogo ya kiongozi anayetafuta sifa ingawa kila binadamu anapenda kusifiwa, na yule anayetimiza wajibu wake na sifa kuja nyuma yake. Ninachokiona kwa Magufuli na timu yake ni kutimiza wajibu wao, jambo ambalo lazima linawapa sifa nyuma yake na litaendelea kuwapa sifa kama watadumu nalo kama ilivyokuwa kwa viongozi ambao tunaadhimisha misiba yao hadi leo, kama hayati Mwalimu Nyerere na Edward Moringe Sokoine.

Kiongozi mmoja wa zamani wa Afrika Magharibi, Ibn Batuta, alipata kusema kwamba "Tunafanya haya (kuwatumikia wananchi) kwa sababu tunataka hata tukifariki dunia, watu wasitutafute katika makaburi yaliyopakwa chokaa bali watutafute kwenye nyoyo za wale tuliojitahidi kuboresha maisha yao." Hilo analosema Ibn Batuta ndilo ambalo viongozi wengi hawalijui ama wanalijua lakini kutokana na ubinafsi wao wanashindwa kulitekeleza.

Rais John Magufuli, tangu akiwa Waziri, alikuwa akijitahidi kuwatumikia wananchi ukweli wa kuwatumikia, jambo ambalo anaendelea nalo na kwa hakika litaendelea kumpa sifa hata baada ya kuondoka madarakani na hata kuondoka duniani siku yake ikifika.

Hatuwakumbuki akina Nyerere, Sokoine au Abeid Amaan Karume kwa sababu ya sura zao nzuri au mbaya na wala hatuna sababu ya kuwatafuta kwenye makaburi yao huko walikozikwa. Bali unaweza kuwapata mara moja kwenye nyoyo za Watanzania wengi kwa sababu waliwatumikia kwa dhati, ukweli wa kuwatumikia. Nimalizie kwa kurudia tena kusema kwamba kama Rais Magufuli na timu yake wanatafuta sifa, basi hilo ndilo tunataka kuliko wakifanya vinginevyo.
 

0 comments:

Post a Comment