Wednesday 31 December 2014

[wanabidii] Neno La Leo: Usiuanze Mwaka Mpya Kwa Chuki Kwa Wanadamu Wenzako


Ndugu zangu,

Tumeanza Mwaka Mpya. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Lakini, lililo baya kwa mwanadamu ni kuanza mwaka kwa chuki. Maana, mwanadamu huangamia pia kwa roho yake ya chuki.

Kuna miongoni mwetu wenye kuwachukia wenziwao kwa vile tu wanafanya bidii ya kazi. Kwamba wanafanikiwa kwa wanayoyafanya. Badala ya kuwaiga, wao huhangaika sana na kujenga husda. Hufanya hila za kuwazuia wenzao wasipige hatua. Hufikia hata kuwazushia tuhuma za uongo. Ni kutaka kuzichafua tu, taswira za wenzao kwenye jamii. Wenye chuki na hila huzani kwamba watakifikai kilele cha furaha maishani, pale wanapoyaona maanguko ya wengine. Hapana, hawajui kuwa chuki na hila hupelekea kwenye kuangamia kwao pia.

Aristotle, Mwanafalsafa wa Uyunani ya Kale aliamini, kuwa kuna aina tatu za furaha kwa mwanadamu; Mosi, furaha itokanayo na kuishi maisha ya raha na starehe. Pili, furaha itokanayo na kuishi kama mtu huru na unayewajibika kwa jamii yako. Na tatu, furaha itokanayo na kuishi maisha ya mtu anayefikiri na ni mwanafalsafa.

Aristotle aliamini, kuwa ili furaha ya mwanadamu iwe na ukamilifu, basi, matatu hayo, yawepo kwa wakati mmoja.

Na ni vigumu yote yakawepo kwa ukamilifu na kwa wakati mmoja. Lililo jema ni kutafuta uwiano. Maana, ni hatari kwa mwanadamu kuwa mroho sana wa chakula. Ni hatari vile vile kwa mwanadamu kukosa chakula.

Miongoni mwetu wanadamu kuna walio na ubinafsi mkubwa. Ni wenye kuitaka furaha ya kuwa na raha na starehe, hata kwa gharama za wanadamu wenzao.
Ni hao wenye hata kutumia siasa kutimiza matakwa yao ya kuwa na raha na starehe. Hata kama kuna wengine hawana hakika ya kula yao ya kesho.

Ni hawa wasiowajibika kwa jamii yao. Na kwenye kundi hili kuna wenye wivu, chuki na kutenda yalo ya hila kwa wanadamu wenzao. Yote ni kwenye kuitafuta furaha yao. Hata kama ni kwa kuwaumiza wenziwao. Maana, wanapoona kuna mwanadamu mwenzao aliye huru, mwenye kufikiri na anayewajibika kwa jamii. Basi, huyo kwao ni adui. Watamwandama kwa kumuwinda.

Na kwa mwanadamu, hakuna jambo la hatari kama kuwindwa na mwanadamu mwenzako. Maana, mwanadamu mwenzako anageuka kuwa ni adui. Hivyo, katika hali hiyo unaweza kuwindwa na mtu au watu usiowajua. Wewe huwaoni, lakini wao wanakuona na kukufuatilia nyendo zako; unachosema, unachoandika na hata unaokutana nao.

Na katika hali hiyo ni heri mwanadamu uwindwe na simba, maana, simba akikuwekea mtego akakukosa, basi atajiendea zake. Hana habari tena na wewe. Lakini, kwa mwanadamu mwenye choyo, wivu, hila na inda, akikuwekea mtego akakukosa, nawe ukajua kuwa umekoswakoswa, basi, busara ni kuwa makini zaidi.

Mwanadamu kama adui atatafuta njia nyingine kuhakikisha kuwa hata lambo linalokufanya uishi kama samaki, nalo linakaushwa. Ufe, basi. Ni furaha yake. Ili iweje? Mungu anajua.

Maana, tofauti na simba, mwanadamu hakuachi kirahisi na kujiendea zake. Itakuwa hivyo kama itabaki, kuwa kwenye kutimiza raha na starehe zake anazozitaka. Kwenye ubinafsi wake, wewe, kama mwanadamu mwenzake, ni kikwazo.
Na kosa lako laweza kuwa moja tu; kutaka kuwa mtu huru. Mwenye kufikiri na kuwajibika kwa jamii unayoishi.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa.
Iringa.


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment