Friday, 1 August 2014

[wanabidii] Mchakato wa Katiba

Ndugu zangu Watanzania nafasi tuliyonayo sasa ni muhimu tukaitumia vizuri ili kuandika katiba yetu upya ili kukidhi matakwa ya sasa na vizazi vijavyo.

Nchi yetu ina bahati kupata viongozi wasikuvu na wenye nia njema na Taifa letu na ndio maana Mhe. Rais Kikwete alikubali hoja ya kuandika upya katiba licha ya kwamba haikuwa kwenye ilani wala vipaumbele vya Chama Cha Mapinduzi.

Na CCM kwa kuwa nia yake ni njema kwa Watanzania na ndio maana ikaridhia na mchakato ukaanza kwa utaratibu uliokubalika na wadau wote na ikatungiwa sheria.

Sheria hiyo ndio inayofuatwa ambayo ilihitaji uundwaji wa tume ikusanye maoni kwa wananchi na kutengeneza rasimu ya katiba ambayo itawasilishwa kwenye bunge maalumu la katiba (BMK) ili rasimu ile ijadiliwe na hatimaye BMK litoe rasimu ya mwisho itakayopelekwa kwa wananchi ili uamuzi wa mwisho ufanywe na wananchi wenyewe kama wanaikubali au wanaikataa hiyo rasimu iliyopitishwa na BMK.

Sasa hapa kinachonishangaza ni kuwa kama tulikubali uteuzi wa BMK na mjadala ukaanza kwa nini katikati ya mjadala baadhi ya watu wanasusia ? Kwa nini wasiendelee na mjadala na wakashindana kwa hoja ? Je ni kweli watu hawa wana nia njema na Taifa letu au wana maslahi fulani ila wanatumia hii kama sababu ?

Mimi kama mwamnamichezo huwa kabla ya kuanza mchezo tunakubaliana kanuni, taratibu na sheria itakayotumika katika mashindano husika na mkishaanza timu moja katikati ya mchezo inasusa ni dhahiri timu hiyo inapoteza sifa za uanamichezo na matokeo yake ni kutoa ushindi mwepesi kwa mshindani wake.

Kama kweli kundi hilo lilikuwa linataka katiba basi warudi kwenye uwanja wa majadiliano na watoe hoja na hatimaye mwenye hoja yenye mashiko atashinda lakini wakumbuke wenye uamuzi wa mwisho ni wananachi na sio wajumbe wa BMK. Hivyo basi uamuzi wowote utakaopitishwa bado sio wa mwisho bado kuna nafasi ya kuamua kwa maslahi ya Taifa.

Kuhusu rasimu ya tume ya Warioba, mimi nadhani Watanzania tuwe wakweli naomba nitumie mfano wa kikao cha sherehe za kawaida (mf. Harusi) mnapokutana kundi kubwa kujadili namna ya kufanikisha sherehe ile hamuwezi kundi lote kukubaliana kila kitu na pengine mnaunda kamati ndogo ya kutengeneza mambo muhimu kama bajeti, ratiba n.k sasa kamati ndogo inatengeneza rasimu ya bajeti kulingana na maoni ya baabhi ya watu na kamati ile inaleta rasimu ya bajeti kwenye mkutano mkubwa wa sherehe na mkutano ule unaamua kukubali baadhi ya mapendekezo, mengine kuyaboresha, mengine kuyabadili na mengine kuyakataa. Sasa baada ya hapo kinachokubaliwa na mkutano huu ndicho cha wote na wote tuna wajibu wa kukitekeleza kwa mujibu wa makubaliano.

Sasa kwa BMK kuboresha mapendekezo ya tume ya Warioba kuna tatizo gani ? Kila kipengele cha rasimu kimejadiliwa na kutolewa mapendekezo, vingine vimekubaliwa, vingine vimeboreshwa na vingine havijakubaliwa sasa hapa tatizo ni nini mbona ni utaratibu wa kawaida kwenye taratibu za mikutano ? Kama nilivyoeleza hapo juu.

Cha ajabu hapa nini ? Labda tueleweshane, tume ya Warioba imefanya kazi yake imemaliza, sasa hatua inayofuata ni BMK nalo linapokea rasimu linajadili na linatoa rasimu yake ambayo ndio itaamuliwa na wananchi.

Hivi tulitarajia kila kilichopendekezwa na tume ya Warioba kipite kama kilivyo ? Sasa kazi ya BMK ni nini ? Mbona hata katika Bunge la kawaida Serikali au Mbunge yoyote analeta hoja na hoja ile inajadiliwa na hatimaye inapitishwa kama ilivyo au inapitishwa na marekebisho au inakataliwa na mwisho wa siku uamuzi wa Bunge baada ya majadiliano ndio unaheshimiwa.

Sasa kwa nini leo baadhi ya watu wanataka kutuamisha eti kila kilicholetwa na tume ya Warioba ndio sahihi, kama ni hivyo basi sheria ingesema baada ya tume kukusanya maoni, maoni yale kama yalivyo yapelekwe kwa wananchi kwa uamuzi. Lakini sheria iko wazi na ndio inayofuatwa sasa kwa nini leo watanzania tunataka kuvunja taratibu tulizojiwekea wenyewe ?

Kama unakwenda kwenye majadiliano na wewe unasema lazima hoja yako ndio ipite basi bado hujakomaa na hujui hata taratibu za majadiliano. Inabidi kwanza uelimishwe ili uwakilishi wako uwe na tija, vinginevyo utapoteza rasilimali za watu bure na mwisho kusiwe na tija.

Kitendo cha kususa hakina faida kwa Taifa wala kwa wananchi/makundi wanayowakilisha.

Ni muhimu tuwe na wanasiasa wenye ukomavu wa kisiasa na wenye kuweka mbele maslahi ya Taifa na sio maslahi binafsi.

Ni muhimu tujue kuwa kwenye mchakato wowote kuna kupata na kukosa hivyo viongozi na wawakilishi wetu wawe tayari kwa yote.

Nashauri wale wote waliosusa BMK kurejea kwenye majadiliano kwenye BMK na watoe hoja zao humo na wenye hoja zenye mashiko watashinda na hatimaye watuletee rasimu tutakayoamua sisi wananchi.

Phares Magesa

Sent from my BlackBerry® smartphone provided by Airtel Tanzania.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment