Wednesday 30 July 2014

[wanabidii] Neno La Leo: Kamba hukatikia pabovu, ya kwetu itakatikia kwenye Katiba endapo...

Ndugu zangu,

Mimi nisingependa iwe hivyo, lakini, naziona ishara za nguvu hasi zenye kutupeleka huko.

Tulishafanya kosa kama taifa, kwamba hili la Katiba kuwaachia wanasiasa kwa wingi wao kulijadili na kimsingi kulitolea maamuzi.

Na kosa tunalokwenda kulifanya sasa ni kudhani ni wanasiasa hao hao wenye kuhasimiana na kupigania uongozi wa dola, kuwa peke yao wataupeleka mchakato wa kupata katiba mpya kwenye mwisho mwema.

Sikupata kufikiri kuwa hili la katiba litakuwa chachu ya kutugawa Watanzania kwenye makundi. Nahofia, kuwa tunakoelekea sasa ni kwenye kugawika kwenye mafungu.

Naam, naiona hatari iliyo mbele yetu. Hatari ya mchakato wa Katiba kuzalisha chuki na uhasama miongoni mwetu. Maana, tumeshaanza kuona maswali yakiulizwa, yenye kutafuta ' wachawi' wanaozuia kupatikana kwa Katiba Mpya. Ndiko tulikofikia.

Bado naamini katika dhamira njema ya Rais wetu Jakaya Kikwete ya kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Nilimsikia na kumwona Rais, kwa macho yangu akitangaza dhamira yake hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2013. Sikuwa na shaka hata chembe kuwa maneno yale yalitoka ndani ya moyo wake, sina shaka hiyo hata hii leo.

Ninachohofia, ni kuwa ajenda ya Katiba Mpya imeshatwaliwa na wanasiasa ' Wasakatonge'. Ni Wasakatonge wenye kusumbuliwa sana na swali la ' Kesho yangu itakuwaje?' Si kesho ya wengine walio wengi.

Ni nani basi atakayejibu swali la wanasiasa wasakatonge juu ya kesho yao itakavyokuwa?

Maana, ni hao wenye kupanda kwenye migongo ya wananchi wakidai wanazungumza kwa niaba yao, wakati kimsingi wamo kwenye ushindani wa kisiasa.

Ni kosa lile tulilolifanya kama taifa, kuwaachia wanasiasa kwa wingi wao kuamua hatma ya nchi yetu kupitia Katiba.

Nini kifanyike?
Kama taifa, katika mazingira ya sasa , mchakato huu wa katiba waweza kuwa ndipo ulipo ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania.

Kama hakutakuwepo kwa mazingira ya kupatikana kwa katiba ya maridhiano, basi, ni heri mchakato mzima ukasitishwa na kusubiri wakati muafaka.

Maana, katiba ya ' Bora Liende' haiwezi kutuacha wamoja na salama kama taifa. Yumkini itakuwa ni Katiba ya Mpito, na huko kutakuwa ni kuihujumu dhamira njema ya Rais wetu Jakaya Kikwete ya kutupatia Watanzania Katiba Mpya ya miaka 100 ijayo.

Hakuna jinsi, kwa kulinda heshima na hadhi ya nchi yetu. Hadhi na heshima ya Rais wetu, pande zenye kuhusika na mvutano huu ni lazima ziitafute meza ya mazungumzo, na kushirikishwa watu wenye hekima na wasio na ushabiki wa vyama.

Maana, kamwe wahusika hawawezi kuikimbia meza. Wakae, wajadiliane, na kama ilivyo desturi ya majadiliano, hupati kila unachokiweka mezani, vingine unavipoteza, na vingine unavipata. 

Na mwishowe, maridhiano yafikiwe, kwa maslahi ya nchi tuliyozaliwa.

Ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,
0754 678 252

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment