Wednesday 30 July 2014

[wanabidii] Hotuba - Mweusi wa Msituni na Mweusi wa Nyumbani na MALCOLM X

The Field Negro
and The House Negro ( Mweusi wa Msituni na
Mweusi wa Nyumbani ). Na baada ya hotuba
hii naomba ujiulize mwenyewe kama wewe ni Field Negro
au ni House Negro!?;

"Kulikuwa na aina mbili za watumwa. Kulikuwa na
yule wa nyumbani na mwengine anayezurura.
Yule wa nyumbani aliishi katika nyumba na
bwana wake. Alivaa vizuri. Alikula vizuri pia kwani
alikula kile kilichoachiwa na bwana wake.
Akiwekwa darini au chini kabisa mwa nyumba
(katika msingi), hata hivyo bado aliishi karibu na
bwana wake. Waliwapenda wamiliki wao kuliko
hata hao mabwana kujipenda wenyewe. Walidiriki
kujitolea hata maisha yao ili kuilinda nyumba ya
mmiliki wake. Tena kwa haraka kuliko hata huyo
bwana mwenyewe. Kama tajiri wake akisema,
"Tuna nyumba nzuri hapa" basi yule mnigro
atarukia, 'Kweli bosi, tuna nyumba nzuri." Kila
wakati ambapo bosi atatumia 'sisi' na yeye
hatosita kutumia neno hilo. Hivyo ndivyo
walivyokuwa.
Kama nyumba ya bosi ikashika moto, yule
mtumwa atakimbia zaidi kuuzima moto kuliko
hata mwenye nyumba mwenyewe. Kama bwana
akiumwa, utamkuta mtumwa wake akiuliza, vipi
bosi hata sisi tunaumwa (kwa hali ya kumsikitikia
na kumliwaza bosi wake)!? Alijitahidi kumtambua
bosi wake zaidi ya bwana wake kujitambua
mwenyewe. Na hata ukienda kumtembelea
mwenzako huyu ukimuasa mtoroke! Utakuta
anakuangalia kwa jicho la mshangao na kusema,
"He! Umewehuka!? Una maana gani unavyosema
tutoroke?! Wapi nitakaa katika nyumba nzuri
kama hii? Wapi ntavaa nguo nzuri kuliko hizi?
Wapi ntakula chakula kizuri kuliko hiki?" Huyo
ndiyo Nigro wa nyumbani. Kwa kipindi hiko,
aliitwa 'Niga' wa nyumbani. Na hivyo ndivyo
tuwaitavyo sasa, kwani bado tunao humu ndani
wanazunguuka zunguuka kuturudisha nyuma
mitaani.
Huyu Mnegro wa kisasa anampenda bosi wake
sana. Anataka aishi karibu naye. Atadiriki kulipa
mara tatu ya thamani ya nyumba ili apate nafasi
ya kuishi karibu na mabosi wake (wazungu), na
kutamba kwa wenzake, "Mimi ndio Mnegro pekee
hapa. Ndio pekee katika kazi hii na ndio pekee
katika shule hii." Tunakwambia wewe sio
chochote zaidi ya mtumwa wa nyumbani tu kama
wale wanegro wa zamani. Na kama mwenzake
akija kukushauri kuondoka hapa, unasema kile
kile alichosema mnegro wa kale katika
mashamba, "Unamaanisha nini ukisema
tuondoke? Tutoke Marekani? Nchi hii nzuri ya
wazungu? Sijasahau lolote Afrika." Na wakati
umeiacha akili yako Afrika.
Katika kipindi hiko hiko cha kilimo cha kutumia
watumwa, kulikuwa na kundi la pili ambalo ni la
Mnegro asiye na makazi kwa bosi wake. Hawa
walikuwa wengi. Sema kweli hawa walikiona cha
moto. Walikula yaliyosazwa ndani. Walikula vile
vilivyoachwa na watu wale wachafu (nguruwe)
ndani. Siku hizi mnaita Chit'lins (chakula
kitokanacho na utumbo wa nguruwe). Zama hizo
waliziita kama zilivyokuwa, matumbo! Na baadhi
yenu bado ni walaji matumbo hayo hapa.
Mnegro huyu wa shambani alipigwa kuanzia
asubuhi mpaka jioni. Aliishi bandani tu. Alivaa
mitumba. Alimchukia bwana wake. Nasema
alimchukia bwana wake na inaonyesha alikuwa na
akili. Yule wa nyumbani alimpenda bwana wake
huyu alimchukia, tena kwa kuwa walikuwa wengi,
waliwachukia mabwana zao. Kama nyumba ya
bosi wao ikishika moto, wala hutamkuta
akijisumbua kuuzima moto ule, bali akijitenga
kuomba dua upepo uzidi kuvuma na moto
uongezeke. Kama bwana wa watumwa akiumwa,
basi wataomba afe kabisa. Kama mtu akija kwa
hawa na kuwaambia watoroke. Hawakuuliza
tunaelekea wapi bali walihisi sehemu nyengine
yoyote ni bora kuliko ya hapa. Tunao watumwa
hawa Marekani ya sasa, na mimi ni miongoni
mwao. Hatusikii siku hizi wanegro wakilalama eti,
"Serikali yetu ina matatazo' bali wanasema
"Serikali ina matatizo". Nishawahi kumsikia
mmoja akisema, "Wanaanga wetu" na wakati hata
haruhusiwi kusogelea maeneo hayo. Au mtu
atumie "Jirani zetu, wanaanga wetu au wanamaji
wetu" kwa hawa wazungu, bila shaka atakuwa
kapotelewa na akili. Nasema huyu Mnegro
atakuwa kapotelewa na akili.
Kwa kuwa bwana wa watumwa wa zama hizo
alimtumia Tom kulinda wenzake, ndio hicho hicho
kinachofanyika sasa kwani hawa vibaraka sio
lolote zaidi ya kuwa ni wajomba Tom wa kisasa
tu. Kina wajomba Tom wa karne ya 20
wanatumika kutulinda sisi na wanaturudisha
nyuma. Wanatufanya tupende amani ambayo ni
ya uongo. Tusiwe na vurugu. Huyo ni yule yule
Tom anaekufanya uwe hivyo ili uendelee
kutawaliwa. Ni sawa sawa umeenda kwa tabibu
wa meno ambaye atakutoa jino lako, utampiga tu
pale atapoanza kuvuta jino. Sasa itabidi akuweke
vitu katika taya zako ili usikie ganzi, na hapo
utakuwa unaumia kwa amani kabisa. Damu
itakuwa inamwagika katika taya zako na wewe
hatuahisi chochote kikiendelea. Eti kwa sababu
kuna mtu amekufanya uumie kimya kimya!
Hahaha!
Wazungu wanatufanyia jambo hilo hilo mitaani
humu. Anapotaka kukufunga fundo kichwani
mwako, kukutumia atakavyo na asiwe na hofu ya
wewe kupigana naye, huwa wanawatumia hawa
kina wajomba Tom, wanaojifanya viongozi wa dini
kama ile ganzi ya kwenye meno, wakituelekeza
tusiache kuumia ila tuumie kimya kimya! Kama
mchungaji Cleage alivyosema, wanatufundisha
damu yetu imwagike mitaani. Hii ni aibu
ukizingatia yeye ni mchungaji wa dini. Kama ni
aibu kwake nadhani mnaelewa kwangu
itamaanisha nini.
Hakuna kitu kama hicho katika kitabu chetu
Qur'an kama nyie mnavyoiita Koran!
kitufundishacho kuumia kwa amani. Dini yetu
inatutaka tuwe na akili. kuwa na ustahifu
(uungwana) lakini pia kuwa na amani ya kweli.
Tii sheria. Mheshimu kila mtu. Lakini kama mtu
akijaribu kunyanyua 'kamkono' chake kukudhuru,
usisite kumpeleka kaburini. Hii ndio dini bora.
Tena ndio ile ile dini ya zamani. Hii ndio dini
mama na baba walikuwa wakiiota. Jicho kwa
jicho, jino kwa jino, kichwa kwa kichwa na (uhai)
maisha kwa (uhai) maisha. Hii ndio dini bora. Na
kwa yeyote anayepinga dini hii isifundishwe, ni
mbwa mwitu anayetaka kukufanya chakula chake.
Hivi ndivyo ilivyo kwa wazungu hawa wa
Marekani. Ni mbwa mwitu na wewe ni mbuzi.
Muda ambao sijui mchungaji, au padri
anakufundisha usimkimbie mzungu huyu na tena
anakufundisha usimpige vita mzungu si jengine
ila atakuwa mnafiq kwako na kwangu mimi.
Uweke maisha yako rehani kiasi hicho?! La hasha,
yalinde maishe yako, linda uhai wako. Ndio jambo
lenye thamani zaidi kwako. Na hata kama
ikatokea unahitaji kukata tamaa nayo basi jitahidi
iwe mechi suluhu.
Mabwana hawa wa watumwa waliwachukua kina
Tom, wakiwavalisha vizuri, wakiwalisha vizuri na
hata kuwapa elimu kidogo. Waliwakabidhi makoti
marefu na kofia nzuri juu na watumwa wengine
wote wawatazame wao. Kisha ikawa rahisi
kuwatawala wale waliobakia kupitia Tom. Nyenzo
hiyo hiyo iliyotumika kipindi hicho ndiyo itumikayo
leo. Anamchukua Mnegro mmoja na kumfanya
mashuhuri, anamjenga, anamtangaza na
kumfanya awe mzungumzaji na kiongozi wa
wanegro."


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment