Thursday, 31 July 2014

[wanabidii] Hatari na changamoto zinazoukabili UKAWA

NI wazi kwamba Uchaguzi Mkuu ujao wa Tanzania unaotazamiwa kufanywa Oktoba 2015 utakuwa ni mtihani mkubwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

 Kwanza utakosa uhalali iwapo vyama vikuu vya upinzani vitaususia kama vilivyoahidi kufanya endapo uchaguzi huo utafanywa kwa mujibu wa Katiba ya sasa.

Kwa hivyo mengi yatategemea jinsi vyama vya upinzani vitavyozicheza karata zao Tanganyika na Zanzibar.

Turufu kubwa iliyo mikononi mwa upinzani ni mkakati wa vyama vyake vikuu kuendelea kushirikiana ili viing'oe CCM kutoka kwenye madaraka.   Vyama hivyo vilianza kushirikiana kwa dhati baada ya kutanabahi kwamba vitimbi vya kibabe vya CCM katika Bunge Maalumu la Katiba vinaweza vikalifikisha taifa pabaya na huenda vikasababisha vurugu na hata umwagaji wa damu.

Vitimbi hivyo vina lengo moja tu: kulilazimisha taifa liyakubali mapendekezo ya CCM kuhusu Katiba mpya, hasa pendekezo lake la kutaka muundo wa Muungano wenye serikali mbili uendelee.

Tangu vyama vya upinzani viungane na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimekuwa vikiahidi kwamba katika Uchaguzi Mkuu ujao vitamsimamisha mtetezi wao mmoja kugombea kila nafasi kutoka ya urais, ubunge, uwakilishi (Zanzibar) na ya viti vya serikali za mitaa.

Iwapo Ukawa hautoivunja ahadi hiyo na iwapo Umoja huo utaamua kushiriki katika uchaguzi basi hakuna shaka yo yote kwamba CCM italemazwa laisa kiasi.  Tokea hapo chama hicho kinaonyesha kila dalili ya kuchoka.

Ufisadi, ukosefu wa itikadi ya kizalendo na nakisi ya uongozi  adilifu ni miongoni mwa majanga mengine yanayokikumba chama hicho. Na hayo ni baadhi tu ya mambo yanayozifanya serikali zake zote mbili — ya Muungano na ya Zanzibar —zionekane dhaifu.

Ndiyo maana upinzani unajinadi kuwa una nguvu za kujiona kuwa ni paka shume na CCM kuwa ni kipanya. Na upinzani unaotumai utaweza kukirukia na kukishambulia hicho kipanya na kunyakua madaraka. Haitokuwa rahisi hivyo.

Ijapokuwa CCM kimechoka, hata hivyo, kina hazina kubwa ya hila na vitimbi pamoja na mazoea ya kutumia ubabe.  Kimekwishajitayarisha kuitumia hazina hiyo ili kujilinda kisiangushwe.

CCM inatambua kwamba kitachoweza kukinusuru ni kuzuka kwa mipasuko au hata mianya ndani ya Ukawa. Yakizuka hayo wafuasi wengi wa upinzani wataanza kujiuliza nini hasa dhamira za viongozi wao.

Uwezekano wa kuzuka mianya ndani ya Ukawa upo. Na inaweza ikazukakwa njia mbili.

Kwanza, mianya ndani ya Ukawa inaweza kuwa ni ya kujitakia. Chanzo chao kinaweza kuwa sintafahamu, choyo, wivu au uchu wa madaraka miongoni mwa viongozi wa upinzani.

Mivutano aina hiyo si ajabu kutokea ndani ya vyama vya upinzani katika nchi zenye demokrasia isiyopevuka. Kwa kawaida huzidi kushika kasi uchaguzi mkuu unapokaribia.

Pili, nchini Tanzania mianya hiyo inaweza ikasababishwa na CCM ama kwa kuwanunua baadhi ya viongozi wa upinzani au kwa kuwafitinisha.

Kwa sasa mabishano baina ya CCM na Ukawa yanazidi kupamba moto kuhusu suala la Katiba mpya.  Na badala ya kulitafutia ufumbuzi wa dhati suala la kukwama kwa mchakato wa Katiba pande zote mbili zinaendelea kupakana matope kwenye mikutano yao ya hadhara na kwenye vyombo vya habari.

Endapo viongozi wa upinzani watafanikiwa kuwahamasisha wananchi wamiminike barabarani kuandamana dhidi ya serikali kuna hatari ya serikali kutetemeka na kubabaika isijuwe cha kufanya isipokuwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Inaweza ikawakamata na kuwafikisha mahakamani au hata ikawaua.

Viongozi wa upinzani nao huenda wasinusurike. Serikali inaweza, kwa mfano, ikawatia nguvuni na kuwashtaki baadhi yao kwa kuwasingizia kuwa wanachochea ghasia. Au inaweza ikawatega kwa shtuma nyingine na kuwachukulia hatua kali.

Hatua kama hizo za kimabavu zitazaa moja ya matokeo mawili. Tokeo la kwanza ni serikali kujichimbia yenyewe kaburi lake kwa kuwafanya wapinzani wazidi kuwa ngangari kwani kwa mujibu wa kanuni moja ya kisiasa kila serikali inapoukandamiza umma ndipo umma unapozidi kuja juu kuipinga serikali.

Tokeo la pili ni kuzuka mpasuko miongoni mwa viongozi wa upinzani, hasa ikiwa patamwagika damu. Baadhi yao huenda wakaingiwa na hofu na wakawa tayari kuiridhia serikali na wengine wakaamua kuendelea kusimama kidete.

Ushahidi uliopo ni kwamba kati ya CCM na Ukawa mkosa ni CCM kwa jeuri yake ya kukataa kuyasikiliza matakwa ya wananchi. Na pili, kwa kwenda kinyume cha makubaliano ya awali kwamba Bunge Maalumu la Katiba halitojadili kingine ila Rasimu ya Pili iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa waziri mkuu wa zamani Joseph Warioba. 

Kwa hakika, suala kuu linalokwamisha shughuli za Bunge la Katiba ni hilo pendekezo la Rasimu ya Tume ya Warioba kwamba muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu badala ya mbili kama ilivyo sasa na kama ulivyo msimamo unaoshinikizwa na CCM.

Aprili 16 wajumbe wa Ukawa walitoka nje ya Bunge Maalumu la Katiba wakiapa kwamba hawatorudi mpaka CCM itaposalimu amri na kukubali kwamba kitachojadiliwa ni Rasimu ya Tume ya Warioba.

Inavyoonyesha ni kwamba maji yamemzidia unga Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta.  Ndiyo maana akawa anafanya dhihaka katika utekelezaji wake wa shughuli za Bunge hilo. Akijaribu kujitoa kimasomaso Sitta ameunda Kamati ya Mashauriano akisema kwamba madhumuni yake ni kuleta suluhu ili wajumbe wa Ukawa warudi Bungeni Agosti 5.

Sitta anajidai eti hajui nini kilichojiri katika vikao vilivyopita vya Bunge hilo. Sasa anawasihi wajumbe wa Ukawa wahudhurie vikao vya Kamati ya Mashauriano. Wajumbe wa Ukawa walimpuuza wakimwona mpuuzi kwa sababu walipoanza kulisusia Bunge la Katiba walieleza wazi kwa nini walifanya hivyo.

Walisema kuwa hilo Bunge linawabagua na linawapendelea wajumbe wa CCM dhidi yao.  Pia walisema kwamba hawakuweza kuvumilia matusi aliyokuwa akitukanwa Warioba.

Waliongeza kwamba wanataka Bunge hilo liijadili Rasimu ya Katiba ya Tume ya Warioba na si waraka wa CCM unaoshinikiza muundo wa Muungano wa serikali mbili.

Njia gani zitumike kuunusuru mchakato wa Katiba kama unaweza kunusurika? Kuna wenye kushauri kwamba utungwaji wa Katiba mpya uachiwe viongozi wajao kwa sababu kwa muda uliobaki ni muhali kabisa kupatikana Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Pendekezo jingine lililotolewa ni kulivunja Bunge la Katiba na kufanywa kura ya maoni kuwauliza wananchi iwapo wanataka muundo wa Muungano wenye serikali mbili au wenye serikali tatu.

Visiwani Zanzibar kuna wenye kupendekeza kwamba hiyo kura ya maoni iwaulize Wazanzibari iwapo wanautaka Muungano uendelee au la.

Mapendekezo yote hayo yana matatizo yake.  Kubwa ni hatari iliyopo ya CCM, kwa ubabe wake, kutumia hila za kupata matokeo inayoyataka katika kura ya maoni.

Moja ya changamoto kubwa zinazoukabili Ukawa ni namna ya kuandaa mkakati madhubuti wa kupambana na serikali iliyopenya na kusambaa katika mazingira yote ya mamlaka nchini Tanzania.

Kwa hivyo, ili wafanikiwe ni muhimu viongozi wa upinzani wasihitilafiane na kuzozana juu ya mbinu za kupambana na serikali.  Kadhalika, inafaa wajipangie kanuni rasmi za uongozi wao. Isiwe leo kiongozi wao mmoja anasema hili na kesho mwingine aseme jingine lenye kukinzana au kupingana na lililosemwa leo na mwenzake.

Kwa sasa hali ya mambo ndani ya Ukawa si ya kukatisha tamaa, kwa hakika inatia sana moyo.  Lakini kuna haja ya kuwakumbusha viongozi wake kwamba umoja huo ukiraruka kazi ya kuutia viraka na kuwapatanisha wanaohasimiana haitokuwa kazi rahisi.

Upinzani ukiendelea kuungana unaweza ukaizuia CCM isiukabe.Tukikumbuka kwamba Tanzania ni nchi isiyojiendesha bila ya msaada wa wafadhili hatua moja ya kutumiwa na wapinzani ni kuzibembeleza serikali za wafadhili ziwashurutishe watawala wa Tanzania waache kuukorofisha mchakato wa kidemokrasia wa kulipatia taifa Katiba inayoridhiwa na wananchi.

Kwa hakika, wafadhili wanapaswa kushinikiza wafikishwe mahakamani viongozi wenye kukiuka haki za binadamu pamoja na wale wenye kutoa matamshi ya ubaguzi, vitisho au ya uchochezi kama yale yaliyotolewa naWaziri William Lukuvi akiwa kanisani.

Lukuvi alifanya uchochezi alipoonya kwamba Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka Zanzibar ijitenge ili iwe dola ya Kiislamu. Matamshi kama hayo aghalabu huwa ni chanzo cha umwagaji damu.

Matamshi yake  ni miongoni mwa sababu zilizowafanya wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine  walisusie Bunge hilo na kuzidisha mpambano kati yao na CCM.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/hatari-na-changamoto-zinazoukabili-ukawa#sthash.f4Z7a30a.dpuf

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment