Sunday 1 September 2013

[wanabidii] Safari hii ya Goma ihitimishiwe Kigali

Safari hii ya Goma ihitimishiwe Kigali

Na Manyerere Jackton, JAMHURI

Meja Khatibu Mshindo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amekufa katika mapambano nchini DRC. Amekufa kishujaa. 

Amekufa akitekeleza maelekezo halali ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayolenga kuwafanya wananchi wa Mashariki mwa DRC waonje tunu ya amani.
Kifo cha kamanda huyu kinapaswa kiwe chachu kwa Watanzania na wapenda amani katika Afrika na duniani kote.
Watanzania tuna historia iliyotukuka ya ukombozi wa wanyonge sehemu mbalimbali duniani. Ndugu zetu wa Msumbiji, Angola, Afrika Kusini, Namibia, Comoro, Ushelisheli, Angola na kwingineko wanatambua hilo. Bila kujali umasikini wetu, tulijitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanyonge katika mataifa hayo tunawakomboa. Wakati tukihaha kutekeleza dhima hiyo ya kiutu, hatukujali kuachwa nyuma kimaendeleo na majirani zetu kama Kenya au Malawi ambao hawakuhangaika kwa namna yoyote. 

Kifo cha Kamanda Mshindo kinapaswa kiwe chachu kwa wapiganaji na makamanda wa JWTZ katika kuhakikisha wananchi wa DRC wanapata amani, wanafaidi matunda ya uhuru, na utajiri wao unabaki kuwanufaisha wao kwanza.

Tumempoteza Mtanzania mwenzetu katika vita ambayo mwasisi wake ni Rais Paul Kagame wa Rwanda. Huyu ni mpenda vita, na ndiyo chimbuko la kundi la waasi wa Kihutu la FDLR. Hili ni matokeo ya ubabe wake alipoamua kushiriki kuwaua Rais Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi, Cyprien Ntaryamira. Aprili 6, 1994 ndege iliyokuwa imewabeba viongozi hao kutoka nchini Tanzania ilipigwa kombora wakati ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Kigali, Rwanda.
Pamoja na marais hao, wengine waliouawa kwenye shambulizi hilo ni Bernard Ciza (Waziri wa Ujenzi wa Burundi), Cyriaque Simbizi, (Waziri wa Mawasiliano wa Burundi, Jenerali Deogratias Nsabimana (Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda), Meja Thaddée Bagaragaza (Msaidizi wa Rais wa Rwanda-masuala ya kijeshi), Kanali Elie Sagatwa (Mjumbe wa Sekretarieti ya Rais wa Rwanda), Juvénal Renaho (Mshauri wa Rais wa Rwanda wa Masuala ya Kigeni), na Emmanuel Akingeneye ambaye alikuwa Daktari wa Rais wa Rwanda.
Wana anga watatu, raia wa Ufaransa nao waliuawa. Nao ni Jacky Héraud (rubani), Jean-Pierre Minoberry (rubani mwenza) Jean-Michel Perrine (mhandisi wa ndege). 
Damu ya watu hawa inamsumbua Rais Kagame.
Taarifa mbalimbali kutoka pande mbalimbali duniani zinamweka mbele kwenye orodha ya waliohusika kwenye mauaji hayo ambayo baadaye yalisababisha kile kilichokuja kujulikana kama mauaji ya kimbari. 

Dola ya Bahima 

Watanzania tuna sababu zote za kupigana vita ndani ya DRC. Hii ndiyo njia pekee sahihi ya kuvuruga mkakati wa Rais Kagame na rafiki yake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda wa kuanzisha Dola ya Bahima. Hii ni dola ya watu wa kabila la Watutsi.
Marais hawa wanaamini Bahima inapaswa kusambaa Rwanda, Burundi, Uganda, sehemu za Tanzania na katika DRC. Tukiwaruhusu waimege DRC, nasi Tanzania tukae mkao wa kunyolewa! Hapa tunapaswa kutambua kuwa kwa huruma yetu tuliwakaribisha maelfu ya wakimbizi wa Kitutsi. Hawa wanajua mengi ya Tanzania. Haitashangaza siku moja wakijiunga na kuanzisha vita kwa madai ya kutaka watambuliwe. Tumeyaona juzi baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaamuru wahamiaji haramu warejee kwao.

Kumetolewa maneno mengi ya vitisho na lawama, kana kwamba ni halali kwa mtu kuishi katika nchi nyingine bila kufuata taratibu. Waliingia nchini mwetu wakiwa na mifugo mingi. Wakajitwalia maeneo makubwa kwa nguvu na kwa hila. Wakawaua wananchi wetu. Wakachoma nyumba na mashamba ya wenyeji. Kama wameweza kufanya hivyo sasa, watashindwa nini hapo baadaye kudai Karagwe na Ngara kuwa ni yao? Tuwe macho sana. 

Rais Kagame alihakikisha anaingiza nchi yake kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, si kwa kutafuta kitu kingine, bali nguvu za kisiasa. 

Chokochoko zake zimepamba moto baada ya ushauri wa Rais Kikwete wa kumtaka aketi na waasi ili wamalize tofauti zao kwa mazungumzo. Alichofanya Rais Kikwete ni kutoa ushauri, na si kumshurutisha! Kejeli, matusi na dharau vilivyotolewa baada ya kauli ya Rais Kikwete, vinaashiria kuwa kuna jambo kubwa zaidi ya hilo la kuchukizwa na ushauri aliompa.
Zipo sababu nyingi zinazomfanya Rais Kagame awe mbogo. Nitajaribu kuziainisha hapa kwa ufupi tu. Mosi, Tanzania tunakubalika sana kimataifa. Kwenye diplomasia tumeiacha mbali Rwanda. Hili linamuudhi sana kwani anaamini yeye ni bora na maarufu zaidi. 

Kitendo cha Rais Barack Obama wa Marekani kuja Tanzania na kuziacha Rwanda, Uganda na hata Kenya kimewaudhi, na kwa kweli tunaweza kusema hii imekuwa nguzo imara iliyoibua mshikamano na mapenzi ya ghafla miongoni mwao. Rwanda ikijiona kuwa ndiyo nchi inayoinukia kiuchumi kwa kasi, ilidhani ina sifa zote za kuiwezesha kutembelewa na Rais Obama. Uganda ambayo ilikuwa mshirika mkuu wa Marekani, inaona Tanzania imechukua nafasi yake. Imeingiwa wivu! Kenya ambayo inaamini Obama ni wao kwa sababu babake ni Mkenya, imechukizwa kuona ikipigwa kumbo na Tanzania. Hawa watatu-Kagame, Museveni na Kenyatta-wameungana kuichukia Tanzania kwa sababu tu ya kumkosa Obama. 

Pili, kinachomsumbua Rais Kagame na washirika wake ni uamuzi wa Tanzania wa kutaka Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC liende hatua kwa hatua. Msimamo wa Tanzania umekuwa kwamba maoni ya wananchi ni muhimu mno kabla ya kuchukua uamuzi wowote. Kwao, Tanzania ndiyo kikwazo cha kuwa na serikali moja ya EAC. Hapa ni vema Watanzania wakakumbuka namna Rais Museveni alivyokuwa amejiandaa kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki. Sidhani kama ameshaufuta mpango huo.

Baada ya kuona Tanzania tukitaka jambo hili liende hatua kwa hatua, watatu hawa wameungana sasa kutaka shirikisho lao la kisiasa, huku wakiiacha nje Tanzania na Burundi. Wanajidanganya bure. Lakini hapana sababu ya kulumbana nao. Kama wanataka kuanzisha, waanzishe tu. Hakuna haja ya ugomvi. Wakianzisha kutakuwa na nchi mbili-hiyo ya Shirikisho, na Tanzania kwa upande mwingine.

Hapa ni vema kwanza tukatambua kuwa Tanzania ni nchi kubwa. Ukichukua Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya, ukaziweka pamoja, bado ni ndogo kwa Tanzania. Hatuna sababu ya kuogopa.

Tatu, hawa jamaa kiu yao kubwa kabisa ni ardhi ya Tanzania. Ukiacha tamaa ya kutaka kuitawala kanda yote hii, kiu yao ya kweli ni ardhi ya Tanzania. Wamepambana kwa hali na mali kuhakikisha kuwa ardhi inakuwa moja ya mambo kwenye shirikisho. Wanataka Mkenya, Mganda, Mnyarwanda na mwanachama mwingine yeyote, akitaka kuingia Tanzania, basi apewe uraia wa kudumu na apata ardhi bila masharti! 

Hoja yetu imekuwa kwamba wao wakija Tanzania watapata ardhi, je, Mtanzania akienda Rwanda au Kenya au Uganda ataipata? Chao chao, chetu chetu sote. Wao hawana mita ya mraba ya ardhi iliyo wazi kwa hiyo wanajua mlengwa na wa kuumizwa hapa ni Tanzania tu. Uroho wao wote ni ardhi ya Tanzania. Hilo tumeapa kuwa haliwezekani. Kama haliwezekani kwa ndugu wa tumbo moja, seuze kwa nchi na nchi? Tukianzisha shirikisho tutapeana nini? Hilo ndilo jambo wanalopaswa kutujibu kwanza. Janja ya kuja kuoa au kuolewa Tanzania haitawasaidia.

Wanachofanya sasa kinatokana na hasira tu

Shirikisho la Rwanda, Uganda na Kenya likianzishwa haliwezi kudumu. Watagombana tu. Rwanda watataka walitawale shirikisho. Hicho ndicho wanachokitafuta. Wakenya hawasumbuliwi na kingine, isipokuwa biashara. Wameingia kwenye mkakati huu kwa sababu wanadhani bandari ya Mombasa inaweza isiwe na maana endapo Rwanda, Uganda na Burundi wataamua kutumia bandari za Tanga na Dar es Salaam; na hiyo nyingine inayojengwa Bagamoyo. Bado ukweli unabaki kwamba kutoka Dar es Salaam hadi katika nchi za Rwanda na Burundi ni karibu mno kuliko kuanzia Mombasa. 
Katika mpango huu sidhani kama Burundi itakubaliana nao. Burundi kuwa karibu na Tanzania kuna manufaa makubwa zaidi kwake kuliko kuwa karibu na hayo mafiga matatu.
Harakati hizi zote zinachochewa na Rwanda, na hapa ndipo ninapokuja na sababu ya nne ya Tanzania kuchukiwa. Rais Kagame amechukia mno kuona majeshi ya Tanzania yakiongoza mapambano ya kuwang'oa M23 ambao ni Wanyarwanda. Kwa miaka yote DRC imekuwa shamba la Rwanda. Kagame ameongoza harakati za kuliibia taifa hilo bila huruma. Ameanzisha vita ili amani isiwepo. Anajua DRC ikitawalika, hatapata mwanya wa kwenda kupora rasilimali, hasa madini. Kwa sasa adui yake mkubwa ni Rais Kikwete na Tanzania kwa sababu tunaziba njia yake haramu ya uchumi.

Kuachwa kwetu solemba EAC

Sioni kwanini tusianzishe Jumuiya yetu kwa kuwakaribisha DRC na Burundi. Sisi ni taifa kubwa. DRC ni taifa kubwa pia. DRC na Tanzania tuna rasilimali nyingi mno. Faida za kujitoa EAC ni kubwa kwetu kuliko kuendelea kuhangaika na hawa wapenda vita. Tuwaache waanzishe yao, na sisi tuanzishe yetu. La, hilo kama haliwezekani, tujikite zaidi SADC ambako kuna soko pana kuliko EAC.
Tukijitoa EAC atakayeumia zaidi ni Kenya maana bidhaa na uwekezaji wake mkubwa kauelekeza Tanzania. Soko lake kubwa lipo Tanzania. Wanajidanganya tu.

Tusiendelee kuwabembeleza watu wasiokuwa na shukrani. Tuwatakie heri katika ndoa yao hii mpya ambayo sioni uhai wake. Hizi ni hasira za mkizi ambazo mara zote humnufaisha mvuvi. SADC ni bora zaidi. Tupeleke nguvu zetu kwenye SADC. 

Kagame na Museveni walisaidiana kuichukua Uganda. Museveni alimsaidia Kagame kuitawala Rwanda. Sasa wanasaidiana wachukue sehemu ya DRC. Museveni anamsaidia Kagame katika hili. Tutambue kuwa inayofuata ni Tanzania. Si ajabu wale Wanyarwanda waliokuja siku nyingi sasa wakadai wanabaguliwa, na kwa sababu hiyo wakaanzisha vita ya kutaka kutambuliwa au kujitenga na kuwa sehemu ya Rwanda na Uganda (Bahima Empire). 

Njia pekee ya kumwondoa Rais Kagame ni hii aliyotusaidia kuiweka, yaani vita. Kuichokoza Tanzania ni njia ya kuelekea ukingoni mwa utawala wake. Amepigana kwa muda mrefu na wasiojua vita. Amejaribu kuitisha Tanzania akidhani atafanikiwa. Kinachotakiwa sasa ni kumwonyesha kazi. Safari iliyoanzia Goma inastahiki ihitimishiwe Kigali. Kama kasahau, arejee kwenye historia ili ajue kilichompata nduli Iddi Amin Dadaa. Buriani Kamanda Khatibu Mshindo. 

manyerere@hotmail.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment