Sunday, 1 September 2013

[wanabidii] Nashauri, Media Yetu Iache Kupiga Ngoma Ya Vita...!



Ona hapa moto wa Wahutu na Watusi ulivyoanza kwa jambo dogo sana...

Fires on the Hills;
-Good morning Sub-chief, how are you?
- Thank you! The mass was beautiful and the sermon digestible,
don't you think so?
- You are becoming very important sub-chief?
People talk a lot about you these days.
- Are you reproaching me something? ( Antoine Lema, Africa Divided, page 37.)

Ndugu zangu,

Goma ya DRC imekuwa Kosovo ya Ukanda Wa Maziwa Makuu. Naziona ishara za janga kubwa linalonyemelea nchi zetu hizi.

Naam, Congo imekuwa Balkan yetu, na Goma ni kama Kosovo. Moto wa vita vya Balkan kule Ulaya ulianzia Kosovo.

Na Afrika moto ukiwaka nyumba ya jirani wahi kushiriki kuuzima, maana, moto unaowaka kwenye nyumba moja unaweza kusambaa ukazifikia nyumba za jirani. Na ukiendelea kupuuziwa, basi, kijiji kizima chaweza kuteketea.

Lililo la muhimu ni kutanguliza hekima na busara. Nimefuatilia kwa karibu kuona jinsi media yetu inavyoripoti kinachotokea DRC Congo. Mathalan, magazeti kadhaa ya siku ya leo yamefanya kazi ya kupiga ' ngoma ya vita'. Imefika mahali hata kuonyesha kuwa ni ' Vita Vyetu'. Na kwamba tunaelekea kupata ushindi mkubwa.

Nimependa analysis za Jarida la ' The East African' ( Agosti 31- Septemba 6)  Na mtu makini akizisoma analysis zile akazimaliza, basi, kamwe hawezi akachukua ngoma ya vita kuanza kuipiga. Kuna hatari kubwa inakuja mbele yetu.

Nalo Jarida la ' The Guardian' la hapa limefanya analysis ya kina na ya kurasa nyingi kuhusiana na chimbuko la mgogoro wa DRC- Congo. Bahati mbaya, nalo pia limeshindwa ku-link tatizo lililopo na wakoloni walioasisi mgawanyiko na chuki miongoni mwa watu wa DRC Congo. Kimsingi  M23 ni sehemu ndogo tu ya tatizo kubwa la Congo.

Bahati mbaya DRC Congo inaangaliwa zaidi kwa kuanzia na alipoondolewa Mobutu.  Tunasahau, kuwa Wakoloni wa Kibelgiji walifanikiwa sana kuwagawa WaCongo. Ikafika mahali Jimbo la Katanga likajitenga na kuunda Taifa lao.

Baada ya Wabelgiji kuwapa Wacongo Uhuru wao 1960, wakafanya hila kuwapa nguvu Waalunda na Wabayeke wa Katanga waunde taifa lao. Na huko ndiko kwenye utajiri mkubwa wa madini ya Congo.

Moise Tshombe akajitangaza kuwa Rais wa Taifa la Katanga, Makao Makuu yake ni Lubumbashi. Na katika kufanya hivyo, Wabelgiji wakawatenga tena Wabaluba wasiwe sehemu ya mamlaka ya Katanga. Wabaluba wako kaskazini ya Katanga kuelekea majimbo ya Kasai na Kivu ambapo Gomba ndipo Makao Makuu ya majimbo hayo.

Ikafika mahali, Moise Tshombe alipiga marufuku ndege ya Rais wa Congo Huru, Joseph Kasavubu na Waziri Mkuu wake Patrick Lumumba isitue kwenye uwanja wa ndege wa Lubumbashi. Tshombe alijazwa kiburi na Wabelgiji. Na uhasama wa Wabaluba wa Kaskazini na Waalunda wa kusini ukaendelea. Hata hii leo, bado kuna mabaki ya mgogoro huu wa tangu mwaka 1960!

Na hakika, DRC Congo ni mtihani kwa viongozi wa mataifa yetu haya yanayozunguka Maziwa Makuu.

Siamini kuwa suluhisho la mgogoro wa DRC Congo litapatikana kwa njia ya VITA. Naamini katika njia ya siasa, hivyo basi MAZUNGUMZO.

Na Rais wetu, Jakaya Kikwete  aendelee kusimamia kauli yake, kuwa wahusika kwenye mgogoro huu wafanye mazungumzo ya kutafuta suluhu.

Kama nchi, tufanye yote yanayowezekana kuiepusha nchi yetu kuingia kwenye ' Vita vya kiwendawazimu' na majirani zetu. Na media hapa ina mchango mkubwa. Iache kupiga ngoma za vita.

Vita si ngoma ya Lelemama. Vita  ni kitu kibaya sana hususan kwa nchi zetu hizi masikini.

Leo tunaona picha za magazetini za wanajeshi wenye kutembea na silaha. Tujiandae pia kuona picha za raia wasio na hatia kwa maelfu wakiyahama makazi yao. Wengi wao ni akina mama na watoto migongoni.

Mbali ya raia kuawa, vita huzaa wakimbizi pia. Vita hupelekea akina mama kubakwa mchana wa jua kali. Hivyo, vita huendana na uvunjwaji wa haki za kibinadamu. Vita husimamisha shughuli za kiuchumi. Ni mambo mabaya sana.

Na Chifu  kwenye mazungumzo ya hapo juu kabisa alijibu nini baada ya kukasirishwa?

Chifu alikuwa Mtutsi. Alirusha konde kwa Mboyumutwa ( Mhutu). Naye akalikwepa konde lile. Akakimbia. Tukio hili tunasoma kwenye vitabu, kuwa ndilo liliashiria mwanzo wa mgogoro wa kitabaka kati ya Watutsi na Wahutu.

Maana, wakati akikimbia, Mboyumutwa njiani alikutana na watu wa kabila lake. Nao walijawa na wasiwasi. Walishaarifiwa kilichotokea. Siku iliyofuatia, Wahutu wakaandama katika kitongoji cha Gitarama.

Inaandikwa, kuwa shambulizi lile alilofanyiwa Mboyumutwa, kiongozi mashuhuri wa Wahutu, ndilo likawa cheche iliyowasha moto mkubwa wa uhasama, kati ya Watutsi na Wahutu. ( Antoine Lema, Africa Divided)
Mchango mdogo kwa kidogo nilichojitahidi kukifahamu..

Maggid,
Iringa
http://mjengwablog.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment