Saturday 21 December 2013

Re: [wanabidii] TAARIFA YA MBUNGE WA NZEGA , MHE HAMIS KINGWANGALA KUFUNGA MWAKA 2013

mkuu umekosea jina. Jina la Mbunge wa Nzega ni Hamisi Kigwangalla na siyo Kingwangala


2013/12/21 Abdalah Hamis <hamisznz@gmail.com>
Nzega: Tumefika Wapi Leo? Tunaelekea Wapi Kesho? 

Taarifa ya Ofisi ya Mbunge Kufunga Mwaka 2013.

 
Utangulizi

Ukiitazama Nzega ya leo si ile Nzega ya Miaka ya 90 ama ile ya miaka ya 70, alipozaliwa Mbunge wetu Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.), imebadilika sana, imekuwa kwa kasi sana; idadi ya watu, magari na nyumba imeongezeka sana. Utoaji wa huduma zote muhimu umezidiwa kasi na ukuaji wa mji. Changamoto zilizopo leo ni nyingi na nzito sana. Kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, shule ni chache na zinatoa elimu isiyokidhi ubora unaohitajika, viwanda hakuna  ukilinganisha na miaka ya nyuma, migodi midogo midogo iliyokuwa asili ya Nzega imefungwa na serikali, mvua zimepungua kutokana na uharibifu wa mazingira hivyo uzalishaji wa mazao ya biashara na kilimo umeathiriwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, miundombinu ya barabara imeongezeka kwa wingi haswa maeneo ya vijijini na mijini japokuwa bado ni duni na haitoshi na pia huduma za kibenki ni duni na hazijawafikia wananchi walio wengi kule vijijini. 



Pamoja na mapungufu haya Nzega inafaidika kwa kuwa kwenye nafasi nzuri kijiografia, kwamba ni makutano ya barabara kuu ziendazo Kigoma, Kagera hadi Rwanda na Burundi na ile inayokatiza kwenda Mwanza hadi Musoma na Tabora hadi Mbeya. Kama zikiunganishwa kwa lami, Nzega inaweza kuwa kituo muhimu kwa biashara. Pia nafasi yake kijiografia imefanya Nzega iwe na mchanganyiko mzuri wa watu kimakabila kiasi kwamba mchanganyiko huu unatoa fursa ya kuleta uzoefu na ujuzi mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali ambao unapafanya Nzega pawe mahala palipochangamka (vibrant and dynamic). 



Mwaka 2010, kwenye uchaguzi Mkuu, Nzega ilifanya uamuzi sahihi wa kumchagua Mbunge mwanamapinduzi, mwanamabadiliko na mpiganaji mahiri na makini, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) ambaye anajitahidi kupambana na changamoto hizi usiku na mchana pasi na kukata tamaa ama kuchoka. Mafanikio ya kazi yake yanaonekana na siyo ya kutafuta. Ifuatayo ni ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) hadi kufikia Desemba 2013.

 

 

1. Hali ya Jimbo

Hali ya jimbo ni shwari; amani, upendo na usalama umetamalaki japokuwa mpaka tunaandika taarifa hii kuna malalamiko ya watu wa kijiji cha Mwanshina, ambako kuligundulika uwepo wa dhahabu hivi siku za karibuni na kupelekea wananchi kujumuika pale kuanza shughuli za uchimbaji; bahati mbaya sana wamezuiliwa na askari wa kutuliza ghasia (FFU) waliopokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega. Mazungumzo yanaendelea kujua ni kwa nini serikali imewazuia wananchi hawa ili hatma ya mgodi huu ijulikane. Pili, kuna malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Ipala ambao wanadaiwa na serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega kuvamia eneo la msitu wa hifadhi. Ufuatiliaji wa uhalali wa katazo la Mkuu wa Wilaya ya Nzega lililoambatana na uvunjifu mkubwa wa haki za wananchi, ambapo wamedumu toka kabla ya uhuru, unaendelea.  



Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega imeendelea kuhudhuria shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo harusi, misiba, mahafali za wanafunzi, harambee na pia kufanya ziara za kikazi kijiji kwa kijiji kupitia 'Operesheni Wafuate Watu'. Pia ahadi za Mbunge ama wasaidizi wake kwenye maeneo mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa – hadi sasa ni zaidi ya asilimia 95 ya ahadi zote alizotoa mbunge zimetekelezwa ukiachilia chache sana ambazo ni za siku za karibuni. Kuna ligi kubwa ya kiwilaya inayofadhiliwa na Mbunge wa Nzega inaendelea katika hatua ya robo-fainali kwenye tarafa nne za Wilaya ya Nzega – mshindi wa kwanza atapata 'Kombe la Kigwangalla' na fedha taslim TZS 1,000,000, wa pili atapata TZS 500,000 na wa tatu TZS 300,000. Timu zote zilizoingia nane bora zitazawadiwa seti moja ya jezi kila timu.



Mbunge wa Nzega anaendelea kupigana kuhakikisha azimio la Baraza la Madiwani la kuanzisha Kampuni ya Benki Jamii ya Nzega (Nzega Community Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Construction Corporation Ltd - NCCCL) linatekelezwa haraka. Tunatarajia mchakato huu utafanikiwa kutokana na uwepo wa takriban TZS 2.3 bilioni zilizopatikana kutoka kampuni ya Resolute Tanzania Ltd kama ushuru wa huduma (service levy) na ambazo zitatumika kama mtaji wa kuanzia wa benki (TZS bilioni 1) na zinazobaki kwa ajili ya kununulia mashine za kuchongea barabara na kuchimbia visima zitakazomilikiwa na kuendeshwa na kampuni hizi mbili tofauti ambazo zinatarajiwa kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya Halmashauri, wanaushirika na wananchi wengine watakaopenda kununua sehemu ya hisa za makampuni haya mawili.

2. Vipaumbele Vya Jimbo

2.1       Mapinduzi Kwenye Sekta ya Elimu Nzega:

(i.)                Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, mpaka sasa kwa kufanya jitihada binafsi na kwa kutumia pesa za mfuko wa jimbo (milioni 43) akishirikiana na Diwani, Mhe. Ramadhani Nchimani, Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Ndala, Serikali ya Kijiji cha Kampala na wananchi kwa ujumla, ameanzisha ujenzi wa shule mpya ya 'high school' (kidato cha tano na cha sita) pale Kampala, Ndala (Shule hii imepewa jina la Chief Ngelengi High School); ujenzi unaendelea kwa kasi hivi sasa. Shule ya pili ya High School itakuwa ni ile ya Chief Ntinginya, ambapo Mbunge wa Nzega Dkt. Hamisi Kigwangalla, kufuatia makubaliano na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nzega Mjini chini ya Diwani na Mwenyekiti wake Mhe. Kizwalo Dominic waliazimia kuanzisha ujenzi wa mabweni na madarasa ya ziada ili kuipandisha hadhi shule hii iwe ya kidato cha tani na cha sita. Shule ya tatu ya High School inamaliziwa kujengwa Kata ya Puge, Tarafa ya Puge kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mbunge (ambayo imetoa sh milioni 13), Diwani Mhe. Alex Nyassani, Serikali ya Kijiji cha Upungu na wananchi kwa ujumla (ambao walianzisha majengo hayo); pia Halmashauri ya Wilaya tayari, kwa ushawishi wa Mbunge wa Nzega na Diwani wa Kata ya Puge, imetenga fedha taslimu sh milioni 28 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa shule hiyo. Shule ya Nne ya High School inamaliziwa kujengwa kule Kata ya Lusu (pale Hamza Azizi Ali Sekondari) na wawekezaji wa mgodi, Kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, kufuatia jitihada za kiufuatiliaji na ushawishi wa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) na Mhe. Said Mgalula (Diwani, Lusu) wakishirikiana na wananchi, kwamba ni lazima mgodi ujenge miradi ya maendeleo ya jamii kabla haujafungwa. Ni matarajio yetu kwamba shule hizi zitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi kabla ya mwaka 2014 kuisha. Tunawaomba wananchi wote kwa ujumla, wadau mbalimbali wa maendeleo na serikali tutimize wajibu wetu, tumuunge mkono Mbunge wetu tulete mapinduzi ya kielimu Nzega. 

 

(ii.)              Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na shirika lisilo la kiserikali la PeerCorps Trust Fund ameweza kuanzisha mpango wa kusomesha watoto yatima na wanaotoka familia zenye kipato duni, mfuko huu unaoitwa Hamisi Kigwangalla Scholarship Fund ulianzishwa mwaka 2008 na umeendelea kusomesha watoto na kutoa misaada mbalimbali ya kielimu. Mpaka sasa zaidi ya watoto 576 wamefaidika na mpango huu. Na kila kata kuna wanafunzi 10 kutoka katika makundi haya wanalipiwa ada chini ya mpango huu. Japokuwa mfuko unakumbana na changamoto nyingi ikiwemo kupata maombi mengi zaidi ya uwezo wa mfuko na kuna baadhi ya kata mpaka sasa mfuko haujaweza kupata fedha za kulipa ada kwa baadhi ya wanafunzi, japokuwa Mhe. Mbunge anawataka walimu, wazazi/walezi na viongozi wa Kata hizo wawe wavumilivu na kwamba ada hizo zitalipwa kabla watoto hao hawajahitimu kwa kuwa majina yao tunayo na yaliishapitishwa kufaidika na mpango huu.

 

(iii.)             Mwezi Januari mwaka 2014 Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, atauanza mwaka kwa kuendelea kugawa vitabu 100 vya Kiada na 50 vya ziada kwenye shule zote za Sekondari za Kata za Jimbo la Nzega pamoja na Kompyuta kwenye shule 5 za sekondari kama ambavyo amekuwa akifanya toka achaguliwe kuwa Mbunge wa jimbo hili.

 

(iv.)            Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha tamasha la utamaduni wa watu wa Nzega litakalokuwa likifanyika kila mwaka mjini Nzega. Tamasha hilo ambalo linaitwa Mtukwao Festival (www.mtukwao.org) litakuwa ni kivutio cha watu na kuleta fursa ya biashara kwa wakazi wa Nzega, na sehemu ya kuitangaza Nzega na utamaduni wake kwa wageni, tayari limepata usajili wa serikali na maandalizi yanafanyika kulizindua mnamo Julai 2014 kwa mara ya kwanza, baada ya mipango ya kulizindua Julai 2013 kama ilivyotangazwa hapo awali kushindikana.

 

(v.)              Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameanzisha ujenzi wa chuo binafsi mjini Nzega eneo la Uchama kitakachokuwa kinatoa wahitimu kwenye fani za Uganga, Uuguzi na Ualimu kwa ngazi za Vyeti na Stashahada ili kuongeza nguvu kazi kwenye shule za sekondari za kata, zahanati na vituo vya afya. Malengo ni kusomesha bure walau wanafunzi watano - kwenye kila kozi, wasio na uwezo, mbali na wale wanaojilipia, kwa makubaliano ya kuhakikisha wanaajiriwa kwenye wilaya ya Nzega kwa kipindi kisichopungua miaka mitano. Hii itaongeza idadi ya watumishi kwenye huduma muhimu kwa wananchi na pia uwepo wa chuo utakuza fursa za kiuchumi na ukuaji wa taswira ya mji wa Nzega. Tunatarajia chuo hiki kitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi mwaka 2014 Mwezi Septemba.

 

2.2  Kuendesha Harakati za Kupigania Haki na Usawa kwa wanaNzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na wananchi wa Nzega, madiwani na watendaji wa halmashauri ameongoza mapambano ya kudai haki za Nzega dhidi ya wawekezaji wa Mgodi wa Golden Pride Project, kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, na kufanikiwa kupata mafanikio yafuatayo: mgodi umekubali na tayari umelipa sh bilioni 2.34 kama ushuru wa huduma (service levy) kwa halmashauri ya wilaya ya Nzega, bado kuna madai ya sh bilioni 4 za ushuru wa huduma yanayoendelea kufuatiliwa, ambazo ni malimbikizo ya ushuru huo toka mgodi uanzishwe takriban miaka 14 iliyopita; amefanikiwa kuishawishi serikali kuwa wananchi waliopoteza mali zao kutokana na uharibifu uliofanywa kupisha mgodi wana haki ya kifuta jasho na sasa serikali inaungana na Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla kuwabana wawekezaji waanzishe mfuko wa kuwahifadhi wananchi hao; na jambo kubwa la tatu ni kwa kutumia nguvu ya umma kushawishi wawekezaji watekeleze ahadi za kujenga miradi ya maendeleo Nzega (Kituo cha Afya Lusu, Maabara kwenye sekondari 10 n.k.). Mbunge wa Nzega ataendelea kushawishi vikao vya halmashauri na kusimamia utekelezaji wa miradi itakayowagusa wanaNzega wengi zaidi, kama vile kuanzisha benki ya jamii ya watu wa Nzega ambayo itatoa mikopo kwenye SACCOS za kila kata, kununua mitambo yetu wenyewe ya kuchimbia visima kwenye kila kijiji, kujenga soko jipya na stendi mpya kubwa ili kukuza fursa za biashara ndogondogo kwa wananchi n.k. Mhe. Mbunge amekuwa akipigana bega kwa bega na wananchi wa Kijiji cha Mwabangu kuhakikisha wanapata haki ya kupatiwa leseni yao iliyopokwa kinyemela na wajanja wachache kwa faida yao ama fidia ya ardhi ya mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Isungangwanda.

 

2.3  Kuwezesha Wananchi Kushiriki Shughuli Mbalimbali za Kukuza Kipato Chao: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, amefanikiwa kuleta mapinduzi ya kijani kwenye kilimo cha zao la pamba na zao la alizeti kupitia uhamasishaji wa kampuni ya MSK Solutions Ltd ambayo inatoa mbegu bora, pembejeo, zana za kilimo, elimu ya kilimo bora na uwezeshaji wa wagani vijijini, soko la uhakika la mazao hayo na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao vijijini (Imekamilisha ujenzi wa maghala kule Ndekeli (Tarafa ya Puge), Igalula (Tarafa ya Mwakalundi), Nhabala (Tarafa ya Bukene) na imeanza ujenzi wa ma-godown mapya kule Nhobola (Tarafa ya Nyasa) na Usongohala (Tarafa ya Bukene). Mafanikio ni kuongezeka kwa wakulima wa pamba kutokea wakulima 355 mwaka 2008 hadi kufikia wakulima 24,000 wa pamba mwaka 2012 na kufanya idadi ya kilo za pamba zilizovunwa kufikia takriban milioni 6 kutoka kilo 20,000 mwaka 2008. Pia idadi ya wakulima wa alizeti imeongezeka kutoka wakulima 400 mwaka jana hadi kufikia 3500 mwaka 2013.

 

Makampuni ya wanunuzi wa pamba yameongezeka kutoka kampuni moja ya MSK na kuwa manne hivi sasa – hali inayoleta ushindani kwenye soko na hivyo kupandisha bei zaidi kwa faida ya mkulima. Japokuwa kampuni ya MSK Solutions Ltd imeamua kuacha kuhamasisha pamba na kujikita zaidi kwenye alizeti itaendelea kukumbukwa kwa kutia chachu uhuishaji wa kilimo cha zao hili kilichokuwa kimekufa.

 

Mipango inaendelea kuwashawishi wawekezaji wajenge viwanda vya kuchambua pamba na kukamua mafuta ya kula kutokana na alizeti ya Nzega, tayari halmashauri ya Nzega imeazimia kutenga viwanja 10 kwenye eneo maalum la kujenga viwanda. Pia Mbunge wa Nzega amewezesha wananchi kujiunga katika vikundi vya ushirika wa SACCOS vipatavyo 9 na yupo kwenye harakati za kuvijengea uwezo vifanye kazi za kukuza uchumi kama vile kilimo, mifugo ya kuku kwa kuzalisha vifaranga na mayai, na shughuli za ufundi kwa vijana. Mbunge wa Nzega amegawa mashine mbili kwenye SACCOS ya vijana nay a wazee kwa ajili ya kuangulia vifaranga. Ili kuhakikisha chama kinakuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo vijijini, Mbunge wa Nzega akishirikiana na mwenzake wa Bukene wamegawa mbegu za alizeti kwenye kila kata. Pia Mbunge wa Nzega amegawa pikipiki 10 kwenye kata 10 ili kuweka urahisi zaidi wa kufikisha huduma za ushauri wa maendeleo kwa wakulima vijijini.

 

2.4  Ujenzi wa Miundombinu Nzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameweza kushawishi vikao mbalimbali vya maamuzi na kuhakikisha azimio la kujenga barabara za lami Nzega Mjini linafanikiwa, hivi sasa tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kutekeleza hilo kwenye mwaka wa fedha wa 2013/14; pia kufunga mataa ya kuangaza mji mzima wa Nzega. Mbunge wa Nzega pia kupitia mfuko wa Jimbo amejenga daraja korofi na lililosahaulika kwa muda mrefu la Butandula, na sasa anatafuta namna ya kuhakikisha pia daraja lingine la Nhobola nalo linajengwa, tayari ametenga sh milioni 8 za mfuko wa jimbo kutekeleza hilo.

 

Mradi wa barabara ya Nzega – Tabora kwa kiwango cha lami – Mbunge wa Nzega kwa kutumia nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Tabora, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha serikali inaleta fedha za kukamilisha mradi huu ndani ya muda uliopangwa na pia kusimamia kuhakikisha barabara hiyo na nyingine za mkoa wa Tabora, zinajengwa kwa viwango vya ubora unaostahiki, na wananchi wanapata ajira na kulipwa fidia ya mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi huu.

 

Pia Mbunge amehakikisha barabara korofi kama za kutoka Mbagwa – Nkiniziwa, Busondo – Ndekeli, Busondo – Mwakashanhala zinaingia kwenye bajeti ya ujenzi mwaka huu wa fedha 2013/14 na kuhakikisha zinajengwa, pia barabara nyingine muhimu kama za Muhugi – Mizibaziba – Ndekeli – Ndala zinaingizwa kwenye bajeti, lengo likiwa ni kuhakikisha Nzega inakuwa na mtandao mzuri wa lami mahala pote. Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.) amefanikiwa kuhakikisha mradi wa kupeleka umeme Ndala kutoka Nzega unatekelezwa kwa viwango vya ubora unaofaa, na sasa anahangaika kuhakikisha pia maeneo ya Mbogwe, Wela, Miguwa, na yale ya Usagali, Kaloleni hadi Mirambo Itobo nayo yanapata mradi wa Umeme. Tayari maombi yake yameingizwa kwenye orodha ya miradi ya Umeme Vijijini (REA Phase II) na hivyo maandalizi ya awali ya upembuzi yakinifu yataanza muda wowote kuanzia sasa. Sambamba na jitihada hizi, Mbunge amefanikiwa kuishauri na hatimaye kuishawishi halmashauri ya Nzega kuanzisha kampuni ya ujenzi (NCCCL) na kuinunulia mitambo ya kuchongea barabara, mpango ambao upo kwenye hatua za utekelezaji.

 

2.5  Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Nzega: Baada ya kutoridhishwa na namna miradi ya maji ya benki ya dunia na ile ya serikali inavyosuasua, Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameshauri na hatimaye kuishawishi Halmashauri wanunue mitambo ya kuchimba visima na kuiweka chini ya usimamizi wa kampuni ya ujenzi Nzega (NCCCL) ili kuondoa yale matatizo kwamba mkandarasi amelipwa achimbe kisima kimoja akikosa maji basi na pesa ya serikali ndiyo imeishaliwa. Pesa za kununulia mitambo hiyo zitatokana na mapato yaliyopatikana kutokana na ushuru wa huduma uliolipwa na kampuni ya Resolute. Tukiwa na mitambo yetu tutahakikisha tunachimba kisima na maji yanapatikana kwenye kila kijiji bila shida ndipo twende kijiji kingine. Pia Mhe. Mbunge amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Mkoa wa Tabora unaanza kutekelezwa – na kwa sasa hatua ya utafiti wa awali ilishamalizika na tunatarajia upembuzi yakinifu utafanyika mwaka huu na pengine mwakani kuanza kutekelezwa, ukizingatia hii ni ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Jakaya Kikwete. 

 

2.6  Upatikanaji wa Huduma Bora za Afya kwa Umma: Mhe. Mbunge, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameamua kuanzia mwaka 2014 ataweka ratiba maalum ya kutumia taaluma yake ya udaktari kutibu wagonjwa kwenye vituo mbali mbali vya afya Nzega. Pia ameandaa mkakati kabambe wa kuleta madaktari bingwa wanaoruka (flying doctors) kwa ajili ya kuweka kambi ya tiba maalum mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya wananchi wa Nzega. Kwa kushirikiana na madiwani wenzake wa halmashauri ya Nzega wamefanikiwa kuhakikisha vituo pamoja na nyumba za walimu zilizoanza kujengwa na wananchi vinamaliziwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi – tayari bajeti imetengwa kumalizia vituo vyote mwaka 2013/14, na anaendelea kuhamasisha vijiji vingine ambavyo havijaanza kutekeleza mpango huu vianze mara moja ili tubaki tukitafuta namna ya kupambana na chamngamoto nyingine za watumishi, vifaa na madawa.

 

N.B: Kuna mambo mengi yanayofanyika Nzega kwa ushawishi wa Mbunge na Madiwani, yakitekelezwa na serikali kutokana na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, mwaka 2010 – 2015, lakini si yote yaliyoripotiwa hapa.

Taarifa hii imetolewa na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega, pia inapatikana hapa www.hamisikigwangalla.com na http://kigwangalla.blogspot.com

Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb.)

Leo Siku ya Jumamosi, Desemba 21, 2013.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment