Wednesday 28 June 2017

[wanabidii] MJADALA KUHUSU RASLIMALI ZETU: UMAKINI MAKINI UNAHITAJIKA KATIKA MIJADALA IJAYO

Baada ya ripoti za rais kuhusiana na madini kutolewa na mambo yaliyofuata sasa watanzania tumerudi katika busara kubwa. Busara kubwa kwamba madini ni yetu. Busara kubwa sana kuwa haiwezekani tukaendelea kuibiwa. Busara kubwa kwamba hata waliojaribu kumpinga rais sasa wako kimya au wana lugha tofauti.
Haiepukiki kuamini kuwa huko nyuma tuliibiwa. Haiepukiki kuwa watanzania wenzetu katika ngazi mbalimbali za dhamana walizokabidhiwa, walitusaliti. Hata kama tutasema au tutanyamaza lakini kila tunapowaona na wao wanajua kuwa tunajua, kuwa walilisaliti taifa. Wapo tutakaowachukulia hatua. Wapo tutakaowaacha au kwa kuwaheshimu au kwa kuwahurumia na wengine kwa kinga tulizojiwekea bila kujua kuwa zitatuumiza. Lakini hatuamini kuwa hawajui kuwa tunajua walichokifanya. Mijadala ipo. Mfano Tutamshitaki waziri mstaafu na kumuacha aliyekuwa anamwagiza. Tunafanya hivyo huku tukijua kuwa tuliyemkamata alifanya makosa kwa sababu kuagizwa na tuliyemuacha. Lakini ukweli uko palepale. Wahaya wanasema "Empisi ekanyampila eibale. Eti olayesiza kyonka wakaulila". Yaani chui alilijambia jiwe. Akaliambia japo umenyamaza lakini umekasikia.
 
Wakati hilo likifanyiwa kazi, jingine linalosubiriwa ni mjadawa na hao "wawekezaji".
Huku nyuma walitwambia uwekezaji ni garama kubwa kiasi kwamba  inabidi watugawie kitu kidogo baada ya kuchimba madini kwa sababu kuchimba madini ni aghali sana. Tukakubali. Au niseme viongozi wetu wakakubali. Sasa hiyo haitarajiwi.
Nimekuwa nikifikiri. Ngoja niandike hicho ninachokifikiri. Kama ningechangia msingi wa kujadiliana katika marekebisho ya mikataba ya madini ningesema hivi: Kuna pande mbili:
Upande mmoja ni Tanzania yenye madini. Ni mali yake. Kwa haki nchi inaweza kuendelea kubaki nayo au kuyachimba inavyotaka.
Upande wa pili ni wa wawekezaji. Wana mitambo, Ujuzi wana wajuzi nk.
 
Pande hizi mbili zinahitaji kuungana na kufaidiana. Ilikuwa aibu kujiambia kuwa thamani ya mitambo, utaalamu na wataalamu vina thamani kuliko dhahabu dhahabu yetu. Haiwezekani kwa mfano kutumia ng'ombe kupata mbuzi. Kwa nini usikae na ng'ombe wako. Kwa nini wazungu watwambie wana mbuzi mwenye thamani kuliko ng'ombe wetu. Kama ni hivyo si wakae na mbuzi wao?!
 
Wawekezaji waje na kila walicho nacho. Nasi tukutwe na tulicho nacho. Tutumie vya kwao kuyafukua na kuyaleta juu ya ardhi madini yetu na tuambizane: Mmetumia kiasi gani? Kiasi watakachotumia wawekezaji ndicho kiasi tunachotaka kwanza. Yaani wakitumia dola milioni moja kuyachimbua tunatoa milioni mbili. Moja yetu, moja yao. Ile thamani ikibaki tunagawana kati kwa kati.
Nchi hii imedanganywa sana. Kuna wakati sheria ilikuwa inasema kila mradi wa madini asilimia ishirini na tano (25%) imilikiwe na watanzania. Wajamaa wakawa wanakuja wanamdanganya mtanzania kuwa ana hiyo asilimia lakini hawampi kiasi hicho. Tulipoanza kuandika kuwa basi hao watanzania waulizwe hiyo 25% wameiweka wapi, sheria ikabadilishwa.
Niliwahi kuona picha ya hazina ya dhahabu ya uingereza. Hazina ambayo ndiyo inasaidia kusema Uingereza ni tajili. Hazina inayosaidia kuituliza hela ya Uingereza. Zamani za Nyerere benki kuu ilikuwa inanunua dhahabu kutoka kwa watanzania wanaochimba dhahabu kwa kutumia vijiti. Sehemu ya dhahabu hiyo ilikuwa inawekwa akiba. Nina mashaka kama manyang'au waliopita waliibakiza. Umefika wakati sehemu ya dhaahabu ya Tanzania ikawekwa hakiba. Kama hapa si salama watuwekee hao wanaoweza kuitunza. Lakini iwe yetu. Jamani, tunajua kuwaiga. Tumeiga matamshi, tumeiga kuvaa, tumeiga miondioko. Tumetelekeza lugha yetu ili tusionekane washamba kuongea vizuri lugha yetu. Kwa nini tusiige ujanja wao!? Kwa nini tusiige uzalendo wao kwa nchi zao nasi tukathamini yetu?!
 
Elisa Muhingo
0767 187 507

0 comments:

Post a Comment