Saturday 21 December 2013

[wanabidii] Isemavyo Katiba (1977) kumpata W/Mkuu: Rais atamteua Mbunge wa kuchaguliwa

Nukuu kutoka kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977)

SURA YA PILI
SEHEMU YA TATU: WAZIRI MKUU, BARAZA LA MAWAZIRI NA SERIKALI 

Ibara ya 51
Ibara ndogo ya (1).

Waziri Mkuu

Kutakuwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais kwa kufuata masharti ya ibara hii na ambaye kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais kwa kiapo kinachohusika na kiti cha Waziri Mkuu kitakachowekwa na Bunge.

Ibara ndogo ya (2)

Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne, baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua
Mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika Jimbo la Uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye Wabunge wengi zaidi Bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye Wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na Wabunge walio wengi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, naye hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za Wabunge walio wengi.

Ibara ndogo ya (3)

Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, Waziri Mkuu atashika kiti cha Waziri Mkuu hadi- (a) siku ambapo Rais mteule ataapa kushika kiti chake; au (b) siku ambapo atafariki dunia akiwa katika madaraka; au (c) siku atakapojiuzulu; au (d) siku Rais atakapomteua Mbunge mwingine kuwa Waziri Mkuu; au (e) atakapoacha kushika kiti cha Waziri Mkuu kwa mujibu wa masharti mengineyo ya Katiba hii. 

Ibara ya 52
Ibara ndogo ya (1)

Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Ibara ndogo ya (2)

Waziri Mkuu atakuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.
Ibara ndogo ya (3)

Katika utekelezaji wa madaraka yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe.

Ibara ya 53
Ibara ndogo ya (1).

Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii, Waziri Mkuu atawajibika kwa Rais kuhusu utekelezaji wa madaraka yake.

Ibara ndogo ya (2)

Serikali ya Jamhuri ya Muungano, chini ya mamlaka ya Rais, ndiyo itakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya sera ya Serikali kwa jumla, na Mawaziri, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, watawajibika kwa pamoja Bungeni kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Ibara ya 53A
Ibara ndogo ya (1).

Bila ya kujali masharti ya ibara ya 51 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo na ikapitishwa kwa mujibuwa wa masharti ya ibara hii.

Ibara ndogo ya (2)

Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, hoja yoyote ya kutaka kupitisha kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitatolewa Bungeni endapo-
(a) haina uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu kwa mujibu wa ibara ya 52 ya Katiba hii, wala hakuna madai kwamba Waziri Mkuu amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
(b) haijapita miezi sita tangu alipoteuliwa;
(c) haijapita miezi tisa tangu hoja ya namna hiyo ilipotolewa Bungeni na Bunge likakataa kuipitisha.

Ibara ndogo ya (3)

Hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitapitishwa na Bunge isipokuwa tu kama-
(a) taarifa ya maandishi, iliyotiwa sahihi na kuungwa mkono na Wabunge wasiopungua asilimia ishirini ya Wabunge wote itatolewa kwa Spika, siku angalau kumi na nne kabla ya siku inapokusudiwa kuwasilishwa Bungeni;
(b) Spika atajiridhisha kuwa masharti ya Katiba kwa ajili ya kuleta hoja yametimizwa.

Ibara ndogo ya (4)

Hoja iliyotimiza masharti ya ibara hii itawasilishwa Bungeni mapema iwezekanavyo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.

Ibara ndogo ya (5)

Hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu itapitishwa tu iwapo inaungwa mkono na Wabunge walio wengi.

Ibara ndogo ya (6)

Endapo hoja ya kura ya kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu itaungwa mkono na Wabunge wengi, Spika atawasilisha azimio hilo kwa Rais, na mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku mbili tangu Bunge lilipopitisha azimio la hoja ya kura ya kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu atatakiwa ajiuzulu, na Rais atamteua Mbunge mwingine kuwa Waziri Mkuu.

Ibara ya 54
Ibara ndogo ya (1).

Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote.

Ibara ndogo ya (2)

Rais atahudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri na ndiye atkayeongoza mikutano hiyo. Na endapo Rais hayupo basi mikutano itaongozwa na Makamu wa Rais na kama wote wawili Rais na Makamu wa Rais hawapo Waziri Mkuu ndiye ataongoza Mikutano hiyo.

Ibara ndogo ya (3)

Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara ya 37(1) ya Katiba hii, Baraza la Mawaziri litakuwa ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais juu ya mambo yote yanayohusika na utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, na litamsaidia na kumshauri Rais juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo kwa mujibu wa maagizo maalum au maagizo ya jumla yatakayotolewa na Rais.

Ibara ndogo ya (4)

Mwanasheria Mkuu wa Serikali atahudhuria mikutano yote ya Baraza la Mawaziri na atakuwa na haki zote za mjumbe wa mikutano hiyo isipokuwa hatakuwa na haki ya kupiga kura katika mikutano hiyo.

Ibara ndogo ya (5)

Suala kama ushauri wowote, na ni ushauri gani, ulitolewa na Baraza la Mawaziri kwa Rais, halitachunguzwa katika mahakama yoyote.

Ibara ya 55
Ibara ndogo ya (1).

Mawaziri wote ambao ni wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa ibara ya 54 watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

Ibara ndogo ya (2)

Pamoja na Mawaziri waliotanjwa katika ibara ndogo ya (1), Rais aweza, baada ya kushauriana na Waziri Mkuu, kuwateua Naibu Mawaziri. Naibu Mawaziri wote hawatakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri.

Ibara ndogo ya (3)

Rais aweza kuteua idadi yoyote ya Naibu Mawaziri ambao watawasaidia Mawaziri katika utekelezaji wa kazi na shughuli zao. -(4) Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge.

Ibara ndogo ya (5)

Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1) ikitokea kwamba Rais anahitajiwa kumteua Waziri au Naibu Waziri baada ya Bunge kuvunjwa, basi aweza kumteua mtu yeyote ambaye alikiwa Mbunge kabla ya Bunge kuvunjwa. Ibara ya 56


Waziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

Ibara ya 57
Ibara ndogo ya (1).

Muda wa kushika madaraka ya Waziri na Naibu Waziri utaanza tarehe atakapoteuliwa kushika madaraka hayo.

Ibara ndogo ya (2

Kiti cha Waziri au Naibu Waziri kitakuwa wazi litokeapo lo lote kati ya mambo yafuatayo:-
(a) endapo mwenye madaraka atajiuzulu au kufariki dunia;
(b) ikiwa mwenye madaraka hayo atakoma kuwa Mbunge kwa sababu yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa Bunge;
(c) ikiwa Rais atafuta uteuzi na kumuondoa kazini mwenye madaraka hayo;
(d) iwapo atachaguliwa kuwa Spika;
(e) iwapo Waziri Mkuu atajiuzulu au kiti chake kikiwa wazi kwa sababu nyingine yoyote;
(f) ukiwadia wakati wa Rais mteule kushika madaraka ya Rais basi mara tu kabla Rais mteule hajashika madaraka hayo;
(g) iwapo Baraza la Maadili linatoa uamuzi unaothibitisha kwamba amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. 58. Mawaziri na Naibu Mawaziri watashika madaraka yao kwa ridhaa ya Rais, na watalipwa mshahara, posho na malipo mengineyo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

Ibara ya 59
Ibara ndogo ya (1).

Kutakuwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambaye katika ibara zifuatazo za Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Mwanasheria Mkuu" ambaye atateuliwa na Rais.

Ibara ndogo ya (2)

Mtu yeyote hatastahili kuteuliwa kushika madaraka ya Mwanasheria Mkuu isipokuwa tu kama kwa mujibu wa Katiba hii ana sifa maalum, kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 109(8) zinazomwezesha kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Jaji wa Mahakam Kuu ya Zanzibar, na amekuwa na mojawapo ya hizo sifa maalum kwa muda usiopungua miaka mitano.

Ibara ndogo ya (3)

Mwanasheria Mkuu atakuwa ndiye mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na, kwa ajili hiyo, atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mambo yote ya kisheria, na kutekeleza shughuli nyinginezo zozote zenye asili ya au kuhusiana na sheria zitakazopelekwa kwake au atakazoagizwa na Rais kuzitekeleza, na pia kutekeleza kazi au shughuli nyinginezo zilizokabidhiwa kwake na Katiba hii au na sheria yoyote.

Ibara ndogo ya (4)

Katika kutekeleza kazi na shughuli zake kwa mujibu wa ibara hii, Mwanasheria Mkuu atakuwa na haki ya kuhudhuria na kusikilizwa katika Mahakama zote katika Jamhuri ya Muungano.

Ibara ndogo ya (5)

Mwanasheria Mkuu atakuwa Mbunge kutokana na wadhifa wake, na atashika madaraka yake mpaka-
(a) uteuzi wake utakapofutwa na Rais au 
(b) mara tu kabla ya Rais mteule kushika madaraka ya Rais, na atalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

Ibara ya 60
Kutakuwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri ambaye atakuwa ndiye mtendaji mkuu katika Ofisi ya Baraza la Mawaziri, na atatekeleza shughuli zifuatazo kwa kufuata maagizo ya jumla au maalum atakayopewa na Rais, yaani:
(a) kuanda ratiba ya mikutano ya Baraza na kutayarisha orodha ya shughuli za kila mkutano;
(b) kuandika na kuweka kumbukumbu za mikutano ya Baraza; (c) kutoa taarifa na maelezo ya maamuzi ya Baraza kwa kila mtu au chombo cha umma kinachohusika na uamuzi wowote; na

Ibara ya 61
Ibara ndogo ya (1).

Kutakuwa na Mkuu wa Mkoa kwa kila mkoa katika Jamhuri ya Muungano ambaye, bila ya kuathiri ibara ndogo ya (3), atakuwa ni kiongozi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Ibara ndogo ya (2)

Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
Ibara ndogo ya (3)

Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar watateuliwa na Rais wa Zanzibar baada ya kushauriana na Rais.

Ibara ndogo ya (4)

Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5), kila Mkuu wa Mkoa, atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa; na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za Mkuu wa Mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.

Ibara ndogo ya (5)

Pamoja na wajibu na madaraka yake yaliyotajwa kwenye masharti yaliyotangulia ya ibara hii, Mkuu wa Mkoa kwa mkoa wowote katika Tanzania Zanzibar atatekeleza kazi za shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakazokabidhiwa na Rais wa Zanzibar, na kwa mujibu wa Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 1984 au sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment