Sunday 22 December 2013

[wanabidii] HOTUBA YA WAZIRI MKUU MIZENGO P. PINDA , KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 14 WA BUNGE

HOTUBA YA WAZIRI MKUU MIZENGO P. PINDA , WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 14 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 21, DESEMBA 2013


I:                UTANGULIZI

a)            Masuala ya Jumla

 

Mheshimiwa Spika,

1.   Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa Dodoma kwa takriban siku 15 za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi za Mkutano wa 14 wa Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa hivi leo.

 

Mheshimiwa Spika,

2.   Nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Asha Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu. Wengi wetu tunafahamu uwezo mkubwa wa Dkt. Asha Rose Migiro na bila shaka ndiyo sababu Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia sifa nzuri alizonazo. Pamoja na kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje ya Bunge lako Tukufu.

 

Mheshimiwa Spika,

3. Tangu Mkutano wa 13 wa Bunge baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia fursa hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Lakini katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Azimio la Bunge kuhusu kuungana na Nchi ya Afrika Kusini, katika kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga ubaguzi wa rangi, Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba 2013. Wote tunakubaliana kwamba huu ni msiba Mkubwa kwa Dunia nzima na hasa kwa wale wanaomfahamu Mzee Mandela na historia yake.

 

4.   Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwakilisha vyema Watanzania wote katika msiba huu mkubwa wa Afrika na Dunia nzima. Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela tarehe 15 Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa kuitangaza Tanzania Dunia nzima katika ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani Afrika katika Karne ya 20. Ninaamini kwamba hiyo ni Historia ambayo haitafutika vizazi vingi vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga na kufuata nyayo zake.

 

 

b) Maswali Mheshimiwa Spika,

 

5.   Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kuuliza maswali ya msingi 170 na ya nyongeza 458 ambayo yote yalijibiwa na Serikali. Aidha, maswali 17 ya msingi na 15 ya nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa Mawaziri kutoa majibu ya maswali hayo kwa umahiri mkubwa.


 

Mheshimiwa Spika,

6.           Pamoja na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako lilikamilisha kazi kubwa

zifuatazo:

 

Kwanza: Bunge lilijadili na kukamilisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];

 

Pili:

Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge za Sekta

 

Mtambuka.

Tatu:

Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge

 

zinazosimamia Fedha za Umma; na

Nne:

Kujadili Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za Kisekta.

 

7.   Aidha, Bunge lako Tukufu lilijadili kwa utaratibu wa Hati ya Dharura Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka 2013 [The Excise (Management and Tariff) (Amendment) Bill, 2013]. Mwisho Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 ulisomwa kwa mara ya kwanza.

 

8. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili Taarifa hizo na kutoa maoni na ushauri kwa uwazi mkubwa na kwa kina.

Mapendekezo na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umepokelewa na Serikali na utazingatiwa kwa uzito unaostahili.

 

II:              KILIMO

a)  Hali ya chakula Nchini Mheshimiwa Spika,

9.          Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa 13, hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi

 

kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2013 katika maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula na lishe inaonesha kuwa jumla ya Watu 828,063 wanakabiliwa na upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya Tani 16,119 za chakula cha mgao kwa Halmashauri zenye mahitaji ya chakula cha msaada. Hadi kufikia tarehe 16 Disemba 2013, jumla ya Tani 13,716 zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika. Tani 2,402 zilikuwa hazijachukuliwa na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga,

Mpwapwa na Manyoni.

 

10.        Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua chakula hicho kufanya hivyo kabla ya tarehe 15 Januari 2014. Ambao


hawatatekeleza maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria. Nitumie nafasi hii kuwahakikishia Wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.

 

b) Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini Mheshimiwa Spika,

11.   Kutokana na miezi hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua. Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika soko hapa Nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 536.86 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikia Shilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba, 2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10 kwa kilo mwezi Novemba, 2013.

 

12.   Pamoja na kuwepo kwa hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa na zile za kipindi kama hiki mwaka jana. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu. Halmashauri zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela wa chakula kutoka mashambani na majumbani mwa Wakulima kwa lengo la kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha.

 

 

 

c) Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa

 

Mheshimiwa Spika,

13.   Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ilipanga kununua Tani 250,000 za nafaka. Wakala umeendelea na kazi hiyo na hadi kufikia tarehe 11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa umekwishanunua kiasi cha Tani 218,499 za nafaka sawa na Asilimia 87.4 ya kiasi kilichopangwa kununuliwa. Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Desemba, 2013, Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba ya jumla ya Tani 233,808 za nafaka. Kati ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi na Tani 493 ni za Mtama.

 

14.   Wakati huo huo, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unaendelea kuhamisha chakula kutoka katika maghala yake yaliyoko katika Mikoa iliyozalisha ziada kwenda kwenye maghala yaliyoko kwenye Mikoa yenye upungufu wa chakula ili kukabiliana na mahitaji ya chakula cha msaada kitakachohitajika kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe 9 Desemba, 2013, jumla ya Tani 44,129 za Mahindi zimekwishahamishwa. Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kununua chakula katika Mikoa yenye ziada ya chakula na kukipeleka katika Mikoa yenye upungufu wa chakula.


 

 

d) Hali Halisi ya Usambazaji wa Pembejeo

 

Mheshimiwa Spika,

15.   Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali ilichapisha jumla ya vocha 2,796,300, kwa ajili ya pembejeo za Kilimo kwa msimu wa Kilimo wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12 Desemba, 2013, Tani 74,925 sawa na Asilimia 96 za mbolea ya kupandia na Tani 42,295 sawa na Asilimia 91 ya mbolea ya kukuzia zilikuwa zimekwishafikishwa katika Mikoa husika kulingana na aina ya mazao yanayohitaji mbolea hizo. Aidha, Maghala ya Wakala wa Mbolea Jijini Dar es Salaam yana akiba ya kutosha ya mbolea hiyo. Nirejee kutoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha kuwa vocha zote zinatolewa kwa walengwa kwa wakati sambamba na aina ya pembejeo inayomlenga Mkulima husika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.

 

e) Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.

 

Mheshimiwa Spika,

16.   Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni 109.6 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kununua Tani 250,000 za nafaka. Hadi kufikia tarehe 19 Desemba, 2013 NFRA ilikuwa imenunua jumla ya Tani 218,499 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 109.25 na kwa ajili hiyo. Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri ya wastani wa Shilingi 500/= kwa kilo ya mahindi, zoezi hilo lilikuwa na matokeo mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita na liliwavuta Wananchi wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia nafaka. Hadi sasa Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa ajili ya zoezi hilo na imehakikisha kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa NFRA wamelipwa fedha zao. Aidha, natambua kuwa NFRA ilitumia baadhi ya Wakala kukusanya nafaka hiyo kutoka kwa Wakulima na kama nilivyosema katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali inatambua kuwa Wakala hao kutoka Mikoa ya Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga wanaidai Serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8.65 Niwaombe Wakala wote wanaoidai Serikali kuendelea kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa deni hilo kwa vile kiasi cha deni lao lipo ndani ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ununuzi wa nafaka katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.

 

 

III:            MPANGO WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA

 

 

Mheshimiwa Spika,

 

17. Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial Inclusion Framework). Uzinduzi wa Mpango huu ulifanywa na Malkia wa Uholanzi Mheshimiwa Máxima Zorreguieta


Cerruti ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa.

 

Mheshimiwa Spika,

 

18.   Lengo la Mpango huo ni kusimamia ukuzaji wa huduma za kifedha kwa jamii Nchini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Fedha. Vilevile, Mpango unalenga kusogeza huduma karibu kwa jamii pana zaidi ya Watanzania kwa kutumia mifumo ya Teknolojia mbalimbali katika kufikisha huduma za kifedha kwa Wananchi na hasa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi waliopo Vijijini ambao wengi wao wako nje ya mfumo rasmi wa kifedha. Teknolojia hizo ni pamoja na:

 

(a)         Huduma za Kibenki za moja kwa moja na kupitia Wakala (Agent Banking);

 

(b)        Huduma za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali kama vile M-PESA, TIGO

PESA, AIRTEL MONEY na Easy PESA.

 

(c)        Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of Sales – POS).

 

19.        Aidha, Mpango huu utaweka mazingira linganifu na yaliyo bora kwa kutumia Sayansi na Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi, kuimarisha Sekta ya

 

Fedha katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa ujumla. Mpango huu pia utawezesha kuongeza kasi ya upatikanaji wa Chakula, masuala ya Lishe na

 

Maendeleo Vijijini kwa ujumla.

 

Mheshimiwa Spika,

 

20.   Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika Nchi mbalimbali Barani Afrika unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo rasmi wa Taasisi za Kifedha ni Asilimia 24 tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi waliopo kwenye Mfumo rasmi wa Asasi za Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOs) ni Asilimia 22. Asilimia 78 ya Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na wengi wao ni kutoka Vijijini hasa Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unalenga kufikia Asilimia 50 ya Watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha ifikapo mwaka 2016.

 

Mheshimiwa Spika,

21.        Kiwango hiki kidogo cha Wananchi walio katika Mfumo rasmi wa huduma za

 

kifedha unatokana na changamoto zifuatazo:

 

Moja: Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha Vijijini ni hafifu hususan barabara, mawasiliano, makazi na huduma za kiusalama;


Mbili:        Wananchi wengi wa Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua

umuhimu na faida ya huduma za kifedha. Aidha, utamaduni wa

kujiwekea akiba na kukopa ni mdogo; na.

 

Tatu:       Taasisi nyingi za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa Vijijini

ambao ni Wakulima hawana fedha za kutosha kuweza kuweka akiba

katika Taasisi hizo na uwezo wao wa kukopa mikopo ni mdogo, hivyo

wakipeleka huduma zao huko hawatapata faida.

 

Mheshimiwa Spika,

 

22. Zipo faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Wananchi wengi wa Vijijini hasa Wakulima. Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:

 

Moja:

Kuwezesha Wananchi kujiwekea Akiba na pia kupata mikopo ya

 

kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za

 

kijamii hivyo kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;

Mbili:

Huduma za Kifedha Vijijini zinawawezesha Wananchi wengi hasa

 

Wakulima kupata mikopo ya pembejeo na mikopo ya ununuzi wa

 

mazao;

Tatu:

Huduma za Kifedha Vijijini ni Mkombozi wa Makundi maalum kama vile

 

Vijana, Wanawake, Wazee, na Walemavu. Aidha, zinasaidia Wananchi

 

kujiongezea kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na

 

kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki;

 

na

Nne:

Kuwepo kwa Huduma za Kifedha Vijijini kunaongeza Usalama wa

Chakula, kulinda mazingira na kufanya Vijiji kuwa ni sehemu nzuri ya kuishi. Mheshimiwa Spika,

23.   Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuanzisha Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini kwa mfano tumeweza kuanzisha Benki nyingi Nchini. Tayari tunazo Benki takriban 52 zenye matawi zaidi ya 609 kote Nchini. Lakini pia tunazo huduma za Bima kwa Makampuni Binafsi zaidi ya 27 na Mawakala wa Bima takriban 600. Ipo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Umma 5, Masoko ya Mitaji na Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban 5,600.

 

24.   Aidha tunazo huduma za Kifedha kwa kutumia Huduma za Kifedha kupitia mtandao (PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (POINTS OF SALES – POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo zaidi ya 55,000 ambapo Waajiriwa wa moja kwa Moja (Direct Employment) wanakadiriwa kufika takriban 100,000.


Mheshimiwa Spika,

25.   Maisha bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na kutumia Teknolojia na kurahisisha maisha. Kwa mfano, huduma za M-PESA peke yake zinawezesha malipo kwenye biashara mbalimbali zaidi ya aina 300 ikiwemo manunuzi kwenye Supermarket na maduka ya kawaida. Huduma hizo ambazo zinatolewa pia kwa njia ya TIGOPESA, AIRTEL MONEY, EASY PESA zinaweza kulipia Luku, Ada za shule na Vyuo, Tiketi za ndege, kufanya marejesho Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya Makampuni haya yameunganisha huduma zao na Benki zaidi ya 20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard Chartered, Amana Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia huduma za jumuishi za kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka Akaunti ya Benki kwenda M- PESA, TIGO PESA n.k. halafu akazitoa kupitia Wakala. Kwa sasa Watumishi walio Vijijini hawana tena sababu ya kufunga Ofisi kufuata mishahara Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha na wanaweza kutoa pesa kupitia Wakala, na kwa kufanya hivyo ufanisi na tija kwa Watumishi unaongezaka. Mheshimiwa Spika,

26.   Ni kweli kwamba tunayo kazi kubwa ya kutekeleza Dhana ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini. Lakini ni ukweli kuwa Uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha una manufaa makubwa na mengi ikiwemo kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini kwa kupeleka maendeleo Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo ya Milenia. Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango huu utatuwezesha kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi. Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za Kifedha na Vituo vya Kifedha kupitia mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala kuongeza jitihada katika kusambaza huduma za Kifedha Vijijini ambako ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

 

IV:        NISHATI NA MADINI

 

 

a)       Mradi wa Gesi

 

Mheshimiwa Spika,

 

27.   Kama ambavyo Wananchi wengi wanafahamu, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafishia Gesi Asilia katika maeneo ya Madimba, Mtwara Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa. Pia ujenzi wa Bomba la kusafirishia Gesi hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam unaendelea vizuri. Mradi huu utakapokamilika utaunganisha maeneo yanayozalisha Gesi Asilia hususan Mnazi Bay-Mtwara, Songo Songo, Kisiwani, Mkuranga, Ntorya na maeneo yaliyogunduliwa Gesi katika eneo la bahari ya kina kirefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi Asilia mbali na matumizi mengine, inatumika katika kuzalisha umeme ambao kwa sasa Asilimia kubwa unazalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta yanayoingizwa kutoka Nchi za nje na hivyo kuligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.


Mheshimiwa Spika,

28.        Katika utekelezaji wa mradi huu, Kazi zifuatazo zimekamilika hadi kufikia

 

 

tarehe 30 Novemba, 2013:

Moja:

Kukamilika kwa upakuaji wa Shehena ya Sita (6) ya Mabomba ya Mradi

 

yapatayo 4,444 ya umbali wa Kilomita 51.169 katika Bandari ya Mtwara.

Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013 ni 24,935 ya

 

 

umbali wa kilomita 295.5;

Pili:

Kusafisha Mkuza wa Mabomba, tayari Kilomita 498.5 zimekamilika;

Tatu:

Usafirishaji wa mabomba kutoka kwenye yadi za kuhifadhia na

 

 

kuyasambaza kwenye Mkuza tayari kwa kuyaunganisha kwa

 

 

kuchomelea. Hadi sasa mabomba ya Kilomita 186.9

 

 

yamekwishasafirishwa;

Nne:

Uchimbaji wa njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa Kilomita 27.0

 

 

umekamilika;

Tano:

Uwekaji wa mabomba kwenye njia yake sambamba na kuweka Mkongo

 

wa Mawasiliano (Fiber Optic Cable) umekamilika Kilomita 21.1;

Sita:

Kufukia bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano. Tayari  Kilomita

 

7.30 za Bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano zimefukiwa; na

Saba:

Utafiti wa njia ya Bomba la Baharini nao umekamilika.

 

Hayo ni maeneo machache ambayo nimeona niyataje.

 

 

Mheshimiwa Spika,

 

29.   Ni kweli kwamba kazi za mradi huu ni kubwa lakini kwa ujumla zinaendelea vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo za mradi huu ambazo tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi wa Mradi ambao sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi wa Gesi na Mafuta. Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi ni za kitaalamu sana, malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC) ni kuajiri wafanyakazi Wakiwemo Wazawa mapema ili waweze kushiriki na kujifunza kwa vitendo shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi hatua kwa hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa ujenzi. Utaratibu huu utasaidia kupata wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania watakaoendesha (operations) na kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi kwa kipindi chote cha matumizi.


Mheshimiwa Spika,

30.   Vilevile moja ya makubaliano katika Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huu, Mkandarasi anawajibika kuwapeleka Wafanyakazi kwenye mitambo na mabomba yanayofanya kazi kwa sasa kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja ili wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia shughuli zote za kuendesha mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi. Malengo ya TPDC ni kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti wakati wa kipindi cha ujenzi ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi Wafanyakazi wote wawe wamekwishapata uzoefu wa kutosha.

 

Mheshimiwa Spika,

31.   Kampuni nyingi zilizopo Mtwara zinazojishughulisha na mambo ya utafiti na uzalishaji wa Gesi na Viwanda vinavyohusiana na matumizi ya Gesi, zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa. Kwa mfano, Mpango wa kujenga mitambo ya kutengeneza Gesi kuwa kimiminika (LNG) wa Kampuni ya British Gas Tanzania utakuwa na utengenezaji wa ajira nyingi za kiwango kuanzia Kada ya Chini na Kada ya Kati ambayo itasomesha Watanzania kupitia VETA katika fani mbalimbali. Wako watakaosomeshwa katika fani ya Vyuma, wengine ujenzi, uhandisi wa miundombinu na ufundi wa vyuma na umeme.

 

32.   Katika Kada ya Kati, Kampuni ya Gesi Tanzania wanatarajiwa kusomesha wataalamu 16,756 waliofaulu vizuri masomo ya Kidato cha Nne. Takwimu zinaonesha kuwa kwa Mtwara tu, kumekuwapo ajira mpya 400, na Watanzania wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta ni sawa na Asilimia 70 ya watoa huduma hiyo Nchini. Asilimia 30 iliyobaki ya watoa huduma inatolewa na Wageni.

 

 

33.   Katika Kada za Juu, Kampuni itasomesha na kuajiri Wataalamu wa Jiolojia, Uhandisi, Kemia na Sayansi husika kwenye Gesi na Mafuta. Matokeo yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa VETA 370 wamesomeshwa kuhusu Gesi na Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa na Wanafunzi 12 wa Kada za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na Mafuta ndani na nje ya Nchi.

 

Mheshimiwa Spika,

34.   Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya British Gas Tanzania wamegundua gesi kiasi cha Futi za Ujazo Trilioni 13. Katika kuandaa na kuendesha mradi wa uzalishaji Gesi nyingi kiasi hicho ni dhahiri kwamba ajira zitapatikana kwa maelfu ya Watanzania. Katika hatua ya ujenzi, mradi utatoa ajira kwa maelfu; na katika uzalishaji (operations) ajira nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini, na katika mnyororo wa usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii kuwapa Watanzania matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa mengi sana, kuanzia upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha Wananchi


wetu kuhusu manufaa ya mradi huu katika Nchi yetu. Ni fursa ya kipekee ambayo Wananchi wetu wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha bora.

 

V:            MATUMIZI YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs)

 

Mheshimiwa Spika,

35.   Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Serikali ililiarifu Bunge lako Tukufu kuhusu mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devices- EFDs). Mashine hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata mapato stahiki bila udanganyifu. Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye Hifadhi Kuu ya Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.

 

Mheshimiwa Spika,

36.        Katika utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka huu, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi 200,000 kati ya 1,500,000 ili waweze kutumia Mashine za

 

Kielektroniki. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye biashara kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika zoezi hili, Wafanyabiashara Wadogo wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile Wamachinga na wale wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata kidogo.

Mheshimiwa Spika,

37.   Katika utekelezaji wa zoezi hili kumejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wafanyabiashara Nchini hususan wa Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na matumizi ya Mashine hizi. Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu: Bei kubwa ya ununuzi wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za kutolea Risiti; Mchakato uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa wa kutumia Mashine hizo; na Gharama za matengenezo.

 

Mheshimiwa Spika,

38.   Kwa kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine za Kielektroniki zinafanya kazi zifuatazo:

Moja: Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya

 

kuandikia risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;

 

Pili:                   Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi

 

na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua

miaka mitano;


Tatu:

Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa siku,

 

kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi

 

kisichopungua miaka mitano;

Nne:

Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja

 

kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na

 

Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya

 

Taifa ya Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;

Tano:

Mashine zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka

 

kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu

 

Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;

Sita:

Kutuma na kupokea fedha kwa njia ya "Mobile Money". Utaratibu

 

huu unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na

 

huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji,

 

Simu, n.k;

Nane:

Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza

 

inayoeleweka kwa Wananchi wengi;

Tisa:

Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania

kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza Kodi halali. Mheshimiwa Spika,

39.   Msingi wa bei ya kununulia Mashine hizi za Kielektroniki umezingatia pamoja na mambo mengine, manufaa na faida nyingi nilizozitaja kwa mtumiaji na ubora wa mashine zenyewe. Aidha, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali Duniani unaonesha kuwa mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo juu zinauzwa na wasambazaji kwa kati ya Shilingi 600,000/= (Dola 375) hadi Shilingi 778,377/= (Dola 486) ikilinganishwa na bei za Mashine za Kielektroniki za Nchi nyingine zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania ambazo zinauzwa bei kubwa za kati ya Dola za Kimarekani 360 hadi 870. Pamoja na bei hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana na Wasambazaji wa Mashine hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei hizo.

 

Mheshimiwa Spika,

40.   Kuhusu bei za karatasi za kutolea Risiti uchunguzi unaonesha kuwa karatasi hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/= hadi Shilingi 4,500/= kuzingatia ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo. Karatasi hizo zina uwezo wa kutoa wastani wa risiti kati ya Risiti 200 hadi 1,000 kulingana na urefu wa "Paper Roll"! au Bunda. Bei ya Karatasi hizi zinazojulikana kama "Thermal Paper" umezingatia kwamba ni za kisasa na hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza usalama.


Mheshimiwa Spika,

41.   Kuhusu utaratibu uliotumika kuwapata Watengenezaji na Wasambazaji wa Mashine hizi za Kielektoniki na Wasambazaji wa karatasi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa ushindani wa Kimataifa na haukuwa na dosari yoyote.

 

 

Mheshimiwa Spika,

42.   Katika kutafuta Watengenezaji na Wasambazaji, kwenye Awamu ya Kwanza Watengenezaji Wanne (4) na Wasambazaji Sita (6) walipatikana kwa kutumia Zabuni ya wazi ya Kimataifa (International Competitive Tendering) kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi Desemba Mwaka 2009 mpaka Mei 2010 makubaliano yaliingiwa kati ya kila Mtengenezaji na Msambazaji aliyechaguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya "Memorandum of Understanding (MOU).

 

43.   Kwenye Awamu ya Pili ya utekelezaji wa utaratibu huohuo wa Zabuni ya Watengenezaji ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News, The African, Tovuti ya TRA na Tovuti ya PPRA. Jumla ya Wazabuni Kumi na Nne (14) walituma maombi ambayo yalifunguliwa mara moja baada ya saa Nne asubuhi tarehe 27 Septemba 2012. Watengenezaji wa Mashine Wanne (4) walichaguliwa kati ya Kumi na Nne (14) waliokuwa wameomba na Wasambazaji Watano (5) walipatikana kati ya Tisa waliotuma maombi yao ndani ya muda. Kwa kifupi, huo ndio utaratibu uliotumika ambao ulikuwa wa wazi na ushindani.

Mheshimiwa Spika,

44.   Ili kuhakikisha ubora wa Mashine hizi za Kielektroniki, Watengenezaji wametoa "Guarantee" ya muda wa miaka mitatu kwamba Mashine inayoharibika bila kukusudia na watawajibika kutoa mashine nyingine na pia kutoa elimu ya matumizi ya mashine hizo. Vilevile, kwa mujibu wa Mkataba ulioingiwa kati ya Wasambazaji na TRA, Wasambazaji wanawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo kila zinapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji kutafuta watengenezaji wao wenyewe. Napenda kuwahakikishia Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na kuwawezesha kulipa kodi stahiki Serikalini.

 

Mheshimiwa Spika,

45. Kwa kutambua umuhimu wa mashine hizi katika kuongeza Mapato ya Ndani; na ili kuyashughulikia malalamiko ya baadhi ya Wafanyabiashara yaliyojitokeza, Serikali imesogeza mbele muda wa mwisho wa kununua Mashine za Kielektroniki hadi tarehe 31 Desemba, 2013. Lengo ni kuwawezesha Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa kununua mashine hizi na kujifunza namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa

elimu kuhusu matumizi endelevu na faida za Mashine za Kielektroniki kwa


Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na huduma. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Mfumo huu wa Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu na kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.

 

VI:        USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

 

Mheshimiwa Spika,

 

46. Tarehe 16 – 25 Oktoba 2013 nilifanya ziara ya kikazi Nchini China kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Keqiang.

 

Katika ziara hiyo, nilifuatana na Viongozi wa Serikali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa Asasi za Sekta Binafsi Tanzania na Watendaji Wakuu wa Serikali na Mashirika ya Umma ambao walishiriki kwenye mazungumzo na Wabia wetu kwa upande wa Jamhuri ya Watu wa China.

 

Mheshimiwa Spika,

 

47.   Dhamira kubwa ya ziara hiyo kimsingi ilihusu; kukuza mashirikiano ya kibiashara na utalii Nchini, kufanya mazungumzo na vyombo vya fedha ili kupata mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili marafiki, kuona Sekta Binafsi ya Tanzania inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa China na mwisho kutoa shukrani kwa misaada na mikopo ambayo Nchi yetu imepokea kutoka Jamhuri ya Watu wa China.

 

Mheshimiwa Spika,

 

48.   Kama mnavyojua Taifa la Jamhuri ya Watu wa China ni miongoni mwa Nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na limepiga hatua kubwa sana katika maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika Taifa la China, nilitoa mwaliko wa kuwakaribisha ili kushirikiana na Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wake katika Nyanja za kiuchumi, utamaduni na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na soko kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.

 

Mheshimiwa Spika,

 

49.   Katika ziara hiyo nilipata fursa ya kutembelea Miji ya Beijing, Shenzhen, Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata nafasi ya kukutana na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China. Kutokana na Mikutano hiyo, baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma wameanza kuja Nchini kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ili kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi.


Mheshimiwa Spika,

 

50.   Kwa ujumla ziara hii ilikuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano, pamoja na kuendeleza na kudumisha ushirikiano ambao umeanzishwa na Viongozi waasisi wa Nchi hizi mbili yaani Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong wa Jamhuri ya Watu wa China, kwenye ziara hiyo, niliweza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Bwana Li Keqiang, pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China. Ninaamini tukijipanga vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.

 

Mheshimiwa Spika,

 

51.   Ziara yangu pia ilifanikisha kutiwa saini kwa Mikataba ya ushirikiano wa Tanzania na China katika eneo la Sayansi na Teknolojia na katika Utalii. Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu uuzaji wa bidhaa za baharini za Tanzania Nchini China na kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao la Pamba Nchini. Aidha, Mikataba ya Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na Makazi baina ya Makampuni ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya Umeme – TANESCO, Shirika la Taifa la Maendeleo – NDC na Shirika la Taifa la Nyumba – NHC ilisainiwa.

 

Mheshimiwa Spika,

52.   Mafanikio mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuyashawishi Makampuni makubwa ya usafiri wa anga na Mawakala wa safari za kitalii kuwekeza Tanzania. Katika jitihada hizo nilikutana na Makampuni ya China Hainan, China Southern Air Line Holding Company na China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited.

53. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa kiasi kikubwa Makampuni haya ya Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha utayari wao wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na China. Aidha, Kampuni ya

China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited ambayo inafanya biashara ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali duniani wameonesha nia ya kuja kuwekeza hapa Nchini katika Sekta ya Hoteli kubwa za Kitalii. Kampuni ya China Merchants Holdings International Limited ambayo imehusika katika ujenzi wa Bandari kubwa na Mji wa Shenzhen katika Jimbo la Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia ubia na Serikali yetu katika ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na Mji wa Bagamoyo unaotarajiwa kuwa "Trade Hub" ya Afrika.

 

Mheshimiwa Spika,

54.   Tanzania imedhamiria kuendeleza uchumi wake kwa lengo la kufikisha Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa Kati kabla au ifikapo mwaka 2025. Viashiria vyote vinaonesha hivyo, na ndio sababu Makampuni yote niliyozungumza nayo wakati wa ziara hiyo yameonesha shauku kubwa ya kuja kuwekeza Tanzania katika Sekta mbalimbali na mengine tayari yapo Nchini kutekeleza miradi mbalimbali. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kwa upande wake


tutajitahidi kupokea Uwekezaji huo na hivyo kunufaika na matokeo tunayotarajia. Aidha, tutaendelea kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na uwekezaji ili kuweza kuvutia Mitaji na Wawekezaji wengi zaidi pamoja na Watalii kutoka China na maeneo mengine duniani.

 

VII:       JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

 

Mheshimiwa Spika,

55.   Mtakumbuka tarehe 7 Novemba, 2013 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihutubia Bunge ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 Kampala Nchini Uganda, Wakuu wa Nchi hizo akiwemo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete walikutana na waliidhinisha na kuweka Saini Itifaki ya Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki. Aidha, Viongozi hao walizitaka Nchi Wanachama kukamilisha taratibu za kuridhia Itifaki hiyo ifikapo mwezi Julai, 2014.

 

Mheshimiwa Spika,

56.   Manufaa ya Umoja wa Fedha ni pamoja na: kupunguza gharama ya kufanya biashara katika Nchi Wanachama; kuwezesha Nchi Wanachama kuwa na kiwango kidogo na tulivu cha Mfumuko wa Bei; kuwa na viwango vidogo vya riba ya kukopa; na kuepusha athari za ubadilishaji wa fedha ndani ya Jumuiya kwa kuwa na Sarafu Moja. Matarajio ni kujenga ukanda tulivu wa kifedha (Monetary and Financial Stability Zone) utakaorahisisha na kusaidia ukuaji wa biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya.

 

Mheshimiwa Spika,

57.   Katika Mkutano huo wa Kampala Wakuu wa Nchi pia waliridhia Mfumo wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuagiza kuwa ifikapo mwezi Januari 2014, Nchi Wanachama ziwe zimeanza utekelezaji wake na kuukamilisha ifikapo au kabla ya mwezi Juni 2014. Aidha, Wakuu wa Nchi walipokea Taarifa kuhusu maendeleo ya Mpango Kazi wa kuelekea kuanzisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Walitumia muda wa Mkutano huo kujadili hali ya usalama iliyopo katika Nchi hizi na waliona kuna umuhimu wa kuongeza juhudi katika kukabiliana na Ugaidi.

 

Mheshimiwa Spika,

58.   Kwa ujumla Mkutano huo ulikuwa na mafanikio sana hasa katika kuimarisha Umoja wa Jumuiya. Aidha Wakuu wa Nchi wote kwa pamoja walitumia muda huo kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha kwamba mahusiano yetu kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanadumu na tunaendelea kuijenga Jumuiya na kuiimarisha kwa nguvu zetu zote.


X:            PROGRAMU YA KUBORESHA MIJI NCHINI (URBAN LOCAL GOVERNMENT

STRENGTHENING PROGRAMME-ULGSP)

 

Mheshimiwa Spika,

59.   Wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge, nilieleza kuhusu Programu ya Kuboresha Miji Nchini (Urban Local Government Strengthening Programme-ULGSP) ya miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2013 hadi 2018. Huu ni mwendelezo wa Programu ya Uendelezaji na Uboreshaji Miji Nchini (Tanzania Strategic Cities Programme -TSCP); ambao kwa sasa unakaribia kumalizika utekelezaji wake. Programu hii ya ULGSP kwa sasa inahusisha Manispaa 11 na Miji 7. Manispaa hizo ni Tabora, Morogoro, Shinyanga, Lindi, Sumbawanga, Musoma, Songea, Singida, Iringa, Bukoba na Moshi. Miji mingine inayohusika ni Kibaha, Geita, Babati, Korogwe, Mpanda, Njombe na Bariadi. Halmashauri hizi zinazojumuisha Manispaa na Miji 18 ziko tayari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, ambavyo ni pamoja na:

 

i.       Kuongeza Bajeti ya mapato kila mwaka;

ii.       Kutokuwa na Hati Chafu za Hesabu za Halmashauri,

iii.       Kuunda Kamati za kushughulikia matatizo yanayotokana na Programu

kwenye ngazi ya Halmashauri, ngazi ya Kata na Mitaa;

iv.         Kuhakikisha Programu hiyo imetangazwa na kueleweka na wakazi wa

Halmashauri za Manispaa na Miji;

v.         Kuhakikisha kuna Wakuu wa Idara wa kutosha;

vi.         Kuhakikisha Sheria za Manunuzi zinafuatwa;

 

vii.         Kuhakikisha Watu watakaohamishwa na Programu na kulipwa fidia

hawazidi nyumba 20;

 

viii.         Kuhakikisha miradi iliyotekelezwa inalingana na thamani ya fedha

iliyotumika;

 

ix.        Kutekeleza miradi ya miundombinu iliyoko kwenye menu;

 

x.         Kupeleka taarifa za kila robo mwaka za miradi kwa muda unaotakiwa;

 

xi.        Kuhakikisha kuna Master Plan ya Mji;

 

xii.         Kuhakikisha ukusanyaji wa kodi ya majengo unaongezeka kati ya Asilimia 5

 

hadi 30; na

 

xiii.         Kuhakikisha taarifa za Mkaguzi wa Ndani zinaenda kwenye vikao vya

Halmashauri kila robo mwaka.

 

Ukikosa hapa fedha hizo hazipatikani.

 

Mheshimiwa Spika,


60.   Nimetaja baadhi ya Vigezo kwani viko zaidi ya 200 na vinagusa kila Sekta ya Halmashauri. Upimaji wa vigezo vyote vitafanyika mara 2 kwa mwaka; na Halmashauri zitakazoshindwa kufikia Alama (Marks) 60 na kuendelea, watapunguziwa fedha za miradi yao. Hivyo, Mikoa na Mabaraza ya Madiwani lazima yahakikishe kuwa vigezo vyote vinasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu. Aidha, TAMISEMI wawachukulie hatua za kisheria wale wote watakaozembea katika kutimiza vigezo hivi na kuathiri maendeleo ya Wananchi.

 

Mheshimiwa Spika,

61.   Programu hii ambayo ni ya kwanza Afrika itatumia Dola za Kimarekani 255, fedha ambazo zilikuwa zitolewe mwezi Julai mwaka huu, lakini kutokana na matatizo ya ubadhirifu yaliyojitokeza kwa Wasimamiaji wa fedha zilichelewa kutolewa. Hata hivyo, baada ya kuwapeleka wahusika wa ubadhirifu kwenye Vyombo vya Sheria, Wafadhili waliridhika na hatua zilizochukuliwa, hivyo tarehe 27 Novemba, 2013 Wafadhili walitoa fedha za Awamu ya Kwanza, ambazo zilitumwa kwenye Halmashauri hizo 18. Miradi iliyopo kwenye Programu ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na mifereji ya mvua, uwekaji taa barabarani, ujenzi wa Stendi za Mabasi, upimaji viwanja, utengenezaji wa madampo, kuweka miundombinu ya majitaka na uboreshaji wa makazi. Hii ni baadhi ya Miradi ya Miji iliyoibuliwa na Halmashauri zenyewe kufuatana na matatizo ya Miji hiyo. Hivyo, ninawaomba TAMISEMI – wasimamie Programu hii vizuri ili Miradi husika iweze kutatua matatizo ya Wananchi katika maeneo yao na kuhakikisha Mapato ya Halmashauri yanaongezeka. Lengo ni kuwezesha Halmashauri hizo kujitegemea baada ya Miradi hiyo kukamilika.

 

 

XI: USIMAMIZI NA UDHIBITI WA FEDHA KATIKA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

 

 

Mheshimiwa Spika,

62. Kama ambavyo itakumbukwa, wakati wa majadiliano ya Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa za Serikali za Mitaa, kwa mwaka 2011/2012, Waheshimiwa Wabunge walionesha masikitiko yao kwa vitendo vya ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na baadhi ya Halmashauri Nchini.

Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia mjadala huo walidai kuwa Serikali imekuwa haichukui hatua dhidi ya Watumishi wanaofanya makosa katika Halmashauri. Napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha za Umma, Serikali imejitahidi kuimarisha usimamizi na utendaji katika eneo hili. Jitihada hizi zimedhihirishwa na Matokeo ya Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo yanaonesha kuongezeka kwa ubora wa Hati za Ukaguzi zinazotolewa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan kuanzia mwaka 2000 hadi sasa. Kwa mfano, mwaka 2000/2001 Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unaonesha kuwa Halmashauri


zilizopata Hati safi zilikuwa 16 sawa na Asilimia 14 ya Halmashauri zote. Aidha, Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 23, sawa na Asilimia 20 na Halmashauri zilizopata Hati Chafu zilikuwa 75 sawa na Asilimia 65 ya Halmashauri zote.

 

Mwaka 2005/2006 Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati Safi iliongezeka hadi kufikia 53, sawa na Asilimia 43 na Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 67, sawa na Asilimia 54 na Halmashauri zenye Hati Chafu zilikuwa Nne (4), sawa na Asilimia Tatu (3).

Mwaka 2011/2012 taarifa za Ukaguzi ziliimarika zaidi ambapo Halmashauri zilizopata Hati Safi ziliongezeka maradufu hadi kufikia 104, sawa na Asilimia 78 na zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 29, sawa na Asilimia 21 na hakukuwa na Halmashauri iliyopata Hati Chafu.

Mheshimiwa Spika,

63.   Jitihada hizi ni kubwa. Hivyo, Serikali itaendelea kuimarisha Usimamizi na Udhibiti na Mapato na Matumizi ya Serikali katika Sekta zote na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji na kudhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za Umma. Lengo ni kuongeza kasi ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu na Kukuza Uchumi kwa haraka.

 

Mheshimiwa Spika,

 

64.   Pamoja na jitihada hizo za Serikali zinazoonekana, napenda kuwahakikishia kwamba Watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za Umma wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi, kushushwa vyeo, na kufikishwa mahakamani. Aidha, kesi za Watumishi hao ziko katika Mahakamani na katika Vyombo vya nidhamu vya Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao kuhakikisha kwamba tunajenga nidhamu. Kutokana na hatua hizo kati ya mwaka 2011/2012 hadi Septemba, 2013 jumla ya Wakurugenzi 52, Wakuu wa Idara 65 na Watumishi wengine 749 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri mbalimbali Nchini. Hatua hizo za kinidhamu ni kama ifuatavyo:

i)        Waliofukuzwa kazi ni 232,

ii)       Waliosimamishwa kazi ni 186,

iii)      Waliovuliwa Madaraka ni 33,

iv)      Waliopunguziwa Mshahara ni 1,

v)       Walioshushwa Cheo ni 32,

vi)      Walipewa ONYO ni 113,

vii)     Waliofikishwa Mahakamani ni 233,

viii)    Waliofikishwa Polisi na TAKUKURU ni 36.

Serikali itaendelea kusimamie eneo hili kuhakikisha fedha za Umma zinatumika vizuri.

 

Mheshimiwa Spika,


65.   Pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa Watumishi hao mmoja mmoja, Serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana na tatizo la ubadhirifu wa mali za Umma katika Halmashauri.  Juhudi hizo ni pamoja na kuongeza uwezo kwa kuajiri Wahasibu wa kutosha katika Halmashauri zetu; kuanzisha Kamati za Mapato na Matumizi katika ngazi zote za Halmashauri na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Kamati za Mapato na Matumizi za Halmashauri zote. Mbinu nyingine zinazotumika ni kufanya Ukaguzi Maalum kubaini ufisadi na ubadhirifu wowote uliojitokeza. Kwa mfano, Katika mwaka wa fedha 2011/12 kumefanyika Kaguzi maalumu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kumi na nne (14), ambazo ni Kilindi, Kiteto, Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda. Kaguzi hizo zimesaidia sana katika kujenga nidhamu ya Watumishi katika Halmashauri hizo.

 

Mheshimiwa Spika,

66.   Serikali pia imeweza kubadili na kuweka Mfumo wa 'Lawson' katika kila Halmashauri ili kumaliza tatizo la Mishahara kwa Watumishi waliofariki, walioacha kazi, wastaafu, n.k. Vilevile kuna Mfumo wa Epicor 9.05 ambao zinasaidia kudhibiti Bajeti za Mapato na Matumizi katika Halmashauri Nchini. Mafunzo kuhusu matumizi ya Mifumo hii mipya yanaendelea kutolewa ili kuweza kutumia mifumo hii kwa ufanisi. Vilevile, Wakuu wa Mikoa walikwishaagizwa kuhudhuria Vikao vya Baraza za Halmashauri; katika kujadili Hoja za Ukaguzi ili Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali aweze kufuta zile zilizojibiwa kikamilifu. Hoja ambazo hazikupata majibu kikamilifu, Sheria zifuatwe na wenye kuhusika na ubadhirifu wowote wachukuliwe hatua zinazostahili. Aidha, Maafisa Masuuli (Wakurugenzi) wanaohusika na Hoja mbalimbali za Ukaguzi wanapaswa kuitwa kwenye Halmashauri walizotoka ili kujibu hoja zinazowahusu bila kujali wamehamishiwa wapi.

 

XI:        HITIMISHO

 

Mheshimiwa Spika,

67.   Tumekuwa na muda mzuri wa kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Nchi yetu hapa Bungeni kwa kipindi chetu tulichokuwa katika Mkutano huu. Napenda niwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza Vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge,


Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.

 

68.   Niwashukuru Wabunge wote kwa kujadili vizuri hoja za zilizojitokeza hapa Bungeni. Lakini kipekee niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri Wanne waliokubali kubeba jukumu ka kuwajibika kwa yote yaliyotokea. Tunawashukuru kwa uzalendo wao kwa Nchi yetu na tunawatakia kila la kheri katika maisha yao. Mheshimiwa Spika,

69.   Tunahitimisha shughuli za Bunge hili tukiwa tumebakiza siku chache kabla ya kufika Mwisho wa Mwaka huu 2013. Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema atujalie katika siku hizi chache tuweze kusherehekea Sikukuu njema ya Krismas na tuvuke salama mwisho wa mwaka na kuingia Mwaka Mpya 2014 kwa Amani na Furaha!.

 

Mheshimiwa Spika,

70.   Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wote tunavyofahamu, tutakuwa na Bunge la Katiba litakalofanyika mapema mwakani na kwa tarehe itakavyopangwa. Kutokana na utaratibu huo ni dhahiri kwamba wengi wetu tutakutana wakati wa Bunge la Katiba. Nitumie fursa hii kuwatakia safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu na wengi wenu niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya hadi tutakapokutana wakati wa Bunge la Katiba.

 

Mheshimiwa Spika,

71.   Baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi litakapokutana kwa Mkutano maalum wa Kumi na Tano wa Bunge la Bajeti tarehe 06 Mei, 2014 saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu hapa Dodoma.

 

Mheshimiwa Spika,

72.       Naomba kutoa hoja. 

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment