Saturday, 31 May 2014

[wanabidii] Profesa Muhongo anapata wapi jeuri hii?

Ndugu Mhariri,
Wakati anasoma bajeti ya Wizara yake, Profesa Muhongo akimchana Dr Ole Sendeka bungeni kwa kumkejeli na kumdhalilisha hadharani huku akifikia hatua ya kutaka kuweka hadharani matokeo yake (Ole Sendeka) ya mtihani wa kidato cha nne aliokaa mwaka 1984 katika Shule ya Sekondari Monduli.

Isingekuwa busara za Spika Makinda ni dhahiri kwamba Muhongo angeanika matokeo ya Ole Sendeka hadharani.

Badala ya kujibu tuhuma za ufisadi wa fedha za umma unaomkabili yeye (Profesa Muhongo) na mshirika wake (Maswi), Muhongo alitumia muda wa umma vibaya kwa kumshambulia Ole Sendeka kama mtu binafsi na kumdhalilisha vya kutosha.

Kwa jinsi ninavyofahamu mimi, ushahidi ukishatolewa bungeni, kama alivyofanya Dr Kafulila na Dr Ole Sendeka, ni jukumu la tume ya maadili ya bunge kuuchunguza na kuona kama unakidhi haja na kisha kuwapelekea TAKUKURU na mahakama waufanyie kazi.

Sasa inakuwaje Madam Spika akamruhusu Prof Muhongo apoteze muda wa umma kwa kumshambulia Ole Sendeka kama mtu binafsi huku akikwepa tuhuma za ufisadi zinazomwandama yeye na Maswi? Hili suala sio sawawa hata kidogo.

Aidha, inaonekana kwamba Prof Muhongo ni mtu wa ajabu sana kwa jinsi anavyojisifu kwa usomi wake bila kuzingatia kwamba sisi watanzania tumemtuma akatuwashie umeme sio kututangazia usomi wake! Mh Mbowe aliomba muda uongezwe ili kila mbunge apate nafasi ya kuhoji namna mambo yanavyokwenda ovyo kwenye wizara hii lakini Prof Muhongo akambeza na kumdharau.

Majisifu ya kila siku ya profesa Muhongo na kuringia usomi wake sio tija kwa watanzania. Watanzania tunataka umeme na tunataka mafisadi wanaokula fedha za umma washughulikiwe.

Sisi hatuna haja na usomi wa Muhongo. Hata kama Wizara hii ikiongozwa na mtu aisiyekwenda shule kama vile Kapteni Komba au Prof Majimarefu, sisi hatuna shida na hilo. Shida na taabu yetu ni kuona kila mtanzania anapata huduma ya umeme wa uhakika.

Profesa Muhongo anatakiwa ajiandikishe kwenye chuo siasa cha CCM Kivukoni, akajifunze taaluma ya siasa na namna ya kuheshimu watu na mawazo yao, tofauti na jinsi anavyotenda mambo kwa sasa. Kutaja matokeo ya mtihani ya Ole Sendeka bungeni haikuwa hoja ya msingi. Hoja ya msingi ilikuwa ajibu tuhuma zinazomkabili yeye na msaidizi wake wa karibu (Maswi). Vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na watu wa chama na serikali haviwafurahishi wananchi hata kidogo. Wananchi wanataka mawaziri wachapakazi watakaowaletea maendeleao endelevu. Hawataki mawaziri domo kaya wanaoringia usomi wao wakati wanashindwa kutumia usomi huo kuwaletea wananchi maendeleo. Kutamba kwamba amewahi kuwa Rais wa wanajioljia Afrika hakutuongezei shibe na wala hakutupunguzii njaa. Muhongo anapaswa kupima kila neno linalotoka kinywani mwake na kutathimini madhara yake kabla ya kuropoka.

Kutaja hadharani matokeo ya mtihani ya mtu anayetetea wananchi, ni utovu wa maadili ya uongozi na nidhamu kwa kiongozi mkubwa kama Muhongo ambaye anategemewa kuwaletea watanzania maendeleo. Matokeo ya mtihani ya mtu ni SIRI, hayatakiwi kutajwa hadharani—hii ni NYARA ya serikali. Muhongo na hao watumishi kengeufu wa Baraza la Mitihani (NECTA) waliomchapia matokeo ya Ole Sendeka yafaa wachukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka miiko ya utumishi wa umma.
 
Thobias Odhiambo,
Dar es Salaam,
Simu: 0719 786 226

0 comments:

Post a Comment