Maji Yawatesa Akinamama na Wanafunzi Kishapu
Na Thehabari.com, Kishapu
WASWAHILI wanasema 'maji ni uhai' na maisha bila maji ni kadhia. Kimsingi mwanadamu anahitaji maji safi na salama katika kuendesha maisha yake ya kila siku. Na kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama eneo fulani huchangia kiwango fulani cha ugumu wa maisha kwenye familia.
Hali hii ndiyo inayowakumba wakazi wa baadhi ya vijiji vya Kata ya Kishapu, Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga. Tabu ya maji katika vijiji kama Lubaga, Isoso, Mwanuru pamoja na Kishapu yenyewe ni msamiati wa kawaida. Vijiji hivi hupata hauweni katika msimu wa masika pekee ambapo maji hutiririka hata kwenye mito ya msimu (masika).
Lakini mbali na familia kutaabika kusaka maji umbali mrefu kwa ajili ya matumizi ya kila siku, lipo kundi ambalo huathirika zaidi na kero za maji kwa kuwa kundi hilo ndilo linalotegemewa kutafuta maji katika familia kwa matumizi anua. Kundi hilo ni wanawake na watoto wakiwemo wanafunzi.
Makundi haya ndiyo yenye majukumu ya kutafuta maji kwa matumizi ya nyumbani (kwenye familia) wakati wote kulingana na mfumo wa kifamilia na tamaduni za wakazi wa maeneo haya. Kadri ya msimu wa ukame katika vijiji hivyo unavyozidi kushamiri ndivyo umbali wa kuyafuata maji kwa matumizi uendelea kuongezeka.
Kwa hali hii akina mama na wanafunzi hutembea kati ya kilimita tano hadi 10 kufuatilia maji kwa matumizi ya familia, kulingana na umbali wa kijiji chao kwenda kwenye chanzo kikuu (ambacho hata hivyo si cha uhakika) cha maji yaani Mto Tungu. Chanzo hiki cha maji nacho hukauka kipindi cha kiangazi na hali kuwa ngumu zaidi.
Enock Manyenye Shimba ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lubaga, anasema huduma ya maji wanayotegemea licha ya kupatikana umbali mrefu haitosherezi kwa matumizi. Anasema Kijiji hicho hutegemea maji ya Mto Tungu ambao upo umbali wa kati ya kilimeta tano hadi kumi. "Kijiji chetu ni Kikubwa wapo baadhi ya wanakijiji hulazimika kutembea hadi kilimeta 10 kutafuta huduma hii...licha ya kuwa haitoshelezi kwa matumizi," anasema Shimba.
Anaongeza kuwa kadri ya msimu wa kiangazi unapochanganya maji katika Mto Tungu nayo huadimika hivyo wananchi kutegemea kuchimba visima vya muda ndani ya mto huo ili kupata masalia ya maji ardhini chini ya mto huo. "Hali hii huwa sio kazi nyepesi maana wananchi huchimba na kufukia visima hivi kila maji yanapoisha kwenye eneo la kisima...kwa sababu visima hivi huwa vifupi unakuta kikichimbwa kisima kinaweza kutumia muda mfupi na maji kukauka eneo hilo kisha tunachimba eneo lingine," anasema Shimba.
Shimba anasema kundi la wanawake na wanafunzi ndio watafutaji maji wakubwa katika familia nyingi za Kijiji cha Lubaga na maeneo ya jirani na kijiji hicho. Anaendelea kusema kuwa hata visima ambavyo hutumika hutoa maji kidogo kidogo jambo ambalo husababisha uwepo wa foleni kwa wanavijiji maeneo ya visimani.
Kiongozi huyo wa kijiji cha Lubaga anasema mwaka 2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kijiji chao kilipewa ahadi ya kuchimbiwa visima virefu vya maji na Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Seleiman Nchambi ahadi ambayo anasema hadi leo wanaifuatilia lakini bado haijatekelezwa. "Ahadi hii nimeikuta hata katika nyaraka za ofisi ya kijiji lakini bado haijatekelezwa," anasema Shimba akizungumza na mwandishi wa makala haya kijijini hapo.
Hata hivyo kwa akinamama ambao umri umeenda zaidi kilio cha maji huwa maradufu. Ester Bundera (60) ni mkazi wa Kijiji cha Isoso, anasema katika kijiji hicho shida ya maji ni kubwa hasa miezi ya kiangazi. Anasema wao hulazimika kuyafuata maji hadi mji mdogo wa Mhunze ulipo Mto Tungu umbali ambao ni takribani kilometa 10 kwenda tu.
"Hapa kijijini kwetu upo mto mdogo unaojulikana kama Nkonze ambao hutoa maji msimu wa masika tu tena kwa shida...maji haya huyapata kwa kuchimba visima vidogo vidogo mtoni kutokana na kutoka kidogo kidogo huwa ni ya kugombea, lakini kuanzia mwezi wa saba mto huu visima vyake hukauka hivyo kulazimika kwenda Mto Tungu," anasema.
Bi. Anastazia Christopher ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Karume kilichopo Kijijini Isoso, akielezea shida ya maji ambayo wanakijiji hicho huyapata katika Mto Nkonze anasema familia zisizo weza kuvumilia foleni na vurugu za kuchota maji yanayotoka taratibu visimani hulazimika kwenda mtoni usiku muda ambao wakazi wengi huwa wamepungua jambo ambalo ni hatari kiusalama.
"Wanawake ndio wachotaji wa maji wakubwa pamoja na watoto wao hulazimika kwenda vizimani majira ya saa mbili na saa tatu usiku muda ambao panakuwa pametulia na kuanza kuchota maji...unajua huku kwetu wanyama kama fisi ndio ambao hututishia hivyo unaweza kuomba vijana wakusindikize kisimaji majira kama hayo," anasema Bi. Christopher.
Aidha anasema matumaini ya kupata huduma ya maji safi na salama kijijini hapo sasa yanazidi kuyeyuka, kwani ulikuwepo mradi unaodaiwa kufadhiliwa na UNDP ambao ulisambaza mabomba hadi kijijini hapo, lakini umekwama kwa zaidi ya miaka 10 tangu uanze bila kufanya kazi. Kwa sasa mabomba yaliokuwa yametandazwa yanang'olewa na Serikali na kupelekwa maeneo mengine kitendo ambacho anasema kinazidi kuwakatisha tamaa. Anasema kijiji hicho pia ni miongoni mwa vijiji vilivyoahidiwa kuletewa maji na Mbunge Nchambi ahadi ambayo bado ijatekelezwa.
Hata hivyo kilio cha maji hutofautiana kutoka kijiji kimoja hadi kingine kutokana na umbali wa kijiji husika na chanzo cha maji wanachokitegemea. Kwa msingi huo hali ya huduma ya maji ni mbaya zaidi katika Kijiji cha Kishapu, ambacho wananchi hutegemea maji ya mabwawa ya mvua ambayo si safi na salama kwa matumizi ya binadamu. Kipindi cha kiangazi ukame unapokausha mabwawa wanakijiji hulazimika kusafiri hadi eneo la Mto Tungu kupata huduma ya maji. Umbali kutoka katika kijiji hicho hadi mtoni Tungu ni takribani ya zaidi ya kilometa 30 jambo ambalo ni kero zaidi kwa wanakijiji. Na wanaoshindwa kufuata maji ya bure katika mto Tungu hulazimika kununua kwa wachuuzi wa maji ambao huyafuata machimboni Mwadui.
Bi. Khadija Said ni mmoja wa wakazi wa Kishapu, anasema kero ya huduma ya maji eneo lao ni zaidi. Wananchi wakati mwingine hulazimika kutumia maji ya madibwi ambayo si safi na salama kutokana na hali ngumu. Vilio vya maji katika vijiji mbalimbali vya Kata ya Kishapu havipo kwa wazazi tu. Wanafunzi nao baada ya kurudi shuleni jioni hulazimika kuanza shughuli ya kusaka maji kwa ajili ya matumizi.
Unapopita maeneo ya Mto Tungu nyakati za jioni utakutana na baadhi ya wanafunzi ambao ama wanakuwa wanachota maji au kufua sare zao za shule eneo la mto huo. Kundi hili hujulikana kirahisi kwa kuwa huwa wamevaa nusu sare za shule, yaani kwa wanafunzi wa kiume baadhi huwa wamevaa suruali za shule na shati la nyumbani, huku wa kike wakiwa na sketi za shuleni na juu vazi la nyumbani.
Biashara ya maji kwa baadhi ya vijiji ni kubwa na inafanywa na wanaume kwa kutumia matoroli. Wachuuzi hawa wa maji hutumia toroli lenye uwezo wa kubeba madumu manne ambayo kila dumu linauwezo wa kuchukua lita 20. Wachuuzi hawa huuza maji yao kwa madumu manne kwa pamoja, yaani shilingi 1,000 kwa madumu manne. Lakini licha ya kundi hili kuwa mahiri kwa uchotaji maji ya biashara si wanaotoa msaada wa maji katika familia zao. Jukumu hilo lipo kwa watoto na akina mama kwa matumizi ya nyumbani.
Wanyama wanaofungwa na binadamu kama ng'ombe, mbuzi na kondoo nao ukubwa na ukame huu. Wanyama hawa hulazimika kunywa maji kwenye chanzo kimoja na binadamu (Mto Tungu) kutokana na shida ya maji. Kutokana na usimamizi mbovu wa vyanzo vya maji Mto Tungu pia hutumika vibaya kwa kile baadhi ya wananchi kuingia ndani ya mto na kufanya usafi kama kufua nguo ndani ya mto.
Maxmilian Lugembe ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kishapu. Katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anakiri uwepo wa shida ya maji kwa kata nzima ya Kishapu na maeneo mengine yanayoizunguka kata hiyo. Hata hivyo anasema hali hiyo inasababishwa na jiografia ya eneo hilo. Anasema maeneo mengi ya vijiji vya kata hiyo ni vigumu hata hupatikanaji maji ya uchimbaji visima virefu kwa matumizi ya kawaida.
"Yapo maeneo ambayo tumejaribu kuchimba visima virefu lakini hupati maji...ukiangalia visima vinavyochimbwa ni vile vinavyochimbwa kwenye mto baada ya maji yanayotiririka kukauka mtoni, hapo ndio wananchi wanapata maji. Yapo maeneo mengine tumejaribu lakini hupati maji kabisa, eneo hili ni tatizo," anasema Ofisa huyo wa Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, George Kessy anaungana na kauli ya mtendaji wake. "Ni kweli suala la maji ni Tatizo kwa wilaya nzima ya Kishapu, tena ni kubwa sana...hivyo wapo sahihi wananchi wanapolalamikia suala hilo. Hakuna chanzo cha maji cha uhakika eneo hili," anasema Kessy katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya.
Hata hivyo anasema juhudi zinafanywa kuhakikisha wanapata maji ya uhakika eneo hilo. "Lengo la halmashauri ni kuhakikisha eneo letu linapata maji kutoka kwenye chanzo cha maji cha uhakika...na mchakato umesha anza, kuna mpango wa kuleta maji kutoka Ziwa Victoria na hili lipo kwenye mchakato," anasema mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mbunge Nchambi akizungumzia ahadi za maji alizotoa wakati wa kampeni na utekelezaji wake anasema hali ni nzuri kiutekelezaji ukilinganisha na hali ilivyokuwa ahapo awali. "Niliahidi maji jimbo zima la Kishapu yaani jumla ya vijiji 114, wakati naingia madarakani nimekuta hali ni mbaya ya huduma za maji...lakini hadi sasa tunapozungumza zaidi ya vijiji 30 vinapata maji safi na salama huku jitihada zingine zinaendelea," anasema Nchambi.
Anabainisha kuwa ameingia madarakani na kukuta Jimbo zima la Kishapu likipata maji kwa chini ya asilimia nne, lakini kwa sasa vijiji vingi vimeongezeka. Utekelezaji wa ahadi zake juu ya huduma za maji unaenda awamu kwa awamu hivyo kila kijiji kitapata maji safi na salama. "Ahadi yangu mimi ni miaka mitano, ilani ya CCM (Chama Cha Mapinduzi) ni ya miaka mitano, ninaenda kwa awamu yaani vijijini 10 kwa kila mwaka kwa wilaya," alisema mbunge huyo.
Anasema upo mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ambao bomba lake linatokea Mkoa wa Shinyanga, mradi ambao utavinufaisha kihuduma za maji vijiji vingine vingi kutoka Jimbo la Kishapu. Anawashauri wananchi kuwa wavumilivu kwani juhudi zinaendelea kufanywa kuhakikisha maji yanasambazwa katika vijiji vyote vihitaji.
Akitoa ufafanuzi juu ya zoezi la ufukuaji mabomba yaliosambazwa kwa baadhi ya vijiji anasema, kwanza mabomba hayo si salama kutokana na kukaa muda mrefu ardhini bila kutumika. maji yanayotoka eneo la Kishapu yalifungwa mabomba mapya, mabomba yanayofukuliwa kwa sasa yamekaa muda mrefu ardhini bila kutumika hivyo si salama. Anasema utakapofika mradi wa Ziwa Victoria yatafungwa mabomba mapya na kusambaza maji vijiji husika.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
Joachim Mushi, Mhariri Mkuu wa gazeti tando la Thehabari.com
Mail address:- mushi@thehabari.com/ jomushi79@yahoo.com/ info@thehabari.com
Mobile:- 0717 030066/ 0786 030066/ 0756 469470
Web:- www.thehabari.com
http://joemushi.blogspot.com
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 comments:
Post a Comment