Monday, 1 April 2013

[wanabidii] Nilivyopotea Kwenye Pori La Jongomero!



Ndugu zangu,

Kunako saa tano asubuhi ( Jumatatu ya Pasaka) nilifika na makamanda wangu kwenye lango kuu  la kuingilia Ruaha National Park.  Hii ni hifadhi ya pili kwa ukubwa hapa Tanzania. Na inasemwa, kuwa ukubwa wake ni sawa na nchi ya Ubelgiji.

Pale getini Ruaha Park kuna ' mwanakijiji' wangu ( Mtembeleaji wa Mjengwablog) aliyenilaki kama kawaida yake na kuniulizia habari za  Bi Mkora. Huyu ni mfanyakazi wa Ruaha National Park.

Kisha kijana huyu akanielekeza nifuate route 6. Akaaniambia,   kwamba  mbele kidogo kwenye njia hiyo nitawakuta ' sharubu' chini ya mbuyu. Sharubu ni jina la porini la mnyama simba.

Basi, mimi niliyedhani nalijua vema pori la Ruaha, maana, huwa sihitaji hata guide,  nikakamata ramani yangu ( Pichani). Nikashika usukani na kuongoza kuelekea route 6.

Nikautafuta mbuyu sikuuona, mara nikaona tairi za gari zikielekea kwenye njia ambayo haikuwa na alama. Nikazifuata tairi zile . Hapo ukawa ni mwanzo wa kupotea.

Baada ya kilomita 20 porini nikaelewa kuwa nimeshapototea. Maana, huko porini nikazikuta njia nyingine na ile niliyojia ikawa haipo tena kichwani. Na tairi za gari nilizokuwa nikizifuata nazo zikapotea.

Kamanda wangu Olle akachukua simu na kuangalia GPS na google map kujua tuko wapi. Akaniambia tuongoze kuelekea kulia kuitafuta Msembe. Na baada ya robo saa porini nikamwambia aangalie tena. Alipowasha simu tu na betri ya simu ikawa imekwisha.

Kilichobaki ikawa kutumia uzoefu tu. Na huko porini tukakutana na makundi makubwa ya tembo ambayo sijawahi kuyaona maishani mwangu. Niliwaona ngiri wengi pia. Mvuanyingi  ikaanza kunyesha ghafla na njia ikazidi kuwa mbaya.

Hatimaye nikaikuta njia rasmi ya mbugani na mbele nikakiona kibao kinachoelekeza kuwa zimebaki kilomita 30 tu kufika Jongomero. Ni umbali wa kilomita 80 kutoka Msembe, Makao Makuu ya Park ya Ruaha na lilipo geti la kutokea!

Nikainza safari ya kukatisha pori kurudi Msembe. Na akiba ya mafuta ilibaki robo tenki tu. Ilikuwa na maana moja tu, kuwa kama ningepotea tena porini, basi, tulikuwa ni watu wa kulala porini, maana , hata network ilikuwa haipatikani.

Hatimaye tukafika Msembe HQ na getini pia. Yule mwanakijiji wangu pale getini akaniuliza;

 " Mwenyekiti, umewaona sharubu?!"
Jibu;
 " Ndio, nimewaona ngiri wengi wenye masharubu!"

Naam, pamoja na yote hayo, kuna mengi niliyojifunza nikiwa porini, na namshukuru sana kijana yule  ' mwanakijiji' wangu kwa kunipoteza porini.

Usiku Mwema.
Maggid,
Iringa.
http://mjengwablog.co.tz



--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment