Katuni ya Kibanda ilivyomaliza Taaluma ya habari
Na TANpress
MEI 3 YA KILA MWAKA ni siku ya uhuru wa habari,hivyo wadau wa habari hukutana mahali fulani kutathimini mwenendo wa uhuru wa kutoa maoni katika nchi husika.
hivyo kwa kuwa ni wiki ijayo nimeona nitoe maoni yangu mapema kabisa ili kutoa nafasi ya mjadala.
MARA nyingi huwa navutiwa na michoro ya katuni kwenye magazeti, ingawa mimi sina kipaji cha kuchora lakini huwa nasema pengine ningewa kipaji hicho ingekuwaje?
Huwa najisifu kuwa pengine ningekuwa mchora katuni ningeifanya kazi hiyo kwa ubora na umakini mkubwa zaidi kuliko hii ya kuandika.
Katuni ni kitu nachokipenda kwa kweli jinsi ambavyo kinawasilisha ujumbe mzito kwa njia ya michoro, ndio maana hata nikichukua gazeti liwe la kiingereza au Kiswahili huwa nakimbilia kwanza kwenye kibonzo baada ya hapo ndipo nitasoma habari zinazonivutia.
Kutokana na mapenzi makubwa niliyonayo kwenye katuni au vibonzo ndipo yakanijia mawazo wakati nikifikilia juu ya kutekwa na kuteswa kwa mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Absalom Kibanda, siku ya Machi 5 Mwaka 2013.
Nilifikiria mateso aliyoyapata mhariri huyo, nikasikitika jinsi ambavyo taaluma ya habari imetendewa ukatili mkubwa.
Nikakumbuka kuwa aliyefanyiwa hivyo, ni mwandishi wa habari,mhariri, mwenyekiti wa jukwaa la wahariri, hivyo kibanda alikuwa taswira ya habari hapa nchini.
Nikafikiria kuwa jinsi ambavyo ningechora katuni kuhusiana na tukio hilo,mchoro wangu ungesimamaje kuwakilisha taswira ya tukio hilo.
Nikajiuliza kuwa ikiwa mtu huyu mhimu kwenye taaluma ya habari ameng'olewa meno ya mbele bila ganzi maanake ni kwamba taaluma ya habari nchini imekuwa kibogoyo.
Kwamba sasa waandishi na watangazaji hawataweza kusema na kutangaza wazi wazi habari, wakasikika kwani ni vibogoyo hawana meno tena.
Kwamba mchoro wa katuni yangu ungeelekea kwenye macho, ili mwandishi wa habari aweze kufanya kazi yake kwa makini anatakiwa awe na jicho kali, ndio maana wanaitwa jicho la jamii, sasa wametobolewa.
Kwa hiyo ukiitazama katuni hiyo kwa makini unaona kwamba taaluma ya habari nchini imeingia gizani, wandishi hawataweza kuona kwa ufasaha yale yanayofanywa na jamii au dola.ni vipofu sasa.
Ndio maana wananchi wanashangaa kuona wabunge wanaochafua bunge kwa kumdharau Spika lakini anayelalamikiwa ni Spika badala ya walengwa ambao ni wabunge wanaotaka kumuonyesha mafunzo waliyopata JKT.
Hakuna anayewakemea wazi wazi bila kutaja cheo au kiti cha Spika hii inadhibitisha jinsi ambavyo tumetobolewa macho hakuna anayeona ukweli tena.
Mchoro wa katuni hiyo unaelekea chini ya Mabega na kukutana na mikono ya Mwandishi wa habari, itakumbuka kuwa bila mikono mwandishi hawezi kukaa kwenye kompyuta na kuandika habari kwenye mitandao zinazoitwa za uchochezi.
Mhariri Kibanda licha ya kutobolewa jicho ili awe kipofu pia amekang'olewa na kucha na kukatwa kidole kama njia ya kuwanyanganya wandishi haki ya kuandika chochote.
Ili kuhakikisha wandishi wa habari za mitandao hawaendelei na shughuli zao ikabidi kibanda akatwe kidole ,sawa na mkono hivyo kuwafanya wandishi wa habari washindwe kuandika habari.
Taaluma ya habari sio tu imekatwa mikono bali imenyofolewa kucha na kuachiwa maumivu makali yatakayowafanya wandishi wachanganyikiwe washindwe kuandika habari za uchunguzi.
Mwandishi mwenye maumivu ya kucha kisha amekatwa mkono hawezi kuwa makini kuandika habari zitakazolikomboa taifa badala yake atabaki analilia kidole chake.
Ukifuatilia mchoro wa katuni bila kujali nani amehusika na uovu huo unagundua kuwa taaluma hiyo kwa miaka ya hivi karibuni imefanyiwa ukatili mkubwa unaweza kupelekea uhuru wa maoni ukapungua kama sio kutoweka kabisa.
Kosa kubwa la kuuwa uhuru wa habari lilianzia pale mwandishi wa kituo cha Chaniel 10 alipouwawa mchana kweupe na hatua stahiki hazikuweza kuchuliwa.
Chanzo cha mwanahabari huyo Daudi Mwangosi kuuwawa septemba Mwaka 2012kilitokana na kukamatwa kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe mkoa wa Iringa Godfrey Mushi.
Hivyo mwanahabari huyo akataka kuhoji polisi sababu ya kukamatwa kwa mwanahabari huyo ndipo askari hao walipoanza kumshambulia kwa kichapo na baadae mlio kama wa bomu ulisikika eneo hilo na mwandishi huyo na askari mmoja waliaguka chini ikawa ndio mwisho wake.
Licha ya wandishi kujitokeza kuandamana kwa kulaani dola lakini laana zao hazikuwa na nguvu wala hazikuathiri serikali kwasababu wandishi waliendelea kushirikiana nayo kama kawaida, hata pale Rais wa Nchi alipogoma kutoa rambi rambi ya kifo hicho.
Ni katika kipindi hicho ndio maadui wa uhuru wa habari walidhani wameshinda na taaluma ya habari imekufa kutokana na jamii kushindwa kujitokeza hadharani kupambana na uovu huo kama ilivyotokea Tunisia mara baada ya mmachinga kujilipua akiipinga dola.
Tangu afariki mwandishi huyo na hatua madhubuti zikashindwa kuchukuliwa ndio sababu ya kuzaa haya ya Kibanda na sasa uhuru wa habari unaelekea kuto weka kwa mbali wandishi wanakuwa vibogoyo na vipofu.
Kama jamii ya watanzania ingeungana kipindi kile na kujitokeza kwa pamoja kulaani tukio lile kwa kuitia dola misuko suko ya hatari ambayo ingelazimisha wakuu wa usalama kukutana kwa dharura kujadili hali hiyo kisha kuja na majibu kuwa jambo baya kama hilo halitawakuta tena wanahabari wala kwenye jamii.
Kwa kuwa hakuna misuko suko iliyotokea na kwa kuwa laana za wandishi hazikuwashika ,walengwa ndio maana leo anapotokea kiongozi mhimu kwenye taaluma ya habari anaumizwa vibaya wenyengine wanatumia bunge kudhihaki kwamba Kibanda ni nani hata atekwe.
Dhihaka za namna hiyo hutolewa na watu walioshiba amani lakini nchi ambazo zimeonja machafuko yaliyoletwa na dharau kama hizo, tayari kiongozi huyo alipaswa kufukuzwa kazi kama sio kujiuzulu kwani anaweza kuletea dola balaaa.
Kinachoshangaza zaidi ni kuona miezi miwili inamalizika tangu mwenyekiti wa jukwaa la wahariri ,(TEF)atekwe na kuumizwa lakini hakuna aliyekamatwa, wakati aliyekuwa RPC wa mkoa wa Mwanza aliuwawa usiku wa manane lakini wauwaji walikamatwa mapema.
Hali hiyo ndio inaifanya jamii kukosa uaminifu na vyombo vya usalama ikiaminika kwamba pengine nchi hii hutoa haki ya kulinda raia wake kwa upendeleo, hivyo wapo raia wa daraja la kwanza ambao wakiumizwa tu serikali inafanya haraka kuwatafuta wahusika.
Hali hii ikiachwa iendelee tunaweza tukazika uhuru wa habari tukidhani tunajipa ahueni ,kumbe baada ya muda sisi tunaoshikilia dola tutakuwa nje ya ulingo na wengine watakuwa ndani ya dola ,kwakuwa tulisha haribu mfumo huo ,tutakosa sehemu ya kutolea maoni.
Kuna watu tunawafahamu zamani walikuwa kwenye mfumo wa dola na walikuwa sehemu ya kukandamiza uhuru wa habari lakini leo hii wapo nje ya mfumo huo wanajaribu kutumia vyombo vya habari kama sauti ya kudai haki zao.
Hatuwezi kushiriki kukandamiza uhuru wa habari, tukadhani kuwa kuna kitu tutafaidika nacho katika siku za baadaye , kwani muda utakapohitajika kwa kuvitumia vyombo hivyo ,vitakuwa vimepoteza meno na macho ya kuona.
ni malize kwa kusema kuwa ni kweli dola imeshindwa kuwakamata waliomjeruhi Mhariri Kibanda ili tuombe msaada katika shirika la upelelezi la marekani FBI, litusaidie kama lilivyofanikisha kumkamata kijana aliyelipua bomu mitaa ya Bostoni?
ni malize kwa kusema kuwa ni kweli dola imeshindwa kuwakamata waliomjeruhi Mhariri Kibanda ili tuombe msaada katika shirika la upelelezi la marekani FBI, litusaidie kama lilivyofanikisha kumkamata kijana aliyelipua bomu mitaa ya Bostoni?
Kama jibu ni ndio tuvunje kwanza ofisi ya mkurugenzi wa upepelelezi wa makosaji ya jinai ndipo tuombe msaada nje, ile ofisi haitusaidii kitu zaidi la kula kodi zetu.
SIR MOBNI SARYA
TANZANIA NEWS FORUMS
DIRECTOR
www.mobinday.blogspot.com 0753399579
0 comments:
Post a Comment