Sunday 8 December 2013

[wanabidii] HOSPITALI ZA UMMA=KIFO!!

USHUHUDA WA KUTISHA KUTOKA HOSPITALINI YA SERIKALI!!!!!
 
Siku za hivi karibuni niliwahi kumuuguza rafiki yangu wakati akitibiwa katika hospitali ya serikali. Nilichoshuhudia huko kinasikitisha na kustaajabisha sana. Kimenipelekea niamini kwamba hospitali za umma ni makaburi ya kuzikia roho za watanzania wasiokuwa na hatia.
 
Huyu jamaa yangu alikuwa hospitalized kwa ajili ya tatizo la kutapika na kuharisha damu. Alifikishwa hospitalini hapo takribani saa 2:00 za asubuhi lakini kutokana na ugoigoi na kutokujali kwa madaktari, alikuja kuchukuliwa vipimo mnamo saa 11:00 jioni. Wakati vipimo vinasubiriwa daktari alianza kumtibu kwa kuhisi. Kwanza alibashiri kwamba huenda mgonjwa anaumwa homa ya matumbo (typhoid), hivyo alimtundikia drip yenye dawa ya taifoidi. Kuanzishwa kwa matibabu haya hakumpa mgonjwa afueni yoyote, badala yake maumivu yalizidi huku akiendelea kujisaidia mabonge ya damu iliyoganda.
 
Daktari alipoona hali inazidi kuwa mbaya, ikabidi ambadilishie dawa. Safari hii alibashiri ugonjwa tofauti kabisa—vidonda vya tumbo. Akamuandikia dawa zingine tena—zile za taifoidi tukaachana nazo licha ya kwamba tulishatumia pesa nyingi kuzinunua. Hata baada ya kumbadilishia dawa, hali ya mgonjwa haikuonyesha matumaini yoyote. Kadri muda ulivyosegea ndipo hali ilipozidi kuwa mbaya zaidi. Mimi na jamaa yangu tuliyekuwa naye pale hospitali tulishikwa na butwaa. Tulifikia hatua ya kutaka kumchukua mgonjwa wetu tumpeleke hospitali yoyote ya binafsi akatibiwe. Lakini kwa kuwa mgonjwa alikuwa mikononi mwa madaktari tulizidi kupiga moyo konde. Wakati huo ngozi ya mgonjwa ilishaanza kubadilika na kuwa ya manjano.
 
Kwa bahati nzuri alikuja daktari mmoja kumpokea yule wa asubuhi. Wakati anagawa dawa kwa wagonjwa alimfikia mgonjwa wangu. Akautazama mwili wa mgonjwa na kugundua kwamba rangi imeanza kubadilika kutoka ya manjano kuwa ya kijivu. Alimchunguza kwa kumbonyeza kwenye kucha na kumchungulia chini ya macho yake. Alitanabahi kwamba mgonjwa ana upungufu mkubwa wa damu. Alimuagiza nurse achukue damu ya mgonjwa na kuipeleka maabara kupima kundi la damu. Ili kuepuka ucheleweshwaji kwenye maabara, mgonjwa alibainisha kundi lake la damu. Kumbe aliwahi kupima siku za nyuma, hivyo kundi la damu yake alikuwa analifahamu. Baada ya masaa kadhaa mgonjwa alitundikiwa chupa (unit) moja ya damu na ilipoisha akaanza kupata nafuu. Na yale maumivu ya kichwa na viungo aliyokuwa akiyapata yakawa yamepungua kwa kiasi kikubwa. Rangi ya ngozi yake ikaanza kurejea kawaida. Daktari alishauri atundikiwe drip ya maji huku akisubiri kuongezewa unit nyingine ya damu.
 
Baadaye nilienda kwenye benki ya damu kuomba mgonjwa awekewe unit nyingine ya damu kama daktari alipokuwa ameshauri, nikaishia kupigwa danadana mpaka siku iliyofuata. Kesho yake nilifanikiwa kulazimisha mgonjwa awekewe damu nyingine—akafanikiwa kuwekewa chupa ya pili. Baada ya nusu ya damu kuingia, mgonjwa alianza kuhisi kuchefuchefu na maumivu makali ya kichwa. Hali ikazidi kuwa mbaya kadri muda unavyoenda. Nikamuita daktari na kumueleza kuhusu hali ile. Daktari akachukua uamuzi wa kuondoa ile chupa ya damu iliyokuwa imetumika nusu. Ndipo mgonjwa akapata afueni na kurejea katika hali ya kawaida. Nikaingiwa na wasiwasi kwamba huenda ile damu aliyokuwa ametundikiwa itakuwa na hitilafu ya kiufundi lakini daktari aliniondoa hofu kwamba hiyo ni hali ya kawaida kutokea—eti damu ili-react! Haya, bwana.
 
Katika siku hizi zote bado majibu ya kimaabara yalikuwa bado hayajatoka na zilikuwa zimepita siku nne (4) tangu mgonjwa huyu alazwe hosiptalini pale. Mgonjwa alikuwa akitibiwa kwa kudhania na kuhisi. Mara ahisiwe kuwa na taifoidi, mara vidonda vya tumbo, nk—ilimradi hakuna anayejali! Lakini jambo la kusikitisha na kustaajabisha ni kwamba katika siku zote hizi mgonjwa alikuwa akitibiwa kwa dawa za kununua kwani tuliambiwa kwamba hospitali haina hata kidonge kimoja cha dawa. Hakika hakukuwa hata na kidonge kimoja cha bure kwenye stock ya hospitali. Dawa zote zilizokuwa zinaandikwa na madaktari zilikuwa zinanunuliwa kwenye duka la dawa lilipo kwenye lango la kuingilia hospitalini humo. Ikiwa dawa iliyoandikwa itakosekana kwenye duka hilo, kama ilivyokuwa inatokea mara kwa mara, ilinibidi niende nikainunue kwenye maduka ya dawa ya mjini. Yaani Hospitali ya rufaa eti inakosa hata bomba moja la sindano, kidonge kimoja cha panadol, piliton, diclofenac, nk!
 
Baada ya kukaa hospitalini kwa muda wa siku tano (5), Mungu alitenda muujiza mgonjwa wangu akapata nafuu na kuruhusiwa kuondoka. Hakuwahi tena kuongezwa damu nyingine baada ya ile chupa ya pili kudunda. Mgonjwa aliruhusiwa bado tukiwa na madawa lukuki aliyoandikiwa na ambayo alipaswa kunywa ili kusaidia kubaini ugonjwa wake. Kuna dawa moja inaitwa barium meal (barium sulphate) ambayo alitakiwa anywe ili kusaidia kubaini kama alikuwa anasumbuliwa na vidonda vya tummbo au la. Lakini mpaka anaruhusiwa, hakuwa amejua ni nini hasa kilichokuwa kimemsibu hadi kuvuja damu ndani ya mwili (internal bleeding), hali iliyopelekea kujisaidia na kutapika mabonge ya damu. Ila tunamshukuru Mungu tu kwamba aliongezewa damu iliyosaidia kutetea uhai wake, vinginevyo hata tungeweza kumpoteza kutokana na upungufu mkubwa wa damu uliokuwa unamkabili. Tulikata shauri ya kutorudi tena hospitali ya umma kwani kupona kwa wagonjwa katika hospitali hizi ni kwa kudra za Mungu—kwa kuwa kule hakuna dawa wala vifaa tiba hata kidogo.
 
Cha kushangaza na kukera zaidi, wagonjwa walikuwa wanaambiwa kwamba dawa za bure/kuchangia hakuna; lakini mtu akitaka za kununua zipo tele kwenye famasi ya hospitali. Inawezekanaje tuambiwe hakuna dawa lakini dawa za kununua zipo tele, tena kwenye famasi ya hospitali? Kama sio ufisadi ni nini? Labda huu ndio utaratibu wa serikali—kwamba dawa zote zinunuliwe lakini ushauri utolewe bure. Ama ni mpango mahususi wa kuwaua raia wasiokuwa na hatia? Haya maswali yanapaswa kujibiwa na serikali kwani ndiyo inayokusanya kodi kutoka kwa raia na kuahidi kutumia kodi hizo kwa manufaa ya umma. Ndiyo inayopaswa kujibu kodi zetu zilipo na kama huko ziliko zinamnufaisha nani zaidi ya wananchi. Wagonjwa wanachokifuata kwenye hospitali za umma ni kuandikiwa dawa za kununua na kupata ushauri wa bure. Kama hali ni hii, kuna umuhimu gani wa hospitali za umma basi? Si zifungwe zote ili wananchi wakatibiwe kwenye hispitali binafsi na wale wasiokuwa na uwezo wafie nyumbani!
 
Hii ni moja ya hospitali za rufaa, ambayo tungetarajia itoe huduma nzuri na za kuridhisha lakini huduma zake ni tofauti na hadhi yake. Kwa mujibu wa utafiti wangu hospitali hii ina majengo na vyumba vya kutosha kwa ajili ya kutolea huduma za kitabibu na utawala. Ingekuwa majengo ndiyo tiba, basi hakuna mgonjwa hata mmoja ambaye angekufa kwa kukosa huduma za kiafya. Kama hali kwenye hospitali ya rufaa ndiyo hii, je huko kwenye hospitali za chini—mkoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati—hali ikoje?
 
Nilishuhudia sio chini ya wagonjwa watano wakifariki kila siku kutoka kwenye kila wodi katika wodi zisizopungua 12! Hii maana yake ni kwamba kila siku hospitali hii huua wagonjwa wasiopungua 60 kwa siku au 1,800 kwa mwezi. Kwa mwaka mzima idadi hii inafikia wagonjwa 21,600. Hii ni idadi ya watu wanaotosha kukaa kwenye kijiji kimoja. Kwa lugha nyingine ni kwamba hii hospitali huteketeza kijiji kizima cha watu kila mwaka. Na vifo hivi vinahusisha hospitali moja tu ya umma. Tukijumlisha idadi ya watu wote wanaouliwa katika hospitali zote za umma, hesabu yake inatisha! Mauaji haya ni makubwa na mabaya kuliko yale yaliyofanywa na M23 au yanayoendelea kufanywa na vikundi mbalimbali vya kigaidi kama vile alqaeda, alshaabab, bokoharamu, nk. Hapa ndipo mtu unapogundua kwamba kwa mwaka mzima serikali hii inaua watu wengi zaidi ya wale wanaouliwa kwenye vita vya kigaidi.
 
Matukio niyoshuhudia mle wodini yanatisha sana kuyasimulia. Kuna babu mmoja aliletwa mle wodini majira ya jioni. Alikuwa anaharisha na kuhisi maumivu makali ya tumbo. Tofauti na umri wake, maumivu yale makali yalimsababisha alie kama mtoto mdogo. Wakati akiendelea kulalamika na kulia, daktari alikuwa anamsikia na kumpita kama vile hamuoni. Hali ilipokuwa mbaya zaidi, kijana alokuwa ameambatana na yule babu akamsihi daktari amsikilize babu yake na kumsaidia kwa kadri atakavoweza. Daktari akamsadia kwa shingo upande—akamuandikia dawa za kununua. Alimuandikia akanunue maji ya dripu, vidonge vya maumivu (panadol/piliton/diclofenac?), gloves, mabomba ya sindano, set ya vifaa vya kutundikia maji, nk. Akamuelekeza akanunue vifaa hivyo kwenye famasi ya hispitali au kama atavikosa huko akanunue kwenye duka la dawa lilipo mkabala na lango la kuingilia hospitalini. Kwa bahati mbaya sana, yule kijana hakuwa na fedha za kununulia vile vifaa.
 
Ikabidi wasamalia wema mle wodini wamsaidie baadhi ya vidonge walivyoandikiwa wagonjwa wao kwa makubaliano kwamba angevirejesha siku inayofuata. Babu alimeza hivyo vidonge vya kuazima lakini havikusaidia kitu. Bado alizidi kulalamika na kulia kama mtoto mdogo. Alianza kuharisha maji maji mwanzoni lakini kadri muda ulivyoenda, akaanza kuharisha damu na hatimaye akaishiwa nguvu kabisa. Aliendelea kuteseka hivyo usiku kucha hadi ilipofika saa tano asubuhi ya siku iliyofuata akafariki dunia hata kabla ya kupata tiba yoyote ya maana na bado akiwa hajachukuliwa vipimo.
 
Kwa uzoefu wangu, yule babu alifariki kutokana na taifoidi iliyokomaa/sugu (chronic and severe typhoid) kwani dalili zote zilionyesha kwamba alikuwa akiumwa ugonjwa huo. Kwa mujibu wa mjukuu wake aliyeambatana naye hospitalini, alidai kwamba kabla ya kufikishwa pale alikuwa akitibiwa kwenye zahanati moja ya serikali na kwamba tiba kubwa aliyokuwa akiipata huko ni vidonge vya kutuliza maumivu alivyokuwa akivinunua—kwa kisingizio kile kile cha ukosefu wa dawa kwenye hospitali za umma!
 
Katika wodi ile (Ward No.8) nilishuhudia wagonjwa wengine wasiopungua watano (5) wakifariki, sio kwa sababu ya kuugua magonjwa ya kutisha, ila kwa sababu ya ukosefu wa dawa. Wagonjwa walikuwa wakifariki kutokana na magonjwa ya kawaida kabisa kama vile malaria, typhoid, dysentery, safura, nk. Haya ni magonjwa ya kawaida kabisa yanayoweza kutibiwa kwenye zahanati na vituo vya afya au kwenye hospitali za wilaya na mkoa. Badala yake wagonjwa hukimbilia kwenye hospitali za rufaa wakidhani kwamba kule kuna afadhali kumbe yale nayo ni makaburi tu!
 
Jambo lingine nililoshuhudia pale ni kwamba madaktari wapya (interns) huachiwa wafanye kazi wenyewe bila usimamizi wa dakari bingwa au mzoefu. Matokeo yake daktari mpya akipata kesi inayomshinda, hasa wakati wa usiku, hana wa kumuuliza. Hii hupelekea hawa madaktari wapya kubuni tiba na hatimaye kuua wagonjwa kwa kuwafanyia majaribio ya kitabibu. Jamani mwili wa mtu sio wa kufanyia majaribio hata kidogo. Mwili sio kipande cha mbao kwamba daktari akikosea upasuaji atakata kipande cha nyama au mfupa kutoka sehemu nyingine aje aunganishe kwa gundi kupata kiungo kipya.
 
Ndugu zangu, kwa hali hii mtu asije akazidiwa kwenye zahanati au hospitali ya binafsi, akajifariji kukimbilia hospitali ya mkoa au rufaa ya serikali. Kule utakuwa unakimbilia kwenye kifo. Ni afadhali ubaki huko kwenye zahanati/hospitali ya binafsi ukafie huko kuliko kuwasumbua ndugu zako wakupeleke kwenye hospitali ya umma iliyo mbali uje uwape shida ndugu zako kusafirisha maiti yako umbali mrefu kwenda kuzika nyumbani. Mtu yeyote mwenye ufahamu simshauri aende akatibiwe hospitali ya umma. Labda upelekwe kule ukiwa kwenye ambulance na ukiwa hujitambui. Vinginevyo, usikubali kwenda kufa kirahisi na kwa haraka kwenye hospitali ya serikali. Bora ubaki kwenye hiyo hospitali/zahanati ya umma Mungu anaweza kufanya muujiza ukapona. Ugonjwa ukishinikana kwenye hospitali ya binafsi ni bora ukarudi kwenye tiba mbadala kuliko kujidanganya kwenda hospitali ya rufaa ya umma. Utakufa siku hiyo hiyo!!!

0 comments:

Post a Comment