Wednesday 4 December 2013

Re: [wanabidii] Migiro atendewe haki, aondolewe CCM

Kabla ya kumuondoa Migiro na kumuweka kwenye nafasi nyingine kama anavyopendekeza Mashaka ni lazima mfumo uwe umebadilika.
Mfumo gani? Labda niseme mfumo wa Chama kimoja na tumeukubali mfumo wa vyama vingi vya siasa. Nasema hivyo kwa sababu wanaowaweka akina Migiro katika nafasi za Chama wanafanya hivyo kwa kuangalia kuwa Tanzania inastahili kukijenga chama Tawala. Bila kwanza kutambua kuwa vyama vinasaidia kuijenga nchi na si kinyume chake haiwezekani kwanza watu muhimu kuondolewa kwenye vyama kwa manufaa ya Taifa.
Korea wamelijua hilo. wanajenga nchi kwa manufaa ya nchi.
Mimi nilitarajia Mogiro akishachaguliwa kuwa mbunge angeenda bungeni mara moja. hadi jana alikuwa anatembea na katibu mkuu wa CCM katika kukiimarisha chama. makusudi ya ziara ni kusikiliza matatizo ya wananchi ILI CHAMA KIRUDISHIWE HESHIMA. Wakati chama kinaheshimika na matatizo yakiwepo hakukuwa na haja ya kumtafuta katibu mkuu kama kinana wala hakukuwa na haja ya Katibu mkuu kwenda kuwaona wananchi. Hii ni tofauti na mtizamo wa Korea.
Kwa hiyo mpaka mzungu mmoja aje aendeshe 'semina' KWA VIONGOZI WETU KUWONYESHA HILO. aU MFADHILI MMOJA ATOE MASHARTI hayo kama sehemu ya kutupatia hela za kununulia vyandarua au madawa. Vinginevyo tena ni vizuri akina Migiro wakae huko huko otherwise wanaweza kuwa frastrated. Watoke huko wakosoe jambo ambalo litaonekana ni la Chama halafu waishi? Thubutu!

From: Mashaka Mgeta <mgeta2000@yahoo.com>
To: "mabadilikotanzania@googlegroups.com" <mabadilikotanzania@googlegroups.com>; "wanabidii@googlegroups.com" <wanabidii@googlegroups.com>
Sent: Wednesday, December 4, 2013 11:45 PM
Subject: [wanabidii] Migiro atendewe haki, aondolewe CCM

Migiro atendewe haki, aondolewe CCM
 
Na Mashaka Mgeta
 
MWANZONI mwa mwaka huu, niliposhiriki ziara ya kitaaluma nchini Korea Kusini, moja ya mambo niliyojifunza huko, ni namna nchi hiyo inavyowatumia raia wake waliowahi kuzitumikia taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa duniani.
 
Wanaporejea nyumbani (Korea Kusini) watumishi hao wanateuliwa kuziongoza taasisi nyeti kwa maendeleo na ustawi wan chi na watu wake, yaani Wakorea.
 
Mfumo huo pamoja na mambo mengine, unalenga kuchota ujuzi na uzoefu uliopo nje ya mipaka ya Korea Kusini, iingizwe katika mifumo ya utendaji na utekelezaji ndani ya nchi hiyo, na baadaye kujumuishwa katika michakato iliyopo.
 
Hivi sasa kasi ya maendeleo na ukuaji uchumi wa taifa hilo `unapaa' sawia na 'baraka' walioyojaliwa katika teknolojia ya habari.  Limetoka kuwa umasikini wa 'kutupwa' na kuwa moja ya mataifa wafadhili.
 
Nimelikumbuka jambo hilo lililo miongoni mwa mengi niliyoyashuhudia huko, kutokana na dalili za kutothaminiwa ama kutumiwa vema kwa rasilimali watu, hususani wataalamu na watendaji waliowahi kufanya kazi nje ya mipaka ya nchi. 
 
Mmoja wa watu `wanaoangukia' kwenye kundi la kutotumiwa vyema, kwamba ujuzi na uzoefu wake ungethaminiwa kwa kuwekwa kwenye taasisi isiyofungamana na upande wowote hasa katika siasa, ni Dk Asha-Rose Migiro.
 
Migiro aliyewahi kuutumikia Umoja wa Mataifa katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu, amerejea nchini na kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM anayeshughulikia  siasa na uhusiano wa kimataifa, ndani ya chama hicho.
 
Si kosa kwa Migiro mwenye asili ya uanachama wa chama hicho, kukitumikia, hata ikibidi akabaki kuwa ndani yake hadi ukomo wa maisha ya dunia utakapotimilika.
 
Lakini jambo la msingi kujadili, pamoja na kuwatambua wataalamu na wajuzi wdengine waliopo nchini, kuwapo ndani ya utendaji wa CCM kuna manufaa ya kiasi gani katika kuinufaisha nchi kwa tija inayostahili?
 
Unapokuwa na kiongozi mtendaji mwenye ujuzi na uzoefu wa kimataifa kama Migiro, akabaki 'kutupwa' katika utendaji wa chama cha siasa badala ya kuwa ndani ya taasisi ya kitaifa isiyofungamana na upande wowote, kwa mtazamo wangu inakuwa haifai.
 
Hatua hiyo inakuwa sawa na kutomtendea haki Migiro na hata kama ilitokana na utashi wake binafsi, anakuwa hajaitendea haki nafsi yake.
 
CCM ni taasisi ndogo katika upeo wa kimataifa alionao Migiro, kwamba kama angelitumikia taifa nje ya mfumo wa chama cha siasa, bila shaka angelitumikia taifa katika uwazi na uhuru usiofungamana na maslahi ya kisiasa.
 
Ninajua wapo wana-CCM waliowahi kuzitumia taasisi za kikanda na kimataifa, ingawa si kufikia 'daraja' alilolifikia Migiro, na waliporejea 'wakatupwa' kulitumikia taifa kupitia CCM.
 
Inaweza kujengwa dhana kwamba CCM ni chama tawala kinachounda serikali. Ni ukweli usiopingika.
 
Lakini lazima ikubalike kwamba mtumishi wa taifa anayebanwa sheria, kanuni na taratibu zilizojikita katika misingi ya kulitumikia taifa pasipo kuingiliwa ama kuhusisha maslahi ya kisiasa, anashugulikia maslahi mapana ya umma kuliko ya chama cha siasa.
 
Leo nimemtumia Migiro kama mfano, kutokana na ukubwa wa nafasi aliyoifikia katika Umoja wa Mataifa na jinsi `anavyohangaishwa' katika masuala yenye maslahi zaidi ya katika siasa na si maendeleo, ukuaji uchumi na ustawi wa Watanzania pasipo kujali tofauti za kiitikadi.
 
Watetezi wa mfumo wa kutotambua umuhimu wa wataalamu na wenye ujuzi na uzoefu unaoweza kuchagiza kasi ya maendeleo, ustawi na ukuaji uchumi, wanaweza kunipinga, ikibidi kupitia propaganda za majukwaani.
 
Ingawa watafanya hivyo,  si rahisi kuliondoa wazo lililo bora, kuhusu thamani ya wanataaluma na wenye ujuzi na uzoefu na namna wanavyotumika kwa maslahi ya nchi na si vyama vya siasa.
 
Kwa muda mrefu sasa Tanzania imeshuhudia wanataaluma na wenye uzoefu na ujuzi 'wakitupwa' ama wao wenyewe kujiunga katika taasisi za kisiasa.
 
Wapo wasomi magwiji waliobobea, ambao katika utumishi uliojikita katika taaluma zao, walisifika, waliaminika, wakajiweka katika ya hitaji ya umma, kwamba walilitumikia taifa na kuleta tija.
 
Lakini wanataaluma hao walipoingia na kushiriki siasa, wakabadilika na kuwa wenye fikra na matendo yasiyolingana na uwezo wao, bali kuwa mithili ya wanafunzi waliohitimu kidato cha nne na kukabidhiwa dhamana walizonazo.
 
Ni rahisi kuwataja kwa majina na nyadhifa zao, ingawa pia hata pasipo kuwaja, wanaweza kujulikana kwa maana miongoni mwao hata sasa wanatakiwa 'kufukuzwa' katika nafasi zao, kwa maana wanavurunda!
 
Hiyo ni moja ya dalili za athari zinazotokana na 'kuwatupa' wanataaluma 'mikononi mwa siasa', zikawaathiri hata kushindwa kulitumikia taifa kwa ufanisi na tija inayostahili.
 
Migiro ingawa hajaingia katika kundi hilo, binafsi ninaziona dalili za kuelekea huko. Kwa maana ndani ya chama cha siasa, hawezi akatoka nje ya yale yaliyokusudiwa na taasisi inayoitwa CCM.
 
Atabaki 'kuicheza ngoma inayopigwa CCM' pasipo kujali kama inagusa hisia na matakwa ya raia wote wa Tanzania ama vinginevyo. Msingi unakuwa ni kuyamudu mapigo, mirindimo na miondoko ya CCM, basi!
 
Kama nilivyosema awali, Migiro anatumika katika makala haya kama mfano wa mmoja wanaothirika na mfumo wa kutojali wanataaluma na wenye ujuzi na uzoefu, kulitumikia taifa badala yake wakawekezwa kwenye siasa.
 
Ninatambua kuwa siasa ina nafasi kubwa katika kuboresha ama kuathiri mifumo ya kijamii katika nchi yoyote duniani. Lakini watekelezaji wa hali hiyo wanapaswa kuwa walioivishwa katika sekta hiyo na si waliojipambanua na kuutumikia umma mpana kama Umoja wa Mataifa.
 
Kwa hili, ninazisihi mamlaka husika zimuachie Dk Asha-Rose Migiro aitumikie Tanzania, ili heshima yake ibaki kutoka alipoishia na sasa amerejea nchini.
 
Alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN, sifa zilielekezwa kwa Tanzania. Aliiweka ramani ya Tanzania kimataifa na kwa namna hiyo, kurejea kwake kumfanye aitumikie Tanzania na si taasisi ya kisiasa, ingawa uanachama wake unaweza kubaki pale pale.
 
 
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540/716635612 ama barua pepe: mashaka.mgeta@guardian.co.tz au mgeta2000@yahoo.com.
Mwisho.
Source: NIPASHE Desemba 4, 2013
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.


0 comments:

Post a Comment