Wednesday 6 September 2017

[wanabidii] Mimba shuleni, msimamo wa Rais Magufuli ni sahihi

KATIKA kipindi chake cha uongozi cha kiasi cha miezi 21 mpaka sasa, Rais Dk. John Magufuli amefanya mambo mengi.

Aidha, amesema mambo mengi, mengine yakiwa yamewashitua watu wengi. Vilevile, ametoa maelekezo na maagizo mengi. Ametifua na kutikisa wengi na mengi. Ameleta hofu ya kutosha kwa baadhi na kuzua matumaini makubwa kwa wengine.

Ukweli ni kwamba ameingia madarakani kwa kujitangaza kwa namna tofauti na baadhi ya viongozi wakuu waliomtangulia. Hiyo ndiyo maana kuu ya mabadiliko ya uongozi wa juu wa nchi. Ni somo kuwa mabadiliko ya uongozi wa juu wa nchi ni jambo kubwa kwa Tanzania na wananchi wake.

Lakini kwa sababu baadhi ya Watanzania wenye umri wa kutosha na walioshuhudia mabadiliko ya nyuma ya awamu mbalimbali walikuwa hawajapata kuona mtikisiko (turbulence), kama wa sasa, wameshtushwa na kuogopeshwa na mabadiliko kutoka kwa Rais wa Nne kwenda Rais wa Tano wa Tanzania.

Kubwa hapa la kukubali ni kwamba hiyo ndiyo hali halisi ya sasa. Rais mpya, utendaji mpya, staili mpya ya uongozi mpya, hata kama mazingira yanabakia yale yale na sera zinabakia zile zile.

Rais Magufuli ni muumini wa utawala (governance) wa kutumia hoja ya nguvu (hard power) kwa msingi mkuu wa vyombo vya dola. Waliomtangulia, kwa jumla na hasa Rais Kikwete, walikuwa waumini wa utawala kwa njia ya nguvu ya hoja (soft power) ambako nguvu ya kiongozi mkuu imo katika uwezo wake wa kushawishi (persuasion) na si kwa njia nyinginezo.

Baadhi ya hatua zake na kauli zake zimeungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wananchi. Nyingine, hata hivyo, zimezua mijadala na hata hofu kubwa ndani ya jamii.

Muhimu kwetu Watanzania, kama yeye Rais anavyotuomba wakati wote, tuendelee kumwombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumjalia busara, hekima, werevu wa kutosha wa kujifunza na kupata uzoefu bora wa uongozi, ili azidi kuongoza mapambano ya kuleta maendeleo zaidi ya nchi yetu katika mazingira ya amani, tulivu, umoja na mshikamano bila nchi yetu kukumbwa na kugawanywa na mabalaa ambayo yamekuwa sehemu ya historia ya Afrika huru mpaka sasa. Ataweza tu.

Rais Magufuli anajua fika kuliko sisi sote kuwa bila ya haya, hakuna kiwango chochote cha utumbuaji wa majipu kitakachoiwezesha nchi yetu kubaki salama, ya utulivu, ya upendo, ya amani, ya umoja, ya mshikamano na kupata maendeleo.

Watanzania hawana shaka ya kuwa Rais Magufuli ataendelea kuongozwa na haya, kama waliomtangulia, katika kuibakiza Tanzania kama Kisiwa cha Amani katika Bara lililokumbwa na mawimbi mengi na ya kutosha.

Lakini kwa maoni yangu, pengine hakuna kauli mbili bora zaidi amepata kuzitoa Rais Magufuli katika uongozi wake wa mikikimikiki mingi mpaka sasa kuliko zile ambazo amezitoa katika ziara ya karibuni ya Mkoa wa Pwani. Wakati wa ziara hizo amesema mengi, kama ilivyo kawaida yake, lakini yako mawili yaliyogusa hisia zangu binafsi.

Ya kwanza ilikuwa ni msimamo wa serikali yake kuhusu mjadala wa karibuni ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Haki ya Mtoto wa Kike ambayo pia ni Haki ya Kibinadamu (Human Right) ya kuruhusiwa kurejea shuleni na kuendelea na masomo baada ya kupata mimba na akaweza kujifungua salama kwenye umri ambako mimba ni tishio kubwa.

Ya pili ilikuwa ni maagizo yake kwa wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya na miji kununua dawa na utaalamu wa kukabiliana na kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria nchini kutoka kwa Kiwanda cha Dawa za Malaria kilichoko mjini Kibaha kilichojengwa kwa msaada wa taifa la Cuba na kwa nguvu nyingi za Serikali ya Tanzania.

Kwa sababu hii ni mijadala mikubwa ya nchi na maendeleo ya Tanzania, nitajitahidi kuitenganisha. Leo nianze tu kwa kuunga mkono msimamo wa Rais Magufuli kuhusu mimba za wanafunzi, nikijaliwa baadaye katika siku zijazo, nitajadili agizo lake kuhusu kiwanda cha kuunga jitihada za nchi yetu kutokomeza malaria katika jamii ya Watanzania.

Akizungumza kwenye ziara hiyo, Rais Magufuli, kama ilivyo hulka yake, alitoa msimamo wa serikali yake kuhusu mimba za watoto wa shule. Alisema kuwa haitatokea mtoto wa kike kupata mimba akiwa shule na akaruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua wakati wa kipindi chake cha Urais.

Kwa maana ya dhamana ya uongozi wa miaka mitano aliyopewa Oktoba 25, 2015, imebakia takribani miezi 39. Akiweza kuchaguliwa tena mwaka 2020, tunazungumzia miezi 99. Huo ndio muda anaouzungumzia anaposema hilo halitatokea katika muda wa Urais wake. Katika hali ya utulivu ni muda mfupi sana. Lakini katika hali tofauti muda huo unaweza kuwa mrefu mno.

Najua fika kuwa Rais amepingwa na wengi hasa kwenye mitandao ya kijamii, iliyojipatia zaidi umaarufu wa kukosoa zaidi kuliko kujenga. Binafsi, kwa hili, napenda kumuunga mkono Rais Magufuli.

Hapa ameweka msimamo kama Kiongozi Mkuu wa nchi na si kama mwana-mitandao ama mwana-harakati ambaye hawajibiki kwa yoyote isipokuwa kwa hisia zake mwenyewe.

Na wala kwenye hili, Rais Magufuli hajaanzisha wala hajasema jambo jipya. Viongozi wote wakuu wa nchi hii waliomtangulia- kuanzia Mwalimu Julius Nyerere hadi Jakaya Kikwete- wamedumisha sera hii hii. Alichofanya ni kutamka msimamo wa kihistoria wa nchi yetu na kwa namna yake mwenyewe ambayo wakati mwingine inawatisha baadhi ya watu na kuwachukiza wengine.

Kama nilivyoeleza, alichokisema Magufuli si kipya hata kidogo. Ndiyo sera ya kihistoria ya nchi inayojaribu kuelemisha watu wake kutoka kwenye ujinga ambao umelibakiza Bara la Afrika nyuma ya dunia nyingine iliyobakia.

Tofauti yake na viongozi wengine waliomtangulia ni jinsi alivyolisema hili. Kama nilivyoeleza hapo juu, wakati mwingine upinzani kwa Rais Magufuli ni jinsi anavyowasilisha hoja zake. Wakati mwingine anakuwa na hoja nzuri na ya msingi kabisa, kama ya mimba za utotoni, anaiwakilisha kwa namna ya ugomvi kiasi cha kuonekana kama hoja mpya na pengine yenye kulenga kuumiza baadhi ya watu ama baadhi ya makundi ndani ya jamii yetu.

Wataalamu wa mawasiliano watakueleza kuwa nguvu ya hoja ni jambo la msingi kabisa. Lakini pia wataongeza kuwa uwasilishaji wa hoja yenyewe pengine ni wa msingi zaidi. Uwasilishaji wa hoja wa Rais Magufuli umekuwa wa namna ya wakati mwingine kuzusha upinzani kwa hoja za msingi kabisa, upinzani ambao usingekuwa wa lazima, kama hoja zingewasilishwa kwa namna tofauti isiyokuwa yenye hisia kali zaidi, zenye hisia za nguvu na hata hisia za ugomvi.

Hata hivyo, hoja hiyo hii siyo sehemu ya makala hii kwa leo. Kubadilisha staili ya uwasilishaji hoja ni changamoto ya wasaidizi wa Rais Magufuli mwenyewe na wale wenye wajibu wa kumshauri kuhusu mawasiliano. Hiyo si kazi ya makala hii. Wapo wenye uwezo zaidi na weledi zaidi wa kuifanya kazi hiyo.

Kauli kali ya Rais ilikuwa ni majibu kwa baadhi ya wakubwa wakiwamo baadhi ya wabunge wetu na baadhi ya taasisi zisizokuwa za kiserikali ambazo zinashikilia bango kuwa watoto ama wajukuu wetu wa kike waruhusiwe kurudi shule na waendelee na masomo baada ya kuwa wamebeba mimba wakiwa wanafunzi shuleni.

Kwa maana ya mjadala huu, tunazungumzia wanafunzi wa shule za chekechea, za msingi na sekondari, yaani miaka mitano hadi miaka 18, kwa sababu kwenye nafasi ya elimu ya vyuo vikuu hili ama linaruhusiwa ama halizuiwi tokea miaka hiyo wakati mama yetu fulani maarufu alipojenga hoja yake binafsi mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, miaka hiyo, baada ya kuwa amepata uja uzito akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baadhi ya watetezi wa hoja ya watoto-wazazi (child mothers) kurejea shuleni ni kwamba hiyo ni sehemu ya haki ya mtoto wa kike kupata elimu ambayo, kwa hakika, ina manufaa makubwa mno kwa familia na jamii kwa jumla. Hili halina mjadala. Ni hoja ya maana pia.

Lenye mjadala hapa ni haki ipi kubwa zaidi na yenye maana zaidi kati ya kupata mimba na kurejea shuleni ama kupata elimu kwanza kabla ya kupata mimba. Kwa sababu haki ya kupata elimu, iwe kwa mtoto wa kike ama wa kiume, bila kujiingiza katika mambo ya kuvuruga haki hiyo zikiwemo mimba za shule ama za utotoni ni haki kubwa zaidi ya kibinadamu.

Haki ya Kupata Elimu inaelezwa kama Haki ya Msingi ya Binadamu katika kipengele cha 26 cha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu lenye vipengele 30 liloidhinishwa kwa Azimio Nambari 217A la Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika katika Jengo la Palais de Chaillot mjini Paris, Ufaransa, Desemba 10, mwaka 1948 – miaka 69 iliyopita na halijabadilishwa.

Kwa hakika, Azimio hilo la Umoja wa Mataifa linasisitiza kuwa kwa sababu ya umuhimu wake, elimu hasa katika ngazi yake ya mwanzo (elementary stage) na ya msingi (fundamental stage) inatakiwa kutolewa bure na kuwa elimu katika ngazi hizo lazima iwe ya lazima (compulsory) kwa binadamu wote.

Tokea wakati huo, taasisi kuu za kimataifa na watetezi maarufu na wakubwa duniani wa haki za mtoto wa kike, wamesisitiza kuwa njia bora zaidi ya kumlinda mtoto wa kike ni kumpa elimu na si kumpeleka shule kwa lengo ya kumwezesha arudi shuleni akipata mimba.

Hakuna taasisi ya maana na ama watu makini duniani wamewahi kutanguliza haki ya mtoto kupata mimba na kuruhusiwa kurejea shuleni na kuendelea na masomo. Wote wametanguliza umuhimu wa kumlinda mtoto wa kike ili aweze kupata elimu, tena elimu bora, kwa sababu mchango wake katika maendeleo ya familia na jamii ni mkubwa.

Aidha, hakuna taasisi makini na mtetezi makini wa haki za mtoto wa kike ambaye hajui athari za mtoto wa kike kupata mimba akiwa mtoto. Na hatari hizo ni nyingi zikiwamo uwezekano mkubwa wa yeye mwenyewe – mtoto-mama kupoteza maisha na hata kukabiliana na magonjwa ya hatari ukiwamo ukimwi. Athari hii inayoweza kutokea na utetezi wa mimba kwa watoto wetu wa kike, walioko shuleni na nje ya shule, ni athari ya kweli kweli. Si ya kuchezea hata kidogo.

Hata sheria zetu nchini naamini zinatoa adhabu kali za watu wanaoparamia na kuwapa mimba watoto wa shule – miaka mitano hadi 18 – kwa sababu hawa kwa sheria zetu zinatambua kuwa hawa bado ni watoto. Si akinamama wazima wa kusaka mapenzi na mimba.

Shughuli yao kubwa ni kusaka elimu, si kusaka mapenzi na maraha. Hata dini zinalikataa hili, tena si kwa watoto wa kike, bali wa kiume na hata kwa watu wazima.

Taasisi nyingi za kimataifa hujielekeza katika kutoa ushauri wa kuangalia namna bora zaidi ya kuwawezesha watoto wa kike waliopata bahati mbaya ya kupata mimba wakiwa shule kurejea shuleni. Taasisi hizi hazizungumzii haki ya mtoto wa kike kupata mimba na akarudi shule kama wanavyojaribu kulazimisha baadhi ya wabunge wetu.

Taasisi ya mwisho chini ya Umoja wa Mataifa kutoa ushauri wa namna hiyo ni Tume ya Elimu iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown, kuangalia jinsi dunia inavyoweza kujiongezea uwezo wa kugharimia elimu hasa katika nchi masikini.

Katika ukurasa wake wa 99, chini ya kichwa cha habari, Educating Girls, tume inazishauri serikali "Kuunga mkono jitihada za kurejeshwa tena shuleni (re-admission) watoto wa kike ambao elimu yao imevurugwa, kama vile watoto – wazazi (young mothers)". Na tume hii ilikuwa na watu makini sana na wanaojua na kuthamini elimu na hasa elimu ya mtoto wa kike wakiwamo viongozi wa nchi na serikali.

Kwa kukumbushana tu, tume hiyo iliteuliwa na viongozi watano duniani wakiwamo marais wa Chile, Indonesia na Malawi na Waziri Mkuu wa Norway. Na makamishna wa tume hiyo walikuwa pia watu wazito, wakiwamo marais na mawaziri wakuu wastaafu watano, akiwamo Jakaya Kikwete, Rais wa nne wa Tanzania; na hata wafanyabiashara wakubwa kimataifa kama vile Alhaji Aliko Dangote, Mtendaji Mkuu wa Kundi la Kampuni za Dangote; Mwanzilishi wa Kampuni ya Ali Baba na tajiri mkubwa zaidi katika Jamhuri ya Watu wa China, Jack Ma; na Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim.

Wakubwa hawa katika ripoti yao hawatumii kauli za mapambano kama zile za baadhi ya wabunge wetu. Wanashauri kwa sababu wanajua fika kuwa kati ya haki ya kupata elimu, na haki ya mtoto wa kike kurejeshwa shuleni baada ya kujifungua, elimu inakuja kwanza. Kazi kubwa ya mzazi na mwalimu ni kumlinda mtoto wake wa kike ili apate elimu, si kumrejesha shule baada ya kuwa amebeba mimba na kujifungua.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, haki ya mtoto ni haki ya kupata elimu, si haki ya kupata mimba. Kwa mbwembwe zao, Wamarekani wangesema Education – Stupid! Kwamba hakuna ngazi nyingine ya haraka zaidi ya kuitoa jamii katika umasikini kuliko elimu.

Na wala kwa kusema hili, hakuna asiyeelewa lilivyo jambo la kusononesha sana kwa mzazi kuona mtoto wake, ama mjukuu wake, ama dada yake anapata mimba akiwa shule. Wengine wanapata mimba katika mazingira ya kulazimishwa, kutishwa na hata kwa sababu ya umri mdogo, kurubuniwa tu na majambazi na mapapa wa kuvutiwa na mapenzi ya watoto wadogo.

Wakati mmoja akifanya ziara ya Mkoa wa Katavi, Rais Kikwete alishtushwa sana na ripoti iliyoonyesha kiwango kikubwa sana cha wanafunzi wa kike kupata mimba tena wengi wakiwa shule za msingi. Alipouliza kwa nini, aliambiwa, kwa namna ya utani wa kutisha kabisa, kuwa kuwasubiri watoto wakue na hata kuingia sekondari wanakuwa wamekuwa "wazee". Ukweli wa jibu hilo haukuwa utani hata kidogo. Ulikuwa ni ukweli unaothibitisha kuwa tamaduni zetu bado ni changamoto kubwa katika kuwalinda watoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni.

Kubwa hapa ni ukweli kuwa mimba za utotoni na za watoto wa shule zinavuruga na hata kukatisha maisha na matumaini ya watoto wa kike.

Baadhi yetu ni wazazi na katika maisha yetu tumeyashuhudia haya mambo ya kusononesha ambako mimba moja tu inatosha kurudisha nyuma vizazi viwili, vitatu vya familia.

Hivyo, baadhi yetu tulipigwa butwaa kuwaona baadhi ya wabunge wetu hasa wale wa kike, wakiwamo mawaziri, ambao wao walisoma shule na hadi kumaliza chuo kikuu bila kupata mimba wakitetea hoja ya namna hii. Mmojawao wa watetezi amepata kuwa hata Waziri wa Elimu.

Jambo kubwa hapa la kukubali ni kwamba hakuna mtu anayesema kuwa mjadala kuhusu jambo hilo ni mbaya. Si mjadala mbaya, lakini ni mjadala ambao wakati wake haujafika hapa nchini. Hakuna anayesema kuwa hoja si ya msingi. Ni hoja ya msingi kabisa. Lakini wakati wake haujafika. Wakati ukifika hoja hii itakuwa rahisi kukubaliwa na watu wengi na itakuwa na upungufu mkubwa wa utata.

Kwa sasa ni mjadala ambao unachangia tu kuwachanganya watoto wetu wa kike ambao wanaweza kuamini kuwa inawezekana ukachanganya masomo na mapenzi na ukaweza kufanikiwa, hata kama kweli wapo wachache wamepambana na wakaweza kufanikiwa hata baada ya kupata mimba wakiwa shuleni.

Waliofuata njia hiyo na wakafanikiwa katika maisha ni wachache. Hiyo si njia ya kawaida ya kila mtoto wa kike kupitia. Ni njia ya mtoto jasiri, mwenye ujasiri kwanza wa kukabiliana na kulala na mwanaume ambalo kwa watoto wengi wadogo wa kike ni jambo kutisha.

Hivyo, kwa baadhi ya watu lilikuwa jambo la kushangaza kuona baadhi ya viongozi wetu wakijenga hoja ya kuwachanganya, kuwarubuni na kuwavuruga watoto wetu. Kwa wakati huu, ni hoja ya kurudisha nyuma maendeleo – kwa kasi zaidi, ari zaidi na nguvu zaidi.

Uzuri wa mijadala ya Bunge inatawaliwa na hoja. Mmoja wa wabunge waliosimama kidete kupinga hoja hii ni Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, mwalimu kwa taaluma, na mke wa Rais aliyemtangulia Rais Magufuli madarakani. Wapo wengi walimpinga ndani na nje ya Bunge na kujaribu kumkejeli. Hili ni la kawaida kabisa na nina uhakika halikumsumbua Mama K, mama wa chuma kama anavyojulikana kwa walio karibu naye.

Lakini mama Salma Kikwete anazungumza kwa uzoefu mkubwa na uchungu wa hakika wa mzazi. Ningependa kujua na kuona mwanamke mwingine katika historia ya Tanzania aliyejitahidi kufanya mengi kwa ajili ya Mtoto wa Kike.

Huyu ni Mama wa Shoka, Mama wa Mfano. Yeye alibuni wazo, akapata ushauri, akajenga shule na anaendesha shule ya mfano ya watoto wa kike waliotokana na mazingira hatarishi na katika umasikini mkubwa nchi nzima. Shule iko Nyamisati, Wilaya ya Mukuranga, Mkoa wa Pwani.

Nadhani waliompiga kwa hoja bungeni walifanya hivyo kwa ushabiki tu na kwa wivu wa kumpinga mke wa Rais mstaafu na bila kuona ushahidi wa nini mama anakifanya. Ushauri wangu kwao wajipe muda na nafasi na watembelee shule hii ya WAMA-Nakayama, ili wapate ushuhuda wa shida za mtoto kike wa Tanzania. Itawasaidia kujenga hoja bora zaidi za kutetea msimamo wao katika siku zijazo.

Kwa nchi yetu ambako sekta ya elimu bado inakabiliwa na changamoto kubwa na za msingi kabisa kuleta mjadala huu, tena kwenye ngazi kubwa kama Bunge, ni kuchangia kuwachanganya watoto wetu tu bila sababu za msingi.

Kwa nini hatuelekezi nguvu zetu katika mambo ya msingi kwenye sekta hii. Kwa nini hatuelekezi nguvu zetu katika kuboresha kiwango cha elimu? Kwa nini hatuelekezi nguvu zetu katika kuondokana na vyeti feki vinavyozalisha viongozi feki?

Kwa nini hatuelekezi nguvu zetu katika kuondokana na kutunga vitabu vya kiada vyenye makosa ya kitoto na ya kutosha? Kwa nini hatuelekezi nguvu zetu katika kuboresha mazingira ya wanafunzi na watoto wetu kusoma kwa uhakika – majengo bora ya shule, kuwapo kwa huduma za msingi kama hata vyoo, madawati, upatikanaji wa chakula, upatikanaji wa usafiri wa uhakika na mambo mengi tu.

Maswali ni mengi na ya msingi– kwa nini ilituchukua karibu miaka 45 ya uhuru kuanza kukabiliana na uhaba wa walimu, uhaba wa vitabu vya kufundisha na kufundishia, kwa nini tulilazimika kuziomba nchi wafadhili kama Marekani kutuchapishia vitabu vya masomo ya sayansi? Kwa nini tunaendelea kuwa na uhaba wa maabara za masomo ya sayansi?

Kwa nini kwa mfano, ilituchukua miaka 45 na viongozi wakuu wanne kuweza kuanza kujenga sekondari za kutosha kwa ajili ya watoto wetu? Mpaka mwaka 2005, ni asilimia 22 ya wahitimu wote wa shule za msingi walikuwa wanaingia sekondari. Kisa, hakuna shule za kutosha mpaka ubunifu wa Serikali ya Rais Kikwete ulipoongeza idadi ya sekondari nchini kutoka 1,745 mwaka 2005 hadi 4,753 mwaka 2015. Na wala sina hakika kama kweli shule hizo zinatosha kwa kasi ya kuzaliana ya asilimia tatu kwa mwaka.

Uchunguzi wa uhakika unaonyesha kuwa mwalimu katika nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara anaingia na kuwa darasani kwa saa mbili na dakika saba tu kwa siku. Kwa muda mwingine anakuwa katika shughuli zake za kibiashara ama za kilimo.

Kwa nini wabunge wetu hawakerwi na hali hiyo? Kwa nini hawajadili jambo hili bungeni? Kwa nini hawatafuti namna ya kumlazimisha mwalimu kuingia darasani? Kwa nini wasitafute namna ya kumlazimisha akishaingia darasani akae darasani angalau kwa saa saba na wakati wote akifundisha na si kufanya mambo yake?

Kwa nini wabunge hawatetei maslahi ya mwalimu – haki zake za msingi yaani mshahara wa kumwezesha kuishi vizuri na kulipa haki zake nyingine? Kwa nini wabunge hawatetei angalau kuwapa nusu tu ya mshahara ambao wao wabunge wanalipwa?

Kubwa zaidi ni kwa nini sisi Watanzania tunaendelea kudandia sera na mambo ya wakubwa wa Magharibi kwa sababu ya vipesa kidogo tu. Hoja hii ya kuruhusu watoto wa kike kurejea shule baada ya kupata mimba ni hoja ya wakubwa, si hoja ya watu masikini kama sisi.

Ni sehemu ya mpango mpana wa Wakubwa hawa wa kuendelea kuidumaza Afrika kwa sera za Cultural Imperialism – ubeberu wa kitamaduni ambako sisi Waafrika tunaelekezwa kufanya mambo ya ovyo na tunayakubali.

Utaambiwa kula magimbi ama mhogo ni jambo baya na kuwa lazima ule mkate na uwezo wa kununua mkate huna. Utaambiwa ni muhimu kuunga mkono sera za ushoga kwa sababu ni haki za binadamu. Utaambiwa kuunga mkono mambo yasiyokuwa ya Kiafrika ama, ya kibinadamu kama vile ndoa za jinsia moja.

Utaambiwa rangi yako ya mwili, weusi, ni ubaya na hivyo utashawishiwa kununua dawa za kujichubua, ambayo ni jambo la hatari kabisa kwa afya na ustawi wa uchumi.

Wengine sasa wameanza kushawishiwa kutumia dawa za kuongeza na kupanua viungo vyao vya miili kama matiti na makalio. Confusion na chaos tupu! Na sisi Waafrika tunaendelea kukubali.

Na ni jambo la kushangaza kwamba Confusion hii inaendelea katika kipindi ambacho sasa tuna wasomi wengi zaidi na walibobea zaidi katika nyanja mbalimbali ndani ya Bunge, ndani ya Serikali na ndani ya taasisi zetu – madaktari na maprofesa na watu wenye uwezo mkubwa wa kisomi hata kama si wa kuelimika.

Kwa nini mkanyangiko huu hatukuuona wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere ambaye aliongoza nchi yetu na wasomi wachache sana bila kuwa na maprofesa wala madaktari lakini nchi ikaenda vizuri kiasi chake kwa mazingira ya wakati huo. Kizazi cha sasa kinazuzuliwa na nini? Ni kwa kujenga nyumba Mbezi Beach ama Mbweni ama Tegeta? Ama na kuendesha 'maVogue' ama magari mengine ya kifahari? Kwa nini tunachezewa kiasi hiki na hawa Wakubwa? Tunababaishwa na rangi? Kitu gani kinatuzuia tusione maslahi yetu ya kweli kweli kama Taifa na kuyatetea ipasavyo, tena kwa akili, na si kwa ubabe ambao unaweza kutugharimu?

Hebu kwa muda tukubali, muda tu, hoja ya watoto kuruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua na tujiulize maswali ya msingi na halisi kabisa. Mtoto-mzazi anarejea shuleni akiwa na msongo kiasi gani wa mawazo kuhusu mtoto wake mdogo? Je anamwachia nani mtoto wake? Anarudi naye shuleni? Akienda naye shuleni nani atamtunza wakati yeye akiwa darasani? Akimwacha nyumbani nani anabakia naye-mama yake, bibi yake ama jirani yake ama anakuwa wapi?

Enzi za zamani za mababu na mabibi wa baadhi ya makabila kutunza, kwa siri, wajukuu wao wakati watoto wanaendelea na shule, siamini kama zipo tena. Hali ya uchumi imebadilika kiasi cha kwamba hilo haliwezekani tena!

Binafsi najifikiria nilikotoka. Hivi mtoto wa kike kutoka pale kijijini katika Mkoani Kagera au Kilimanjaro ambaye amebahati kuingia shule vizuri, anaweza kweli akarejea na kuendelea na masomo baada ya kupata mimba?

Hili ni jambo linawezekana kweli? Na hapa nakuwa mkweli kwa kutoa mifano ya maeneo ambako elimu inaheshimiwa kwa kiwango kikubwa kidogo tu kuliko pengine maeneo mengi ya nchi yetu.

Binti huyu ambaye amefanikiwa na kufikia hatua ya sekondari aweze kurudi kijijini, akabiliane na mapapa wa kiume wa Kihaya, ama Kisukuma, ama Kinyambo, ama Kijita, ama Kikara, ama Kisubi, ama Kihangaza, ama Kizinza, ama Kinyarwanda, ama Kichagga, ama Kipare, ama Kimasai, au Kiiraq, ama Kikurya bila kupata mimba nyingine na aweze kurejea salama shuleni na kuendelea na masomo baada ya kuwa amejifungua? Inawezekana naendelea kuishi katika nchi nisiyoilewa vizuri?

Raia Mwema.

Virus-free. www.avast.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment