Kwamba shughuli zote za uendeshaji wa mamlaka za dola zitafuata
misingi ya uwazi, ukweli na uwajibikaji na kuwa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania litakagua na kudhibiti utendaji wa vyombo vya
dola pamoja na kuridhia mikataba muhimu ya umma. Baraza la Wawakilishi
la Tanganyika na la Zanzibar yatafanya hivyo kwa mamlaka za Tanganyika
na Zanzibar kila moja kwa eneo lake na kwa mambo yahusuyo serikali
husika na si vinginevyo.
UCHAMBUZI NA UFAFANUZI WA MAONI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA
CHA WANANCHI) KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA:
1. DIRA YA TAIFA:
a) Lengo kuu la Taifa letu ni kujenga Tanzania yenye haki sawa kwa
wananchi wote na inayoheshimu haki za binadamu kwa vitendo.
b) Amani na utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo. Haki sawa kwa
wananchi wote ndiyo msingi wa kuendeleza amani na utulivu wa kweli.
Kila Mtanzania ana wajibu wa kujenga jamii inayoheshimu haki za kila
mwananchi ili kudumisha amani na utulivu.
c) Wananchi wote wawe na fursa ya kujiendeleza kwa juhudi zao wenyewe
na kwa mchango wa kila Mtanzania tujenge Taifa linalojitegemea lenye
neema kwa wote, uzalendo na mshikamano wa kitaifa linaloweza kuhimili
ushindani wa kiuchumi katika ulimwengu wa utandawazi.
d) Kujenga utamaduni wa kuchapa kazi kwa bidii, nidhamu, uadilifu na
tija ya hali ya juu na kila Mtanzania awe na ari ya kujifunza na
kujiendeleza katika maisha yake yote.
e) Kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kuvumiliana na kupendana bila
kujali tofauti zetu za ukanda, kabila, rangi, dini na jinsia.
f) Kutumia maliasili na raslimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi
wote huku tukizingatia ulinzi wa mazingira.
2. MAADILI NA MISINGI MIKUU YA TAIFA:
2.1 MAADILI
CUF inapendekeza katiba iainishe Maadili ya Taifa. Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ni nchi inayoongozwa na maadili yafuatayo:-
a) Binadamu wote wanastahili heshima na ulinzi wa utu wao.
b) Haki sawa kwa Watanzania wote. Haki hizo ni za kiuchumi, kisiasa,
kiutamaduni na kijamii.
c) Ni wajibu wa kila Mtanzania kuchapa kazi kwa bidii na kujiendeleza
katika maisha yake yote.
d) Umoja na mshikamano wa Watanzania wote.
e) Ubaguzi wa rangi, dini, kabila, kikanda, jinsia haukubaliki kabisa
katika kuendesha shughuli za umma.
f) Maliasili na raslimali za Tanzania zitatumiwa kwa manufaa ya
Watanzania wote na kuzingatia ulinzi na uhifadhi wa mazingira.
Kwa kuzingatia maadili ya Taifa viongozi wataheshimu na kufuata
maadili yafuatayo:-
a) Kuwa uongozi ni dhamana na utatumiwa kwa ajili ya maslahi ya Taifa
na ya wananchi wote kwa ujumla na kamwe hautatumiwa kwa maslahi
binafsi, ubaguzi, upendeleo au kwa ajili ya kujilimbikizia mali;
b) Kuwa mali na rasilimali za umma zitatumiwa na kulindwa kwa maslahi
ya Taifa na kamwe viongozi wa umma hawatatumia nafasi na mamlaka
waliyokabidhiwa kutwaa, kuiba, kufuja au kujibinafsishia mali na
rasilimali za umma;
c) Kuwa rushwa, ufisadi na uhujumu wa uchumi wa Taifa ni maangamizi ya
Taifa, hivyo viongozi hawatashiriki kwa namna yeyote ile katika
vitendo vya rushwa, ufisadi na uhujumu wa uchumi wa Taifa;
d) Kiongozi hatafanya maamuzi katika mambo yenye mgongano kati ya
maslahi yake binafsi na maslahi ya umma;
e) Viongozi wa umma hawatafanya biashara, kuajiriwa au kuifanyia kazi
taasisi yoyote binafsi kwa ajili ya kujinufaisha binafsi.
2.2 MISINGI
CUF inapendekeza katiba iainishe masuala ya Msingi ya demokrasia, haki
na usawa. Taifa litaongozwa na kuishi kulingana na misingi mikuu
ifuatayo:-
a) Kwamba chanzo cha mamlaka ya dola ni wananchi kwa hivyo mamlaka za
dola zitapata uhalali wake kutokana na ridhaa ya wananchi na serikali
zote tatu na mabunge yote matatu yatawajibika kwa wananchi;
b) Kwamba, ufisadi, ujinga, maradhi na umaskini ni maadui wa Taifa kwa
hivyo lengo kuu la sera, sheria na serikali zote tatu na juhudi za
wananchi wote ni kuwaangamiza maadui hawa;
c) Kwamba wananchi wanayo haki ya kushiriki katika shughuli za mamlaka
za dola kwa mujibu wa Katiba.
d) Kwamba haki, usawa na ustawi wa kila mwananchi ndio ngao ya umoja,
undugu, mshikamano na amani ya Taifa;
e) Kwamba kuheshimu na kulinda utu na haki zote za binadamu na pia
kutii Katiba na sheria ndio msingi mkuu wa utamaduni wa Taifa;
f) Kuhakikisha kuwa hakuna unyonyaji wa mtu na mtu mwingine;
g) Kwamba maliasili, mazingira na utajiri wa Taifa ni rasilimali za
Taifa kwa ajili ya wananchi wote wa Tanzania kwa kizazi cha sasa na
vizazi vijavyo na kamwe hazitafujwa, kupokonywa au kuvunwa kinyume cha
maslahi ya Taifa;
h) Kuhakikisha kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa kwa
ulinganifu na kwa uadilifu;
i) Kuhakikisha kwamba kila kitendo cha mamlaka ya dola au cha kiongozi
yeyote mwenye madaraka kina lengo la kuliletea Taifa manufaa kwa maana
ya kuweka maslahi ya Taifa bila ya kujali maslahi binafsi:
j) Kwamba ni wajibu wa dola kumwandaa raia kielimu na kiujuzi ili
kumwezesha kila mmoja kumudu kupata na kuendesha shughuli halali na
kujipatia riziki yake ama kwa kuajiriwa au kwa kujiajiri;
k) Kwamba haki za binadamu zilizotamkwa na Tangazo la Dunia la Haki za
Binadamu la mwaka 1948 kuhusu haki za Binadamu na zilizotamkwa katika
Mkataba wa Haki za Binadamu na za Jamii wa Umoja wa Afrika wa mwaka
1981 pamoja na mikataba au mikataba ya nyongeza iliyoundwa au
itakayoundwa na Umoja wa Mataifa au umoja wa Afrika au Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki kwa minajili ya kutunza, kuhifadhi na kutetea haki
za binadamu au sehemu ya jamii kama vile wanawake, watoto, wazee na
walemavu vitachukuliwa kuwa ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na serikali zake.
l) Kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake,
kujiunga na chama cha siasa au taasisi na vyama vya kijamii ikiwa ni
pamoja na kushiriki katika shughuli za chama au taasisi aliyojiunga
kwa hiari yake mwenyewe.
m) Kwamba dola na vyombo vyake vyote vitatoa haki na fursa sawa kwa
raia na wananchi wote wa Tanzania bila ya kujali jinsia, rangi,
kabila, ukanda, dini, itikadi ya kisiasa wala hali ya mtu;
n) Kwamba aina zote za dhuluma, uonevu, vitisho, ukandamizaji,uhujumu
wa uchumi, ufisadi, ubaguzi, upendeleo na rushwa zinakuwa mwiko na
kukomeshwa kabisa;
o) Kwamba shughuli zote za uendeshaji wa mamlaka za dola zitafuata
misingi ya uwazi, ukweli na uwajibikaji na kuwa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania litakagua na kudhibiti utendaji wa vyombo vya
dola pamoja na kuridhia mikataba muhimu ya umma. Baraza la Wawakilishi
la Tanganyika na la Zanzibar yatafanya hivyo kwa mamlaka za Tanganyika
na Zanzibar kila moja kwa eneo lake na kwa mambo yahusuyo serikali
husika na si vinginevyo;
p) Kwamba serikali itazisaidia na kuziimarisha taasisi za kijamii ili
ziweze kutoa huduma za kuharakisha shughuli za maendeleo ya wananchi
na kukuza utamaduni wa kidemokrasia.
Katika utetekelezaji wa kazi na wajibu wake, mamlaka zote za dola
zitakuwa na jukumu na wajibu wa kutii na kuzingatia maadili na misingi
yote iliyotamkwa kwenye Sehemu hii ya katiba na misingi hii itakuwa
chanzo cha sera na sheria za nchi.
3. HAKI ZA BINADAMU NA WAJIBU MUHIMU:
3.1. HAKI YA USAWA
a) Haki za binadamu ziendane na maadili ya kitanzania. Binadamu wote
huzaliwa huru, na wote ni sawa. Sheria zote kandamizi kama zile
zinazohusiana na masuala ya ugaidi zipitiwe upya na au zifutwe, kila
mtu anastahili heshima na kuthaminiwa utu wake na iwe ni marufuku
kumtesa, kumtweza au kumdhalilisha mtu;
b) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi
wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria;
c) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na Mamlaka yoyote katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au inayotumika nchini kuweka sharti
lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake
isipokuwa kama imefanyika hivyo ili kurekebisha athari mbaya ya
ubaguzi wa jinsia au kundi lolote la watu;
d) Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu
yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka
ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria;
e) Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au na mamlaka yoyote
inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika
utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya Nchi;
3.2. HAKI YA ELIMU NA AFYA:
a) Kila mtu ana haki ya kuelimishwa. Elimu ya msingi itolewe bure na
iwe ya lazima kwa kila mtoto. Elimu ya ufundi stadi iwe wazi kwa wote.
Na elimu ya juu iwe wazi kwa wote kwa kutegemea sifa ya mtu. Serikali
iwalipie watu wote wenye vipaji vya kuendelea na elimu ya juu bila
ubaguzi wowote.
b) Elimu ya uraia itolewe katika ngazi zote za elimu kwa madhumuni ya
kuendeleza maadili ya Taifa, kukuza mshikamano na umoja wa kitaifa na
uelewa wa haki za binadamu na kuendeleza kuelewana, kuvumiliana na
urafiki kati ya Watanzania wa kabila, rangi na dini mbalilmbali.
c) Kila Mtanzania ana haki ya kupata huduma za msingi za afya, kupata
hali bora ya maisha yeye mwenyewe pamoja na familia yake na kupata
chakula, mavazi, nyumba, matibabu na hifadhi za lazima kwa maisha
yake. Pia ana haki ya kutunzwa wakati akiwa hana ajira kwa sababu
ambazo haziko chini ya uwezo wake, wakati wa ugonjwa, wa kutojiweza,
ujane, uzee au anapokosa riziki yake kwa kutoweza kujisaidia. Mafao
yote haya yalingane na uwezo wa uchumi wa Taifa.
3.3. HAKI YA KUWA NA FAMILIA:
a) Kila mtu anayo haki ya kuwa na familia, kuoa na kuolewa kwa hiari
bila kuwekewa pingamizi kutokana na rangi, kabila, dini, jinsia,
itikadi au hali yake ya maisha;
b) Ndoa itafungwa kati ya mume na mke kwa hiari na familia itakuwa
kitengo muhimu katika mfumo wa jamii kitakacholindwa na kustawishwa
kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi;
c) Wanandoa watakuwa sawa na kufaidi haki sawa kwa mujibu wa katiba.
d) Watoto ni hazina na rasilimali kuu ya Taifa hivyo Mamlaka za dola
na za kijamii zitahakikisha kuwa kila mtoto anapata ulinzi, hifadhi,
lishe, tiba, malezi ya kimaadili na elimu bora.
3.4. HAKI YA KUMILIKI MALI
a) Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali binafsi kwa njia halali ama
peke yake au kwa ushirikiano na mtu yeyote mwingine;
b) Ni marufuku mtu yeyote ambaye anamiliki mali binafsi kwa halali
kunyang'anywa au kutaifishiwa mali yake isipokuwa pale tu ambapo
amelipwa fidia stahili na inayomridhisha, na kwamba sababu ya
kumyang'anya au kutaifisha mali husika ni kwa maslahi ya juu ya umma
na kwa mujibu wa sheria ;
c) Ikiwa mali inayotaifishwa ni makazi basi mamlaka ya dola
itahakikisha kuwa aliyetaifishiwa makazi yake anapewa ardhi mbadala na
muda wa kutosha kujenga makazi mbadala;
3.5. HAKI YA KUMILIKI ARDHI;
a) Ardhi ni mali ya Watanzania wote katika ujumla wao kama Taifa.
b) Raia wa Tanzania peke yao ndiyo watakuwa na haki za kumilikishwa
ardhi.
c) Kila Mtanzania atakuwa na haki ya kumilikishwa ardhi anayoitumia
peke yake kwa shughuli za uchumi na kijamii.
d) Kutakuwa na ardhi itakayosimamiwa na mamlaka za vijiji, halmashauri
za wilaya, miji, manispaa na majiji. Ardhi iliyobaki itamilikiwa na
Serikali Kuu.
e) Ardhi ya Umma itakuwa chini ya udhamini wa Rais kwa niaba ya Raia
wote kwa mujibu wa sheria.
f) Katiba itamke kuwepo kwa Tume ya Ardhi itakayosimamia ardhi ya
umma, kutoa ushauri pamoja na kushughulikia masuala yote ya utoaji
ardhi kwa wananchi na kuweka kumbukumbu ya masuala yote ya ardhi.
3.6. HAKI YA KUCHAGUA NA KUCHAGULIWA KUWA KIONGOZI:
a) Kila mwananchi aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki
ya kupiga au kupigiwa kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na
wananchi kwa ngazi za vitongoji, vijiji, mitaa, kata na majimbo. Umri
wa chini wa kugombea nafasi ya Urais uwe miaka 30
b) Bunge litunge sheria na kuweka masharti yanayolinda na kuwezesha
utekelezaji wa haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi.
c) Pawepo haki kwa mwananchi mwenye sifa za kuchaguliwa kuwa kiongozi
kugombea binafsi bila kushurutishwa kujiunga na chama chochote cha
siasa.
d) Usifanyike uchaguzi wowote ule pasina kuhakikisha utaratibu wa
uhakiki wa watu wote wenye sifa za kupiga kura kikatiba wameingizwa
katika orodha halali ya wapiga kura katika Daftari la kudumu la wapiga
kura.
3.7. HAKI YA KUKUSANYIKA NA KUANDAMANA:
Raia wanayo haki ya kukusanyika, kuandamana kwa amani na kufanya
mikutano bila kizuizi na utakuwa wajibu wa Mamlaka ya dola kuhakikisha
kuwa raia wanapokusanyika, kuandamana kwa amani au kufanya mkutano
hawabugudhiwi na kunyanyaswa na vyombo vya usalama au mamlaka yoyote
wa serikali.
3.8. UHURU WA KUJIAMULIA MAMBO:
a) Raia wa Tanzania kwa pamoja wanayo haki ya kujiamulia mambo yao
wenyewe na kukubaliana katika mambo yanayohusu uhuru wa nchi, siasa na
jinsi ya kujiletea maendeleo ya uchumi na utamaduni;
b) Raia wa Tanzania kwa pamoja wanayo haki ya kumiliki na kuvuna na
pia wanao wajibu wa kuhifadhi rasilimali asili na utajiri wa nchi yao
na ni marufuku kwa mtu yeyote au mamlaka ya dola au binafsi kuweka
saini mkataba wowote unatwaa au kudhoofisha haki hii au kuruhusu
umiliki na uvunaji wa rasilimali asili na utajiri wa nchi kuwa
mikononi mwa watu wasio raia au mashirika ya nje pasipo na ubia wa
raia wa Tanzania;
c) Watanzania wanayo haki ya kulinda na kuendeleza utamaduni wao
pamoja na mifumo ya maisha, uchumi na mila bora zinazoendana na
utamaduni wao;
d) Ni wajibu wa kila mwananchi kuachana na mila potofu ambazo
zikiendelezwa zinawakandamiza wanawake, watoto, mtu yeyote au sehemu
ya jamii kiafya , kimwili na kisaikolojia.
3.9. UHURU WA KUTOA MAWAZO, HABARI, TAARIFA NA MAONI;
a) Kila raia anayo haki ya kutoa mawazo, habari, taarifa na maoni bila
kuingiliwa na mamlaka yoyote ile na sheria zote zinazokandamiza uhuru
wa kutoa mawazo, taarifa, habari na maoni hazitakuwa na nafasi.
b) Vyombo vya habari vyote vinawajibika kwa jamii na taifa kwa ujumla
kwa hivyo vinapaswa kurusha habari na taarifa ambazo jamii yetu
inazihitaji ili kupata mustakabali mwema.
c) Vyombo vya habari vya serikali ni mali ya umma na vitawajibika
kurusha taarifa na habari zake bila kuegemea upande wowote na kutoa
fursa sawa kwa watumiaji wote.
d) Nyakati za matukio makubwa ya kitaifa kama vile chaguzi mbalimbali,
kumbukumbu za kitaifa na matukio makubwa ya huzuni na furaha na
masuala yote yenye maslahi kwa taifa yatapewa kipaumbele na vyombo vya
habari vya serikali bila kujali yanatoka serikalini, taasisi za
kijamii, vyama vya siasa n.k. matukio haya yataoneshwa kwa usawa bila
kubagua.
3.10. HAKI YA KUPATA DHAMANA
a) Kila raia ana haki ya kupewa dhamana pale ambapo atakuwa
anashikiliwa na vyombo vya dola na ni marufuku raia kushikiliwa bila
sababu za msingi.
b) Haki ya dhamana inaweza kuondolewa pale tu ambapo raia anashikiliwa
na vyombo vya dola kwa makosa ya uhaini, mauaji ya kukusudia na
unyang'anyi wa kutumia silaha.
4. VYAMA VYA SIASA:
a) Vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu viwe na uwezo wa kikatiba
wa kuungana kwa ajili ya kuunda chama kimoja kushiriki katika uchaguzi
siku ishirini na moja (21) kabla ya tarehe iliyotangazwa na Tume ya
uchaguzi kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni na vyama vilivyoungana
visipoteze uasili na usajili wao wa kudumu.
b) Mtu yeyote asilazimishwe kujiunga na chama cha siasa au chama
chochote cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au
falsafa yake isipokuwa kama falsafa yake inapinga waziwazi maadili ya
Taifa na misingi muhimu ya haki za binadamu;
c) Utaratibu wa vyama vya siasa kuweka wagombea katika uchaguzi wa
viongozi wa ngazi zote za vyombo vya uwakilishi vya dola
hautamlazimisha raia kuwa mwanachama wa chama cha siasa ili kupata
sifa ya kuteuliwa kuwa mgombea.
d) Bunge litunge sheria na kuweka mipaka ya matumizi ya haki kwa
baadhi ya watendaji wakuu wa vyombo vya dola ili kulinda uhuru, ubora
wa utendaji wa wakuu hao na imani ya umma kwa ujumla kwa vyombo
wanavyoviongoza.
5. TUME YA UCHAGUZI;
a) Kuwepo na Tume huru za Uchaguzi ambayo ni asasi huru ambayo
haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya
Serikali au kutoka chama chochote cha siasa, katika kutekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa sheria. Tume itakuwa na wajumbe wafuatao
watakaoteuliwa na Rais, kutokana na majina yatakayopendezwa kwake na
sekta za jamii husika na hivyo pawepo na wajumbe wa tume wakiwemo;
i. Mjumbe mmoja kutoka kila chama cha Siasa chenye wabunge wa
kuchaguliwa.
ii. Mjumbe mmoja anayewakilisha mashirika na taasisi zisizo za
kiserikali zinazoshughulikia uongozi wa jamii;
iii. Mjumbe mmoja anayewakilisha taasisi za kidini za kiislamu.
iv. Mjumbe mmoja anayewakilisha taasisi za kidini za kikristo.
v. Mjumbe mmoja anayewakilisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa.
vi. Mjumbe mmoja anayewakilisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
vii. Mjumbe mmoja anayewakilisha walemavu.
viii. Mjumbe mmoja anayewakilisha wanawake.
ix. Mjumbe mmoja anayewakilisha vijana.
x. Mjumbe mmoja anayewakilisha wazee.
b) Tume ya Uchaguzi itachagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti wake
yenyewe na wajumbe wake watakula kiapo cha uaminifu mbele ya Jaji wa
Mahakama ya Rufani kabla ya kuanza utekelezaji wa majukumu yake;
c) Wajumbe wote wa Tume, Mwenyekiti, Makamu na Makamishna wasiwe na
wadhifa mwingine wowote kwenye vyombo vya umma.
d) Tume ya Uchaguzi itaajiri sekretarieti na watendaji wake na
kuendesha shughuli za uchaguzi kwa uhuru bila vitisho wala ushawishi
wa mtu, taasisi au mamlaka yoyote kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa
na sheria iliyotungwa na Bunge;
e) Fedha za matumizi ya Tume ya Uchaguzi zitengwe moja kwa moja na
Bunge kutoka kwenye Mfuko wa Hazina wa Taifa (Consolidated Fund)
f) Tume itakuwa na watendaji wake wenyewe mpaka katika kila
halmashauri.
g) Majina yatakayopendekezwa kwa Rais yatatokana na watu ambao siyo
viongozi wa chama chochote cha siasa, na uteuzi utakaofanywa na Rais
sharti uthibitishwe na Bunge.
h) Wajumbe wa Tume Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
kwa kufuata kanuni kwamba endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka sehemu
moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wake atakuwa ni mtu
anayetoka sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
uchaguzi huo uwe umefanyika katika mkutano wa kwanza wa Tume ya
Uchaguzi.
i) Tume ya Uchaguzi ya Taifa itasimamia chaguzi zote toka ngazi ya
vitongoji, vijiji na mitaa, madiwani, wabunge na Rais.
j) Bunge litunge sheria ya Uchaguzi na kuweka masharti kuhusu mambo
yafuatayo;
• Utaratibu endelevu na wa kudumu wa uandikishaji wa wapiga kura
katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa
wanachi unaofanywa nchini Tanzania;
• Utaratibu wa kudumu wa kutunza na kuhakiki wapiga kura waliomo
kwenye daftari la kudumu la wapiga kura;
• Utaratibu wa kumwezesha mpiga kura aliyejiandikisha sehemu moja
kupiga kura sehemu nyingine au kuhamisha usajili wake wa kupiga kura;
• Kutaja wajibu na shughuli za tume za Uchaguzi na utaratibu wa kila
uchaguzi ambao utaendeshwa na Tume hizo;
k) Uchaguzi unaofanywa na wananchi nchini Tanzania utafanyika katika
vipindi vya mara kwa mara vilivyowekwa na sheria ya uchaguzi na
katiba.
l) Uchaguzi utakaofanyika ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania
utahusisha;
• Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
• Rais wa Tanganyika na Zanzibar,
• Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
• Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na la Zanzibar
• Madiwani na wenyeviti wa Serikali za Mitaa za Tanganyika na Zanzibar
m) Mambo mengine ya kuzingatia;
• Uchaguzi wa madiwani ujumuishwe katika serikali za mitaa.
• Rais ashitakiwe akiwa madarakani au akiwa nje ya madaraka.
• Matokeo ya uchaguzi yanaweza kuhojiwa mahakamani.
• Mtanzania yeyote anaweza kuchaguliwa kuwa Rais kwa vipindi
visivyozidi viwili.
6. MFUMO WA UCHAGUZI:
a) Katiba mpya itamke kuwepo kwa mfumo wa uwiano wa kura kwa uchaguzi
wa wabunge, madiwani na wajumbe wa serikali za vijiji na mitaa. Ikiwa
kiti cha Mbunge yeyote aliyechaguliwa kuwakilisha jimbo la uchaguzi
kitakuwa wazi kwa sababu nyingine yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa
Bunge basi orodha ya chama alichokuwa mbunge aliyepoteza nafasi yake
itatumiwa kujaza nafasi hiyo kwa kuzingatia jinsia ya mbunge
aliyetoka. Ikiwa mbunge aliyetoka ni mwanamke litachukuliwa jina la
mwanamke anayefuatia katika orodha na kadhalika kwa mwanaume. Ikiwa
Mbunge aliyetoka alikuwa mgombea binafsi basi orodha ya chama
kilichopata kura nyingi na kuwa cha pili katika eneo hilo itatumiwa
kuteua mbunge. Ikiwa mgombea binafsi mwingine ndiye aliyekuwa wa pili
basi yeye ndiye atakayeteuliwa kuwa mbunge.
b) Kila Chama kitaandaa orodha ya wagombea nafasi ya ubunge. Orodha
hii itabadilishana majina kijinsia. La kwanza likiwa la mwanamke la
pili litakuwa la mwanaume. Bunge litatunga sheria kugawa maeneo ya
uchaguzi na vigezo vya kutumia kuamua idadi ya viti vya bunge katika
kila eneo. Vyama vya siasa vitaandaa orodha ya wagombea wa ubunge
katika kila eneo kufuata utaratibu wa kubadilishana majina kijinsia.
c) Mgombea uchaguzi katika kila eneo la uchaguzi atatakiwa atimize
masharti yafuatayo:-
i. Awe amependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa,
ii. Awe amepata uteuzi wa Tume ya Uchaguzi kwa kuwa na sifa ya kuwa
mgombea
iii. Kama ni mgombea binafsi awe ametimiza masharti ya ugombea binafsi
yaliyowekwa na Katiba na sheria ya uchaguzi;
d) Hapatakuwa na haja ya viti maalum vya wanawake kwani orodha za
vyama zitakuwa na asilimia 50 wanawake na asilimia 50 wanaume. Chama
kikipata wabunge 10, watano watakuwa wanawake.
e) Rais atatangazwa kushinda uchaguzi ikiwa atapata asilimia 50 + 1au
zaidi ya kura zote. Ikiwa hakuna mgombea aliyepata asilimia 50+1 ya
kura zote uchaguzi wa Rais utarudiwa na wagombea wawili walioongoza
kwa kura watateuliwa kuwa wagombea katika uchaguzi wa marudio wa Rais.
7. MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA:
CUF inapendekeza uwepo wa muundo wa serikali Tatu. Serikali ya Jamhuri
ya watu wa Tanganyika, serikali ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. CUF inapendekeza kuwa na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano pamoja na masuala mengine, katiba
itayokuwa na mambo muhimu yafuatayo;
a) Itamke kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni MUUNGANO wa nchi
mbili (2) zilizokuwa huru na kila nchi kuwa na mipaka yake.
b) Nchi hizo mbili zimeungana kwa mkataba wa Muungano (Articles of
Union) wa 1964 ambao ndiyo sheria mama. Katika uandikaji wa katiba
mpya Mkataba huu upitiwe upya kufikia muafaka wa mambo ya Muungano.
c) Katika Muungano huo mambo muhimu yaelezwe kama vile kutokuvunja
Muungano, kwamba kila nchi ina haki sawa kwa mambo yasiyokuwa ya
Muungano na kwamba nchi hizo mbili kila moja itakuwa na Katiba yake
ambayo itaelezea utaratibu wake wa kuendesha nchi yake kwa maslahi ya
watu wake.
d) Katiba ya Jamhuri ya Muungano ielezee vipi Serikali ya Jamhuri ya
Muungano itapatikana (Serikali Kuu, Bunge na Mahakama) na kuonesha
dhahiri kuwa serikali ya Muungano itakuwa na uwakilishi sawa wa pande
mbili za Muungano ili kuondoa manung'uniko ya upande wowote.
e) Mahakama ya Muungano itakuwa ni Mahakama ya Rufaa kama vile
ilivyokuwa mahakama ya rufaa ya Afrika Mashariki hapo zamani. Kesi
kuhusu uchaguzi wa Rais zitasikilizwa na Mahakama hii.
f) Katiba ya Jamhuri ya Muungano ielezee kuwepo kwa haki za binadamu
na namna zitakavyolindwa na kama haki hizo zikivunjwa mtu anaweza
kwenda Mahakamani kutafuta haki yake.
g) Katiba za nchi mbili hizi kila moja itaelezea utaratibu wa nchi
husika kwa kadri ambavyo wananchi wa nchi husika wanataka kuendesha
serikali zao. Ni vizuri baada ya kupitia Mkataba wa Muungano (Articles
of Union) na kukubaliana upya mambo ya Muungano, Wananchi wa Tanzania
Bara (Tanganyika) wangeandika katiba yao kuhusu mambo yasiyo ya
Muungano na Wananchi wa Zanzibar wangepitia Katiba yao kuona kama
inakidhi mahitaji ukizingatia makubaliano mapya ya mambo ya Muungano.
Baada ya kuwa na Katiba hizo mbili, ndipo Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ingeandikwa kuzingatia mambo ya Muungano yaliyokubaliwa na
pande mbili. Kwa mchakato wa sasa Zanzibar tayari ina katiba na kwa
hiyo Tanganyika itabidi kuwa na "Interim constitution" itayoelezwa
ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili Tanganyika iweze kuandaa
katiba yake au kubadili iliyokuwa ya Tanzania na kuifanya kuwa ya
Tanganyika kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Tanganyika au kwa
kadri ambavyo wananchi watapenda iwe.
h) Kwa mambo ya Muungano Katiba ya Jamhuri itatamka wazi kuwa vyombo
vya Muungano vitagawiwa kwa utaratibu utaokubalika ili kuonesha
uwakilishi wa nchi zote mbili (Zanzibar na Tanganyika). Utaratibu huo
uwekwe vizuri ili usivunjwe, na uwe ndani ya Katiba Mpya.
i) Nchi mbili hizi pale zinapozungumzia jambo la Muungano au si la
Muungano lakini Serikali ya Jamhuri inahusika, basi uwakilishi ya nchi
zote mbili katika suala hilo lazima upatikane.
j) Mhimili wenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa
shughuli za umma utakuwa ni Bunge la Muungano, Baraza la Wawakilishi
la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar;
k) Katika kutekeleza majukumu ya serikali ya Muungano vyombo vya dola
vya Muungano vitakuwa na kipaumbele cha kwanza kuliko vyombo vya dola
vinavyotekeleza mamlaka ya Tanganyika na Zanzibar; ilimradi kwamba
majukumu yaliyokabidhiwa kwa Tanganyika na Zanzibar hayatakabidhiwa na
kutekelezwa na vyombo vya dola vya serikali ya Muungano. Majukumu
yaliyokabidhiwa kwa serikali ya Muungano yanaweza kukabidhiwa kwa
vyombo vya dola vyenye mamlaka vya Tanganyika na vya Zanzibar ili
yatekelezwe na vyombo hivyo kwa niaba ya Serikali ya Muungano.
8. MAMBO YA MUUNGANO
Makubaliano/Mkataba wa Muungano(Articles of union) kwa pande zote
mbili yapitiwe upya na masuala ya Muungano yanaweza kuwa ni pamoja na:
a) Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
b) Ulinzi na Usalama;
c) Polisi
d) Uraia.
e) Uhamiaji.
f) Utumishi katika Serikali ya Muungano.
g) Mamlaka ya juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari.
h) Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote
halali (pamoja na noti) mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na
shughuli zote za kibenki, fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo
yanayohusika na fedha na mikopo ya nje.
i) Haki za Binadamu.
9. MUUNDO WA SERIKALI NA BARAZA LA MAWAZIRI
9.1. RAIS NA MADARAKA YAKE
a) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na Rais mtendaji ambaye
atachaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais na Makamu wa Rais watagombea kwa pamoja. Ikiwa Rais anatoka
upande mmoja wa Muungano Makamu wa Rais atoke upande wa pili wa
muungano.
b) Rais atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi
Mkuu.
9.2. MUUNDO WA BARAZA LA MAWAZIRI NA MADARAKA YAKE:
a) Mawaziri hawatakuwa wabunge. Watateuliwa na Rais na kuidhinishwa na
Bunge.
b) Kutakuwepo na wizara zisizozidi 15, na ikitokea Rais anataka
kuongeza wizara nyingine sharti apate ushauri na ithibati ya Bunge.
Suala la idadi ya baraza la mawaziri lisiwe utashi wa Rais
anayechaguliwa kushika nafasi hiyo pekee.
c) Wizara za Jamhuri ya Muungano ni pamoja na
i) Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
ii) Wizara ya Mambo ya Nje
iii) Wizara ya Mambo ya Ndani
iv) Wizara ya Fedha na Uchumi
v) Wizara ya Sheria na Katiba
vi) Wizara ya Utumishi wa Serikali ya Muungano
d) Wizara za Serikali za Tanganyika ni pamoja na
i) Wizara ya Fedha na Ucumi
ii) Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Misitu
iii) Wizara ya Biashara na Viwanda
iv) Wizara ya Nishati na Madini
v) Wizara ya Elimu, Michezo na Utamaduni
vi) Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
vii) Wizara ya Afya na huduma za jamii
viii) Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji
ix) Wizara ya Ajira na Hifadhi ya Jamii
x) Wizara ya Maji na Mazingira
xi) Wizara ya Miundombinu, Usafiri na Mawasiliano
xii) Wizara ya Habari na Utalii
xiii) Wizara ya Utumishi wa Serikali ya Tanganyika
(e) Waziri Mkuu haitakuwa nafasi ya kikatiba.
10. BUNGE NA MAMLAKA YAKE:
a) Bunge liwe mhimili huru wa dola na Rais asiwe sehemu ya Bunge
b) Bunge liwe chombo kikuu cha kutunga sheria. Serikali itapendekeza
sheria mpya lakini lazima zijadiliwe na kupitishwa na Bunge.
c) Kabla ya sheria kuanza kutumika itabidi ikubaliwe na Rais kwa
kuweka sahihi yake. Ikiwa Rais ataikataa sheria iliyopitishwa na
Bunge, sheria hiyo haitahitaji idhini ikiwa baada ya kurudishwa
Bungeni itaungwa mkono na theluthi 2 ya Wabunge wote.
d) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba mamlaka ya Bunge
kujadili, kubadili au kupitisha mapendekezo ya bajeti ya serikali.
Bunge lisimamie na kudhibiti mapato na matumizi ya serikali na
litafanya hivyo kwa kujadili, kupitisha au kukataa mswada wowote au
sehemu ya mswada unaohusu mambo yafuatayo:-
i. Kutoza kodi au kubadilisha kodi;
ii. Kuagiza kwamba malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na
mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au kubadilisha kiwango hicho;
iii. Kufuta au kusamehe deni lolote linalotakiwa lilipwe kwa Serikali
ya Muungano.
e) Pamoja na kazi zake nyingine zitakazotajwa katika katiba, Bunge
litakuwa pia na wajibu wa kuidhinisha uteuzi utakaofanywa na Rais kwa
vyeo vifuatavyo:-
i. Waziri au Naibu Waziri;
ii. Balozi;
iii. Gavana wa Benki Kuu;
iv. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
v. Mwanasheria Mkuu;
vi. Mkurugenzi wa Mashtaka;
vii. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
viii. Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Maadili
ix. Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ardhi
x. Makamishina wa Mamlaka zilizoundwa kwa mujibu wa sheria
xi. Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama
10.1. SPIKA NA NAIBU WA SPIKA
a) Pawepo na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na Wabunge kutoka
miongoni mwa watu wenye sifa za kuwa wabunge ambaye atakuwa ndiye
kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine
vyote nje ya Bunge;
b) Waziri, Naibu Waziri, Mbunge au mtu mwenye madaraka ya aina
nyingine yoyote itakayotajwa na Sheria itakayotugwa na Bunge hataweza
kuchaguliwa kuwa Spika. Spika hatakuwa Mbunge.
11. MAMLAKA YA MAHAKAMA;
11.1. MASHAURI YA KATIBA (MAHAKAMA YA KATIBA);
a) Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na mamlaka
ya mwanzo na ya asili kusikiliza mashauri yanayotokana na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
b) Endapo shauri la kikatiba litafunguliwa Mahakama Kuu ya Muungano
kwa mujibu wa ibara hii, mahakama hiyo itaitwa "Mahakama Maalumu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" na itakuwa na mamlaka ya
kulisikiliza na kutoa uamuzi wa usuluhishi au hukumu yenye nguvu ya
kisheria juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba au
sheria za nchi;
c) Pande zenye haki ya kufungua shauri la kikatiba mbele ya Mahakama
Maalumu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni:-
i. Serikali ya Muungano;
ii. Serikali ya Tanganyika;
iii. Serikali ya Zanzibar;
iv. Raia wa Tanzania ikiwa ni pamoja ya taasisi zenye uhai wa kisheria
ambazo pia zimesajiliwa na Watanzania na si raia wa kigeni.
11.2. MAMLAKA YA RUFAA
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na mamlaka ya
kusikiliza rufaa kutoka kwenye Mahakama Kuu ya Tanganyika na ya
Zanzibar kuhusiana na mambo yote ya Muungano isipokuwa yale ambayo ina
mamlaka ya asili na ya pekee ya kusikiliza mashauri yake kwa mara ya
kwanza. Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka masharti
kuhusu utaratibu wa kupeleka shauri mbele ya Mahakama Kuu ya Muungano
na uendeshaji wa shauri au kesi ya jinai pamoja na utaratibu wa rufaa
kwenda Makama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilimradi
kwamba sheria yoyote haitatungwa inayoweka vipengele vya kiufundi
vinavyodhoofisha au kutwaa haki ya mlalamikaji au mtuhumiwa mbele ya
sheria.
11.3. MAHAKAMA YA RUFANI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
a) Kutakuwa na Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itakayojulikana kwa kifupi kama "Mahakama ya Rufani", ambayo mamlaka
yake yatakuwa kama yatakavyoelezwa na katiba zote Tatu.
b) Mahakama ya Rufani itakuwa na mamlaka ya kusikiliza rufani yoyote
kutoka Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama
Maalumu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama kuu ya
Tanganyika na Mahakama Kuu ya Zanzibar; Kesi za kupinga matokeo ya
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano itasikilizwa moja kwa moja na
Mahakama ya Rufani.
11.4. TUME YA KUAJIRI YA MAHAKAMA YA MUUNGANO;
Kutakuwa na Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Muungano ambayo itakuwa na
mamlaka ya kuajiri watumishi wote wa mahakama za Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na pia mamlaka ya kupendekeza majina ya watu wanaostahili
kuteuliwa kushika nafasi ya jaji wa Mahakama Kuu ya Muungano na
Mahakama ya Rufani ya Muungano.
12. VYOMBO VYA DOLA VYA TANGANYIKA NA ZANZIBAR; (SERIKALI YA
TANGANYIKA NA YA ZANZIBAR)
a) Kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar ambazo zitakuwa na
mamlaka mamlaka kamili katika Tanganyika na Zanzibar juu ya mambo yote
yasiyo ya Muungano.
b) Marais wa Tanganyika na Zanzibar watachaguliwa kwa mujibu wa Katiba
ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar; Mfumo wa uchaguzi wa katiba zote
tatu ufanane. Pawepo na Rais Mtendaji Tanganyika na Zanzibar
c) Serikali za Mitaa na Halmashauri zake zitaundwa katika kila wilaya
kwa mujibu wa Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar; Kwa upande
wa Tanganyika wilaya ziundwe upya kwa kuzingatia idadi ya watu, ukubwa
wa eneo na mapato yanayoweza kukusanywa kuendesha halmashauri.
d) Baraza la Wawakilishi la Tanganyika na la Zanzibar laweza kutunga
sheria kuweka taratibu za uendeshaji wa Serikali za Mitaa na
Halmashauri zake, isipokuwa masuala yanayohusiana na Muungano
yatafanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
13. MABARAZA YA WAWAKILISHI
a) Kuwepo kwa mabaraza mawili ya wawakilishi, moja la Tanganyika na
jingine la Zanzibar ambayo yatakuwa na mamlaka ya kutunga sheria
kuhusu mambo yasiyo ya Muungano, kujadili, kusimamia na kudhibiti
shughuli za Serikali za Tanganyika na Zanzibar;
b) Mabaraza ya wawakilishi yawe na wajumbe wanaolingana na idadi ya
majimbo ya uchaguzi yatakayotangazwa na Tume za Uchaguzi za Tanganyika
na Zanzibar;
c) Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watachaguliwa kwa mujibu wa Katiba
ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar ambazo zitafuata mfumo wa uwiano
wa kura kama ilivyoelezwa kwa uchaguzi wa Wabunge wa Jamhuri ya
Muungano.
15. MADARAKA YA UMMA NA SERIKALI ZA MITAA
a) Katiba ya Tanganyika na Zanzibar itamke uwepo wa Serikali za Mitaa.
Katiba ieleze serikali za mitaa ni serikali zenye mamlaka kamili
kwenye mambo yanayosimamiwa na serikali za mitaa na hazitaingiliwa
katika maamuzi yake na serikali kuu. (TUNAPINGA KUWEPO KWA SERIKALI ZA
MAJIMBO AU KANDA)
b) Serikali za mitaa zitakuwa na vyanzo vya mapato vya kuaminika na
endelevu. Kwa upande wa Tanganyika alau asilimia 30 ya mapato ya
serikali kuu yatapelekwa katika halmashauri kwa kuzingatia uwiano wa
maendeleo.
c) Katiba ieleze kwamba serikali za mitaa zitawajibika kwanza kwa
wananchi wa eneo lao. Halmashauri za serikali za mitaa zitakuwa na
haki ya kuteua watendaji wa halmashauri zao na siyo kuteuliwa
watendaji na serikali kuu.
d) Kuwepo kwa vyombo vya serikali za mitaa katika kila wilaya na miji
na katika Jamhuri ya Muungano, ambavyo vitakuwa vya aina na majina
yatakavyowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi la
Tanganyika na la Zanzibar;
e) Baraza la Wawakilishi, litatunga sheria itakayofafanua utaratibu wa
kuanzisha vyombo vya serikali za mitaa, miundo na wajumbe wake, njia
za mapato na utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za vyombo hivyo;
f) Madhumuni ya kuwapo serikali za mitaa ni madaraka kuwa mikononi mwa
wananchi kwa hiyo vyombo vya serikali za mitaa vitaundwa na wananchi
na vitakuwa na haki na mamlaka ya kupanga mipango na shughuli za
utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla;
g) Shughuli na taratibu zote za uchaguzi wa serikali za mitaa
zitafanywa na tume ya uchaguzi ya serikali ya Tanganyika na tume ya
uchaguzi ya serikali ya Zanzibar;
h) Kila chombo cha serikali za mitaa, kwa kuzingatia masharti ya
sheria iliyokianzisha, pamoja na masuala mengine kitahusika na
shughuli zifuatazo:-
• Kutekeleza kazi za serikali za Mitaa katika eneo lake.
• Kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi.
• Kuimarisha demokrasia katika eneo lake na kuitumia demokrasia
kuharakisha maendeleo ya wananchi.
16. USIMAMIZI WA MALIASILI NA RASILIMALI ZA TAIFA:
a) Katiba itamke kuwa maliasili ya madini na raslimali zote nchini ni
mali ya umma na zitumike kwa manufaa ya Watanzania wote.
b) Bunge litapitia mikataba yote ya madini iandikwe upya ili
kuhakikisha Taifa linanufaika na raslimali za nchi.
c) Kwa kuzingatia ukubwa wa mapato ya serikali kutoka sekta ya madini
na hasa gesi, mafuta ya petroli, urani, dhahabu na mengineyo, Bunge
litatunga sheria ya kugawa moja kwa moja kwa wananchi sehemu ya mapato
hayo. Madhumuni ya utaratibu huu ni kupambana na umaskini na
kushinikiza kuwepo kwa utawala bora katika sekta ya madini. Utafiti
unaonyesha mgawo wa fedha taslimu kwa watu maskini hasa wanawake
unaboresha elimu, lishe na afya za watoto wa familia maskini. Vile
vile mgawo wa fedha unasaidia kuendeleza ujasiriamali wa wananchi
wenye biashara ndogo ndogo. Kutumia utaratibu wa malipo ya elektoniki
kupitia simu za mkononi au kadi za elektoniki kutasidia kusambaza
huduma za kibenki kwa watu maskini. Kugawa mapato kwa wananchi
kutahakikisha ushiriki wa karibu wa wananchi katika usimamizi na
utawala wa maliasili.
d) Utafutaji, uvunaji na matumizi ya maliasili utafanywa kwa uangalifu
na utalinda mazingira.
17. TUME YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
a) Maadili ya Taifa yatamkwe katika Katiba.
b) Kuwepo kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo itakuwa na
mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa
madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya katiba hii na sheria ya
maadili ya Viongozi wa umma yanazingatiwa ipasavyo;
c) Maana ya kiongozi wa umma na masharti ya maadili ya viongozi wa
umma itabidi vifasiriwe kwa mujibu wa masharti ya Katiba kuhusu
Maadili ya Taifa, masharti ya Katiba kuhusu sifa za viongozi wa umma
na masharti ya sheria ya maadili ya Viongozi wa Umma au masharti ya
sheria nyingine yoyote itakayotungwa na Bunge;
d) Tume ya Maadili itakuwa na Kamishna wa Maadili na wafanyakazi
wengine ambao idadi yao itatajwa na Sheria itakayotungwa na Bunge.
e) Bunge litatunga Sheria kufafanua na kuainisha misingi ya Maadili ya
Viongozi wa Umma itakavyozingatiwa na watu wote wanaoshika nafasi za
madaraka zitazotajwa na Bunge.
f) Misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaweza kuwa :-
i. Itafafanua nafasi za madaraka ambazo watu wenye kushika nafasi hizo
watahusika nayo;
ii. Itawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa
mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao;
iii. Itaelekeza taratibu, madaraka na desturi zitakazofuatwa ili
kuhakikisha utekelezaji wa maadili;
iv. Itapiga marufuku rushwa, ufisadi na uhujumu wa uchumi wa Taifa
katika shughuli za umma,
v. Itapiga marufuku mienendo na tabia inayopelekea kiongozi kuonekana
hana uaminifu, anapendelea au inahatarisha maslahi ya ustawi wa jamii;
vi. Itafafanua adhabu zinazoweza kutolewa kwa kuvunja misingi ya
Maadili.
vii. Itaweka masharti mengine yoyote yanayofaa au ambayo ni muhimu kwa
madhumuni ya kukuza na kudumisha uaminifu, uwazi, kutopendelea na
uadilifu katika shughuli za umma na kwa ajili ya kulinda fedha na mali
nyinginezo za umma.
g) Bunge laweza kutunga sheria itakayoweka masharti ya mtu kufukuzwa
au kuondolewa kazini kutokana na kuvunja maadili ya viongozi, bila ya
kujali kama kazi hiyo ni ya kuchaguliwa au kuteuliwa.
17. TUME YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA
a) Katiba ieleze kuwepo kwa Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na
kueleza kazi zake
b) Tume hii iwe na uhuru wa kupeleka kesi mahakamani bila idhini ya
DPP
18. MDHIBITI NA MKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI
a) Katiba ieleze kuwepo kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali
na kazi zake.
b) Ofisi ya Mdhibiti iwe huru katika kufanya kazi zake.
c) Bunge litatunga sheria kuibana serikali kutekeleza mapendekezo ya
Mdhibiti.
19. TUME YA TAIFA YA ARDHI
a) Katiba itamke kuwepo kwa Tume ya Taifa ya Ardhi itakayokuwa na
mamlaka ya usimamizi wa ardhi ya umma kwa mujibu wa sheria
itakayotungwa na Bunge.
b) Tume ya Ardhi itasimamia shughuli zote za umilikaji na ukodishaji
wa ardhi kwa mujibu wa sheria
c) Tume itaweka kumbukumbu zote za ardhi ikiwa ni pamoja na hifadhi za
taifa, ardhi ya vijiji, halmashauri, miji, manispaa, majiji na ardhi
ya serikali kuu, umilikaji na ukodishaji wa ardhi.
20. ULINZI WA TAIFA NA VYOMBO VYA DOLA
20.1. ULINZI WA TAIFA
a) Ulinzi wa Taifa ni wajibu wa kila mwananchi na utapewa kipaumbele
katika sera, sheria na shughuli za Mamlaka ya dola;
b) Mtu yeyote isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
hatakuwa na haki ya kuweka saini kwenye mkataba wa kusalimu amri au
kukubali kutekwa kwa nchi au wa sehemu yoyote ya nchi, kuridhia au
kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Tanzania;
c) Hakuna mtu au Mamlaka yoyote itakayokuwa na haki ya kuwazui raia wa
Tanzania kupigana vita dhidi ya adui yeyote anayeshambulia nchi;
d) Uhaini ni jinai kuu dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mtu
yeyote atakayepatikana na hatia ya kosa la uhaini na Mahakama Kuu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atapewa adhabu ya kifo.
e) Uhaini maana yake ni kitendo cha mtu yeyote:-
i. Kumuua, au kujaribu kumuua au kula njama ya kumua Rais wa Jamhuri
ya Muungano la Tanzania; au
ii. Kuanzisha vita au kusaidia adui katika vita dhidi ya Jamhuri ya
Muungano la Tanzania.
21. WAJIBU WA KUTII NA KULINDA KATIBA
a) Kila mtu anao wajibu wa kufuata na kutii Katiba na sheria za nchi;
b) Kila mtu anayo haki kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Katiba
kuchukua hatua za kuilinda Katiba na sheria za nchi;
c) kila mtu anayo haki ya kupinga kufutwa, kubadilishwa au kuvunjwa
kwa Katiba kinyume na utaratibu uliowekwa na Katiba yenyewe.
d) kila mtu anao wajibu wa kuiheshimu mali ya mtu mwingine, kulinda
mali asili, utajiri wa nchi, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote
inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi.
e) Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru,
amani, mamlaka na umoja wa Taifa.
HAKI SAWA KWA WOTE
Tunaomba kuwasilisha,
Prof Ibrahim Haruna Lipumba
--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 comments:
Post a Comment