Friday, 29 March 2013

[wanabidii] Neno Fupi La Usiku Huu: Mtoto Akikumwagia Bakuli La Maji Machafu...!

Ndugu zangu,


Fikiri mtu mzima unajipitia na hamsini zako ukiwa umevalia nadhifu. Ghafla anatokea mtoto wa miaka sita anakumwagia bakuli la maji machafu. Unafanyaje?


Naam, hapo ndipo mwanadamu unatakiwa utangulize hekima na busara. Maana, kwa kawaida, katika hali kama hiyo,  kwa hasira utamzabua kibao huyo mtoto.


Hapana, hupaswi kufanya hivyo hata kidogo. Unapaswa utulie kwanza kama mtu aliyemeza vipande vya barafu. Tafakari kwa kina. Utambue kuwa si bure. Huyo mtoto kuna aliyemtuma, tena si mtoto mwenziwe, bali mtu mzima kama wewe.


Na uione afadhali ya kumwagiwa bakuli la maji machafu kuliko ndoo ya matope. Jiendee zako taratibu. Na ukiweza, si vibaya ukampa pole huyo mtoto aliyekumwagia maji machafu, badala ya wewe kusubiri kupewa pole.

Na nini kingekutokea kama ungemzabua kibao  mtoto huyo?


Jibu;


Ghafla ungemwona mtu mzima mwenzako, yawezekana akawa baba wa mtoto au mama wa mtoto. Na kama ni mama atakujia huku akiwa  amejifunga kibwaya. Atakuuliza,  imekuwaje umpige mtoto wake, na pengine utalipata na tusi la nguoni.

 
Na kama wewe ni mwanamme, basi, utataka kuonyesha uwanaume wako. Eti utamzabua kibao na mama mtu. Hapo sasa watakuja watu wazima wenzako. Wanaume kama wewe. Utaishia kugalagazwa kwenye matope. Kisa? Umempiga mtoto wa watu na kumdhalilisha mke wa mtu!


Naam, yameshakuwa makubwa hayo. Utatoka hapo ukiwa umechafuliwa haswa. Kile ambacho hukukijua, ni kuwa, mtoto yule aliyekumwagia bakuli la maji machafu katumwa na mtu au watu wazima kama wewe.


Ndio, mwogope mwanadamu. Anapokutafuta atakuwekea mitego mingi. Kama wewe ni mgumu kunasa, basi, atajaribu hata mtego wa kukutumia mtoto akumwagie maji machafu.


Na mwanadamu umeumbwa ili uchafuke. Lililo baya kwa mwanadamu ni kujichafua mwenyewe, lakini, siku zote kuchafuliwa kupo. Nako kuna viwango vyake. Yumkini kila siku inayokwenda kuna mwanadamu mwenzako mahali fulani atasema neno baya la kukuchafua. Ni wanadamu wenzako wasiokutakia mema.


Unapojisikia kuna aliyekuchafua, basi, jitahidi tu upasafishe mwenyewe palipochafuka. Na kama u  raia mwema na mwenye adili, basi, jamii nayo imejaa raia wema. Watakusaidia kukusafisha.


Ni Neno Fupi La Usiku Huu.


Maggid Mjengwa,


Iringa.

http://mjengwablog.co.tz

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment