Wednesday, 30 September 2015

[wanabidii] Kosa kubwa la Chadema ni kuwanyima Watanzania uchaguzi

Kosa kubwa la Chadema ni kuwanyima Watanzania uchaguzi

KAMA kuna vitu ambavyo hata mimi mwenyewe si viamini ni kuwa wakati huu wa kampeni mimi ni mmoja wa watu tunaomkataa mgombea wa upinzani. Hili siyo tu linanishangaza lakini linanihuzunisha.

Baadhi ya wasomaji wetu wameandika kuniuliza na kunishangaa kuwa imekuwaje nimegeuka sasa nampinga mgombea wa upinzani. Baada ya miaka ya kupigia kelele mabadiliko imekuwaje sasa sijadandia treni lisilokwenda popote ambalo limeandikwa kwa nje "mabadiliko"?

Mmoja wa wasomaji hawa aliandika hivi wiki iliyopita katika hali ya kunishangaa (nimefanyia uhariri andishi hili ili liweze kusomeka vizuri gazetini): Ndugu miaka 9 imepita tangu niko shule mpaka leo najitegemea kimaisha lakini sikuona makala chovu na mfu ya kugeuka jiwe baada ya kugeukia manyang'au CCM.

Siku zote ulitupa fikra mpya za mapinduzi, ukaenda mbali zaidi kuwa CCM ishukuru Mungu inabebwa je, leo CCM imekuwa malaika? Mfumo CCM uliomtoa Magufuli ni bora na safi kuliko wa Chadema/Ukawa? Madudu ya CCM kuanzia EPA, Kagoda, Meremeta, Radar, Richmond, Deep Green, kuuza tembo na twiga, uuzaji nyumba za umma, Escrow na ushetani mwingine eti ni bora kuliko Lowassa? CCM imetufukarisha na umasikini wa kutisha kwa ufisadi na ujangili kwa maliasili zetu halafu leo umekuwa wakala wao. Tangu lini umenunuliwa? (Clara C.)

Nina uhakika wapo wengine wenye hisia kama za Clara. Jambo moja ambalo Clara labda amelifumbia macho na hakulitilia maanani na ni kweli ni kuwa mfumo uliomtoa Magufuli ndio mfumo uliomtoa Lowassa! Madudu yote ambayo anayasema yametokea Lowassa akiwa CCM na mengine yametokea akiwa Waziri Mkuu na mengine yametokea akiwa Mbunge mwenye wadhifa mkubwa tu (Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge).

Lowassa na Magufuli wote ni matokeo ya mfumo ule ule; hakuna unachoweza kukisema dhidi ya Magufuli ambacho huwezi kukisema dhidi ya Lowassa.

Suala kubwa ambalo limejitokeza na wengi wetu limetukera ni kuwa sasa hivi tunamuangalia Lowassa kwa mwanga wa Chadema/Ukawa wakati tunamwangalia Magufuli kwa mwanga wa CCM. Magufuli hajabadilika na CCM tunaijua vizuri tu. Lowassa ndio amebadilika na amebadilika baada ya kukataliwa CCM.

Hajabadilika kwa sababu alipokuwa CCM aliona mwanga akaamua kujitoa na kujiunga huku kwa ajili ya kupata nafasi ya urais. Hakujiunga na Chadema kwa sababu anaamini ajenda ya upinzani (hajawahi kujionesha kuwa anaamini wala kuonekana anaielewa). Kwa watu makini tunatambua tu kuwa kuja kwake Chadema ni kwa ajili ya njia ya kuupata urais tu; haihusiani hata kidogo na kutaka kuleta mabadiliko au nia ya kuiondoa CCM.

Bahati mbaya Clara na wengine bila ya shaka wanaamua kwa makusudi kupuuzia ukweli kuwa Lowassa alitaka kuwa Rais kupitia CCM na alikuwa tayari amepania kuwa Rais kupitia CCM, kiasi kwamba timu yake ilifikia mahali kuwapiga mkwara wajumbe wa Kamati Kuu kuwa "akikatwa" patakuwa hapatoshi na wengine walifikia mahali pa kusema "hakatwi mtu hapa".

Wengine katika kiburi chao cha ulevi wa madaraka wakafikia mahali pa kusema bila hata kuvuta pumzi "mafuriko hayazuiwi kwa mkono". Lakini Lowassa akakatwa na CCM ikabakia ilivyokuwa; waliokuwa tayari kumfuata walimfuata lakini wengine wakabakia huko huko na CCM haikuparaganyika sana kama watu walivyoaminishwa.

Kinyume chake Lowassa akaingia (baada ya wiki kama mbili za kukamilisha dili) Chadema na mfumo wa Chadema uliomuandaa Dk. Slaa kuwa mgombea wake na ukampitisha Januari na kumthibitisha Aprili (rejea maelezo ya Tundu LIssu) ukamkata mgombea wake, mtu wake na kwenda kwa haraka kumchukua Lowassa.

Simulizi ya kuwa Slaa ndiye aliyemleta Lowassa ni simulizi ya uongo kwa wale wanaojua ukweli. Slaa alitegeshwa akategeka (hili litakuwa somo la siku nyingine).

Sasa Chadema wakaenda kumchukua mwana CCM aliyekataliwa na anayekuja na madudu mengine mgongoni mwake na kumfanya mgombea wake ati kuwakilisha mabadiliko. Na kubadilika wakabadilika kweli kweli. Mwanzoni watu waliamini mabadiliko yanakuja na taasisi yaani Chama, lakini leo mabadiliko yamekuwa ni mtu – Lowassa.

Matokeo yake mpambano huu umekuwa kati ya wanaCCM wawili; ni ukweli ambao hatuutaki kwa sababu tunaamini ati mwana CCM huyu atasaidia kuivunja CCM ile! Lakini kosa kubwa ukiangalia siyo hili la kumchukua Lowassa hasa; ni kosa jingine la kimkakati ambalo ndilo litaipa CCM ushindi.

Chadema walishindwa kuwapa Watanzania uchaguzi mzuri kiasi kwamba wamewalazimisha Watanzania kuamua kuendelea na CCM kuliko kumchagua Lowassa. Lowassa anakuja kama chama cha mtu mmoja ndani ya Chadema! Ni rahisi kabisa kutabiri kuwa baada ya Lowassa kushindwa Oktoba 25, sitarajii kumuona akifanya kazi ya kuijenga upya Chadema au hata kubakia Chadema – kama hatotangaza kuachana na siasa na kustaafu kabisa.

Kosa kubwa ni kuwa kwa baadhi yetu tuliamini kabisa kuwa CCM ingeweza kuondoka mwaka huu kwa njia rahisi kabisa – siyo ngumu ambayo Chadema wameilazimisha. Kwamba ungekuwa ni uchaguzi wa pande tatu. Mgombea wa CCM, mgombea wa Chadema/Ukawa na Lowassa.

Baadhi yetu tulijua ni lazima Lowassa akatwe CCM kwani tishio lake kwa CCM lilitakiwa kujibiwa kwa sababu hakukuwa na jinsi ya Lowassa kuweza kuwa mgombea wa CCM baada ya madudu yote
yaliyotokea tangu wakati wa kutangaza nia na miaka kabla ya mwaka huu wa uchaguzi.

 Lowassa alikuwa ni tishio lenye mgogoro kwa CCM kiasi kwamba kwa Kamati Kuu kumpitisha ingekuwa ni kukivunja chama rasmi. Ilikuwa ni rahisi zaidi kumkata jina lake na kuishi na matokeo ya hilo kuliko kumpitisha kuwa mgombea wa urais na kuishi na matokeo ya hilo.

Lowassa angeenda chama kingine tu; kiu yake na kupania kwake kuwa Rais wa Tanzania kulikuwa na nguvu kubwa kwake na kwa wanufaika wenye kumuunga mkono kiasi kwamba wazo la kuwa angeamua kuachana na kuutaka urais halikuwepo. Lowassa kwa namna moja au nyingine alikuwa ni lazima agombee, ama CCM, au chama kingine.

Kitu pekee ambacho wengi hatukukifikiria ni kuwa angekuja kugombea Chadema. Baadhi yetu tuliona kuwa njia pekee ya kimantiki kwa Lowassa kugombea ni kwenda kujiunga na Chama cha ACT; kwa sababu ACT ilihitaji mgombea mwenye nguvu kwenye urais ili kukipa chama nafasi katika ubunge. Hatukudhania katika miaka milioni moja kuwa Lowassa angeenda Chadema.

Kitu ambacho hatukukijua wakati wote huu ni kuwa mazungumzo ya Mbowe na Lowassa yalikuwa yameanza tangu 2011, yakienda kwa siri nyuma ya Katibu Mkuu wa Chadema. Mbowe na Lowassa walishakubaliana (ukiamini ushahidi ulioko wazi sasa) kuwa endapo angekatwa CCM basi Chadema kulikuwa na nafasi.

Kama Lowassa angeenda ACT, Slaa akasimama na Chadema/ Ukawa na CCM ingempitisha yeyote yule (Magufuli au mwingine) basi Dk. Slaa alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kuliko mtu mwingine yeyote na CCM ingepoteza siyo tu urais lakini hata Bunge kwa kiasi kikubwa kwa sababu ujumbe wa Chadema na Slaa ungekuwa wazi zaidi, wenye kuthubutu zaidi na wenye kuakisi hasa kiu ya mabadiliko ya nchi yetu.

CCM wangegawanyika – tena wangegawanyika vizuri (a clean cut) kwamba wenye kumuunga mkono Lowassa wangeenda naye kokote (kumbuka walisema "Ulipo Tupo"). Hata lile la wabunge wengine na viongozi wengi wa CCM kuhama lingetokea.

Tatizo ni kuwa kwenda kwake Chadema kumewakwaza hata wale waliokuwa wanataka kumfuata; wangeanzia wapi kwenda Chadema wakati Chadema ndio mpinzani mkuu wa CCM?

Hapa ndipo kosa la Chadema lilipotokea; kuwanyima Watanzania uchaguzi wa mtu anayestahili na badala yake kuwarudishia mwana CCM mwingine halafu na kuwataka watu kama mimi kuunga mkono? Tuanzie wapi? Tunaambiwa "mabadiliko" tunauliza "yapi?" tunaambiwa "tutajua baadaye"! Na watu wanatushangaa kwa nini hatudandii hili treni lisiloenda popote.

Ni uamuzi ambao kwa kweli unatushangaza wengi wetu kwamba pamoja na kiu yetu ya mabadiliko hatuko tayari kuuza nafsi na dhamira zetu kuushabikia uongo na ulaghai kwa kisingizio cha kutaka mabadiliko. Safari hii ndugu zangu siyo CCM waliovuruga harakati za upinzani; siyo CCM waliochakachua upigaji kura; safari hii mzigo huu wanabeba viongozi wa Chadema.

Na sisi wengine hatuna budi kuwapinga na hatutashangaa hawa hawa viongozi wenyewe wa upinzani walioshabikia hadharani ujio wa Lowassa wataadhibiwa na wanaChadema majimboni mwao (wakiungana na wanaCCM) ili wasirudi tena kama wabunge.

Hili likitokea watu wasishangae kwa sababu Watanzania wengi wamekwazika na kilichotokea; kwani hata wana CCM waliokuwa tayari kumchagua mtu kutoka upinzani sasa wamekereka na wameamua kubakia na mtu wao.

Wenyewe wanasema "hapa kazi tu"; wakati watu wanaotaka mabadiliko wao wanasema "Hapa Lowassa tu". Kwa wengine huu wala siyo uchaguzi mgumu kivile.

Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment