Friday 18 October 2013

[wanabidii] Tujiulize, Katiba tiba ya maadili yetu?

Na January Makamba

Tujiulize, Katiba tiba ya maadili yetu?


Mwaka 1986, nikiwa na umri wa miaka 12, nilipanga mstari nje ya ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga nikiwa sehemu ya wananchi wengi waliofurika kwenye ofisi hiyo, majira ya jioni.

Wote tulikuwa tukisubiri ugeni mkubwa uliongia kwenye mji wetu mdogo wa Lushoto. Wakati giza linakaribia kuingia, mgeni wetu akaingia na msafara mdogo, akateremka akiwa ameshika fimbo mkononi. Mwili ukanisisimka!

Ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kumwona Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa karibu.

Msisimko ule ulibaki nami kuanzia siku ile na nikapata hamu ya kumfahamu zaidi. Taswira niliyopata ni kwamba alikuwa mtu wa ajabu, mtu mwenye sifa za ziada.

Kadri miaka ilivyokuwa inaenda, taswira sahihi ya Mwalimu iliibuka: Kwamba ni kweli alikuwa mtu wa ajabu kwa maana ya kwamba aliijenga nchi yetu katika taswira yake, kwamba alijulikana na kuheshimika dunia nzima.

Kwamba, aliwapenda watu wake, lakini hakuwa malaika kwani alifanya makosa na hakufanikiwa katika yote aliyotaka yatokee.

Pia, kwamba miujiza ya kifimbo haikuwa ya kweli, bali tuliamini na kuaminishwa hivyo kwa sababu sisi wenyewe tulitaka kumweka juu ya uwezo wa binadamu wa kawaida. 

Takriban asilimia 68 ya Watanzania wamezaliwa baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka madarakani na pengine asilimia 44 baada ya kuwa ameshafariki dunia. Hata hivyo, kwetu sote bado yu hai, siyo kwa sababu tunaona picha zake, bali kwa sababu kwa kila jema tunalotaka kulitengeneza tunamtaja na kwa kila baya tunalotaka kulikemea pia tunamtaja.

Kwa sasa tunatengeneza Katiba Mpya ya Tanzania, lakini sijasikia sana tukimtaja Mwalimu na kukumbuka wasia wake wakati huu tunapojadili jambo hili kubwa.

Ningependa nitumie fursa hii kuukumbuka wosia wa Mwalimu ili utuongoze kwenye jambo hili adhimu. Wakati wa uhai wake, Tanzania ilitengeneza Katiba Mpya tano; 1961, 1962, 1964, 1965 na 1977 - na Zanzibar mara mbili na kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya sasa (ya mwaka 1977) mara 13.

Mabadiliko yote haya yalikuwa ni katika jitihada za kuijenga Tanzania njema zaidi – kama ilivyo dhamira ya Rais Jakaya Kikwete alipoanzisha mchakato huu wa sasa. Katika nyakati zote hizi, Mwalimu alisema mambo kadhaa ambayo yanaweza kutuongoza kwa sasa.

Nataka niwakumbushe hotuba yake ya Juni 28, 1962 ndani ya bunge akijadili pendekezo la Serikali la kuunda Jamhuri ya Tanganyika, ambapo mezani kulikuwa na rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Tanganyika.

Mwalimu alieleza kwamba ulinzi wa haki za wananchi, ulinzi wa uhuru wa wananchi, ulinzi wa urithi wa taifa, ulinzi wa thamani ya mtu na vitu wanavyovithamini, haupatikani kwenye Katiba, bali kwenye misingi na maadili ya taifa (national ethics).

Katiba haizuii vitu viovu kufanyika, bali maadili ya taifa ndiyo msingi wa makatazo yote-kwamba makatazo ya mambo maovu yaanzie ndani ya damu na nyoyo zetu, ndani ya asili yetu, kwamba ifike pahala kwamba jambo hili au lile Watanzania wasikubali lifanyike siyo tu kwa sababu limeorodheshwa kama katazo kwenye Katiba bali kwa sababu siyo asili ya Utanzania, siyo sehemu ya maadili yetu.

Mjadala wa sasa wa Katiba Mpya umejikita zaidi kwenye kuorodhesha makatazo yanayopaswa kuingia kwenye Katiba, kana kwamba Katiba ndiyo itaunda hulka, utashi na maadili. 

Hulka ya uchapakazi hailetwi na Katiba, hulka ya udokozi haiponywi na Katiba – bali na maadili ya kitaifa. Binafsi, naamini kwamba tuwe na mjadala wa aina hii na mjadala wa aina hii hauanzii kwenye majukwaa ya siasa, bali ndani ya familia.

Tujiulize, vijana wa sasa au wazee wa sasa, wanaishi kama alivyoishi yeye? Kilele cha mafanikio ya mwanadamu yeyote ni kuendelea kuwa hai mara baada ya kufariki – kwa kuacha kumbukumbu ya mambo mema ambayo hayafutiki wala kusahaulika, kwa Kiingereza wanasema 'immortality'.

Kupitia uongozi wake, wosia wake, maandiko yake, lakini hasa kwa kuitazama taswira ya Tanzania, Mwalimu bado yu hai. Uamuzi wa kumuua utakuwa wa kwetu sisi wenyewe tuliobaki. 

January Makamba ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment