Tuesday 29 October 2013

[wanabidii] Taarifa ya Wakala wa Majengo ya wa kujenga ofisi za Serikali kupunguza matumizi

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ulianzishwa chini ya sheria Na. 30 ya mwaka 1997 kutokana na iliyokuwa idara ya Majengo chini ya Wizara ya Ujenzi.  Madhumuni ya kuanzishwa kwa Wakala wa Majengo ni kuboresha huduma zilizokuwa zikitolewa na iliyokuwa idara ya majengo kwa kutumia rasilimali kutokana na majengo yenyewe bila kutoka Serikalini/Hazina hatimaye kuchangia ukuaji wa uchumi kwa kupunguza gharama za uendeshaji  serikalini upande wa sekta ya majengo.

Wakala wa Majengo unafanya utafiti kubaini gharama zinazotumika kama kodi ya pango katika ofisi za serikali ili kuhakikisha 
Serikali inaokoa fedha kutoka katika Wizara na Taasisi ambazo zinapanga aidha kwa watu binafsi au mashirika. Katika utafiti unaoendelea imebainika kuwa, Serikali inatumia fedha nyingi katika kodi ya pango katika taasis zake.

Kama ilivyoelekezwa kupitia Sheria ya Wakala (Executive Agency Act) namba 30 ya 1997, TBA imekasimiwa jukumu kubwa la kuhakikisha Serikali na Taasisi zake zinapata ofisi pamoja na kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanapatiwa makazi yaliyo bora na salama. Katika kuondoa tatizo la uhaba wa Ofisi kwa serikali, Wakala umeamua kutafuta ufumbuzi kwa kujenga majengo ya ofisi katika mikoa mbalimbali ambayo yatajulikana kama "TBA Towers".

Majengo haya kwa kuanzia, yatajengwa katika "yard" za Ujenzi zilizopo katika mikoa saba ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Mtwara, Arusha na Tanga.

Mkakati huu utaiwezesha Serikali kupunguza kutumia gharama kubwa katika upangishaji wa ofisi na badala yake fedha hizo zitumike katika maeneo mengine yenye manufaa kwa jamii na uhitaji mkubwa kama vile afya, elimu, Jeshi n.k.

Kama tulivyoeleza awali, dhumuni kuu la mradi huu ni kuipatia ofisi za kudumu Serikali na taasisi zake.
Upangishwaji wa kila jengo utagusa maeneo manne katika utaratibu ufuatao:-
  • Eneo la kwanza litalenga  watu binafsi ambao watapangishwa kwa kodi ya soko ili kuiongezea TBA kipato na kuuwezesha Wakala kujenga majengo mengine kwa kipindi kifupi pamoja na ukarabati wa majengo hayo pale inapobidi,
  • Maeneo mengine mawili  yatalenga  kuzipangisha maeneo ya ofisi Wizara za Serikali pamoja  na Taasisi zake kwa gharama nafuu na;
  • Sehemu ya nne ambayo ni ya mwisho itatengwa maalum kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Ujenzi na taasis zake ambazo awali zilikuwa zikitumia 'yard' hizo.

Manufaa ya mradi huu ni kama ifuatavyo:
  • Wizara, Idara na Taasis za Serikali (MDAs) kupata maeneo/nafasi za ofisi zenye uhakika, zilizo bora na salama kwa gharama nafuu.
  • Maendelezo ya maeneo yaliyochakaa au yaliyoachwa kwa muda mrefu na hivyo kupendezesha miji yetu.
  • Kubadilisha sura ya "Ujenzi yard" kwani sasa zipo katika hali mbaya inayoleta picha mbaya kwa Serikali
  • Kuifanya Serikali na taasisi zake kufanya kazi bila kusumbuliwa na wenye majengo kama ambavyo wamekuwa wakisumbuliwa wakiwa wapangaji katika majengo ya mashirika na watu binafsi.
  • Kuiongezea Serikali mali (asset) isiyohamishika na yenye hadhi.
  • Kuimarisha usalama wa mali na nyaraka za serikali kwa kuondoa adha ya kuhama hama kila wakati.
  • Kupitia mradi huu Wataalam  wa  TBA watajengewa uwezo kitaaluma kwa kutumia vitendea kazi vya kisasa  na pia kuboresha masilahi yao kwa upande wa vipato vyao kwa mfano mishahara, posho mbalimbali n.k

Upatikanaji wa fedha za mradi huu
Kulingana na ufinyu wa bajeti, TBA inatarajia kutekeleza mradi huu kwa njia ya mkopo kutoka katika Taasisi mbalimbali za fedha pamoja na kushirikiana na wawekezaji katika sekta ya miliki (real estate developers).
Hadi sasa, TBA tayari imeishafanya mazungumzo na baadhi ya taasis za fedha zilizopo ndani ya nchi ili kuweza kupata fedha ambazo zitasaidia kuendeleza mradi huu.
Aidha, TBA inaendelea na Mazungumzo na wawekezaji mbalimbali ambao wameonyesha nia ya kutaka kushirikiana na Wakala katika kuwekeza kwenye baadhi ya ujenzi wa majengo hayo.

Teknologia itakayotumika na faida zake
Majengo haya yanatarajiwa kujengwa kwa kutumia teknolojia ya 'Tunnel Form work system' ambayo imethibitika kuwa ni ya haraka na nafuu zaidi ukilinganisha na Ujenzi wa kawaida (conversional method system).
Teknolojia hii, ili iweze kufanya kazi kwa uhakika inahitaji nidhamu ya hali ya juu katika utekelezaji wa ujenzi hivyo, TBA kwa kuzingatia hilo imeamua kuzishirikisha taasisi nyingine za Serikali ambazo ni JWTZ (Suma – JKT) Polisi, Magereza, na TBA Brigedi.

TBA ilifikiria umuhimu wa kushirikisha vikosi hivi vya Serikali kwa sababu zifuatazo:-
  • Kusaidia teknologia hii kubaki nchini kwa kuhakikisha wataalam kutoka taasisi za Serikali wanaipata na kuifahamu; kwani watu binafsi ambao hufanya biashara; ni rahisi kuitelekeza teknolojia hiyo iwapo wataona imeibuka biashara nyingine inayolipa zaidi kuliko teknolojia hii/ujenzi au wanaweza kuipeleka teknolojia hii katika nchi nyingine bila kujali  umuhimu wake kwa taifa letu.
  • Vyombo hivi huweza kufanya kazi mbalimbali za Serikali hata kama kuna wakati Serikali inakuwa haina fedha za kulipa kwa wakati.
  • Kuongeza umoja na ushirikiano miongoni mwa/baina ya taasisi mbalimbali za umma,
  • Taasisi hizi zina rasilimali watu wa kutosha kufanya kazi zinazotakiwa kutekelezwa.

Kwa kuhitimisha TBA inapenda kutoa shukrani kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkiuonyesha hususan katika utoaji wa taarifa kwa umma.Tunaamini mtaendelea kutumia kalamu zenu katika kuelimisha na hata kuutaarifu umma wa Watanzania mambo mbalimbali mazuri yanayofanywa na serikali yao.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment