Sunday, 25 September 2016

[wanabidii] Magufuli unasubiri nini kuvaa sura ya Putin?

MASIKINI au tajiri wote ni binadamu waliozaliwa na jinsia ya kiume na kike hakuna ambaye ana uthibitisho juu ya umaskini au utajiri. Hii inamaanisha leo unaweza kuwa tajiri ila kesho ukawa masikini, lakini pia kuzaliwa masikini sio sababu kwamba utakufa masikini, kwani kila kitu duniani ni maamuzi yaliyo ndani ya kuishi kwako.
Natamani kuona Rais Magufuli anavaa sura ya Rais wa Russia, Vladimir Putin lakini kuna kitu kinaniambia Putin kwa watu wake wengi wanaamini ni kiumbe asiezeeka na umri kwake hausogei (immortal). Ila leo namuona Rais Magufuli tofauti na Magufuli wa mwaka 2010 tayari anaonekana uzee unamkaribia kwa kasi.
Utofauti wa Magufuli na Putin ni miaka 7 – Rais Magufuli kazaliwa mwaka 1959, Vladimir Putin yeye alizaliwa mwaka 1952.  Hawa wote wawili walikuwa watu katika maisha yao ambao hawakufikiria hata siku moja kuwa maraisi kwenye nchi zao au kuwa wanasiasa wakubwa duniani, wakati Magufuli ni mwalimu wa Hesabu na Kemia, Vladimir Putin alikuwa ana ndoto za kuwa Rubani wa Ndege, huku akisoma sheria na kuwa mwana usalama wa Nchi hiyo (KGB).
Putin na John Magufuli walikua na utofauti sana na familia ya Bush au Omar Bongo na Ali Bongo wa Gabon. Kila nikimuona Magufuli na Vladimir Putin wote ni watu wasiopenda sana ubepari. Nakumbuka wakati wa uzinduzi wa fly-over ya Tazara Rais Magufuli hakusita kusema juu ya misaada yenye unafuu na kuisifia nchi ya Japan. Hii ilikuwa ni taswira ya kutosha juu ya hofu ya serikali na namna mahusiano ya kibepari na misaada yenye masharti magumu inayozikwamisha nchi nyingi za Kiafrika.
Lakini sura ya Putin tunaweza kuianza kipindi cha mwaka 1996 na 1999, ikiwa ni kipindi cha pili cha utawala wa Boris Yeltsin. Kipindi hiki kilikuwa cha majanga makubwa nchini Urusi kwani rasilimali zilishikiliwa na mabepari wachache alimaarufu "The Oligarchies", wakati idadi kubwa ya watu Urusi wakiishi katika dimbwi zito la umaskini.
Hali hii ilisababishwa na rais Boris kukumbatia wafanyabiashara wakubwa waliopata mali kwa njia za kifisadi na kukwepa kodi iliyopelekea kufilisi uchumi wa nchi kwa kujilimbikizia mali kwenye mabenki ya ughaibuni.
Mwishoni mwa mwaka 1998, Yeltsin alikuwa na afya mbaya hivyo ililazimika kuandaa mapema mtu atakayerithi nafasi yake kwa masharti ya kumhakikishia Yeltsin usalama atakapostaafu na kulinda maslahi ya mafisadi wake.
Jukumu halikuwa dogo maana aliyewahi kuwa waziri wake mkuu Yevgeny Primakov alionesha nia ya kugombea  na alikuwa akiungwa mkono sana na wananchi wa Urusi kwa sera zake za kupinga ufisadi ili kuleta Urusi mpya tofauti na ile ya Boris.
Ili kumdhohofisha Yevgeny Primakov, Yeltsin na wafuasi wake wakiongozwa na mshauri wa karibu wa rais, Boris Berezovsky, walisuka mpango madhubuti kumuondoa kwenye ramani ya siasa za Urusi.
Kwanza walimtafutia skendo mbaya Primakov, pili Yeltsin akamteua Vladimir Putin kuwa Waziri mkuu. Ikumbukwe Putin alikua mtu asiyefahamika kabisa kwenye siasa za Urusi kwani alikuwa ni afisa usalama wa urusi (KGB) lakini pia hapa kwetu mwaka 1995 hakuna Mtanzania aliekuwa anamjua John Pombe Magufuli zaidi ya majirani zake wa Chato na wanafunzi aliosoma nao.
Kipindi cha mwaka 1995 alikuwa anafahamika Jakaya Kikwete na Edward Lowasa ambao mpaka sasa wanaushawishi mkubwa kwenye siasa zetu. Jicho la Mkapa lilitosha kumuona Magufuli na kumuamini kama ambavyo Yeltsin alivyomuona Putin.
Wakati Vladimir Putin anapata ile nafasi ilikuwa ni lengo la Rais Yeltsin ili nafasi ile iwe chachu ya kumpa umaarufu wa kisiasa Vladimir Putin, pili amlinde Boris na wafuasi wake mara tu atakapo kuwa Rais wa Russia.
Baada ya muda mfupi Yeltsin alikasimu madaraka ya uraisi kwa Putin, baada ya yeye kujiuzulu rasmi Desemba 1999. Putin alijizolea umaarufu mkubwa baada ya kufanikiwa kumaliza propaganda ya vita vya Chechnia na akafanikiwa kujulikana ndani Urusi na wakati huo dunia ilianza kumtambua Putin ni mtu wa aina gani.
Wakati wa uchaguzi nchini Russia Yeltsin na washirika wake walitumia pesa nyingi ili kuhakikisha Vladimir Putin anashinda kiti cha urais na walifanikiwa adhima yao na Putin kushinda kiti cha Uraisi mnamo mwaka 2000.
Baada ya Putin kuwa Rais, ilitarajiwa Yeltsin na wafuasi wake wangeendelea kupeta kwa ufisadi wao. Lakini haikuwa hivyo, kwani Putin aliwageuka mafisadi wote na akaanza kuwasaka mmoja mmoja na kuwashitaki kwa ufisadi na ukwepaji mkubwa wa kodi.
Hapo ndipo maisha ya mabilionaea mafisadi  yakawa magumu, wengi walifungwa na kunyang'anywa biashara zao, wakati wengine iliwalazimu kukimbia nchi, watu kama Roman Abromivich, Boris Berezovsky na Vladimir Gusinksky ni baadhi tu ya waliokimbia nchi na kuishi uhamishoni mpaka leo hii kwa kukwepa mkono wa sheria.
Sote tunaweza kuwa na macho ila inawezekana macho yetu yasiwe na nguvu ya kuona ila kama yanaona basi kuna kila haja Rais Magufuli avae sura ya Putin kama kweli anataka kuujenga uchumi wa Tanzania maana baada ya Putin kuwa Rais kwa miaka nane (8) mfululizo uchumi ulikua kwa kasi sana.
Leo Roman Abromivich, Boris Berezovsky na Vladimir Gusinksky wanakimbia nchini kwao kwa kukwepa kodi watu ambao nchi iliwabeba kwa kipindi chote cha Rais Yeltsin sina shaka ni sawa na matajiri wetu leo ni wengi mfumo wa nchi uliwabeba kwa kipindi kirefu wakiishi kama malaika na kukwepa kodi ambazo zingesaidia maendeleo ya nchi na kukuza uchumi.
Kuna muda Mtanzania anaogopa athari ya tajiri kukimbia nchi, lakini Putin aliweza kugeuka na kuwafunga matajiri wakwepa kodi. Magufuli unasubiri nini kuvaa sura ya Putin.
Nchi yetu bado ina uchumi unaokua kwa sasa hatuna budi kuhangaika na mabepari wakubwa, Nchi inahitajika kujenga mahusiano ya kibepari na nchi ambazo zina uchumi wa kibepari unaokua hii inasaidia sana kupunguza misaada yenye masharti magumu ambayo kwa kiasi kikubwa ndio Chanzo cha kuzalisha mabepari wakwepa kodi.
Ni hatari kubwa sana kwa taifa kuruhusu mkwepa kodi akatawala siasa na uchumi wa nchi. Magufuli vaa sura ya Vladimir Putin itakusaidia sana kufikia Tanzania ya viwanda.


Chanzo Rai

0 comments:

Post a Comment