KATIKA sehemu ya pili ya makala haya wiki iliyopita, tuliona jinsi Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, alivyoyakoroga kwa kile kilichoonekana kuwa uchu wa madaraka kwa kujiona ndiye mrithi mtarajwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akasahau na kutelekeza majukumu yake Zanzibar: kibarua chake kikaanza kuingia dosari uwanja kuota mbigili na kuzua mtafaruku wa kisiasa, Bara na Visiwani.
Tuliona pia jamii ya Kizanzibari ilivyogawanyika kisiasa juu ya suala la Muungano kumuweka Jumbe njia panda, huku akionekana dhahiri kuzusha ghadhabu ya Nyerere juu ya jambo hilo. Je, nini kilitokea?.
Jumbe amshikia gobole Nyerere
Ziara za Jumbe mikoa yote ya Tanzania Bara zilikuwa na lengo la kujikweza ili kujiweka karibu na umma wa Tanzania Bara kama alivyokuwa Visiwani. Hotuba zake ndefu juu ya Umoja na Mshikamano zililenga kumwonesha kama kiongozi ajaye asiye na makuu.
Lakini kilichomshtua zaidi Mwalimu ni harakati za Jumbe za kuwaunganisha Waislamu wote nchini kwa njia ya kufadhili misikiti (kutoka nje), akiwahimiza wajitambue katika mazingira yao "ndani ya Taifa". Kwa kushtushwa na hilo, Ikulu ilitoa waraka mkali kuwakumbusha na kuwaonya viongozi wote kwamba nchi haina dini; lakini Jumbe hakujali, aliendelea kivyake.
Wakati waraka wa Ikulu ukitolewa, Mwalimu alikuwa amekwishasoma nia ya Jumbe na kumuona kama mtu aliyepoteza dira ya uongozi isipokuwa hamu ya maendeleo binafsi na kujitajirisha. Alielewa pia kuwa Jumbe alikosa mvuto visiwani kutokana na udikteta wake na kuifarakanisha jamii ya kizanzibari kisiasa (Wanamapinduzi na Wanamstari wa Mbele) pamoja na kuitelekeza akifukuzia urais wa Muungano kwa gharama ya Wazanzibari. Kwa hayo pekee, ilikuwa rahisi kumtungua.
Mapema mwaka 1983, Rais Nyerere alimteua aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Edward Moringe Sokoine, kuwa Waziri Mkuu. Sokoine alikuwa mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno mengi.
Baada ya miezi michache tu, jina la Sokoine liling'ara miongoni mwa umma wa Kitanzania, akashangiliwa na kuimbwa nchi nzima kama mtetezi na mkombozi wa wanyonge, "ishara ya Rais ajaye". Nyerere akayapata haya na akawadokeza wasiri wake wa karibu juu ya kumkubali Sokoine na nia yake ya kumwachia kiti mwaka 1985.
Jumbe naye akanusa habari hizo kwa mkonga wa pembeni; uhasama na vita kati yake na Nyerere ukaanza kwa Jumbe kushika "gobole" kutaka kumuumbua Nyerere.
Akihutubia kwenye kilele cha sherehe za miaka 20 ya Mapinduzi Visiwani mbele ya Mwalimu Nyerere, Januari 12, 1984; Jumbe aliwaambia Wazanzibari kwamba aliyajua vyema malalamiko yao juu ya kutoridhishwa na jinsi Muungano ulivyoendeshwa; akawaomba wasisikitike ila wamwachie yeye.
Alisema, Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inatoa utaratibu wa kusuluhisha migogoro na kero za Muungano kwa njia ya Mahakama Maalum ya Kikatiba. Hakusema kama alikusudia kutumia njia hiyo au la.
Ghafla, Nyerere alisimama kuzungumza bila kukaribishwa huku ghadhabu ikisomeka dhahiri juu ya paji la uso wake; akalaani wote waliokusudia kupandikiza chuki na kuleta machafuko visiwani, na kwamba hatua kali zingechukuliwa dhidi yao. Jumbe hakujibu hotuba ya Mwalimu.
Ndani ya wiki hiyo, Jumbe, kwa kumtumia Bashir Swanzy, na pengine kwa kumshirikisha pia Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wa zamani kabla ya Jaji Lubuva, Wolfang Dourado; aliandaa "mashitaka" kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Baraza la Mapinduzi dhidi ya serikali (Utawala) ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Tanganyika.
Japo hati hiyo yenye kurasa 100 (wengine wameniambia ni kurasa 89) inaweza kuitwa kama barua ndefu ya madai badala ya mashitaka; lakini kiuhalisia lilikuwa ni kusudio thabiti la kufikisha shauri hilo mahakamani kama wadaiwa hawakutekeleza yaliyomo.
Dai hilo lilisomeka, pamoja na mambo mengine, ifuatavyo: "Tafadhali fahamu kuwa, na taarifa inatolewa hapa rasmi; kwamba, ila kama tu madai haya yatamalizwa kwa maelewano, na kama tu Tume ya Katiba iliyopendekezwa hapo juu itateuliwa haraka ndani ya muda mwafaka, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kutumia mamlaka ya Mahakama Maalum ya Katiba kama inavyoainishwa kwenye Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977,kupata ufumbuzi wa mgogoro huu".
Kwa manufaa ya wasomaji wangu, ibara ya 126 (1) ya Katiba ya Muungano inatamka kuwa, "Kazi pekee ya Mahakama hii ni kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake, kutoa uamuzi wa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba hii iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar".
Yafuatayo ndiyo yalikuwa malalamiko ya Jumbe kwenye Hati hiyo: Kwanza, kwamba Mkataba wa Muungano wa mwaka 1964 unaanzisha Shirikisho lenye Serikali Tatu na si Mbili wala Moja. Pili, kwamba Mkataba wa Muungano (Articles of Union) haukufuta Serikali ya Tanganyika wala Katiba yake; bali ni Sheria ya Bunge
Namba 22 ya 1964 iliyoridhia Mkataba wa Muungano ndiyo iliyofanya hivyo ki-imla.
Tatu, kwamba mambo ya Tanganyika hayakupaswa kuwekwa mikononi mwa Serikali ya Muungano kama Tanganyika haikuwepo, na akawatuhumu Viongozi wa Tanganyika kwa kufuta Serikali ya Tanganyika kinyemela na hila dhidi ya Zanzibar.
Nne, alimtuhumu Rais Nyerere kwa kushindwa kuteua Tume ya Kupendekeza Katiba na kwa kutoitisha Mkutano wa Katiba wa kupitisha Katiba, kama ilivyoelekezwa kwenye Mkataba wa Muungano.
Tano; kwamba, Tume ya Katiba haikuteuliwa kupitisha Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977 na kwa sababu hiyo, Katiba hiyo inakosa uhalali na akataka Tume iteuliwe haraka na ndani ya muda mwafaka. Na Sita; kwamba, kuingizwa kwa dhana ya Chama kimoja na kwa Katiba ya TANU kwenye Katiba ya Mpito ya mwaka 1965, ilikuwa hatua haramu na kinyume cha matakwa ya Mkataba wa Muungano kwa kuwa vyama vya siasa halikuwa jambo la Muungano, hata kama TANU na ASP viliungana kuunda CCM.
Hati yapotea kimiujiza
Wakati madai ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar dhidi ya serikali ya Muungano na dhidi ya Rais Nyerere yakiandaliwa; vivyo hivyo maandalizi ya kesi na ukusanyaji wa vielelezo kwa ajili ya kupeleka Mahakamani yalikuwa yakiendelea endapo serikali ya Muungano na Nyerere wangeshindwa kusalimu amri kwa "shinikizo" la Jumbe.
Wakati huohuo, tayari chama kilikuwa kimenusa mapishi ya Jumbe; na lo, tazama; Hati ya madai yake ilipotea mezani katika mazingira ya kutatanisha kabla hajaitia saini na baadaye kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere.
Haraka haraka, kikao cha dharura cha NEC kikaitishwa mjini Dodoma, Januari 24, 1964 kujadili "uhaini" wa Jumbe; hali "ya hatari" na ya "kuchafuka kwa hali ya hewa" kisiasa Visiwani ikatangazwa na ulinzi kuimarishwa.
Mimi nilishuhudia hali hiyo tete nikiwa sehemu ya "ujumbe" wa "vijana" kutoka Bara waliokwenda Visiwani kusaidia kushusha munkari na "mihemko" ya Wazanzibari kwa nguvu ya hoja. Swali gumu lililoulizwa ni, "kwa nini Serikali ya Watanganyika (na Chama) imemteka na kumtia kizuizini Bara, Rais (wao) aliyechaguliwa na Wazanzibari kwa mujibu wa Katiba yao?".
Bado ni kitendawili kuhusu namna na nani aliyehusika na kutoweka kwa Hati ya "mashitaka" ya Jumbe mezani na kumfikia Mwalimu. Lakini mtu anayetajwa mara kwa mara ni Maalim Seif Sharrif Hamad kwa kushirikiana na vyombo vya usalama wa nchi.
Ofisa Usalama mmoja mwandamizi wa enzi hizo (jina tunalo) ambaye amekiri kwa mwandishi wa makala haya kuhusika na tukio hilo, ameeleza jinsi alivyoinyaka hati hiyo kwa kumshirikisha Maalim Seif, kutoka kwenye "mikoba" ya Jumbe ingali na marekebisho madogo kwa mkono wake kabla ya kuchapwa kama nakala ya mwisho na kumfikishia aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Moringe Sokoine na hatimaye kwa Mwalimu aliyeagiza kuitishwa hima kikao cha dharura cha NEC kumhukumu Jumbe.
Jumbe mbele ya Pilato
Mashitaka dhidi ya Jumbe mbele ya NEC yalikuwa mafupi na thabiti: Kwanza, alituhumiwa kwa usaliti kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano aliyoapa kuilinda na kuitetea; pili, kushirikiana na nguvu ya taifa la kigeni (Swanzy) kuhatarisha usalama wa nchi; tatu, kudhalilisha nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, ukuu wa chama tawala na uchu wa madaraka; na nne, kuhoji bila uhalali wowote, uwapo na uhalali wa Muungano alioapa kuutumikia na kuulinda.
Nafasi ilipotolewa kwa wajumbe wa NEC kujadili; wa kwanza kushika kipaza sauti alikuwa Maalim Seif Sharrif Hamad aliyemtuhumu Jumbe kwa uchochezi na kwa kuwahamasisha Wazanzibari kuhoji uhalali wa Muungano, kudhalilisha ukuu wa hama na kutetea bila uhalali Muungano aina ya Shirikisho lenye serikali tatu.
"Ndugu Mwenyekiti, vitendo hivi ni kinyume cha dira na madhumuni yetu; vinahatarisha usalama wetu, kwa lugha nyingine ni vitendo vya uhaini. Naiomba NEC ifikirie kwa makini juu ya tuhuma hizi na wote wanaohusika waadhibiwe ipasavyo na kikao hiki", alisema Maalim Seif kwa msisitizo mkubwa.
Wazanzibari wengine walioongea kumsulubu Jumbe ni pamoja na Ali Ameir, Hassan Nassoro Moyo, Adam Mwakanjuki, Khamis Darwesh na Shaaban Mloo ambaye katika hotuba yake ndefu alisema, kuanzia mwaka 1980, Jumbe aliyumba kichama na uaminifu na uadilifu wake ukawa wa kutiliwa shaka mbali na kupoteza mvuto na kutokubalika Visiwani. Alisema, hiyo ndiyo ilikuwa sababu kuu kwa Jumbe kugeuka kuwa mpinzani kwa chama na kwa Muungano.
Naye Sheikh Aboud Jumbe alipopewa nafasi kutoa utetezi wake, uliomchukua saa tatu, alisema kwamba yeye hakuwa na uchu wa madaraka. Akaendelea kutoa sababu kuu nne za kisiasa juu ya tatizo la Muungano: kwanza, alisema, ni juu ya mawazo kinzani kuhusu chimbuko la Muungano ambayo hayakwepeki; Pili, Watawala kukataa kujadili maana na utekelezaji wa Mkataba wa Muungano kama ulivyo na ambao aliufananisha na "Cheti cha kuzaliwa cha Muungano".
Tatu, mgogoro wa Muungano kuachwa kukomaa bila kushughulikiwa tangu enzi za Karume; nne, kitendo cha kusikitisha na kisicho na uhalali, kwa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi na ya Baraza la Mapinduzi juu ya Muungano kutopewa nafasi wala kujadiliwa na Tume ya Siyovelwa pamoja na NEC, kilionesha dharau kwa
Wazanzibari,ikizingatiwa kwamba kwa kipindi chote cha uhai wa Muungano, marekebisho yote ya Katiba yametoka Bara.
Akamaliza kwa kusema, hapakuwa na sababu yenye mashiko kwa mjadala juu ya Muugano kuzimwa kwa kuwa hiyo ndiyo maana ya demokrasia na ndiyo demokrasia yenyewe.
Alipooneshwa Hati iliyoibwa ofisini mwake na kuombwa kukubali au kukana yaliyomo, Jumbe alikubali na kudai kuwa "mgogoro" huo ulipofikia hapakuwa na njia nyingine ya utatuzi ila kwa njia hiyo kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Muungano.
Baada ya maelezo marefu kujibu hoja za Jumbe, Mwalimu alisema: "Hapa, mgongano wa mawazo uko dhahiri; Makamu wa Mwenyekiti anasema Serikali Tatu; mimi (Mwenyekiti) nasema kuna Serikali Mbili. Suala ni Mkataba wa Muungano, na kesi imeandaliwa kupelekwa mahakamani", Mwalimu alisema huku akiwaonesha Wajumbe jalada la kesi.
Kisha, Mwalimu akatoa hukumu, akasema, "Makamu, jiuzulu, achia ngazi!".Naye Jumbe akajibu, "Najiuzulu".
Mwalimu akaendelea, akasema: "Unastahili kuheshimiwa; lakini hatupo tayari kulinda heshima yako; umetusaidia kuepusha janga la kitaifa".
Kufikia hapo, Jumbe hakujua kwamba alikuwa amevuliwa nyadhifa zote za kichama na serikali, Visiwani na Bara na kwamba alikuwa chini ya ulinzi kuanzia hapo na baadaye "kizuizini" nyumbani kwake, Kigamboni
Raia Mwema
0 comments:
Post a Comment