JINA la Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, limeibuka katika mgogoro unaokikabili Chama cha Wananchi (CUF), baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kudai kwamba kuingia kwake upinzani ndiyo chanzo cha matatizo yanayoukumba upinzani hivi sasa.
Kauli hiyo ya Lipumba imeungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Profesa Kitila Mkumbo, aliyesema kwamba; "Kinachoendelea sasa ni Lowassa kuwatesa viongozi wa Ukawa kama wao walivyomtesa kwa miaka mingi".
Akizungumza katika mahojiano na Raia Mwema juzi Jumatatu, Lipumba alisema anaamini wafuasi wa CUF wanaomuunga mkono ni wale ambao wanamfahamu na hawakukubaliana na uamuzi wa chama hicho kumuunga mkono Lowassa kuwa mgombea urais wa vyama vilivyokuwa kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
"Tatizo la kwanza hapa ni Lowassa. Kama Lowassa asingekuja upinzani, maana yake ni kwamba vyama vya upinzani vingetumia fomula tuliyokubalina kupata mgombea. Lakini wenzetu Chadema wakamfanya kuwa mgombea wao na hatimaye wa Ukawa.
"Ni kweli kwamba mimi nilimkaribisha Lowassa kwenye upinzani lakini lengo halikuwa kwamba awe mgombea urais. Kama kule alikokuwa (CCM) aliona hapamfai na akaona atatoa mchango kwenye upinzani, sisi tusingeweza kumkataa. Lakini lengo halikuwa awe mgombea.
"Ndiyo sababu mimi na Dk. Wilbrod Slaa tukasema hapana. Mimi ni mwanasiasa lakini nina maadili. Kuna mambo siwezi kufanya hata ikiwa vipi. Mtu ambaye tumemtangaza kuwa fisadi kwa takribani miaka nane tunawezaje leo kwenda kwa wananchi na kusema huyu ndiye mbeba bendera yetu?
"Hatukusilizwa wakati tunasema hapana. Ninaamini kwamba upinzani ulifanya kosa kubwa kumkubali Lowassa wakati ule. Nilitaka kujiweka pembeni lakini wanachama wakasema Mwenyekiti unataka kuondoka lakini chama kitakufa.
"Lakini baadaye nimeanza kuona dalili za kuua CUF. Ukiona umefika wakati chama kinataka hadi kuwafuta ubunge wabunge wake ambao walipambana katika mazingira magumu kupata ubunge wao, ujue hapo kuna ajenda nyingine.
"Na ajenda yenyewe ni kuhakikisha kuwa CUF inakufa Bara na inabaki Chadema peke yake. Ndiyo sababu sishangai kwamba baadhi ya wana Chadema wamekuwa mstari wa mbele kuchochea huu mgogoro wa chama chetu utadhani wao ndiyo wana uchungu kuliko sisi.
" Mimi nimeumizwa kwa ajili ya CUF. Nimelala jela kwa ajili ya CUF. Nimetokwa damu kwa ajili ya CUF. Leo nitakaaje pembeni huku jasho, muda na damu yangu iliyotumika kwa zaidi ya miaka 20 ikionekana kutaka kupotezwa. Ndiyo sababu nimeamua kurejea na kuirejesha CUF ile iliyokuwapo huko nyuma," alisema mchumi mbobezi huyo wa Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani.
Uhusiano wake na Maalim Seif
Katika mahojiano yake hayo na gazeti hili, Lipumba alisema hana ugomvi binafsi na Maalim Seif bali wana tofauti za kisiasa ambazo zingeweza kumalizwa kupitia vikao vya chama pasipo tatizo lolote.
"Sikiliza, mimi na Seif tumeanza kufahamiana zaidi ya miaka 40 iliyopita. Hata huyo Julius Mtatiro (aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya Lipumba baada ya mapinduzi ambayo sasa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema yalikuwa batili), alikuwa hajazaliwa wakati nakutana na Maalim.
"Maalim tumeanza kufahamiana mwaka 1973 wakati tukiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Mimi nilikuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama cha TANU na yeye alikuwa kiongozi wa wanafunzi waliotoka Zanzibar kuja kusoma Chuo Kikuu.
"Sina ugomvi binafsi na Maalim na ndiyo maana nawahurumia vijana ambao wamejiingiza katika mambo haya. Nadhani tatizo ambalo Maalim Seif analo sasa ni kwamba amekubali kuzungukwa na watu wenye siasa zisizotaka Muungano. Kule Zanzibar amezungukwa na ma-Nationalist (wanaotaka Zanzibar ijiondoe kwenye Muungano).
" Kama utakumbuka, kwenye Bunge la Katiba, mimi nilieleza msimamo wa chama ambao ni serikali tatu. Lakini Maalim Seif alizungumza kuhusu Muungano wa Mkataba ambao si msimamo rasmi wa chama. Lakini amezungukwa na watu wasiotaka Muungano na hivyo kuna mvutano kidogo.
" Pengine hao ndiyo wanaomshauri kwamba CUF itumie nguvu zake Zanzibar tu na haina sababu ya kuhangaika na Tanzania Bara. Kwamba CUF kiwe Zanzibar na Chadema ishike Bara. Ndiyo maana hajali kuona wabunge wetu wakifukuzwa uanachama. Hawana shida tena na Bara.
" Nadhani hapa ndipo tofauti ilipo. Lakini hizi ni tofauti ambazo zinaweza kumalizwa kupitia vikao. Msimamo huo wa watu wa karibu na Seif unaungwa mkono na Chadema kwa sababu watafaidika na hali hiyo.
" Mbaya zaidi ni kwamba Chadema hawataki Lipumba awe Mwenyekiti wa CUF. Wao wanajua kwamba wamewafanyia dhuluma Watanzania kwa kumfanya Lowassa kuwa mgombea urais. Wanajua kuna wana Chadema wanaoniunga mkono na nikianza kukijenga upya chama changu, nitavuna wafuasi hata kutoka kwao na utakuwa mwisho wa michezo waliyotufanyia mwaka 2015 kwenye Uchaguzi Mkuu," alisema.
Kuhusu ruzuku
Kutokana na matatizo yaliyopo sasa kwenye chama hicho, kuna utata kuhusu ni wapi hasa ruzuku ya chama hicho italipwa miongoni mwa kambi hasimu zilizopo. Kuna kundi linaloongozwa na Lipumba na lile la Seif.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Lipumba alisema hakuwa amewaza kuhusu jambo hilo lakini akasema ni suala ambalo linaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka na vyombo vilivyo ndani ya chama hicho. Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, Katibu Mkuu ndiye mtia saini wa malipo ya chama hicho na anapokuwa hayupo, Naibu Katibu Mkuu anaweza kutekeleza jukumu hilo.
Kwa upande wake, Mtatiro amesema kwamba Lipumba hataweza tena kuongoza chama hicho kwa sababu amepoteza ushawishi miongoni mwa wanachama wa chama hicho pamoja na vyombo vya uamuzi vya chama hicho.
"Kama mlivyoona wakati wa kikao cha Baraza Kuu, zaidi ya nusu ya wajumbe hawamtaki Lipumba. Kwenye Kamati Kuu ana watu wawili wanaomuunga mkono. Wabunge wanaomuunga mkono hawazidi nane. Sasa huyu atakuwaje mwenyekiti wa taifa wa chama?," alihoji.
Mtatiro pia amepinga uamuzi wa Jaji Mutungi wa kumrejesha Lipumba kwenye nafasi yake hiyo, akisema hakuna sheria nchini inayomruhusu msajili kuhoji au kuingilia mambo ambayo yameamuliwa na vikao halali vya chama.
Hata hivyo, Jumatatu wiki hii, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitoa taarifa mahsusi ambayo, pamoja na mambo mengine, iliweka bayana mamlaka ya msajili huo anavyoweza kuratibu shughuli za vyama vya siasa.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Sisty Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa vyama Dk. Francis Mutungi ilieleza; "Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inawaasa viongozi wa kitaifa wa chama cha CUF, kusoma kwa makini msimamo uliotolewa na Msajili wa
Vyama vya Siasa na kuuheshimu, kwani kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258, Msajili wa Vyama vya Siasa anao wajibu wa kujiridhisha kwamba, mabadiliko yoyote yaliyofanywa katika uongozi wa taifa wa chama cha siasa, ni halali na yamefanywa na mamlaka halali kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za chama husika."
Katika andishi lake refu alilolitoa kupitia gazeti hili, Profesa Mkumbo amesema kwamba tatizo linalosababisha migogoro katika vyama vya siasa nchini ni kwa viongozi na vyama vyao kutazama watu na si misingi iliyosababisha kuanzishwa kwa vyama hivyo.
Alisema kimsingi, mgogoro wa sasa wa CUF umesababishwa na uamuzi wa vyama hivyo kumpokea Lowassa na kumfanya kuwa mgombea urais; wakati vilitumia muda mrefu kumtukana na kumdhalilisha kuwa ni fisadi katika kipindi kirefu huko nyuma.
"Hivyo basi, uamuzi wa kujiuzulu kwa Profesa Lipumba ulijengwa katika misingi ya kuanzishwa kwa Ukawa. Hata hivyo viongozi wenzake waliamua kumeza maneno yao ya miaka mingi na kumkumbatia Lowassa wakiamini kwamba angewawezesha kushinda nafasi ya urais, kitu ambacho kingefuta fedheha ya kumkaribisha ndani ya Ukawa. Hili halikutokea kwa sababu Lowassa hakushinda nafasi ya urais. Ndiyo kusema, katika hali ya kawaida, ile fedheha ilibaki ndani ya viongozi wa Ukawa," alisema.
Raia Mwema
0 comments:
Post a Comment