1. Waziri wa elimu Prof. Ndalichako azibana Nacte, TET kuhusu ubora wa elimu
Hii ni habari kubwa inayochukua nafasi ya kwanza kwa mujibu wa mtandao wa mjengwablog.com.
Nchi yeyote duniano haiwezi kupiga hatua za maana za maendeleo, yawe ya kiuchumi, kijamii hata kisiasa, kama watu wake hawana elimu. Na hapa si suala la elimu tu, bali elimu bora. Kwenye ziara yake Nacte na TET, waziri Ndalichako amehimiza umuhimu wa ubora wa elimu na amediriki kutamka kuwa suala la ubora wa elimu linamkosesha usingizi.
Ni dhahiri Profesa Ndalichako ametwishwa mzigo mzito sana inapohusu kusimamia ubora wa elimu hapa nchini. Ni kwa vile haitarajiwi, katika wakati tulio nao, tuwe na mitazamo ya ' Bora Elimu' badala ya ' Elimu Bora'.
Ifahamike hapa, kuwa moja ya changamoto kubwa kwa nchi yetu kwenye jitihada za kuwa na vijana wenye elimu bora ni LUGHA inayotumika kufundishia na kujifunza mashuleni.
Na hapa tunamkumbusha Profesa kile ambacho Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alikizindua mwaka jana. Alizindua Sera Mpya ya Elimu nchini. Watanzania tuliambiwa, kwamba katika miaka kumi ijayo, Elimu ya Msingi itaunganishwa na Sekondari. Na kwamba lugha ya kufundishia na kujifunzia itakuwa ni Kiswahili, kuanzia Shule za Msingi mpaka Chuo Kikuu,
Sisi wa Mjengwablog.com tuliamini, na bado tunaamini, kuwa kama yale yaliyomo kwenye Sera ya Elimu iliyozinduliwa yatatekelezwa, basi, sio tu utakuwa ni muharobaini wa matatizo yetu ya kuwa na elimu bora, bali ni Mapinduzi Makubwa yatakayobaki katika historia ya kukua kwa nchi yetu kwa karne nyingi zijazo. Bila shaka, kuna changamoto ndogo na kubwa katika kutekeleza mapinduzi haya, lakini, tuna lazima ya kuzikabili na kuzishinda. Maana, mpango huu ulioasisiwa chini ya Rais Jakaya Kikwete, ni mpango wa ' Elimu Kombozi' kwa Watanzania. Happy New Year Prof. Ndalichako!
2. Daraja la Kigamboni kukamilika Februari
Hii ni habari inayochukua nafasi ya pili kwa uzito kwa siku ya leo. Inahusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Daraja lilikamilika litaongeza shughuli za kibiashara pia. Lilianza kujengwa 2012. Wahusika wamemwambia Waziri wa Ujenzi Prof . Mbarawa kuwa litaisha Januari 31. Waziri naye amewataka wahakikishe linamalizika maana wananchi wanasubiri kwa hamu. Angalizo hapa, chonde wataalamu wa ujenzi wasilipue ujenzi kwa kumwogopa waziri. Wajenge kwa viwango stahiki hata kama muda utaongezeka. Daraja linahusu maisha ya watu, na bahari ina mikondo yake. Nguzo zikitetemeka kwa kukosa uimara yaweza kuwa maafa. Wahenga walisema; ' Subra yavuta kheri!'
3. Kesi ya Gwajima na Pengo kuendelea Januari 27
Hii ni kesi yenye mvuto kijamii. Inawahusu viongozi wa kidini, mmoja ni Askofu kwenye Kanisa Katoliki na lenye wafuasi wengi. Tuhuma dhidi ya Askofu Gwajima kumtukana Askofu Pengo zinaifanya kesi hiyo kuwa na mvuto huku jamii ikitaka kujua hatma yake. Ni maneno gani mabaya aliyotamka Gwajima dhidi ya Askofu Pengo? Soma habari hii inayopewa nafasi ya tatu na mtandao wa Mjengwablog.com
Usikose pia kusoma habari bora ya michezo kwa siku ya leo, na katuni iliyochukua nafasi ya kwanza, na nyingine zilizofuatia. Ni kwenyehttp://mjengwablog.com