Sunday, 28 September 2014

Re: [wanabidii] Kosa la 'Rasimu ya Vijisenti'

Hivi lini mwizi akapewa kazi ya kutunga sheria za kuwabana wezi?
em

2014-09-28 1:56 GMT-04:00 mngonge franco <mngonge@gmail.com>:
Ndugu zanguni suburi katiba yenye baraka za watanzania hii ya Sitta na Vijisenti siyo yetu ni yao

2014-09-27 11:43 GMT+03:00 Abdalah Hamis <hamisznz@gmail.com>:
KOSA la awali kwenye rasimu iliyowasilishwa mbele ya Bunge la Katiba na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Rasimu hiyo, Andrew Chenge (Mzee wa Vijisenti), ni upotoshaji wa dhana ya shirikisho kama yalivyokuwa matakwa ya wananchi walio wengi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi, Jaji Joseph Warioba (kushoto), akimkabidhi Rais Jakaya Kikwete rasimu ya katiba.

Katika Rasimu ya Vijisenti, dhana hii imepigwa vita na kupewa sababu kuu tano ambazo kwa leo tutaanza kuzijadili na kuonyesha udhaifu mkubwa uliotumika katika kufikia maamuzi ya kupinga uwazi wa serikali tatu na mfumo mzima wa shirikisho uliolenga kutenganisha mamlaka makuu ya tawala za Zanzibar, Tanganyika na Muungano.

Sababu #1: Wengi wape

Sababu ya kwanza ni kuwa wabunge walio wengi walipinga mfumo huu na hivyo katika misingi ya wengi wape, faida za serikali tatu zikafunikwa na hii demokrasia ya uongo. Katika jambo lenye uzito mkubwa kutokana na maoni ya wananchi, wingi wa wabunge kulikataa haileti uhalali wa dhana nzima ya wengi wape hasa kwa wingi wa watu 400 inapolinganishwa na milioni 45 ya Watanganyika na milioni 1.6 ya Wazanzibari.

Kama hoja ya wingi na upana wa demokrasia ungelizingatiwa, kwanza maoni yaliokusanywa na Tume yalionyesha wananchi walio wengi walipendekeza mfumo wa serikali tatu. Na kwa Zanzibar, ambayo
licha ya udogo wake kieneo na idadi ya watu wake, bado ni mdau mkuu wa Muungano na mwenye hadhi sawa na Tanganyika, maoni yao yalikwenda mbali zaidi kupinga mfumo wa serikali mbili kwa asilimia zaidi ya 60.

Ukizingatia misingi ya utafiti kwa vigezo vya idadi ya watu pamoja na hoja ya upanukaji wa demokrasia, basi Wazanzibari walishasema nini wanataka kwa wingi wao na Tume ya Warioba ikajaribu kuyaakisi matakwa hayo kupitia muundo wa serikali ya shirikisho. Kama hilo lisingelitosha, basi suala hili lingeliitishiwa kura ya maoni wakaulizwa wananchi kabla ya kuhalilisha madhambi ya wabunge 400 waliopitisha mfumo uliokataliwa kwa miaka 50 lakini ukakumbatiwa kwa vitisho na kulazimisha agenda ya vyama katika jambo lenye msingi wa kitaifa.

Sababu #2: Hati ya Muungano

Sababu ya pili ni dhaifu zaidi, hasa inaposema mfumo wa shirikisho ni kinyume na Hati ya Muungano iliyoweka ajenda ya mfumo wa serikali mbili. Udhaifu huo unajidhihirisha kwenye mambo matatu:

Kwanza, kabla ya kuipa uhalali Hati ya Muungano kuwa msingi wa kuutupilia mbali mfumo wa shirikisho, wabunge walioitunga wangelituletea ushahidi kwamba Hati hii iliidhinishwa na Baraza la Mapinduzi kama ilivyoidhinishwa na Bunge la Tanganyika. Ikiwa hadi hii leo dhana nzima ya kuitumia Hati ya Muungano bado ina utata wa kisheria katika kuidhinishwa kwake, tutaitumiaje kama ni msingi usioweza kubadilishwa hata ikiwa mazingira ya kuungana miaka 50 nyuma ni tafauti na ya sasa?

Pili, hata kama tukikubaliana kutokukubaliana juu ya uhalali wa Hati ya Muungano, bado Rasimu ya Vijisenti ina udhaifu mwengine kwenye sababu hii. Kwa mfano, Hati ya Muungano haikuwahi kupendekeza matumizi hata ya jina la Tanzania, sasa kama si halali kulitumia neno shirikisho kuna uhalali upi kulitumia jina la Tanzania? Hati ya Muungano haikuwa na mambo ambayo hii leo yameongezwa na rasimu hii, kwa mfano suala la vyama vya siasa. Kama Rasimu ya Tume ya Warioba iliyotokana na maoni ya wananchi haikuwa na uhalali wa kubadilisha mfumo wa Muungano kwa kuwa Hati ya Muungano haikusema hivyo, Rasimu ya Vijisenti iliyotokana na kundi la wabunge ina uhalali gani wa kuibadilisha Hati hiyo?

Tatu, Katiba ya Zanzibar imeitaja Zanzibar kama nchi, na ilipitishwa na asilimia 66 kwa wingi wao. Sasa iweje tung'ang'anie tafsiri ya Hati ya Muungano (na hili la tafsiri ya Hati ya Muungano ni jambo la kusisitizwa sana maana pana tafauti kati ya kile kinachotamkwa na Hati hiyo na kile kinachotafsiriwa na akina Samuel Sitta na Andrew Chenge), wakati demokrasia ilishaweka sawa kwa hili, tena kwa ushahidi mkubwa zaidi wa maridhiano ya wananchi kuliko ya Hati ya Muungano ambayo hakuna ushahidi wa kuridhiwa na Baraza la Mapinduzi? Je, ikishindikana kufuta sehemu ya katiba ya Zanzibar inayoitamka kama ni nchi kwa Wazanzibari kukataa kufuta sehemu hiyo, tutakuwa tumeuweka Muungano katika sehemu ipi ya kisheria?

Sababu #3: Mkinzano wa sheria na maoni ya Tume

Sababu ya tatu ni kusema kwamba sheria iliyoanzisha mchakato wa katiba inakinzana na maoni ya Tume ya Warioba, kwamba sheria iliagiza kudumisha muungano wa nchi moja, taifa moja na serikali mbili, kinyume na pendekezo la serikali tatu. Kwa uchache, sababu hii ina udhaifu kwenye maeneo mawili:

Kwanza, kama tulivyotangulia kusema kwenye nukta ya hapo juu kwamba Katiba ya Zanzibar inasema Zanzibar ni nchi na ikaweka mamlaka kwa Rais wa Zanzibar kuwa pekee ndiye mwenye nguvu za kugawa mikoa na wilaya. Hiki ni miongoni mwa vifungu vilivyofungwa kisheria, ambapo hakuna wa kukibadilisha kama si Wazanzibari wenyewe, na bahati nzuri tayari asilimia 66 walikubali kuyarejesha mamlaka hayo kwa Rais wa Zanzibar. Sasa ipi ina nguvu zaidi kati ya hiyo sheria iliyoanzisha mchakato wa katiba na Katiba ya Zanzibar? Iweje leo kutaka kufuta demokrasia ya wingi wa asilimia 66 kuendekeza zahma za itikadi ya vyama? Tukumbuke kwa Zanzibar, hili lilipitishwa na wajumbe wa vyama vyote, na kupewa baraka na sehemu zote kuu za kiutawala katika vyama hasa CCM na CUF.

Pili, ukitazama hichi kipengele kinachonukuliwa cha sheria iliyounda mchakato wa katiba, utakuta tafsiri za kisheria zinapingana. Kwamba kubwa hapa lilikuwa ni kuhakikisha uwepo wa muungano wenye nguvu na utakaoondowa kero zake ili kuupa uhai na ufanisi mkubwa. Kwa kutazama maoni ya wananchi wa pande zote, kwa kuzingatia asilimia zaidi ya 60 ya Wazanzibari waliotaka Muungano wa Mkataba, Tume ya Jaji Warioba ilikuwa na wajibu wa kweli kuhakikisha Muungano huu unadumu kwenye msingi wa matakwa ya wananchi na ndio maana ikaja na wazo la muundo wa shirikisho ili kuweka mizania baina ya kuudumisha Muungano na kuakisi matakwa ya umma.

Sasa tujiulize, ikiwa leo hii wananchi wataikataa hii Rasimu ya Vijisenti, haitamaaminisha wameikataa hoja ya kubakia na serikali mbili? Na je, ikiwa demokrasia itakataa mfumo wa serikali mbili, hichi kipengele kinachotajwa cha serikali mbili kitakuwa na uhalali upi bila ya upana wa demokrasia? Sheria haiwezi kuwa na uhalali ikiwa itapingwa na wananchi, na matumizi yake hayatakuwa na tafsiri yoyote zaidi ya uimla. Rasimu ya Vijisenti imekuja na majibu dhaifu ya kupinga dhana nzima ya mabadiliko pamoja na azma ya kulinda Muungano kwa matumizi ya demokrasia badala ya uimla unaojificha.

Sababu #4: Shirikisho litaleta hisia za utaifa

Sababu ya nne ni kwamba matumizi ya neno shirikisho yataleta hisia za utaifa kwa wananchi wa nchi washirika na hivyo kuleta mgawanyiko na uwezekano wa kuvunja Muungano. Hili limetajwa bila ya ushahidi wa kuridhisha na ni sawa na dhana isiyo kichwa wala miguu na udhaifu wake uko kwenye maeneo matatu:

Kwanza, hisia za utaifa hivi leo zipo hata baada ya miaka 50 ya muundo wa muungano wa Serikali Mbili na zinaongezeka kila siku kwa kuwa mfumo huo umekosa haki, heshima na usawa kwa kila upande. Mataifa kama Marekani na Ujerumani, yenye mifumo ya serikali za shirikisho, yana wananchi wenye hisia kali za utaifa wa mataifa yao na sio za maeneo wanayotokea kwa kuwa serikali kuu za shirikisho zimekuwa na uadilifu na zimekubali kubainisha mipaka ya kimamlaka baina yake na serikali za nchi washirika. Kwa hivyo, Serikali Mbili zimepalilia na kukuza hisia za utaifa na serikali ya shirikisho huko ilikotumika imedhihirika kuua hisia hizo kwa kuwa muundo wa muungano si kigezo cha kuhuisha hisia za utaifa wa nchi husika bali ukosefu wa usawa, haki na heshima baina ya pande zinazounda muungano huo ndio sababu.

Pili, umuhimu wa mfumo wa shirikisho ni uwazi, uwajibikaji na ufanisi hasa kwa mamlaka tutayojumuika nayo pamoja katika misingi imara ya haki, usawa na heshima na hivyo kuufanya muungano kuwa ni tunu si ya taifa letu tu bali ya Afrika Mashariki nzima. Sababu zinazotolewa kupinga mabadiliko ya kuelekea mfumo wa uwazi wa shirikisho ni dhaifu, za kitoto na zenye kutia aibu hasa ikiwa ndiyo mawazo ya watu 400 walio wengi waliochaguwa kubaki na mfumo wa mbili.

Tatu, kupinga mfumo wa shirikisho kwa sababu hii ni kule kule tunakosema kila siku kwamba watawala wanajenga mazingira makusudi ya khofu kuwa ndio msingi wa kuusimamisha Muungano badala ya kutoa uhuru wa kweli wa mabadiliko ya muungano wenye nguvu na uhalali. Kulikuwa na hoja kwamba mfumo huu wa serikali mbili ulilenga kuzivutia nchi jirani kujiunga nao, lakini kwa Rasimu hii ya Vijisenti, hakuna vigezo vyovyote vinavyoweka uwezekano huo na imejengwa zaidi kuibana kimamlaka Zanzibar na kuzidi kuitumbukiza Tanganyika katika joho takatifu la Muungano.

Sababu #5: Idadi ya serikali na kero za Muungano

Sababu ya mwisho ni kuwa utatuzi wa kero za Muungano hautegemei wingi wa serikali, ambayo miongoni mwa udhaifu wake ni kwamba inapotosha kabisa kwa kuwa imeanza lakini haikumaliza na suluhisho, hivyo imejengewa mazingira ya kuleta matarajio lakini yakafungwa kwa suluhisho lisilotajwa ili kujadiliwa. Ikiwa ni kweli kero za muungano hazitegemei wingi wa serikali, basi ni haki pia kusema kero za muungano hazitafutika katika mfumo butu wa serikali mbili. Ikiwa tatu ni tatizo na mbili au moja si suluhisho.

Kilichokosekana katika kauli hii ni suluhisho la kusema kero zitamalizwa kwa kura ya maoni ili wananchi wawe na kauli ya mwisho juu ya kero za Muungano. Ikiwa hichi ndicho kikomo cha fikra za akina Sitta na Chenge, kwamba wingi wa serikali si suluhisho basi wasijibebeshe haki ya kuwaamulia wananchi, bali wawaachie wenyewe njia mbadala za kutatua kero hizi.

Hitimisho

Sisi Watanganyika na Wazanzibari tuna mahusiano mazuri na hatutashindwa kutoa suluhu la kero ambazo kwa makusudi Chama cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa kuzirekebisha kwa kujali maslahi yake binafsi badala ya mustakbali wa Muungano wenye nguvu, uhalali na uliojengewa na misingi imara ya heshima, haki na usawa.

Tutawezaje kuleta usawa ikiwa mmoja wa washirika wa Muungano kafichwa ndani ya koti la Muungano? Tutapata vipi haki ikiwa maoni ya wananchi yanachakachuliwa? Tutapataje heshima ikiwa mmoja kavaa joho mwengine kitenge? Wala siamini ni haki kwa Tanganyika pia kuwanyima uwazi wa kujuwa mamlaka yao na matumizi ya kodi za wananchi wao zinavyotumika kwa maendeleo yao.

Ninaloliona linalokidhi hoja ya kubaki na serikali mbili ni maslahi binafsi yanayotumia muungano kujineemesha na uwepo wa elitism maalum ya kula vijisenti vya wananchi huku lawama kubwa zikisukumiwa kwa muungano na hasa Wazanzibari. Tutaendelea kipengele kimoja kimoja kuonyesha mapungufu makubwa na kutoa ushahidi wa kwa nini iitwe Rasimu ya Vijisenti na hivyo wananchi waikatae kwenye Kura ya Maoni kama ikipitishwa na Bunge Maalum la Katiba.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani
Zanzibar Daima OnlineKosa #1 la 'Rasimu ya Vijisenti'

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment