Wednesday, 28 November 2012

[wanabidii] Absalom Kibanda : Kinana ni Kimbunga

YAKO mambo ya msingi katika maisha ya kitaaluma katika fani zote za
kielimu ambayo mtu yeyote anayetambua na kujali vyema wajibu wake
anapaswa kuyasimamia na kuyalinda hata kama atafanya hivyo kwa gharama
ya kupoteza maisha, kuchukiwa, kudharauliwa au kupuuzwa.

Moja ya mambo ya namna hiyo ni miiko ya kitaaluma ambayo aghalab
huongoza na kujenga misingi ya uwepo na kustawi kwa kila fani iwe ni
sheria, elimu, uaskari, uhandisi na hata ukachero.

Uandishi wa habari ni moja ya taaluma ambazo zina miiko na maadili
yake. Zaidi ya hayo uandishi wa habari na waandishi wa habari wanaishi
kwa kufuata na kuzingatia miongozo yao ya kikazi na kitaaluma.

'Ukweli' ni moja ya misingi mikuu ya uandishi wa habari. Huu unaweza
ukawa msingi mama katika taaluma hii adhimu. Ni kwa kuzingatia hilo
ndiyo maana uandishi wa habari unatajwa na magwiji wa taaluma hii kuwa
ni 'noble profession'.

Naandika maneno haya huku nikitambua kwa dhati kwamba, mara kadhaa
wanahabari wa hapa nchini na kwingineko duniani tumekuwa mstari wa
mbele katika kukiuka msingi na muongozo huo muhimu kitaaluma kwa kujua
au kutojua, kwa kukusudia ama kwa bahati mbaya.

Pamoja na mapungufu hayo ya kibinadamu katika taaluma hii ambayo siku
zote nitabakia kuwa mwanafunzi wake, uandishi wa habari unaendelea na
utaendelea kubakia kuwa mhimili wa nne wa dola baada ya serikali,
Bunge na Mahakama.

Iwapo hivyo ndivyo, uandishi wa habari ni taaluma ambayo inao wajibu
wa kusimama juu ya taaluma zote nyingine ambazo aghalab kwa nafasi zao
hakuna hata moja ambayo imepata kuchukua taswira ya mhimili kama
ilivyo kwa uandishi wa habari.

Kwa sababu hiyo basi, kama ilivyo kwa mihimili mingine ya dola,
taaluma hii inao wajibu wa kukubali changamoto zinazoelekezwa kwake na
wakati mwingine kuchukua maamuzi ambayo yanaipa mamlaka na taswira
halisi ya kuonekana kuwa ni mhimili unaojitegemea kifikra, kimatendo
na hata kimaadili.

Nimelazimika kuyasema yote haya katika utangulizi wa makala yangu ya
leo kutokana na kile ambacho kilitokea wiki iliyopita baada ya safu
hii kuwa na makala iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho:
"Namuogopa Abdulrahman Kinana".

Makala ile ilibeba ujumbe rahisi kabisa. Kwanza mbali ya kueleza kwa
sehemu tu kuhusu wasifu wa Kinana kwa mtazamo wa mwandishi wa safu hii
ambaye ni mimi mwenyewe, ilieleza kwa muhtasari tu sababu ambazo
zilimfanya Rais Jakaya Kikwete hatimaye akubali yaishe kwa kumfanya
mwanasiasa huyo abebeshwe jukumu la kuwa Mtendaji Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).

Kama hiyo haitoshi, makala ile ilieleza kwa maneno yaliyo wazi kabisa
kwamba, CCM ilikuwa ikichungulia kaburi na kimsingi mwenendo wa mambo
katika kipindi cha miaka michache tu iliyopita hadi sasa ilikuwa
ikichukua mwelekeo wa wazi wa kupoteza madaraka ya dola.

Ni kwa bahati mbaya sana kwamba, mashabiki wa vyama vya upinzani ambao
siku zote wamekuwa hodari kushangilia hoja zetu za kuikosoa serikali
au kuisuta CCM na viongozi wake kwa kuwaangusha Watanzania katika
maeneo kadha wa kadha walipatwa na hasira kali waliposoma makala ile
na kuona ikiwa na harufu ya kumsifu au kueleza uwezo wa kimikakati,
kiutawala, kisiasa na kiintelijensia aliokuwa nao Kinana na pengine
safu ya uongozi mpya wa chama hicho tawala iliyoundwa wiki mbili
zilizopita.

Kwa sababu tu ya kulemewa kwao na ulevi wa chuki walizoijengea CCM na
viongozi wake pasipo hata kuangalia muktadha wa makala ile, wadakuzi
hao wa mambo kupitia katika mitandao ya intaneti, majukwaa ya jamii,
ujumbe wa maandishi na kwenye simu yangu ya kiganjani na hata kwa njia
ya ana kwa ana wakanisuta na kunitukana kila aina ya matusi ili
kukidhi matakwa yao.

Lile kosa la wanasiasa na wapambe wao kukosa ustahimilivu ambalo
tumekuwa tukiwahusisha nalo watawala, likachukua sura na mwelekeo
tofauti.

Siri zikafichuka kwamba ndani ya mioyo ya baadhi ya viongozi wa vyama
vya upinzani, wafuasi na mashabiki wao kulikuwa na hulka za hatari za
udikteta ambazo ama zinalingana na zile walizonazo baadhi ya wana CCM
na viongozi kadha wa kadha wa kiserikali.

Niseme wazi na kwa kujiamini kabisa kwamba, sikutishwa wala
kubabaishwa na matukio hayo ambayo kwangu hayakuwa mageni hata kidogo
kwani yalifanya kile ambacho nimekuwa nikikabiliana nacho tangu mwaka
1993 wakati nilipoanza kushiriki kikamilifu kuandika makala katika
magazeti mbalimbali nchini na wakati mwingine kutoa maoni na mawazo
yangu kwa viongozi mbalimbali wa kisiasa.

Haraka haraka hoja za kishabiki zilizokosa weledi ambazo zilikuwa
zikivurumishwa na manazi hao wa kisiasa zilinikumbusha ujasiri
niliokuwa nao mwaka 1995 wakati niliposimama imara kupinga mhemko wa
kitaifa wa "Homa ya Augustine Mrema" ambayo ililitikisa taifa kwa
kiwango cha kumchanganya akili Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Nilikuwa na ujasiri aliokuwa nao Jenerali Ulimwengu wa kumpinga Mrema
katika maandishi na hata katika majukwaa ya mijadala.

Bado nakumbuka vyema namna nilivyosafiri kwa daladala kutoka Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam nilikokuwa nikisoma hadi Kariakoo zilizokuwa
ofisi za NCCR Mageuzi na nikapata fursa ya kuwafikia Mabere Marando na
Ndimara Tegambwage nikiwaomba watafakari upya uamuzi wao wa kumpa
Mrema dhamana ya kuongoza harakati ghali za mageuzi katika taifa hili.

Makala nilizoandika katika magazeti ya Rai, Mtanzania, Wakati Ni Huu,
Nipashe na kwingineko katika kipindi hicho cha 1995 na 1996 ambazo
aghalab zilikuwa zikiwaasa Watanzania kupima mambo kwa kina badala ya
kutukuza na kuendekeza ushabiki wa kisiasa ni ushahidi wa wazi wa kile
ambacho nilikuwa nikikisimamia na nimeendelea kukisimamia siku zote.

Haikupita hata miaka miwili kabla ukweli wa kile nilichokuwa
nikikizungumza na kukitetea kwa njia ya maandishi kuthibitika.

Mrema alifanya kile nilichokiona mapema, akawaangusha aliowaongoza na
kuwaporomosha wale waliofikia hatua ya kumuabudu kwa kiwango cha
kumuona mkombozi wao wa kisiasa.

Kama ilivyokuwa kwa Mrema mwaka huo huo wa 1995, nilikuwa miongoni mwa
wanahabari ambao tulimpinga kwa hoja Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
katika harakati zake za kulazimisha aliyekuwa mgombea wake, Benjamin
Mkapa, ateuliwe na kuwa mgombea wa urais wa CCM.

Katika hili, sikukubaliana na kile ambacho Jenerali Ulimwengu na
wenzake walikitetea. Ingawa nilikuwa mpinzani mkubwa wa Mrema,
sikufurahishwa hata kidogo na uamuzi wa Baba wa Taifa kupandikiza
hulka za kidikteta katika kuchakachua mchakato wa urais kupitia katika
tanuri la chama hicho tawala.

Kilichotokea miaka 10 baada ya Mkapa kustaafu urais mwaka 2005 ni
ushahidi wa wazi wa kile ambacho baadhi yetu, japo hatuna majina
makubwa tulikiona mapema.Rais huyo pamoja na kuonekana kwamba
alikijengea heshima kiti cha urais na kuinunua harufu ya maendeleo ya
kiuchumi, alifisha hata ndoto za 'mentor' wake Mwalimu Nyerere. Hili
linahitaji mjadala unaojitegemea.

Sikuishia hapo, mwaka 2005 wakati taifa na fani nzima ya habari
ikiimba wimbo wa Kikwete, Kikwete Kikwete katika misingi ya ushabiki
unaofanana na ule unaotokea leo, nilikuwa miongoni mwa waandishi
wachache ambao tulikataa kuimba wimbo huo huku tukitoa tahadhari za
waziwazi kuhusu hatari ambayo ilikuwa ikilinyemelea taifa.

Ingawa wakati huo nilikuwa Mhariri wa gazeti la Mwananchi Jumapili
ambalo mmoja wa wakurugenzi wake alikuwa Rostam Aziz aliyekuwa
katikati ya kitovu cha kampeni za Kikwete, nilikataa kuwa bendera
fuata upepo na nikaandika mada kadha wa kadha kuhoji kuhusu uwezo wa
mwanasiasa huyo kupewa dhamana ya kuongoza nchi.

Ushahidi wa kile nilichoandika kuhusu hilo uko wazi kabisa. Nilitenda
na kutoa msimamo tofauti kabisa na ule waliokuwa nao baadhi ya
wahariri na waandishi wa habari wa zama hizo kuhusu nafasi ya Kikwete
katika kuliongoza taifa hili.

Hata yeye mwenyewe alipotangaza uamuzi wa kugombea urais kule Chalinze
nilikuwa miongoni mwa wahariri na wanahabari ambao tulikwenda na
kumuuliza maswali magumu kuhusu kugombea kwake.

Alipoteuliwa na chama chake kuwa mgombea kama ilivyotarajiwa na wengi,
nilitafuta fursa na nikafanya naye mahojiano nyumbani kwake Dodoma
nikiwa nimeongozana na mwanahabari mwenzangu, Nyaronyo Kicheere,
aliyekuwa Mhariri wa Habari wa gazeti dada la The Citizen on Sunday.

Niliendelea na msimamo ule juu ya Kikwete kabla na baada ya kuteuliwa
kwake kuwa mgombea urais. Waandishi na wahariri waliokuwa pale ni
mashahidi wazuri kwamba, msimamo wangu huo ulipata kusababisha Rostam
afikie hatua ya kueleza waziwazi kukerwa nao.

Mara kadhaa aliniita nyumbani kwake akijaribu kunishawishi na
kuniaminisha kwamba Kikwete alikuwa ni mwanasiasa hodari na anayeweza
kuliongoza taifa hili pengine kuliko mwingine yeyote.

Kilichotokea baada ya hapo kila mtu anakijua, Kikwete alishinda kwa
kishindo na baadhi yetu ambao tulionekana kuwa vimbelembele kuhoji
uwezo wake tukasutwa kweli kweli kwa kiwango cha baadhi ya wanahabari
wenzetu kutuona wendawazimu.

Kwa sababu ya kuendekeza hulka za kishabiki, wanahabari tulishindwa
kumuandaa Kikwete kuwa rais bora, tulimnyima fursa ya kujipanga
kifikra na kifalsafa na tukaiacha ajenda ya urais iandaliwe kimkakati
na kiintelijensia zaidi. Hiki tunachokiona leo ni matokeo ya
kuendekeza ushabiki wa namna hiyo.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba kile kilichotokea mwaka 1995 na
baadaye mwaka 2005 bado kinaonekana kutofundisha Watanzania. Hulka za
kinazi na kishabiki katika masuala ya msingi bado zinaendelea kutafuna
vichwa vyetu.

Taifa zima linaimba wimbo mmoja tu, Slaa, Slaa, Slaa. Halitaki kusikia
lolote. Ukimgusa Dk. Slaa tena kwa hoja za kumtahadharisha, kumuonya
au hata kwa minajiri ya kumfanya ajiandae kukabiliana na kimbunga kama
hiki cha Kinana, mashabiki wake wanalipuka kwa jazba na kwa hamaki
kubwa.

Ukithubutu kuikosoa CHADEMA au kumgusa yeyote miongoni mwa viongozi
wake kama nilivyofanya miaka mitatu au minne iliyopita wakati
nilipopinga uamuzi wa Zitto Kabwe kugombea uenyekiti wa taifa wa chama
hicho kwa sababu muda wake ulikuwa bado, idadi ya matusi
utakayovurumishiwa kama ni mtu ambaye una moyo mwepesi unaweza ukaacha
kuandika.

Hivi ndivyo ilivyokuwa wiki iliyopita wakati nilipowaonya wapinzani
kukaa chonjo na Kinana kwani kimbunga ambacho alikuwa akielekeza
kukipuliza kuelekea upande wa kambi ya upinzani kinaweza kusababisha
upepo unaovuma sasa kubadili njia.

Sitaki kujifanya mimi ni nabii wa siasa za Tanzania. Hata hivyo bado
naendelea kuamini na kusisitiza kwamba, Kanali Mstaafu Abdulrahman
Kinana si mtu mwepesi, si mwanasiasa wa kumbeza wala kumpuuza.

Kama CHADEMA na mashabiki wanataka kupima kina cha maji kwa sababu tu
ya ulevi wa fikra, basi wanao uhuru wa kufanya hivyo. Tusubiri fainali
2015. Huko ndiko tuendako.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

DELL LATITUDE D 620 & D30

80 GB HardDisk ,CORE 2 DUO , 2.0 GHZ CPU ,2 GB RAM
DVD/CD - RW ,WINDOWS 7 /WINDOWS XP ,WIRELESS , BLUE TOOTH .

TSHS : 380,000 , 1 YEAR WARRANTY

CALL : 0786 806028
Free Delivery in Dar es salaam

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment