Friday, 11 November 2016

[wanabidii] Uwaziri Mkuu ulivyowagombanisha Sitta na Lowassa


SPIKA mstaafu wa Bunge la Tanzania, hayati Samuel Sitta, alipanga kukutana na waandishi wa habari mara baada ya kurejea nchini kutoka Ujerumani alikokuwa akitibiwa, Raia Mwema limeambiwa.

Akizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yake, mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa Sitta alisema marehemu alitoa kusudio lake hilo la kuzungumza na wanahabari siku tano kabla ya kifo chake.

Lengo la mkutano huo, kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, lilikuwa ni kueleza tathmini yake kuhusu mwaka mmoja madarakani wa serikali ya Rais John Magufuli.

"Mzee Sitta alipanga kuzungumza na wanahabari endapo angerudi nchini. Yeye alikuwa na matumaini kwamba angerejea. Ingawa alikuwa hospitali lakini bado alikuwa anawaza taifa lake.

" Sijui kile ambacho alitaka kukisema lakini kwenye mazungumzo alisema mambo mengi aliyokuwa akiyapigia kelele huko nyuma kama ufisadi na kutowajibika ndiyo ambayo yanafanyiwa kazi na Rais Magufuli," Raia Mwema liliambiwa.

Sitta ambaye alikuwa ametumikia serikali zote zilizopita hapa nchini, alifariki dunia nchini Ujerumani usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii. Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya tezi dume.

Miaka 20 ya mwisho
Katika utumishi wake wa umma, Sitta alitumika katika maeneo mbalimbali ikiwamo uwaziri, ukuu wa taasisi za serikali lakini atakumbukwa zaidi kama Spika wa Bunge la Tisa la Tanzania.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati akiwa Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), Sitta alijitambulisha kama mmoja wa majemedari wa kundi lililokuwa likifahamika kwa jina la mtandao ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Kundi hilo lilikuwa na kazi moja kubwa; kuhakikisha kwamba Jakaya Kikwete anachaguliwa na CCM kuwa mgombea wake wa Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Yeye, aliyekuja kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mfanyabiashara tajiri, Rostam Aziz, walitengeneza "utatu mtakatifu" uliofanikisha hatimaye kumwingiza Kikwete madarakani mwaka 2005.
Kikwete alipoingia madarakani, kulikuwa na tetesi kuwa nafasi ya Waziri Mkuu huenda ikaangukia kwa mmoja wao kati ya Lowassa au Sitta.

Sitta, wakati huo, alionekana kuwa na sifa zaidi kwa sababu ya uzoefu wake; alikuwa waziri katika Serikali ya Julius Nyerere, wakati Lowassa na Kikwete wakiwa maofisa wa ngazi za chini kwenye chama na serikali kwenye miaka ya 1970.

Hata hivyo, hatimaye Kikwete aliamua kumpa nafasi hiyo Lowassa; jambo ambalo lilielezwa kumkera Sitta aliyejiona amefanya kazi kubwa na kuwa na sifa za ziada kulinganisha na mbunge huyo wa zamani wa Monduli.

Akiandika tanzia yake juu ya Sitta ambayo imechapwa ndani ya gazeti hili, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alisema kwamba kulikuwa na fununu kwamba wanasiasa hao wawili wana mgogoro wa chinichini.

Zitto ameandika kwamba kulikuwa na tofauti kati ya wawili hao kwa vile Sitta alitaka Bunge lifanye ipasavyo kazi ya kuisimamia serikali lakini Lowassa; kama Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, alitaka serikali iwe na ushawishi zaidi.

"Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu, Edward Lowasa, katika kuleta mabadiliko hayo.

"Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.

"Sio Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi zile. Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Lowasa ataweza kusemea hili siku za usoni," aliandika.

Kilele cha unaoelezwa kuwa mgogoro wa chini kwa chini kati ya Lowassa na Sitta kinaelezwa kuwa ni kujiuzulu Uwaziri Mkuu kwa mwanasiasa huyo kufuatia kashfa ya Richmond.

Kwenye hotuba yake ya kutangaza kujiuzulu, Lowassa aligusia kidogo kwamba inawezekana tatizo kubwa zaidi lilikuwa ni nafasi yake ya Waziri Mkuu na si kashfa hiyo ambayo amekana kuhusika nayo.

Mheshimiwa Spika, lakini nimetafakari kwa makini sana jambo hili nikajiuliza hivi kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo kulikoni?

"Mimi nadhani there is a wish which I am going to grant, ni Uwaziri Mkuu. Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe.
"Mheshimiwa Spika, nimetafakari kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya Serikali yangu nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumwomba niachie ngazi.

"Nafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya Bunge wa kumsingizia mtu," alisema.
Katika mojawapo ya mazungumzo niliyowahi kufanya naye, niliwahi kumuuliza kama kulikuwa na ahadi yoyote aliyowahi kupewa na Kikwete kuwa angepewa Uwaziri Mkuu.

" Sikiliza, sisi kazi yetu kubwa ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Kikwete anaingia madarakani. Hatukuwahi kukaa na kupanga vyeo kuwa huyu atakuwa nani na yule atakuwa nani.
" Labda kuna watu walikuwa wanatarajia vyeo lakini sisi wengine hatukuwa tunawaza hayo mambo. Lakini, baada ya kushinda, kukawa na makundi mawili.

" Kundi la kwanza, ambalo mimi nilikuwa mmoja wao, lilikuwa limejipanga kumsaidia Kikwete atekeleze ahadi zake alizowapa Watanzania. Nafasi yoyote ambayo mtu angepewa, alitakiwa kusaidia kufanikisha aliyoahidi mgombea wetu.

" Halafu kukaibuka kundi la pili ambalo ni watu waliokuwa wamejipanga kujineemesha kutokana na ushindi huo. Hawa hawakuwa na lengo la kuwasaidia Watanzania bali wao binafsi, familia zao na maswahiba wao wa kibiashara na kisiasa," alisema.

Ni Sitta huyuhuyu ndiye ambaye aliwahi kuwaambia rafiki zake kwamba urafiki wake na waliokuwa wanamtandao wenzake (waliokwenda kwenye kundi la pili) umebaki palepale ingawa kwenye mambo ya kitaifa wasingeweza kuelewana.

Hata hivyo, mmoja wa wanasiasa waliohojiwa na gazeti hili, ambaye anahusishwa na kundi lililokuwa likimuunga mkono Lowassa, alisema kuna uwezekano Kikwete alimuahidi Sitta Uwaziri Mkuu; lakini akaja kubadili mawazo baadaye.

" Kwenye siasa JK (Kikwete) hatabiriki. Kwenye mchakato wa kuelekea kutafuta mgombea urais wa chama kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Kikwete aliwashawishi baadhi ya wana CCM maarufu kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo.

" Mimi ninawafahamu watu ambao Kikwete mwenyewe aliwashawishi wachukue fomu za urais na kwamba yeye mwenyewe angewasapoti. Walichukua fomu na wakaja kujua baadaye kwamba Kikwete hakuwa na nia ya kuwaunga mkono.

" Hivyo inawezekana kabisa kwamba Sitta aliambiwa na Kikwete maneno hayo. Kwenye kitabu cha Lao Zu, kiitwacho The Art of War, kuna sehemu anasema ' All Warfare is based on deception'. Kwamba vita yoyote inapiganwa na kushindwa kwa kulaghai.

"Kikwete ana kipaji hiki cha kukuahidi kitu ambacho hatakupa. Yeye huwa anaangalia mwishoni atapata nini kwa kukuahidi alichokuahidi," alisema mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM wa mojawapo ya mikoa ya Tanzania Bara.

Mwili wa Sitta ambaye ameacha mjane na watoto unatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote wiki hii.

0 comments:

Post a Comment