Friday, 5 February 2016

[wanabidii] Agizo la Rais Magufuli kwa wenye mashamba na viwanda aliposimama njiani kuwasalimu wananchi



Agizo la Rais Magufuli kwa wenye mashamba na viwanda aliposimama njiani kuwasalimu wananchi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watu wote waliotelekeza Mashamba na Viwanda walivyouziwa na serikali, kuhakikisha wanafufua mashamba na viwanda hivyo mapema iwezekanavyo, kabla serikali haijavinyang'anya na kuwagawia wanaoweza kuviendesha.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake njiani, wakati akisafiri kwa gari kutoka Dar es salaam kwenda Dodoma.

Amesema mkoa wa Morogoro ulikuwa na viwanda vingi na mashamba mengi makubwa ambayo kama waliouziwa wangeyaendeleza, yangezalisha ajira na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwandani na Mazao ya kilimo, lakini waliouziwa mashamba na viwanda hivyo wameamua kutekeleza ama kubadilisha matumizi, huku wengine wakitumia rasilimali hizo kuombea mikopo katika mabenki jambo ambalo serikali yake haitalikubali.

"Kama nilivyowaahidi wakati wa kampeni na leo narudia, wote walioamua kutumia mashamba na viwanda walivyouziwa na serikali kwa ajili ya kuchukulia mikopo kwenye mabenki badala ya kufanya uzalishaji wavifufue haraka, vinginevyo tutawanyang'anya" amesisitiza Rais Magufuli huku akishangiliwa na wananchi waliomsimamisha katika eneo la Msamvu Mjini Morogoro.

Rais Magufuli pia amesimamishwa na kuwasalimu wananchi wa Wami Dakawa, Magole na Dumila ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa atatekeleza ahadi yake ya kuwapa mashamba atakayonyang'anya kutoka kwa walioyatelekeza, amewataka kuachana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji na badala yake watatue migogoro hiyo kwa kutumia njia za kisheria.

Aidha, amewataka viongozi wote wa Mkoa hadi vitongoji kushirikiana kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kabla haijasababisha madhara, na
ameonya kuwa migogoro hiyo ikileta madhara itakuwa ni kigezo tosha kuwa viongozi hao wameshindwa kutekeleza wajibu wao na wanapaswa kuachia ngazi.

Pamoja na hayo Rais Magufuli amewahimiza wananchi hao kuchapa kazi kwa juhudi hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha, na pia wahakikishe kuwa watoto wote wanaopaswa kuandikishwa shule wanapelekwa shule, hasa baada ya serikali kuamua kutoa elimu bure ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

"Tumeamua kutoa elimu bure na tutatoa elimu bure, na jambo hili limeonesha mafanikio makubwa kwa kuwa hata shule zilizotarajia kuandikisha wanafunzi 45 zimejikuta zikiandikisha hadi wanafunzi 600 kwa darasa moja" alibainisha Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amekagua kipande cha barabara kuu ya Morogoro - Dodoma kilichoharibiwa na maji ya mvua katika eneo la Kibaigwa Mkoani Dodoma, na kujionea kazi za ukarabati zinazofanywa na wakala wa barabara nchini (TANROADS).

Amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, kuongeza wakandalasi wa kukarabati eneo hilo ili kazi ikamilike haraka badala ya kusubiri mpaka baada ya miezi miwili ilivyopangwa na wizara.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kesho tarehe 06 Januari, 2016 atashiriki maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitakazofanyika katika uwanja wa Namfua, Mjini Singida.

Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma

05 Januari, 2016


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment