Monday, 27 April 2015

[wanabidii] Re: [Wanazuoni] Marufuku Ya Vyama Kuwa Na Vikosi Vya Ulinzi Ni Ya Kuungwa Mkono...

Marufuku hii inahusu vikosi vya ulinzi vya CCM pia, yaani Polisi, FFU, n.k.? Kama vyama vya upinzani vingekuwa na imani na kazi inayofanywa na vyombo hivi sidhani kama vingeona umuhimu wa kugharimika kulipa vijana kulinda maslahi yao.
 
Charles.
------------ --------- --------- --------- -------
'Black Cat/White Cat. It's a Good Cat If It Catches Mice.'   - Deng Xiaoping (1904-1997)





On Monday, April 27, 2015 9:42 AM, "Maggid Mjengwa mjengwamaggid@gmail.com [Wanazuoni]" <Wanazuoni@yahoogroups.com> wrote:


 
Marufufu Ya Vyama Kuwa Na Vikosi Vya Ulinzi Ni Ya Kuungwa Mkono
Ndugu zangu,
Nianze kwa kumpongeza Msajili wa Vyama Vya Siasa na IGP kwa kulifanyia kazi hili la vyama vya siasa kuwa na vikosi vya ulinzi.
Ingawa maamuzi ya kupiga marufuku yamekuja kwa kuchelewa, lakini, bado ni ya kupongezwa na wote wenye mapenzi mema na nchi yetu tuliyozaliwa. Ni maamuzi ya kuungwa mkono kwa nguvu zote.
Hakika, yalikuwa ni makosa makubwa katika wakati tulio nao, kuruhusu vyama vya siasa kujipa mamlaka ya kujiandalia vikosi vyake vya ulinzi kwenye nchi yenye watu waliogawanyika inapohusu itikadi za vyama. Si busara pia, kuacha makosa hayo yaendelee kufanyika, kwa vile tu, eti, vyama husika vimeweka taratibu hizo za kuwa na vikosi vya ulinzi kwenye Katiba zao. Kimsingi, vyama vyenye kupingana na marufuku hiyo vina mawili tu ya kuchagua; Mosi, kurekebisha vifungu vya katiba vyao vyenye kuruhusu kuundwa kwa vikosi vya ulinzi, au, kukubali Msajili avifute vyama hivyo. Kwa hilo la mwisho, vyama vitakuwa na uhuru wa kwenda na vikosi vyao msituni na kupambana na dola.
Vinginevyo, jukumu la kuhakikisha raia, bila kujali itikadi zao, wanahakikishiwa Ulinzi na Usalama wao linabaki kuwa ni la Serikali Kuu kupitia Jeshi lake la Polisi. Kama kuna mapungufu kwenye utekelezaji wa jukumu hilo, basi, uwepo mjadala wa kulisemea hilo na hatua zichukuliwe. Na hapa Serikali iangalie pia uwezekano wa kurefusha marufuku ya taasisi kuwa na vikundi vyake vya ulinzi, kuwa ifike mpaka kwenye taasisi za kidini.
Hakika, tunashukuru sana kwa Msajili na IGP kuitikia kilio cha wengi wetu tuliokuwa tukipinga utaratibu wa vyama kuwa na vikosi vya ulinzi. Na hapa nitakumbushia nilichoandika hapa Machi 4 kufuatia mahojiano niliyofanyiwa na mtangazaji wa Zenj FM. Alitaka kupata maoni yangu juu yanayoendelea nchini mwetu. Mtangazaji alianza kwa kuorodhesha changamoto zinazozikabili taifa anazonitaka maoni yangu.
Nilimwambia, kuwa muda wa kwenye radio ni mfupi kuzichambua changamoto hizo lukuki zikaeleweka kwa wasikilizaji. Na nikamwambia, kuwa hata hizo alizoziorodhesha ni chache.
Hata hivyo, nikamwomba mtangazaji nichambue changamoto moja kubwa ninayoiona mimi inalikabili taifa kwa sasa kuelekea Uchaguzi Mkuu. Kwamba inahusu USALAMA.
Nilisema, kwamba katika nchi yoyote iwayo, bila USALAMA kwa maana pia ya uwepo wa Amani na Utulivu, basi, hakutakuwa na maendeleo ya kiuchumi.
Kuna ishara katika nchi yetu, kuwa baadhi ya wanasiasa tuliowapa dhamana za uongozi wanaonyesha kucheza kamari na Amani na Utulivu wetu kama Taifa. Wanachokifanya ni kamari yenye matokeo ya dhahiri, kuwa kama taifa, tutakwenda kupoteza tulicho nacho.Wahenga walisema; Majuto Ni Mjukuu. Burundi na Rwanda ni mfano wa nchi jirani tu zinazojutia hata hii leo kwa kufumbia macho tunachokiona sisi leo.
Kimsingi, vinavyoitwa vikosi vya Ulinzi vya Vyama vya siasa ni moja ya kamari mbaya inayochezwa na wanasiasa itakayopelekea maangamizi makubwa. Haya ni mambo tuliyoiga tangu enzi za Ushoshalisti ambayo hata huko yalikotokea wameyaacha.
Wakati umebadilika. Katika wakati tulio nao, vijana waandaliwe ' Ukakamavu' wa kiakili kuwa na uwezo wa kuelewa itikadi, sera, madhumuni na malengo ya vyama vyao. Wafanye hivyo ili waweze kuvinadi vyama vyao kwa wapiga kura. Kazi ya ulinzi iachwe kwa vikosi vinavyotambulika kisheria na kwa mujibu wa Katiba yetu.
Nchi ina Amiri Jeshi Mkuu mmoja. Sasa hivi vikosi vya kivyama vinakula viapo vya namna gani kwenye Jamhuri? Hivi hatujui maana ya viapo vya kijeshi?
Na hata majina ya vikosi hivi vya kiwanamgambo yanatia mashaka. Mathalan, hivi hatujui maana ya Red Brigades na chimbuko lake?
Red Brigades kilikuwa kikundi cha wanamgambo wenye itikadi kali za mrengo wa kushoto za Ki-Marxist na Leninist kule nchini Italia. Kiliipata umaarufu miaka ya 70 kwa matendo yake ya kutumia njia za utekaji nyara. Mwaka 1970, Red Brigades ilifahamika zaidi kwa kufanikiwa kumteka nyara na hatimaye kumwua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Aldo Moro.
Na si wengi wenye kufahamu, kuwa ni mwaka ule 1978, Mnajimu Sheikh Yahya Hussein alipata umaarufu zaidi kwa kuaminika kuwa alitabiri tukio lile la Aldo Moro kutekwa nyara na Red Brigades. Ni kupitia utabiri wake mwanzoni mwa mwaka huo, kuwa mwaka huo wa 1978 unheshuhudia kiongozi mmoja mashuhuri akitekwa nyara.
Kwa kuhitimisha, nikashauri kupitia mtangazaji yule wa Zenj FM, kuwa umefika wakati wa Serikali kupiga marufuku ya uanzishaji na uendeshaji wa vikundi hivi vya wanamgambo wa vyama. Vyama vya siasa viachwe kufanya siasa, na Jukumu la Ulinzi liachwe kwa vyombo vya ulinzi vyenye kutambulika kisheria na kikatiba. Neno langu la mwisho likawa; Hatujachelewa.
Maggid,
Dar es Salaam.

__._,_.___

Posted by: Maggid Mjengwa <mjengwamaggid@gmail.com>
Reply via web post Reply to sender Reply to group Start a New Topic Messages in this topic (1)

.

__,_._,___


0 comments:

Post a Comment