Nikiwa mpenzi wa "ukweli usiyotiliwa shaka", nimeshawishika katika kuonyesha upungufu yaliyomo kwenye makala ya Padri Baptiste Mapunda iliyochapishwa kwenye Toleo Na. 230 la Machi 14 hadi 20, 2012, ukurasa wa 5, Raia Mwema (ISSN 1821 – 6250) yenye kichwa, "TANZANIA NA OIC: ambapo leo hii kila mwenye ajenda ya siri na OIC anaitumia makala hiyo ktk uchambuzi wake.
Lijue lengo kuu la Azimio la Abuja" kama ilivyoandikwa na Padri Baptiste Mapunda (wa Kanisa Katoliki).Padri Mapunda ameanza kwa utangulizi wenye kulielezea tamko (linaloitwa Abuja Declaration) na taathira ya tamko hilo kwa
Tanzania! Ili kupata matini ya dhamira ya utangulizi wake tutazame ushahidi huu:
"Baada ya kulisoma, nikaridhika na nikaunganisha yanayotokea katika nchi yetu ya Tanzania, juu ya harakati za wenzetu Waislamu ikiwa ni utekelezaji wa tamko hilo muhimu la Abuja." Bila ya kuonyesha harakati za Waislamu wa Tanzania na taathira ya moja kwa moja ya tamko hilo (kama limeridhiwa na Waislamu wa Tanzania au la), Padri Mapunda ameridhika na kuunganisha na kutoa hukumu ya moja kwa moja.
Hapa kuna hoja mbili muhimu ambazo Padri Mapunda alihitajika (kwa mujibu wa uchunguzi na mantiki inayoufanya utafiti uwe wa kisayansi). Kwanza, kwa kuwa tamko la Abuja (Abuja Declaration) lililotolewa tarehe 28, Novemba 1989
nchini Nigeria limekuwapo kwa takriban miaka 22 sasa; na kwa kuwa (kama anavyodai Padri Mapunda) lengo lake lilikuwa kuzifuta imani nyingine zisizokuwa
Uislamu;
nadhani ilikuwa vema aonyeshe jinsi tamko hilo lilivyoathiri Ukristo katika Tanzania na au hata aonyeshe jinsi lilivyotafsiriwa na kufanyiwa kazi na Waislamu wa Tanzania. Pili, (Waislamu wa) Tanzania si miongoni mwa nchi zilizoshiriki na au hata kuridhia tamko hilo; kwa jinsi hiyo, Padri Mapunda alitakiwa aoneshe kisayansi jinsi tamko hilo lilivyowaathiri Waislamu wa Tanzania hata yeye (Padri Mapunda) kufikia hatua ya kuunganisha yale aliyoyaita matukio yanayotokea Tanzania na "tamko la Abuja.".
Padri Mapunda, katika kusisitiza dhamira ya uandishi wa makala yake, anaandika hivi: "Inadaiwa kwamba katika yote hayo lengo kuu la OIC na hasa kupitia Azimio la Abuja ni kuona kwamba Bara lote la Afrika linakuwa la Kiislamu."
Nilistushwa sana na maelezo haya kwa vile mantiki inaonesha kwamba mwandishi (Padri Mapunda) anaandika hapa kwamba, "inasadikiwa" kana kwamba yeye aidha
hajasoma malengo ya OIC au ameamua kwa makusudi kuwapotosha wasomaji wasielewe dhana hizi mbili; yaani OIC na tamko (Azimio) la Abuja."
Katika hali hii imenifanya kufanya upitizi kwa mara nyingine ili nijiridhishe juu ya malengo ya OIC; kwa ujumla, malengo ya OIC kwa mujibu wa Hati Idhini (OIC Charter) hayajabadilika tangu yalipoidhinishwa na wanachama wake.
Akitumia uandishi wa "ujanja wa mbuni kuficha kichwa mchangani ilhali mwili wake uko nje", Padri Mapunda anaandika hivi: "Huu ndio ukweli wa mambo wala si uchochezi wala si propaganda ukitaka ukweli nenda tu kwenye internet utaupata najisomee maandishi mbalimbali juu ya umoja huo wa nchi za Kiislamu, yaani OIC."
Nadhani mwandishi huyu alijua kwamba alichoandika ni"uchochezi" kwa kuwa suala la Tanzania kujiunga na OIC limekuwa likipigwa danadana na serikali yaTanzania kwa shinikizo la Kanisa Katoliki (hili linafahamika). Na vilevile Padri Mapunda anafahamu kwamba alichoandika ni "propaganda;" yaani, uongo uliokolezwa chumvi nyingi dhidi ya OIC!Kwa kujaribu kumuweka sawa Padri Mapunda na "uchochezi" na "propaganda" zake naomba hapa nichore mifano michache ya nchi wanachama wa OIC na demografia yake kidini.
OIC (kwa mujibu wa takwimu za karibuni) ina nchi wanachama zinazokadiriwa kufikia 57 na miongoni mwa nchi hizo ni: Msumbiji (Mozambique); Togo; Lebanon; Uganda; Burkina Faso; Cameron; na Nigeria.
Kwa nchi zilizotajwa tujaribu kuangalia nchi nne (4) kwa uwiano wa kidini kwakurahisha ufafanuzi. Msumbiji ilijiunga mwaka 1994 ina Wakristo asilimia 56.1(%), Waislamu asilimia 17.9 (%) na dini nyingine asimilia 26 (%). Kwa maana hiyo Msumbiji ni nchi yenye Wakristo wengi na iliamua kujiunga na OIC, siyo?
Togo ilijiunga na OIC mwaka 1997 ina dini za kienyeji asilimia 51 (%), Wakristo asimilia 29 (%) ilhali Waislamu asilimia 20 (%). Hii ina maana kwamba, Togo si nchi ya Kiislamu lakini ni mwanachama wa OIC! Na kielelezo kingine ni Cameroniliyojiunga mwaka 1975 ina Wakristo asilimia 69 (%), Waislamu asilimia 21 (%) na dini nyingine asilimia 10 (%). Kwa udondozi huu Cameron ni nchi yenye Wakristo wengi kuliko dini nyingine na ni mwanachama wa OIC.
Tumalizie kwa mfano kutoka Afrika ya Mashariki; Uganda ilijiunga mwaka 1974 (inawezekana hoja ikawa kwamba wakati huo ilikuwa ikitawaliwa na Idd Amin Dada ambaye alikuwa Muislamu) ina Wakristo asilimia 84 (%) na Waislamu wakiwa asilimia 12 (%). Uganda ni nchi yenye Wakristo wa madhehebu ya Roman Katoliki kama asilimia 41.9 (%) na kwa kujiunga kwake tangu 1974 hadi leo (ni mwanachama) na hatujasikia nchi hiyo imekuwa ya Kiislamu kama
anavyodai Padri Mapunda!
Nadhani kungekuwa na hoja nyingine juu ya "Islamization of Africa"lakini kwa kutumia uandishi wa uchochezi na au propaganda zilizopitwa na wakati kwa kutumia ukweli "ghushi" unaotengenezwa na mashine za propaganda
kama "The Ministry."
Katika kuweka dhana na kuthibitisha falsafa ya
uchochezi na propaganda dhidi ya Waislamu na Uislamu, Padri Mapunda anaandika hivi, "Sehemu ya madhumuni ya OIC, kupitia tamko la Abuja ni kufuta katika hali zote imani ya dini isiyo ya Kiislamu katika nchi wanachama.
Na imani ambazo zitabidi zifutwe ni dini ya Kikristo, na nyinginezo ambazo hazikubaliani na imani ya Kiislamu." Haya ni madai mazito sana kuandikwa na mtu anayedhaniwa kwamba ni "kiongozi wa kiroho" na padri wa Kanisa
Katoliki linaloamini juu ya makosa dhidi ya kweli kama inavyobainishwa kwenye fungu la 2475 la Katekisimu ya Kanisa Katoliki!Kwa ujumla, Uislamu unakataza kumlazimisha mtu yoyote kuingia kwenye Uislamu kwa nguvu (tazama Qur'an 2: 256).
Kwa katazo hilo, vilevile Uislamu umeweka wazi juu ya dhana ya kila mtu kuwa na dini yake (tazama Qur'an 109: 1 – 6) kwa falsafa na matini ya aya hizo sidhani kama alichonukuu Padri Mapunda ndio ufafanuzi wa kweli na haki juu ya malengo ya OIC, kama inavyodai makala yake.
Padri Mapunda amejaribu kuonyesha vurugu na sintofahamu zinazotokea Nigeria na lile analoliita Azimio la Abuja! Nadhani hapa pana hoja chaparare inayohitaji (hata hivyo) kujibiwa; kama tamko la Abuja (Abuja Declaration)
liliasisiwa miaka 22 iliyopita,
Boko Haram iemanzishwa na tamko hilo?Je, kwa kila vurugu za kidini na au sintofahamu na mauwaji ya kidini chanzo chake ni tamko la Abuja? Nadhani hii haitakuwa sahihi kwa kuwa suala la vurugu, sintofahamu, songombingo na hata
mauwaji ya kidini yamekuwa yakitokea duniani kutokana na sababu za kibinafsi zaidi
kuliko za dini yenyewe.
Tuchukuwe mfano wa vita vya kidini ndani ya dini moja moja na kwa madhehebu tofauti, kama mfano! Waislamu wa madhehebu ya Sunni na wa madhehebu ya Shia wamekuwa wakipigana na hata kuuwana sehemu tofauti za dunia ya Waislamu; kama wanavyouwana waamini wa madhehebu ya Kikristo (rejea mauwaji yaliyokuwa yakitokea Ireland ya Kaskazini kati ya Wakatoliki na Waprotestant); na hapa napo tusemeje?
Cha kusikitisha sana Padri Mapunda anaandika kwa uangalifu mkubwa sana kwamba:
"Ukichunguza kwa kina unaweza kubaini kwamba utekelezaji wa Azimio la Abuja unakuja polepole, hauna haraka.
Na ninasema wazi kwamba katika uchunguzi wangu nchini Tanzania, mipango hii pia imeanza kutekelezwa kimya kimya na kwa uangalifu mkubwa sana." Hapa inaonyesha kwamba Padri Mapunda amefanya utafiti wa kina na wa kutosha na anazo data (na taarifa) rasmi juu ya matokeo ya taathira ya lile analodai ni Azimio la Abuja.
Padri Mapunda, kama muamini na kiongozi (kwa ngazi ya upadri) anapaswa kufuata vema na kwa makini fungu la 2478 la Katekisimu ya Kanisa Katoliki linalotamka kwamba: Ili kuzuia hukumu ya haraka, kila mmoja awe mwangalifu kadiri inavyowezekana kutafsiri mawazo, maneno, na matendo ya jirani yake kwa namna nzuri.
Hapa naomba nieleweke kwamba jirani ya Wakristo katika Tanzania ni Waislamu (tunaishi ndani ya paa moja la Tanzania) kwa hiyo ni vema na hakitukiheshimiana kwa tofauti za dini zetu, tukipendana kama watoto wa Baba Mmoja (Adam) na tukiabudu kwa kila mmoja na dini yake ilhali wote tunamuelekea Mungu Mmoja kwa imani tofauti.
Uislamu, kama mfumo maisha, hauwezi kumlazimisha yoyote kuingia kwenye dini (Qur'an 2: 256) na dini inayotumia zaidi hekima na mawaidha mema (Qur'an 16:125)
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment