Saturday, 10 May 2014

[wanabidii] UKAWA wanapigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar?

KATIKA mada aliyoitoa Machi 31, mwaka huu wa 2014 kwa vijana wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, Profesa Issa Shivji alionyesha wasiwasi kuwa mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo wa Muungano wa Serikali tatu yangeibua hisia za utaifa wa Tanganyika na Zanzibar.

Maoni haya ya Profesa Shivji yalipingwa na Tume yenyewe pamoja na watu kadhaa, tena kwa maneno makali yaliyomshambulia Profesa Shivji binafsi na kuachana na hoja zake. Wakosoaji wa Profesa Shivji walienda mbali zaidi na hata kumtuhumu kwamba amenunuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Utamaduni wa kutuhumu watu kununuliwa umeanza kuota mizizi na kugeuka kuwa ugonjwa wa kitaifa katika nchi hii. Kwamba kila mtu asiye mwanachama wa CCM anapaswa kutoa maoni yasiyofanana na msimamo wa CCM. Ole wako utoe maoni yako ambayo kwa bahati nzuri au mbaya yakaendana na maoni na msimamo wa CCM basi unaingizwa kwenye orodha ya watu walionunuliwa na chama hiki. Huu ni udhaifu mkubwa sana katika ujenzi wa hoja. Hata hivyo, hii si hoja yangu kwa leo.

Hoja yangu ya leo ni kwamba kile kilichoonekana kwamba ni hofu ya Profesa Shivji sio hofu tena bali ni jambo halisi na la kweli kabisa. Tayari hisia za utaifa wa Tanganyika na Zanzibar zimekwishaanza kujitokeza waziwazi. Sasa watu wanavaa fulana za Tanganyika na katika mitandao ya kijamii watu wanajivunia utanganyika na sio utanzania tena.

Pengine hizi mbwembwe za kuvaa fulana na kujipaka rangi za bendera ya Tanganyika hazitishi sana kama maneno niliyoyasikia Zanzibar katika mikutano ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Kwa kiasi kikubwa, na kwa tafsiri yangu, viongozi wa UKAWA huko Zanzibar walijikuta wakipigania uhuru wa Zanzibar na Tanganyika badala ya kupigania Serikali tatu.

Sijui viongozi hawa kama walikusudia kufanya jambo hili au walijikuta wakilifanya tu kutokana na mazingira na mihemko ya kisiasa iliyokuwepo pale Zanzibar. Ili kuweka vizuri hoja yangu, naomba niwanukuu viongozi wawili wa juu wa UKAWA.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA na UKAWA katika mkutano wa Aprili 30, 2014, pamoja na mambo mengine, alinukuliwa na gazeti la moja la kila siku la Mei mosi, 2014 akiwaeleza wananchi wa Zanzibar kuwa: "Ni jambo la hatari katika mchakato wa Katiba ya wananchi kuwa na woga au hofu…Lazima tuwe tayari kuwaonyesha watawala kuwa tuna umoja imara, tunapigania mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar".

Katika mkutano huo huo, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA na mjumbe muhimu wa UKAWA, Tundu Lissu, alinukuliwa na gazeti jingine la kila siku la Mei mosi, 2014 akiwaambia wananchi kuwa: "Kwa sababu Zanzibar haijawa huru na Tanganyika haijawa huru na ukitaka kujua ukweli wa hili angalia vitabu, kuna jina Tanganyika limefutwa ili kuitawala Zanzibar, sasa inabidi tuseme ili kuleta uhuru wetu". Lissu aliendelea kusema; "Zanzibar inatakiwa kuwa mamlaka kamili".

Baada ya kutafakari maneno haya na muktadha mzima wa mikutano ya UKAWA huko Zanzibar nimejiuliza swali moja muhimu: Je, UKAWA wanapigania uwepo wa Muungano wa Serikali tatu au uhuru wa Tanganyika na Zanzibar?

Pamoja na kuunga mkono umoja wa vyama vya upinzani kwa ujumla wake hasa katika muktadha wa kuimarisha upinzani nchini, jambo ambalo tumeliombea miaka mingi, nalazimika kuhoji dhamira ya UKAWA katika mazingira ya Katiba mpya. Ukichunguza kwa makini maneno ya Mbowe na Lissu unaanza kupata jibu kwa nini CHADEMA na CUF waliokuwa maadui wa kisiasa hadi juzi kiasi cha kushindwa kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge huko Chalinze dhidi ya mgombea wa CCM, ghafla wamegeuka marafiki wa kisiasa bila hata makubaliano rasmi yenye ajenda ya wazi.

Kimsingi CHADEMA sasa wanapigia debe sera ya CUF, ya Zanzibar huru yenye mamlaka kamili pengine bila wao kujua. Inajulikana enzi na enzi kwamba CUF hawataki Muungano uliopo; wanataka tu ushirikiano wa kijirani wa kawaida kama ulivyo katika nchi zingine za Afrika kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) au ile Jumuiya ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS). Lakini zote hizi ni ushirikiano tu na wala sio Muungano. Ndio maana CUF wanataka Zanzibar iwe na mamlaka kamili kuhusu mambo yote nyeti, ikwemo uraia, uhamiaji, fedha, bandari, mambo ya nje na kiti Umoja wa Mataifa na wanajua fika kwamba ukishayatoa mambo haya katika Muungano huna haja ya kuwa na Muungano tulio nao.

Kwa hiyo wenye akili tunajua kwamba CUF hawataki Muungano kwa sababu huwezi ukataka Muungano na hapo hapo ukataka mamlaka kamili. Hakuna Muungano wa namna hiyo duniani bali ni ushirikiano wa kijirani.

Sasa kama hivyo ndivyo, je CHADEMA nao sasa hawataki Muungano? Na je, huu Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ni umoja wa watu wasiotaka Muungano? Kama hivyo ndivyo, kwa nini wasiweke wazi matakwa yao ili waweze kujulikana hivyo na wapate wafuasi kwa sababu hizo? Vinginevyo, viongozi wa UKAWA wana wajibu wa kutuelimisha wanamaanisha nini wanaposema wanapigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar? Uhuru huu wanaupigania kutoka koloni gani?

UKAWA wanasema kwamba wanapigania Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Lakini Rasimu ya Tume hiyo inapendekeza Muungano imara na kwa maoni ya tume pengine imara zaidi kuliko hata huu uliopo. Rasimu haiongelei uhuru wa Zanzibar au Tanganyika na wala haiongelei habari za mamlaka kamili ya Zanzibar kama walivyohubiri wao huko Zanzibar. Hivyo basi UKAWA hawawezi kutafuta uhalali wa ajenda yao kwa kujificha katika rasimu ya tume kwa kuwa wanajua rasimu hii inaungwa mkono na walio wengi.

Kwa hiyo wasiwasi wangu ni kwamba, kupitia ndimi zao huko Zanzibar, ni wazi kwamba UKAWA wanataka uhuru wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa maneno mengine hawataki Muungano au wanataka Muungano lege lege utakaojifia wenyewe mbele ya safari.

Wosia wangu ni kwamba UKAWA wanawajibika kuweka msimamo wao wazi na kututoa wasiwasi baadhi yetu tunaopenda Muungano imara bila kujali aina ya muundo na ambao tunaanza kutishwa na kauli zao.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/ukawa-wanapigania-uhuru-wa-tanganyika-na-zanzibar#sthash.W1y6hDst.dpuf

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment