Sunday, 11 May 2014

[wanabidii] SERIKALI KUHAMASISHA KILIMO BORA BILA KUWA NA SOKO LA MAZAO

Kilimo ni utii wa mgongo wa taifa hili ambao ajira yake ni zaidi ya 85%, nikimaanisha Watanzania waliojiajiri kutokana na sekta hii.Ajira ambayo ikitumika vizuri yawezekana kabisa ikakwamua uchumi wa nchi hii na watu wake kwa serikali kutilia mkazo sekta hii binafsi.

Imekuwa ni desturi ya serikali yetu kuwa kiwanda cha kauli mbiu zisizo na tija kwa kilimo,ingawa serikali imekuwa ikiweka mikakati madhubuti inayoishia kwenye makaratasi na kumuacha mkulima akitaabika na kuzeekea kwenye kilimo ilihali maafisa wa wizara ya kilimo wakiendelea kuendesha warsha,semina na makongamano mbalimbali yaliyo shindwa kumkomboa mkulima huyu lakini serikali imeshindwa kumkomboa mkulima kimkakati.

Tangu kupata uhuru wa nchi hii tumesikia kauli mbiu nyingi za sekta ya kilimo lakini kilimo hiki kimeendelea kudidimia kwa kukosa masoko ya uhakika ya kuuzia mazao ya wakulima,pamoja na ukosefu wa miundo mbinu mizuri kwa mazao ya wakulima, serikali imeendelea kumnyonya nokoa huyu na kujitwalia nafasi ya ubwana hali inayokwenda sambamba na mfumo wa utumwa.

Ukitazama kilimo cha tumbaku,unaweza kulia na ikibidi kuanzisha harakati ambazo zinaweza kuibua mbadala wa kilimo hiki kutokana na kilimo hiki kuwa cha mateso na masumbufu makubwa kwa mkulima,mkulima wa zao hili ana tumia muda mwingi kuanzia kuandaa mbegu,kusia mbegu mpaka kufikia kulima na kuvuna kwa gharama kubwa ambazo mwisho wa siku mkulima huyu anaishia kutaabika na kupoteza matumaini kwa kuwa tu ana lima kwa mazoea kilimo kisicho na ukombozi wa maisha yake ya kila siku.

Mkulima huyu amekuwa kiwanda cha kuzalishiwa madeni toka chama cha ushirika na mabenki mbalimbali yenye kunufaika na kumuacha taabani hana kitu kwa kupoteza nguvu zake,muda wake na mapato yake kwa ujumla.Kila anachogusa mkulima huyu kuhusiana na kilimo cha zao hili kinagusa riba ya mabenki moja kwa moja kwa kuwa serikali imemtengenezea mazingira ya kumwingiza mkulima kwenye kilimo cha mkopo kinachoendana na riba za mabenki.

Ni kilimo chenye gharama kubwa kiuendeshaji ambacho kinatumia mbolea nyingi zenye gharama kubwa ambazo mkulima huyu wa kupinda mgongo hushindwa kuzikabili na kuwa muathirika wa mikopo ya mabenki.Pamoja na mikopo hiyo ambayo imelengwa kwenye mazao yatakayo patikana,serikali nayo inatumia rungu lake kuchukua kodi ya mazao inayozidi mapato ya mkulima kwa kiwango kikubwa sana kitendo kinacho tafsirika kuwa serikali inatumia mabavu yake kuwanyang'anya wakulima kile walichokipata.

Hatukatai serikali kutoza kodi ili kuweza kuendesha mambo yake kwa kuwa vyanzo vya mapato vya serikali hutokana na kodi,lakini kodi hizo zikilengwa kwa kundi Fulani kutozwa kiwango kikubwa ni uonevu dhidi ya kundi hilo.Serikali ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo sekta ya madini ambayo serikali inatoza mrahaba wa 3% ilihali kwa upande wa zao la tumbaku serikali inatoza kiwango cha 78% kwa kila kilo ya tumbaku na kumwacha mkulima akinufaika na 18% ya bei ya tumbaku ambayo ndani yake kuna madeni ya benki yakiambatanishwa na riba.

Kwa mujibu wa soko la tumbaku,unaweza kuona bei ya kilo moja kabla ya makato ni shilingi 25,000/- pesa za Kitanzania,ndani ya shilingi 25,000/- kwa kilo serikali inachukua kodi yake ya shilingi 19,500/- kwa kila kilo na halmashauri ya mji/kijiji inachukua shilingi 1,000/- kwa kilo na kumuacha mkulima huyu dhaifu kubakiwa na shilingi 4,500/- kwa kila kilo ambayo ndani yake kuna madeni ya pembejeo za kilimo aliyokopeshwa na mabenki bila hata serikali kutoa ruzuku kwa pembejeo hizo ili kulinda maslahi ya wakulima.

Pamoja na kodi hiyo kubwa,serikali kwa makusudi mazima imeshindwa kutoa ruzuku kwa wakulima ili angalau waweze kupunguza makali ya kilimo kwa kupunguziwa gharama za pembejeo kama vile serikali inavyojaribu kuwabeba wafanya biashara kiasi cha kuwatengea stimulus package kama fidia ya hasara ya biashara zao wanapo kumbwa na mtikisiko wa uchumi kama ilivyotokea 2010.

Stimulus package hiyo ililengwa kwa wafanya biashara wa viwanda vya pamba na kuwatenga wakulima kama vile hawana haki ndani ya nchi hii.Kitendo hicho ni dhuluma na ubaguzi wa wazi mbele ya wananchi wanao hangaikia masiha yao bila msaada wa serikali yao.

Mabenki siku zote si marafiki wa watu maskini ndo maana bila kujali kipato cha mkulima huyu wameendelea kuwakata madeni yao yote na kumuacha mkulima akiwa hohehahe taabani.Wabunge wapo,tena wanatoka maeneo hayo yanayolimwa tumbaku lakini wamenyamaza kimya wana subiri posho ya kukaa bungeni ilihali wakulima wa maeneo yao wana taabika bila msaada wowote.

Pamoja na dhahama zote wanazo kumbana nazo wakulima,bado masoko ya mazao yao yananunuliwa kwa mfumo wa kukopwa mazao yao.Kwa hali hii utaona kuwa hata ile kauli mbiu ya kilimo kwanza haina tija kwa mkulima huyu wa jembe la kupinda mgongo.Wanao nufaika na mazao haya ya wanyonge ni vikundi Fulani vichache vinavyojiita chama cha ushirika cha mkoa,mabenki yanayo kula riba kutokana na zao hili na wajanja wachache kwenye bodi ya tumbaku.

Serikali inalijua hili lakini imekaa kimya.Huu ni ufisadi mkubwa wanao fanyiwa wakulima zaidi ya ule wa Richmond unaofanywa na serikali yao sikivu.
Kuna haja sasa kwa serikali kulitazama jambo hili kwa mapana na marefu ili kuweza kuongeza ari kwa wakulima waweze kujikomboa na kutumia fursa ya kilimo kujikwamua kutokana na lindi la umasikini uliokithiri.

Kitendo cha serikali kuwa na mipango isiyo na utekelezaji ni usaliti kwa sekta hii kwa kuwa ikitumika vilivyo sit u itawakomboa wakulima bali taifa litaondokana na baa la njaa linalosababisha wananchi kupanga misururu mirefu ya kusotea mahindi ya msaada ilihali nchi yetu ina rutuba nzuri iliyozungukwa na mito na mabonde yenye maji ya kutosha kuikombo nchi kiuchumi ikiwa yatatumika ipasavyo.

Kuendelea kuendesha nchi kwa kauli mbiu ni kuwahadaa wananchi na serikali kujipaka mafuta kwa mgongo wa chupa kwa kuwa si wanaongopewa ni wananchi pekee hata serikali pia inajiongopea kwa uongo ambao mwisho wa siku ni aibu kwa wenyewe.

Tunataka kilimo cha vitendo na mfano,kilimo ni uti wa mgongo,siasa ni kilimo,kilimo cha kufa na kupona,mapinduzi ya kijani na kilimo kwanza havitakuwa na tija ikiwa serikali haina mkakati wa kweli wa kulikomboa taifa kwa kutumia ardhi yetu nzuri.

Lakini pia kilimo pekee bila kuwa na mapinduzi ya viwanda ni sawa na kuchemsha maji kwa miale ya jua ukitegemea yatafikia nyuzi 100.Serikali ifufue viwanda vyote kama kweli ina nia ya dhati,vinginevyo wananchi wataendelea kulalamikia umasikini wao na rais wao hatojua ni kwanini wananchi wake ni maskini ilihali nchi ina utitiri wa rasilimali..

Tukiacha usanii kwa maisha ya wananchi wetu na kujikita kwenye uhalisia wa matatizo yetu hakika utatuzi wa matatizo yetu unaweza kupatiwa uvumbuzi wa kina na kuifanya nchi kuwa kimbilio la wanyonge wenye kuweza kupata sehemu ya ukombozi wa maisha yao.

Serikali kujinadi ina hazina kubwa ya chakula hakuleti mantiki kwa kuwa wananchi wake ni wahanga wa mfumo kandamizi wa kilimo.Kwa kulijua hili na anguko la bei ya mazao yetu kutokana na udhibiti wa masoko toka nje ya nchi kwa wakulima wetu,serikali imejikita kwenye sera ya kilimo chenye tija na sio kwenye kilimo chenye kujenga thamani ya mazao.Wataalamu wetu ndiyo waliotufikisha hapa kiasi cha ofisi ya waziri mkuu kuzungumzia tija ya mazao bila kutaja umuhimu wa soko la mazao hayo.

Si pamba tu kila zao la biashara ni kizungumkuti,sheria ndiyo sheria hazina upenyo wa kumkomboa mkulima zaidi ya kumkandamiza na kumnyonya kwa kutumia sheria.Matokeo yake wakulima wamekuwa wafungwa wa mazao yao bila kupata suluhisho la matatizo yao.

Hatuwezi kuendesha nchi kwa serikali kutunga sheria za udhibiti wa wakulima zinazo tungwa na bodi za mazao na kufungua wigo mpana kwa wafanyabiashara wajanja kuwanyonya wakulima na kuwageuza wakulima manamba wanao lipwa ujira mdogo kwa kazi kubwa.

Kwa kuwa serikali yetu ni sikivu,na kwa kuwa 85% ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo,na kwa kuwa bodi za mazao zimeshindwa kutoa ufumbuzi na suluhisho la matatizo ya wakulima kuna haja sasa kwa serikali kuzipitia sheria hizi upya ikiwa ni pamoja na kuvunja mfumo wa umangimeza ndani ya bodi hizi kwa kuzivunja bodi zenye na kuwashirikisha wakulima juu ya mfumo gani wanaodhani ni rafiki wa matatizo yao kwa utatuzi.
Tukiendelea kufanya siasa kwa maisha ya walio wengi kwa michezo ya kuigiza na makongamano yasiyo na ufanisi kwa utendaji mbovu wa wa kilimo hakika kilimo nacho kitawakimbia wakulima.Tunapozingatia na kuhamasisha kilimo bora tukumbuke na soko imara la mazao bora ili mkulima aweze kunufaika kwa alichokihangaikia.
Like · 

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment