TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Kikwete awasili Japan, kukutana na Waziri Mkuu kesho asubuhi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amewasili nchini Japan jioni ya leo, Jumatano, Mei 29, 2013,
kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Kuzungumzia Maendeleo ya Afrika
ujulikanao kama Tokyo International Conference on African Development
(TICAD - V) unaoanza Yokohama, mji mkubwa wa pili katika Japan,
Jumamosi, Juni Mosi hadi 3, mwaka huu, 2013.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Narita mjini Tokyo, Rais
Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete amepokewa na Balozi wa
Tanzania katika Japan Mheshimiwa Mama Salome Sijaona na maofisa
wengine wa Ubalozi wa Tanzania katika Japan.
Rais Kikwete amewahi kuwasili nchini Japan kabla ya Mkutano wa TICAD
V kwa vile ni mmoja wa viongozi wawili wa Afrika waliopangwa kuonana
na Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shinzo Abe kabla ya kuanza kwa
Mkutano wenyewe wa TICAD V.
Mheshimiwa Abe ambaye ndiye amemwalika Rais Kikwete kufanya ziara ya
kikazi ya wiki moja katika Japan wakati huu anakutana na Rais Kikwete
mapema ili kuweza kupata maoni, msimamo na matarajio ya Afrika kabla
ya kuanza kwa Mkutano wa TICAD V.
Mkutano wa mwaka huu utakwenda sambamba na sherehe za kumbukumbu ya
miaka 20 ya Mkutano wa TICAD ambao ulifanyika kwa mara ya kwanza mjini
Tokyo mwaka 1993.
Mkutano huo – TICAD V utawashirikisha viongozi wa Afrika, viongozi wa
Japan na washirika wa maendeleo ya Afrika ikiwamo Benki ya Dunia (WB),
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa
Afrika (AU) na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na
utafunguliwa na Waziri Mkuu wa Japan mwenyewe, Mheshimiwa Abe.
Wengine waliopangwa kuzungumza kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi wa
Mkutano huo mkubwa ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam
Desalegn ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa
Kamisheni ya Afrika Mheshimiwa Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma.
Mbali na kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Abe, Rais Kikwete pia
atakuwa miongoni mwa kundi la viongozi wa Afrika watakaokutana na
Mfalme wa Japan, H.M. Akihito.
Katika mkutano kati ya viongozi hao wawili, Waziri Mkuu wa Japan
anatarajiwa kuwa atatangaza kuwa Japan inaifutia Tanzania deni la dola
za Marekani milioni 220 likiwa ni deni la mchele ambao Tanzania
iliupata kutoka Japan chini ya mikataba iliyotiwa saini kati ya mwaka
1980 na 1983 kati ya Mamlaka ya Chakula ya Japan na Serikali ya
Tanzania.
Aidha, inatarajiwa kuwa Mheshimiwa Abe atatangaza rasmi kuwa Japan
itagharimia ujenzi wa barabara ya juu kwa juu (fly-over) katika eneo
la Ubungo, Dar es Salaam, kama moja ya hatua za kupunguza msongamano
wa magari katika jiji hilo.
Kabla ya kuanza TICAD V, Rais Kikwete pia atakutana na kuzungumza na
wakuu wa mashirika makubwa na kimataifa ya kibiashara na uchumi ya
Japan ambayo yanaendesha shughuli zake katika Afrika ama yanapenda
kuanzisha shughuli katika Tanzania.
Kesho, Alhamisi, baada ya kuwa amekutana na Mheshimiwa Abe, Rais
Kikwete atakwenda Kawasaki ambako atakutana na viongozi wa Kampuni ya
Natori Holding Management ambayo imeamua kuwekeza katika sekta ya nguo
na kilimo cha pamba katika Tanzania.
Baadaye kesho, Mheshimiwa Rais atatembea Jumba la Makumbusho la
Sayansi la Kampuni ya Toshiba, maarufu duniani kwa utengenezaji wa
kompyuta za aina ya Toshiba na vifaa vingine vya elektroniki. Baadaye,
Rais atatembelea na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya WASEDA kuhusu
nafasi na mchango wa Tanzania katika uhusiano wake na Japan.
Keshokutwa, Ijumaa, Rais Kikwete atatembelea Shirika la Sumitomo
ambalo limewekeza katika ujenzi wa kituo cha umeme cha Kinyerezi cha
Dar Es Salaam ambacho kitatoa megawati 220 na linataka kuwekeza
katika miradi ya miundombinu kwa kushirikiana na sekta binafsi katika
Tanzania.
Akiwa Sumitomo, Rais Kikwete atashuhudia utiaji saini wa ujenzi wa
mradi wa umeme wa Kinyerezi baina ya Sumitomo Corporation yenyewe,
Benki ya Maendeleo ya Japan – JBIC na Wizara ya Fedha ya Tanzania.
Mchana wa keshokutwa, Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa viongozi
wachache wa Afrika walioalikwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Abe
kuzungumzia hali ya Somalia.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Abe anataka kupata mawazo ya viongozi
hao wachache wa Afrika ambayo yatawasilishwa kwenye Mkutano wa 39 wa
wakuu wa Nchi Tajiri na Zenye Viwanda Vingi Duniani – G-8 uliopangwa
kufanyika Lough Erne, Uingereza mwezi ujao, Juni 17-18, 2013.
Aidha, Rais Kikwete siku hiyo hiyo, atakutana na kufanya mazungumzo na
uongozi wa Kampuni ya Marubeni, moja ya makampuni makubwa zaidi ya
biashara katika Japan ambayo imeonyesha nia ya kujenga Kiwanda cha
Kuchakata Gesi Asilia na Kuzalisha Umeme katika Tanzania.
Jioni ya siku hiyo, Rais Kikwete atahudhuria hafla maalum ya kitaifa
inayoandaliwa na Mheshimiwa Abe kwa ajili ya viongozi wote
watakaohudhuria Mkutano wa TICAD V.
Mkutano wa TICAD V miongoni mwa mambo mengine utajadili mchango wa
sekta binafsi, biashara na uwekezaji kama injini za maendeleo, jinsi
gani Afrika inavyoweza kuimarisha sekta ambazo zimejithibitisha kuwa
misingi ya kukua kwa uchumi wa Bara la Afrika, Ajenda ya Maendeleo
baada ya mwaka 2015 ambao ni mwisho wa utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia (MDG's). Hatimaye, mkutano huo utatoa Azimio ya
Yokohama 2013 na Mpango wa Utekelezaji wa Yokohama kwa miaka 2013 hadi
2017.
Mikutano ya TICAD (TICAD Policy Forum and Conference) ilianzishwa
mwaka 1993 na Japan kwa kushirikiana na UN, UNDP na Benki ya Dunia kwa
njia ya kujadili na kuendeleza ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika.
Chini ya mchakato huo wa TICAD, Japan hujenga mazingira ya kuunga
mkono ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika ambalo nalo ndilo
linamiliki na kuongoza jukumu la kimsingi la kujiendeleza kwa
kushirikiana na Bara la Asia na Jumuia ya Kimataifa.
Tokea ulipofanyika mkutano wa kwanza – TICAD 1 mjini Tokyo Oktoba 5-6,
mwaka 1993, imefanyika mikutano mingine mitatu na kujenga mazingira
mazuri zaidi ya jinsi Japan na Jumuia ya Kimataifa inavyoweza
kuchangia maendeleo ya Afrika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Mei, 2013
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 comments:
Post a Comment