Hivi karibuni tumesoma makala nyingi zilizoandikwa na Watanganyika na chache zilizoandikwa na Wazanzibari kukhusu muungano. Makala nyingi zilizoandikwa na Watanganyika zilikuwa zikiusifu na kuutukuza muungano, lakini makala na barua nyingi zilizoandikwa na Wazanzibari, khasa katika mitandao, zilikuwa zinaonesha wazi kutokuridhika kwao na muungano na wengine kutaka muungano uvunjike leo kabla ya kesho. Katika maelezo ya Wazanzibari wengi unaona wazi kuwa muungano umewabana vibaya sana kiuchumi na katika mambo mengi mengineyo yanayoendesha nchi, na tumesoma vile wanavyoona uchungu kuiona nchi yao ilivyotawaliwa kwa mabavu na Tanganyika. Lakini Watanganyika wengi hawahisi hivyo; wanaona utawala wao ni bora kuliko tawala zote zilizotangulia.
Utawala wa Tanganyika kuitawala Zanzibar una muundo wa ukoloni wa Kifaransa ambao ni tafauti na wa Kiingereza. Waingereza walitawala makoloni yao na waliotawaliwa walijua moja kwamoja kuwa wametawaliwa. Lakini, Mfaransa alizifanya koloni zake kuwa ni sehemu ya Ufaransa na mtawaliwa alikuwa na haki ya kuwa "Mfaransa" na hata kuhamia Ufaransa bila ya matatizo na kuweza kushiriki katika maisha na siasa za huko Ufaransa. Huu ndio muundo wa ukoloni wa Tanganyika juu ya Zanzibar. Wafaransa wengi sio kuwa walistaajabu tu kwanini katika hali kama hiyo ya watawaliwa kuwa wana haki Ufaransa kudai uhuru wao, bali Wafaransa wengi waliudhika sana kuona nchi zilizotawaliwa kudai uhuru wao. Sasa nenda ukawaulize waliotawaliwa na Wafaransa, kama vile Algeria, Ngazija na kwingi kwingineko, kwanini basi wakadai uhuru wao usikilize jawabu zao. Watanganyika pia, kama Wafaransa, wanastaajabu sana wanapowasikia Wazanzibari wengi wakidai uhuru wao watokane na utawala wa mabavu wa Kitanganyika, lakini Wazanzibari wengi wanaoathirika na muungano hawana taabu ya kukuelezea yanayowaathiri wao na nchi yao.
Hivi karibuni tumeshuhudia pia gwaride la majeshi ambalo lilikuwa ni sura ya muungano wenyewe. Waswahili wana msemo usemao "mwenye macho haambiwi 'tazama'." Gwaride lilikuwa ni sauti kubwa na ya uwazi kabisa kuwa haya majeshi ndiyo yatakayoulinda muungano. Ukoloni uliokuwa na nguvu kubwa za kijeshi siku zote uliwadharau watawaliwa walipodai haki zao kwa kuwaona watawaliwa ni watu duni na watawala kujiona kuwa wanalo jeshi kubwa na kwa kuamini kuwa nguvu za kijeshi ndizo zitakazowashinda wananchi wanapodai haki yao ya kuishi katika nchi yao huru. Wakoloni waliamini sana kuwa bunduki na risasi zitaweza kuuwa upiganiaji wa uhuru na haki za wananchi waliotawaliwa kimabavu. Watanganyika wenye fikra kama hizi hawajasoma vizuri katika taarikh za ukoloni, na la kusikitisha zaidi ni kuwa hawajasoma vya kutosha kutokana na taarikh yao wenyewe tokea walipoonekana kama ni watu duni na Watawala wao mpaka mtawala mwenyewe kusalimu amri na kuwapa uhuru wao watawaliwa wananchi wa Tanganyika.
Uundaji wa muungano wenyewe, tokea awali, ulikuwa hauna uhalali wowote kutokana na wananchi wala haukuwa na lengo la "umoja" wa haki bali ulikuwa na lengo la kukandamiza. Haiwi ukitaka kuunda "Serikali ya Umoja wa Kitaifa" bila ya kupata ridhaa za wananchi, lakini kuunda kubwa zaidi la muungano na nchi nyingine iwe Marais wawili — Nyerere na Karume – ndio inatosha waamue kufanya hivyo, na baada ya kuungana ndiyo wafanye mazingaobwe yao ya kuuhalalisha muungano batil; hili halikubaliki. Ubaya mkubwa sana ni kuwa Marais hao wawili walizifanya nchi wanazoziwakilisha mamlaka zao binafsi na wakachukua khatua bila ya kuwashauri wananchi kwa njia ya kura ya maoni. Hata mashirika ya biashara hayawezi kuungana bila ya wenye mali zao katika mashirika hayo kuulizwa na kushirikishwa katika kuamua huo muungano. Mashirika mengine inabidi kuwauliza wote waliokhusina na mashirika hayo – wamiliki, wafanyakazi, wanunuzi na kadhalika – Na ukizingatia usanii alioufanya Nyerere ya kumwondosha Wakili Mkuu wa Serikali ya Zanzibar asishiriki wala asiwe na nafasi ya kumshauri Karume kukhusu katiba iliyoandikwa na mawakili wake Nyerere, huku akijua fika kuwa Karume hakusoma na haelewi vizuri yaliyoandikwa kiqanuni, hili pekee linatosha kubatilisha Katiba ya Muungano. Pamepita mazingaombwe makubwa dhidi ya Zanzibar, na hii mizozano ni moja tu katika matunda ya sumu ya usanii uliopitishwa.
Wala matatizo hayatasita milele baina ya Zanzibar na Tanganyika. Wala kuziba viraka katika tambara bovu la Katiba hakutaondosha matatizo bali yatazidi tu kila kukicha. Linalohitajiwa kwanza si kuziba viraka katika tambara raru bali kuwauliza wananchi iwapo wanautaka huo muungano ama la. Pili, iwapo wanautaka pande zote mbili, uwe muungano wa aina gani? Tatu, mambo yepi yawemo kwenye muungano na yepi yasiwemo. Hivi ifanywavyo sasa ya kuchukua maoni ya wananchi wachache au wa kuteuwa ni kuendelea na usanii wa kisiasa wakati matokeo yake yameshajulikana. Hiki ni kiinimacho ambacho hakikhusiani na kuziondosha shida ziliopo na ni mazingaombwe ambayo yanazidi kuzielekeza kubaya hizi nchi mbili.
Hata wananchi wa nchi zote mbili wakisema wanautaka muungano uendelee, mungano wa serikali mbili ni kudanganyana mchana kweupe. Hainiingii akailini pawe na serikali mbili, zilizofanya mkataba wa kuunda serikali ya muungano yenye kushughulikia mambo ya muungano na pia iwepo serikali ya Zanzibar, lakini ya Tanganyika isiwepo lakini badala yake ya Mungano iwe pia ni serikali ya Tanganyika! Ni wazi kabisa kuwa usanii huu ni moja katika mbinu za kuimeza Zanzibar, kama si leo, kesho.
Kama lazima uwepo muungano, basi uwe wa serikali tatu. Mambo ya Tanganyika yawe wazi kabisa kama ni ya Tanganyika na ya Zanzibar yawe ya Zanzibar na ya muungano yawe ya muungano. Wala Zanzibar isipoteze utaifa wake na kiti chake katika Umoja wa Mataifa. Ukija muungano wa Afrika Mashariki, Zanzibar isiwakilishwe na yoyote ila na Wazanzibari wenyewe. Na ikitaka kuingia katika mikataba ya kimataifa isiwe ya kwenda kujidhalilisha Tanganyika kwa kuomba rukhsa kama aombavyo rukhsa mtumwa kwa bwana wake. Kwa mambo yalivyo hivi sasa, kila lililokuwa muhimu, Wazanzibari shuruti wakaombe rukhsa Tanganyika; na wasipopewa rukhsa hawawezi kulifanya hata jambo hilo liwe linatakiwa na Wazanzibari tisini katika mia kama kwa mfano kujiunga na OIC.
Na tujiulize masuala machache tu: Jee, utakapojadiliwa muungano na nchi nyingine kama vile Kenya na Uganda, kweli nchi hizo zitakubali pawe na muungano kama huu, yaani serikali za Kenya na Uganda ziwepo lakini ya Tanganyika isiwepo na badala yake iwe hiyo ya Muungano ndiyo ya Tanganyika pia? Watakubali pia wapoteze viti vyaao vya Umoja wa Mataifa? Watakubali wasiwe na uwezo wa kujiamulia mambo yao ya nje na wasiweze kufunga mikataba na nchi nyingine na wakitaka kufanya hivyo wakaombe rukhusa Dodoma? Au tuseme serikali ya Tanganyika iwepo lakini ya Kenye iwe haipo na ya Muungano iwe pia ya Kenya na maamuzi yote yatoke Nairobi, kweli Watanganyika wataukubali mpango huo?
Kila mwenye akili timamu na aliye mkweli wa nafsi yake katika kujibu masuala haya, atajua kuwa jawabu ni moja tu, nayo ni kuwa usanii huu na mazingaombwe yaliyofanziwa Zanzibar hakuna nchi yoyote itakayoyakubali. Mkweli wa nafsi yake atakwambia kweupe kuwa Tanganyika, Kenya na Uganda hazitakubali kupotezewa mamlaka zao kama vile Tanganyika ilivyoipoteza mamlaka na uhuru wa Zanzibar.
Kambarage na wafuasi wake hawajawahi kuwa na udugu mwema na Wazanzibari. Ndugu mwema hafikirii licha kusema hadharani kuwa angelikuwa na uwezo angeliiburura na kuitokomeza Zanzibar mbali katika Bahari ya Hindi. (Hizi ndizo hisia za chuki za ndani alizokuwa nazo Nyerere. Yaani Zanzibar isiwe karibu na Tanganyika kama ilivyo! Loo! Khatari hii; utasema Zanzibar ina maradhi mabaya sana ya kuambukiza!) Wala ndugu mwema hamghilibu ndugu yake aliyekuwa hakusoma na kumfanyia mazingaombwe ya kumyang'anya nchi yake na kuwaacha watoto wa nduguye, wananchi, katika hali mbaya sana ya kimaisha.
Kwa Wazanzibari na wengi wenye akili zao timamu, muungano huu haujaweza kudhihirisha faida zake bali ni mabaya yaliyozidi, kwani khasara zake ni kubwa zaidi kuliko faida zake. Wakati mwingi umeopotezwa kwenye muungano huu usiokuwa na uadilifu na usawa na wenye kuibana Zanzibar kwa kila njia, huku propaganda zikitangaza kuwa ni "muungano wa aina ya pekee katika Afrika ulioishi miaka 49″ bila ya kututajia sifa hata moja ya uzuri wa muungano wenyewe kwa Zanzibar. Haya ni sawa na kusema kuwa Msumbiji ilitawaliwa na Waportugizi kwa miaka zaidi ya mia nne, kwa hivyo uhusiano wa kikoloni na Upochugizi bora uachiliwe uendelee! Najuwa fika kuwa watawala walioko Tanganyika watastaajabu na kukereka kulinganishwa na Waportugizi, na kustaajabu kwao na hadi kuudhika kwao ni alama kubwa ya kuwa bado hawaelewi kuwa utawala wao ni wa kikoloni na utawala wa kikoloni siku zote ni muovu kwa watawaliwa. Asiyekuwa na uwezo wa kuliona hili si mwingine zaidi ya mtawala muovu.
Ni wazi kabisa kuwa ingelikuwa Zanzibar iko huru kujitendea mambo yake ya ndani na ya nje ingelikuwa iko mbali kwa maendeleo ya kila aina. Ikiwa hukubaliani na mawazo haya alau jaribu uwe mkweli wa nafsi yako; vuta kalamu na karatasi; upande mmoja andika faida za muungano uliopo kwa Zanzibar na upande wa pli andika khasara zake uangalie mwenyewe jinsi khasara zilivyokuwa ni nyingi kuliko faida inayopata Zanzibar kwa "Muungano" ambao kwa hakika si muungano, bali ni kutawaliwa kibeberu. Kwa upande wa Tanganyika hata huna haja ya kuandika chochote, ikutoshe tu kuwa imepata faida ya kuwa na koloni.
Kama muungano huu una manufaa, basi muungano na nchi nyingine za Afrika Mashariki na hata zaidi ya hizi lazima uwe na manufaa makubwa zaidi. Kinachozizuia nchi hizi kuungana ni nini? Hakuna hata nchi moja itakayokubali kuingia katika muundo wa muungano kama ulioko baina ya Tanganyika na Zanzibar. Muungano ambao hauko sawa kwa chochote. Nguvu zote na amri zote zinatoka Dodoma, Tanganyika na Wazanzibari wamejikuta katika hali mbaya ya kutawaliwa na mtawala beberu yuko bukheri wakhamsa waishirini anaona atatawala milele! Kwa bahati nzuri, wako Watanganyika wenye kuiona dhulma hii, nao wameanza kuzipaza sauti zao na kuukemea ubeberu huu unaowakandamiza ndugu zao walioko Zanzibar.
Tumeelezwa na Watanganyika wengi walioandika makala kuwa Watanzania wengi wanautaka muungano uendelee. Ni kweli kabisa kuwa "Watanzania" wengi wanautaka muungano uendelee. Lakini tujiulize: Ni Watanzania kutoka upande gani wa muungano wanaolilia muungano usivunjwe? Jawabu ni kuwa ni Watanganyika wengi ndiwo wenye kuutaka muungano usivunjike. Lakini pia ni ukweli kabisa kuwa si muhimu hata kidogo iwapo Watanzania wengi wanautaka muungano. Ni muhimu Wazanzibari wengi wawe wanautaka au hawautaki huo muungano. Hata iwapo Watanganyika wotewote wenye idadi zaidi ya milioni arubaini wanautaka muungano, muungano unakuwa hauna uhalali iwapo wengi ya Wazanzibari hawautaki, kwani huu ni muungano wa nchi mbili na wengi wa upande wowote ukiwa haupendelei muungano uendelee basi muungano unakuwa hauna uhalali. Kwa Watanganyika kushikilia lazima uwepo muungano ijapokuwa Wazanzibari wengi hawautaki inakuwa ni ya mkoloni kulishikilia koloni lake lisimtoke.
Narejelea tena kusema kuwa iwapo Watanganyika wotewote wenye idadi ya zaidi ya milioni arubaini wakisema wanautaka muungano, na kwa upande wa pili zaidi ya nusu ya Wazanzibari ambao idadi yao hata haitafika milioni moja wakiamua kuwa hawautaki muungano, basi muungano ni batil; na hili ndilo wanaloliogopa wakoloni wafuasi wa Kambarage na ndiyo sababu ya mazingaombwe na usanii wote huu wa hizi tume za maoni ili kuwanyima Wazanzibari na Watanganyika pia haki yao ya kura ya maoni ya kuchagua kama wanautaka au hawautaki muungano.
Inavyoonesha ni kuwa Wazanzibari wengi hawautaki muungano, maana wamechoshwa nao kwa dhiki zake zilizoletwa na usanii na kubanwa Wazanzibari katika kila sehemu ya maisha yao. Juu ya hayo, muungano wenyewe si jambo lililokuwa na umuhimu ukifikiria kwa makini. Na kukusanya maoni ya watu hapa na pale kama ifanywavyo hivi sasa ni mbinu ya kukwepa kura ya maoni. Huu ni usanii wa hali ya juu kabisa ya kuudanganya umma ili kukwepa hiyo kura ya maoni.
Wala muungano hauna umuhimu wa maana ukizingatia kero na mashakil yake. Lenye umuhimu ni ujirani mwema. Hivi mambo yendavyo inaonesha wazi kuwa muungano huu hauwaridhishi Wazanzibari wengi. Na iwapo baada ya kuvunjika muungano Watanganyika watawafanyia Wazanzibari ngumu na vitimbi, basi itazidi kuthibitisha kuwa watawala hawakuwa na niya ya kuwa ndugu na jirani wema tokea awali.
Nawatakia kila la kheri madhulumu watawaliwa,
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 comments:
Post a Comment