Saturday 27 February 2016

[wanabidii] Neno La Leo: Kuna Walioamua Kutetea Uvivu Wao Kwa Kusingizia Freemasons!


Ndugu zangu.,

Ndio, kuna walioamua kutetea uvivu wao kwa kusingizia Freemasons.

Nimekisoma kitabu cha Sir Andy Chande kiitwacho ' A Knight In Africa'. Huko nyuma nilimsikia tu mtu anayeitwa Andy Chande, lakini, kupitia kitabu chake nimemfahamu zaidi alikotokea.

Kupitia simulizi ya maisha yake unaona jinsi Sir Andy alivyo mchapakazi. Anatoa mifano mingi ya kazi alizofanya; kwenye biashara na hata utumishi wa taifa hili. Ajabu ya Sir Andy, ameitumikia Serikali bila hata kuwa Mbunge au Waziri.

Na jioni moja nilipomwona pale kwenye ghafla fupi nyumbani kwa Balozi wa Sweden nikashawishika kuongea naye. Ucheshi niliouona kwenye maandiko yake upo pia kwa Andy unapozungumza naye. Kitabu chake kinasimulia pia historia ya nchi yetu. Kinatusaidia kuelewa tulikotoka, tulipo sasa na kuweza kufikiri juu ya wapi tuendako. Unaposikia leo sakata la sukari, au shirika la ndege ATC au la reli na mengineyo kuhusu mashirika ya umma na viwanda vyetu, basi, kitabu cha Sir Andy Chande ni kama ' kamusi' ya kukusaidia kupata tafsiri.

Andy alikuwa pia rafiki wa Julius Nyerere tangu enzi za kudai uhuru wa nchi hii. Andy na Julius walikuwa ni marafiki wa karibu, waligombana wakapatana, maana, kila mmoja alimuheshimu mwenzake. Nitasimulia mahala pengine juu ya urafiki wa wawili hawa. Julkius alimpenda na kumheshimu Andy kwa kuwa alikuwa ni rafiki aliyekuwa akimwambia ukweli, hata kama Julius atachukia kwa kuambiwa ukweli huo.

Mfano, Andy aliwahi kumkatalia Julius alipoombwa akagombee Ubunge Tabora kwenye uchaguzi wa kura tatu. Andy akatamka; " I would save better as a business man rather than a politician".

Famlia yake, kuanzia babu yake ni ya wafanyabiashara. Pale Bukene, Shinyanga, walianza na biashara ya kuuza magunia. Wakafanya pia biashara ya vinu vya kusaga na kukoboa. Baadae Andy na familia yake wakahamia Dar. Mbele ya Stesheni Kuu ya Tazara iliko sasa kampuni ya Azam ndipo kilipokuwa kiunga cha akina Chande. Walianza kwa kufyeka mapori. Hapo wakaweka vinu vya kukoboa na kusaga.

Asubuhi moja enzi za Azimio la Arusha, mwaka 1967, Andy anasimulia kwenye kitabu chake, kuwa aliamka asubuhi moja kwenda kiwandani kwao. Yeye alikuwa meneja wa kiwanda hicho. Getini akawakuta askari wa FFU. Akaambiwa kuwa kuanzia siku hiyo kiwanda kimetaifishwa. Kikaitwa National Milling Cooperation. Akaingizwa ofisini kwake akabidhi ofisi kwa Meneja mpya ambaye hakuwahi hata kukutana naye mitaani. Kukabidhi mali ya familia kwa mtu usiyemjua!

Alipomaliza kufanya shughuli ya kukabidhi, Andy akumuuliza Meneja Mpya kama angependa aongozane naye akamtambulishe kwa wafanyakazi wengine. Andy akaambiwa imetosha, aende zake tu.

Siku hiyo hiyo Andy akaitwa na rafiki yake Julius aende Ikulu. Hata alipoingia Ikulu, Andy alimwona Julius mwingine. Hakuwa mcheshi kama ilivyokuwa kawaida yake. Julius akamwambia Andy akae kitako na hapo hapo akamfahamisha maamuzi ya kutaifisha kiwanda chao na kuwa Shirika la Umma.

Na cha ajabu, Julius akamwomba rafiki yake Andy awe Mwenyekiti wa Kwanza wa Bodi ya National Milling Cooperation!

Andy akakubali! Na akaifanya kazi ile kwa nguvu zake zote.

Inasikitisha kuona leo Andy anaanikwa kwenye magazeti ya udaku na kutolewa taswira hasi. Tena ni Andy huyu huyu ambaye aliwahi kuwa mmoja wa wajumbe wa Tume iliyokuwa ikipitia filamu zote zinazoingizwa Tanzania kuziangalia kabla umma haujaonyeshwa. Lengo lilikuwa kuhakikisha kuwa filamu hizo za kigeni haziathiri maadili, mila na utamaduni wetu.

Leo Andy amekuwa mhanga wa baadhi ya vyombo vya habari vinavyokiuka maadili, mila na utamaduni wetu, kwa kumuanika hadharani, tena kwa kuweka picha zake, bila ridhaa yake, kuwa ni mwanachama wa jumuiya ya Freemasons, jumuiya ambayo, kwa kupotosha umma, media inadai wanachama wake wanaamudu mashetani!

Naam, kuna waliamua kutetea uvivu wao kwa kusingizia Freemasons!

Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment