Sunday 28 February 2016

[wanabidii] Naona Fahari ya kuwa Mtanzania

Tanzania ni taifa ambalo kwa miaka ya 1960 mpaka miaka ya 1990 lilikuwa likiheshimika sana barani Afrika na ulimwenguni kutokana msingi uliokuwa umewekwa na utawala wa awamu ya kwanza wa Hayati JK Nyerere.

Kuanzia miaka ya 1990 heshima ya Tanzania ilianza kupotea. Kufikia miaka ya 2000 mpaka hivi karibu Tanzania lilikuwa ni taifa lenye kudharauliwa kabisa. Ilifikia hatua hata ukiwa safarini nje ya nchi unajikuta unajuta kuitwa mtanzania au kuwa na passport ya kitanzania. Utapekuliwa sana kuliko raia wa mataifa mengine kwa kuhisiwa kuwa unaweza kuwa na madawa ya kulevya. Mambo ambayo yaliyopelekea heshima ya Tanzania kupotea ni kama ifuatavyo:

1. Umaskini uliokithiri usioendana na rasilimali. Hakuna taifa Afrika linalolifikia Tanzania kuwa na rasilimali nyingi, tuna bahari, tuna maziwa makuu, tuna madini, tuna ardhi yenye mabonde yafaayo kwa kilimo, tuna nguvu kazi ya kutosha. Tofauti na rasilimali pia Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu hivyo ilitarajiwa kuwa imesonga mbele. Umaskini wa Tanzania ni kwa sababu viongozi na watalawa wasiowajibika. Wenye kujali maslahi binafsi.

2. Ufisadi. Ufisadi ni jambo limeipelekea heshima ya Tanzania kushuka. Tanzania ya wakati wa Nyerere ilikuwa ni Tanzania inachukia ufisadi. Sisemi kuwa ufisadi haukuwepo wakati ule. Ufisadi ulikuwepo ila haukuwa ukishika hatamu. Watu walichukia ufisadi na rushwa. Waliokuwa mafisadi waliishi kwa taabu sana. Tofautli na miaka ya karibuni ufisadi umekuwa ni jambo linakubalika. Fisadi na mpiga dili chafu anaonekana mjanja. Mtu anatambulika kuwa ni fisadi hata mataifa ya nje yanamjua kuwa huyo ni fisadi sisi tunamshangilia kuwa ni mkombozi heshima itakuwepo kweli.

Fisadi akipita barabarani na gari la kifahari anaonekana ni mwenyeakili na mjanja huku mtu maskini mwadilifu akipanda daladala anaonekana ni mpumbavu tu. Ufisadi ndio ulioletwa kampuni hewa za kuzalisha umeme na zikichota mabilioni yetu bila kuzalisha umeme. Ufisadi ndio uliofanya nchi kuingia mikataba ya hasara kwenye rasilimali zetu. Nyerere aliifukuza Kampuni ya uchimbaji madini ya Williamson Diamond ya Mwadui ajabu sisi tukaleta kampuni nyingine kwa mkataba wa kutupa kabisa.

3. Madawa ya kulevya. Jambo la tatu lililopelekea kushuka kwa heshima ya Tanzania/Watanzania. Kwa miaka ya karibuni kumetokea ongezeko kubwa sana kwa vijana kitanzania kujihusisha na madawa ya kulevya. Wengi wameripotiwa kukamatwa sehemu mbalimbali ulimwenguni wakiwa na madawa ya kulevya. Imefikia hatua kuwa Mtanzania anakaguliwa sana kwenye viwanja vya ndege vya mataifa mengine. Madawa ya kulevya yamekuwa yakihusishwa na watanzania.

Kutokana mlolongo wa matukio ya kukamatwa na madawa ya kulevya kwamba wengi wanaokamatwa nje ya nchi wanakuwa wakionekana kutoka Tanzania na hayo madawa ya kulevya naweza amini kuwa kiwanda/viwanda vya madawa. Kumbuka kuna raia wa mataifa mengine mfano nigeria wanaokamatwa ndani nchi wakiwa katika harakati za kuondoka na madawa kulevya.

4. Elimu. Ni swala lisilopingika kwamba elimu ya Tanzania imeshuka. Na hii ni ngazi zote kuanzia primary mpaka vyuo vikuu. Hali hii imewapelekea vijana wengi kukosa kujiamini hasa wanapotafuta masoko ya ajira katika anga za kimataifa. Mitaala ya elimu imekuwa ikifanyiwa mabadiliko yasiyokuwa na tija ili kuficha uozo katika sekta ya elimu mfano mpango wa madaraja ya ufaulu.

Usimamizi katika sekta ya elimu ni duni kiasi kwamba hakuna ufuatiliaji juu ya kile kinachotolewa kama kipo katika viwango vinavyohitajika. Ni aibu sana maana si ajabu siku za leo kukutana na msomi wa kiwango cha shahada ya uzamili (Master's Degree) hawezi kujieleza vyema kuhusu mambo ya taaluma yake.

5. Yapo Mambo mengi sana yaliyopelekea kushuka kwa heshima ya Tanzania mengine ni:

a. Uongozi Dhaifu.
b. Kukosekana kwa uzalendo.
c. Kuua viwanda vyetu.
d. Ushirikina. Mauaji ya Albino ili kupata mafanikio kiuchumi na kisiasa. Yote haya yametokana na ukosefu wa elimu.

Mh. John Pombe Magufuli Rais wa awamu ya tano kwa muda mfupi aliokaa madarakani ameonyesha dhamiri ya dhati ya kutaka kurejesha heshima ya Tanzania katika ramani ya ulimwengu. Raia wa mataifa mengine wameanza kuonyesha kuwa Watanzania tumepata rais bora hata wakitamani aende akatawale na kwao.

Binafsi sikuwa mshabiki au mwanachama wa CCM ila Rais Magufuli namkubali kwa yale ambayo amekwisha thubutu kufanya akiwa waziri katika wizara tofauti. Nashangaa sana watu wanaobeza jitihada zinazofanywa na raisi kuondoa matatizo yaliyokuwa yamekithiri kwa wananchi. Mimi rai ni kwamba watanzani kwa miaka mitano mbele
yetu tuweke kando tofauti zetu tujenge taifa letu kwa pamoja.

Mimi ni mmoja wa walipa kodi kupitia mshahara ninaolipwa na mwajiri wa wangu. Nilikuwa ni mtu ambaye nalalamika sana kutokana na kukatwa kodi wakati kodi hiyo sioni manufaa yake kwangu. Yaani unakatwa kodi, mwanao anatozwa michango mashuleni ambapo pengine kodi ingelitosha kushughulikia matatizo hayo, unatozwa kodi wakati huduma za matibabu hakuna katika hospitali za umma, unatozwa kodi wakati barabara ni mbovu ilifikia hatua sikuona raha ya kulipa kodi.

Ila kwa hatua alizoanza kuchukua Mh. Rais naona fahari kulipa kodi hata kodi hiyo itakuwa ni 18% niko tayari kulipa maana najua kwa kodi yangu mwanangu atasoma bure, kwa kodi yangu nitapata huduma za afya bure, kwa kodi ya barabara zitatengenenzwa, kwa kodi yangu mwanangu atapata mkopo kwa masharti nafuu wakati wa kusoma chuo kikuu.

Sasa naona fahari ya mimi kuwa Mtanzania, heshima ya Tanzania imerudi. Hivi karibuni nimekuwa nikipokea hongera kutoka marafiki za wa nje ya nchi kwamba wameona Tanzania tumepatata rais makini. Mtu asiyependa juhudi zinazofanywa na mheshimiwa Rais ni fisadi, mhujumu uchumi, mnafiki, mzandiki na hana uzalendo.
Mimi ni mtanzania, Mungu ibariki Tanzania, wabariki viongozi wake, wabariki watu wake.

0 comments:

Post a Comment