Maggid,
Utenzi wako haueleweki.
1. Wakati wa Rais Kikwete kutoa maoni binafsi ulishapita. Tume aliyounda ilipokea maoni kutoka kwa taasisi na watu binafsi kwa nyakati mbalimbali. Huo ndio uliokuwa wakati wa kutoa maoni.
2. Maoni aliyotoa siku ile mbele ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hayakuwa yake. Ushahidi upo, kwamba yalikuwa maoni ya CCM.
3. Maoni aliyotoa hayakuwa mapya. Yalishapelekwa hadi kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Yalikuwa sehemu ya hoja zilizochambuliwa na Tume hadi kufikia hitimisho la Rasimu ya kwanza na ya pili.
4. Kwa kutumia cheo chake na nguvu ya chama (wingi) Bungeni alikuwa analazimisha kistaarabu, ingawa alifika mahali akatamka kwamba jambo hili (la Serikali tatu) halitawezekana akiwa madarakani. Baadaye akaongeza kitisho kuwa jeshi linaweza kupindua Serikali ya Muungano! What a statement from the Commander-In-Chief of the Armed Forces!
5. Ni nani anayewapangia Watanzania wakati mwafaka wa kuwa na muungano wanaoutaka? Maana huu wa sasa unashinikizwa na watawala. Soma, rejea na tafakari uchambuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
6. Kama watawala hawawezi kuzuia Zanzibar kuwa nchi ndani ya Muungano, wanawezaje kudhania wana uwezo wa kuzuia Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano?
7. Kama hoja ni maridhiano, mbona walikataa tangu mwaka juzi, Tundu Lissu alipowaeleza kuwa kabla ya kujadili idadi ya Serikali au aina ya Muungano, kwanza tuwaulize Watanzania (kwa kura ya maoni) kama wanautaka? Baada ya kujua msimamo wa wananchi kwa mtindo huo, ndipo tujadili kuimarisha wanachotaka.
8. Kwa Rais Kikwete kutoa maoni yake badala ya kuzindua Rasimu ya pili Bungeni, alikuwa anashawishi kila mtu (kila kundi, kila taasisi) arejee kwenye hoja yake ya awali na msimamo aliopeleka kwenye Tume.
9. Tazama hila zinazoendelezwa na Serikali na uongozi wa Bunge kuhujumu Rasimu ya pili (ya maoni ya wananchi) ya Katiba.
Hiki ndicho unachosifia?
Ansbert Ngurumo
Existential Philosopher, Musician, Journalist & Media Manager
Vox Media Centre & Free Media
Tanzania
--http://mjengwablog.com
Ndugu zangu,
Naziona ishara za kuendelea kwa mvumo mbaya wa upepo wa kisiasa na hususan inapohusu hoja ya Muungano na muundo wa Serikali.
Mjadala unaoendelea sasa ni kama vile umefunikwa kwa chandarua kisicho na kinga ya wadudu wenye madhara kama mbu.
Tunakoelekea si kuzuri. Msimamo wangu uko wazi, kuwa tunahitaji muundo wa Serikali Tatu ili tuimarishe Muungano wetu. Kwamba tunahitaji uwepo wa Tanganyika kama nchi.
Lakini, nahofia katika tofauti hizi za mitazamo, kuna wenye kuamini katika Serikali Tatu lakini bila kuwa na nia njema kwa nchi. Na kuna wenye kuamini hivyo wakiwa na dhamira njema pia. Hivyo hivyo kwa wenye kuamini katika Serikali Mbili.
Hivyo, nimeipitia mara kadhaa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa alipokuwa akifungua Bunge Maalum la Katiba. Nimejitahidi kuitafuta mantiki kwa alichokizungumza Rais wa Nchi. Naamini Jakaya Kikwete aliongea kile alichokiamini moyoni mwake. Kikwete alionyesha hofu juu ya Serikali Tatu ingawa aliweka wazi kuwa maamuzi ya mwisho ni ya Wabunge wenyewe. Ni haki ya Kikwete kama mwanadamu kuelezea hisia zake.
Lakini , Jakaya Kikwete si kama Watanzania wengine. Ni Rais wa Nchi. Nikifikiri leo, naamini ilikuwa sahihi kwa Kikwete kukisema alichokisema, hata kama hakifanani na misimamo kama ya kwangu.
Maana, nikiwasikiliza ndugu zetu wa Zanzibar , hasa wenye kuupinga Muungano katika hali iliyopo, na jinsi wanavyojadili, kwa kweli natishikia pia. Na hakika, kwa kuufuatilia mvumo wa upepo wa kisiasa unaoendelea sasa, Jakaya Kikwete alitusaidia kuyaweka wazi mawazo yake binafsi. Maana, ingawa Serikali Tatu na Tanganyika inahitajika, lakini, huu si wakati wake. Ni jambo la kusubiri lije tutakapokuwa tayari kama watu tulioungana; Visiwani na Bara. Na tuanze sasa kufanya jitihada za kuyatafuta maridhiano juu ya kwa nini haya ya kubadilli mfumo wa Serikali kwenda Serikali Tatu wakati wake haujafika.
Maana, kuendelea kujadili Serikali Tatu sasa ni kuzidi kuipeleka nchi yetu tunayoipenda kwenye mgawanyiko na mpasuko mkubwa. Ni busara nionavyo, kuwa Wabunge wetu kule Dodoma watambue kuwa rasimu ya Jaji Warioba, ukiacha muundo wa Muungano na mfumo wa Serikali , ina mengi sana ya muhimu ili kututoa hapa tulipo na kuwasaidia wananchi.
Waitafute busara ya kulisubirisha hili la Muuundo wa Muungano unaopendekezwa na Rasimu ya Warioba na hata muundo wa Serikali. Tubaki na Serikali Mbili na tuboreshe kinachoweza kuboreshwa.
Maana, si kila unachokigawa maana yake kuna kinachobaki. Kugawa pia kuna maana ya kumaliza pia.
Na mengine tuyafanyao katika wakati usio sahihi huzaa kutokuaminiana.
Na kwa mwanadamu pale mtaji wa imani unapomalizika, kinachobakia ni kumaliziana.
Usimwone nyani ana makovu ukadhani ni simba aliyemjeruhi. Nyani huishi kwa kumwogopa zaidi nyani mwenziwe.
Kugawanyika kwa shari ni kutawanya mitaji ya kuaminiana.
Na kitachobaki ni kuumizana, kwa kugombani kiduchu chunguni kilichogandiana…
Ni wakati sasa wa kutanguliza busara na hekima zitakazotunusuru na mpasuko mkubwa zaidi wa kijamii.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
Maggid,
Iringa.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment