Sunday, 2 October 2016

[wanabidii] Dikteta uchwara au demokrasia uchwara?-3

TUNAPOZUNGUMZIA demokrasia hapa nchini ni lazima tuwe na mifano hai kuonyesha ama uchanga au ukomavu wa dhana yenyewe.

Hatuwezi kuzungumzia demokrasia kwa kubwabwaja tu bila ya mifano hai na rahisi ambayo inaweza kueleweka kutokana na ama ushiriki wetu moja kwa moja au kwa kupitaa wawakilishi ambao tunawachagua kwa kutambua kwamba tunalolifanya lina hoja kwetu.
Moja ya asasi ambazo zinatakiwa kuonesha mfano wa ukomavu au uchanga wa demokrasia ni vyama vya

siasa ambavyo vina wanachama kutoka katika kila kundi la mgawanyo wa wananchi. Katika Tanzania vyama vya siasa vinatakiwa kuhakikisha kwamba vinakuwa na wanachama kutoka pande zote za muungano na bila ya kutumia vigezo vyovyote vinavyoweza kutafsiriwa kwamba ni vya kibaguzi au vya kuvunja Katiba ya nchi.

Kwa maneno mengine ni kwamba moja ya asasi za msingi sana katika kujifunza demokrasia na utawala bora katika nchi yetu ni vyama vya siasa. Ni vyama vya siasa ndivyo vinavyotakiwa kusimama imara na bila ya kumung'unya maneno kutetea demokrasia na kuhakikisha pale inapofinyangwa havisiti wala kujiuliza bali vinasimama kidete kuitetea na kuhakikisha wananchi wanatendewa haki.
Kwa mantiki hiyo vyama vya siasa hususan vinavyodai kuwa ni vya kidemokrasia havina budi kuishi kwa kupigiwa mfano na si vinginevyo.

Tujiulize ni chama gani ambacho kimekuwapo tangu kurejeshwa kwa siasa ya vyama vingi nchini na kimekuwa kikifanya uchaguzi wa viongozi wakuu bila ya mikwaruzano wala vitimbi isipokuwa kampeni za kawaida za kisiasa?
Kuna nini ndani ya vyama vyetu vya siasa? Kwa nini demokrasia inayozungumziwa haifanyi kazi ndani ya vyama hivyo?

Inawezekanaje vyama ambavyo vimeshindwa kuwa na utaratibu wa kidemokrasia wa kuheshimu katiba zao wenyewe na kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika bila ya mizengwe na mikwara leo visimame hadharani kudai kwamba upande huu au ule hauna demokrasia?

Ni uhalali gani chama chochote kile ambacho kimeshindwa kufanya uchaguzi bila mizengwe kupiga kelele na kutupa tuhuma huku na kule kuhusu kuminywa kwa demokrasia?

Nani anayeiminya demokrasia ni kiongozi wa chama ambaye hataki kusikia mtu anayezungumzia kushindana naye katika uchaguzi au ni wale wanaokutana na kulumbana na hatimaye kukubaliana kwamba demokrasia iamue mshindi katika malumbano yao?

Ingependeza zaidi kama wanasiasa wetu wanaotaka kutuaminisha kwamba vyama wanavyoongoza vina demokrasia wangejiangalia kwanza ndani ya nyumba zao, haipendezi hata kidogo kusikia kuna kurushiana makonde katika mikutano ya uchaguzi.

Wanachama wanachotaka ni uongozi madhubutu unaoweza kutoa changamoto ya kweli dhidi ya chama tawala na kuonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa hususan katika kuijenga demokrasia.
Ni jambo la hovyo sana kuwa na vyama ambavyo vinajitangaza kuwa ni vya kidemokrasia lakini ambavyo vinafanya mambo tofauti kabisa linapokuja suala la uendeshaji wake wa siasa za ndani.

Tumekuwa tukisikia migogoro ndani ya vyama vikuu vya siasa kutokana eti na kuchuliwa njama za baadhi ya wanachama wao kutaka kujipanga ili kuchukua nafasi ya uongozi wa juu.

Inawezekanaje suala la uongozi au mtu mwanachama kujipanga kuwania nafasi ya juu ya uongozi katika chama liwe ni uhaini? Kwamba watu wanafukuzwa ndani ya chama kwa sababu eti wamekuwa wakila njama za kutaka kunyakua uongozi kwa kutumia katiba halali ni jambo la kutatiza sana.

Iweje uongozi wa juu katika chama cha siasa uwe ni kwa ajili ya aina fulani tu ya watu? Iweje leo kutaka kuwania nafasi ya juu katika chama cha siasa cha kitaifa iwe ni jambo la kuleta machafuko na mivutano ya kutishia uhai wa chama?
Chama kinawezaje kuwa na watu maalum kwa ajili ya kushika nafasi za uongozi wa juu na bado kikajiita kwamba ni chama cha demokrasia?

Demokrasia uchwara ni hatari sana kuzidi udikteta uchwara. Demokrasia uchwara hutengeneza wafalme ndani ya vyama na uthibitisho ni jinsi ambavyo kumekuwapo na vitimbi vya kila aina ikiwa ni pamoja na
kutimuana kila linapojitokeza jina la mtu anayetaka kugombea nafasi ya uenyekiti katika vyama hivyo.
Katiba ipo lakini kila jitihada zinafanyika kuhakikisha kwamba mtu fulani tu ndiye anakuwa mgombea pekee wa uenyekiti au akipatiwa mpinzani basi anakuwa ni dhaifu mno kiasi cha kutokuwapo na ushindani wa kweli.

Tunapotuhumu kwamba dalili za udikteta zinajitokeza kupitia staili ya utawala ya Rais Magufuli basi ni vyema tukakubali pia kwamba tayari udikteta wa kweli upo ndani ya vyama vyetu vya siasa vinavyotaka kutuaminisha kwamba hali ya siasa nchini ni mbaya.

Inasikitisha kwamba wahubiri wa demokrasia ndio walio mstari wa mbele kuhakikisha kwamba hakuna demokrasia ndani ya vyama wanavyoviongoza na wanavyovitumia kama majukwaa ya kuonesha jinsi wanayothamini demokrasia. Hizi ni hadaa za kisiasa na hazitakiwi kufumbiwa macho.

Kuna wanaohoji kuhusu siasa kuwa ni kazi na kwa hivyo kwa Rais Magufuli kutoa angalizo kuhusu maandamano yasiyo na ukomo na mikutano ya hadhara inamaanisha amezuwia watu wa siasa kufanya kazi ya siasa. Huo ni ufinyu tu wa makusudi au wa kutokuelewa siasa maana yake nini.
Kazi ya siasa si kuandamana na kuitisha mikutano ya hadhara tu. Mwanasiasa ni mtu anayeuandaa umma kwa ajili ya mabadiliko katika uchumi, siasa na jamii.

Kazi hiyo ni kubwa na si lazima iwe katika maandamano na mikutano ya hadhara tu kama wanavyotaka kutuaminisha waliotangaza mapambano na Rais Magufuli.
Ukweli ni kwamba uchaguzi umemalizika. Uchaguzi mwingine ni mwaka 2020. Kuendelea na malumbano ya siasa kama vile nchi ipo katika kipindi cha kampeni ni kuivuruga jamii.

Uchaguzi unafanyika ili kutoa fursa ya miaka mitano kwa aliyeshinda kuongoza nchi. Kujipanga kwa ajili ya kumvuruga kutumia kampeni za kisiasa ni kumwondoa katika mstari na akikubali basi amekwisha.

Ni vyema tukaiga ustaarabu wa waliotutangulia katika demokrasia ya vyama vingi kwamba tunapomaliza uchaguzi hatuanzi uchaguzi mwingine, bali tunaingia katika kipindi cha kuijenga nchi na si kuibomoa kwa kulazimisha mambo ambayo hayataisaidia kusonga mbele kama maandamano yasiyo na ukomo na mikutano ya hadhara ya kujiandaa kwa uchaguzi ambao tayari umekwisha kupita.

Kama nilivyohitimisha wiki iliyopita ni kwamba kati ya Dikteta Uchwara na Demokrasia Uchwara mimi nachagua Dikteta Uchwara kwani una tija kwa taifa letu na ni udikteta ambao hauvunji wala kusigina Katiba, tofauti na demokrasia uchwara ambao unasigina Katiba waziwazi. Tuachane na siasa za kampeni za kudumu kwani hazitusaidii kuijenga nchi yetu.

Chanzo Rai

0 comments:

Post a Comment