Thursday, 8 December 2016

[wanabidii] Taarifa kwa vyombo vya habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
COASTAL UNION FOOTBALL CLUB (TANGA, TANZANIA)
Uongozi wa klabu ya soka Coastal Union yenye makao yake makuu mkoani Tanga, imepokea kwa masikitiko adhabu iliyotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Bodi ya Ligi kutokana na vurugu zilizofanyika katika mechi namba 15B kati ya Coastal Union na KMC ya Dar es Salaam.
Adhabu hiyo inahusisha kucheza mechi mbili katika uwanja wa nyumbani Mkwakwani bila mashabiki na mechi moja katika uwanja mwingine mbali na nyumbani (Neutral ground). Mechi hizo tatu ni adhabu kubwa kwetu kwa sababu timu iliyo ligi daraja la kwanza inategemea mashabiki katika ushindi.
Hali hiyo itawakumbusha mashabiki wetu kuacha mihemko isiyo na maana kila wanapoona waamuzi hawatekelezi wajibu wao, tunawaomba mashabiki wetu wajifunze kupitia adhabu hii. Ikiwa kutatokea vurugu nyingine itadhihirisha namna mashabiki wasivyo na huruma na viongozi wao.
Wakati huo huo uongozi unawatangazia wanachama wake kuwa tayari kambi imeshaanza tangu Disemba 6, 2016 kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi ya Soka Daraja la Kwanza.
Wachezaji tayari wamesharipoti kambini tangu mwanzoni mwa mwezi huu na mazoezi yameanza rasmi Desemba 6 mwaka huu, na mazoezi yanaendelea kama kawaida chini ya kocha Mohammed Kampira. Na wasaidizi wake.
Ari iko juu na katika kufanya marekebisho ya kikosi, uongozi umefanya usajili wa washambuliaji wawili Ahmed Shiboli na Abuu Mshamu ili kuogeza nguvu nab ado uongozi upo kwenye mazungumzo na wachezaji wengine wanne. Wakiafikiana na matakwa yetu tutawasajili.
Aidha safu mpya ya uongozi chini ya Mwenyekiti Steven Mnguto, inawahakikishia furaha mashabiki wa Coastal Union, katika kumalizia mzunguko wa pili.
Vilevile uongozi unawakumbusha wanachama na mashabiki kutimiza wajibu wao kwa kulipia ada za uanachama na wale waliotoa ahadi ya fedha na vifaa wafanye hivyo ili kusaidia uendeshaji wa kambi na matumizi mengine wakati wa ligi ikiwemo, chakula, malazi, mishahara/posho na usafiri hasa ikizingatiwa kwa sasa timu haina udhamini wa uhakika.
IMETOLEWA NA MSEMAJI WA TIMU
HAFIDH KIDO
8/12/2016
Mwisho
 

0 comments:

Post a Comment