Monday, 2 February 2015

[wanabidii] JANUARY MAKAMBA NA TATIZO LA AJIRA

MAKAMBA NA TATIZO LA AJIRA.

"Ni changamoto gani kubwa zinawakabili
vijana wa Tanzania? Wanasiasa wengi
wamekuwa wakisema watamaliza tatizo
la ajira nchini. Kuna mawazo gani mapya
kutoka kwa viongozi wa kizazi kipya ya
kumaliza tatizo hili?"

Tatizo la ajira lipo kwa vijana wa mijini na vijijini, vijana waliopata bahati ya
kupata elimu ya juu na hata ambao wameishia la saba au kidato cha nne. Ukiwa
umesoma, ajira tatizo, ukiwa haujasoma ajira pia tatizo.

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, inakadiriwa kwamba wapo Watanzania
milioni 23 kwenye soko la ajira – kwa maana ya watu wenye umri na uwezo
wa kufanya kazi. Hawa ni watu wengi sana. Na kila mwaka wanaingia vijana
900,000 kwenye soko la ajira. Hawa ni wengi sana.

Moja ya sera za msingi za CCM ni kuwawezesha wananchi kiuchumi
ili waweze kumiliki na kuendesha uchumi wa nchi yao na waweze
kunufaika na uchumi unaokua. Katika kufanya hivyo, lazima wawe na
maarifa ya kisasa kwa kuwa tupo kwenye mazingira ya uchumi wa
kisasa.

Yapo mambo ambayo Serikali imekuwa inafanya kumaliza tatizo la ajira. Mimi
nitajaribu kuongelea mambo mapya ya kuongezea zaidi ya yale tunayofanya
sasa.

Kwanza kabisa, ni muhimu kubadilisha mtazamo na kuondokana na
dhana ya ajira au dhana ya kuajiriwa. Tuchukue dhana mpya ya kipato.
Kimsingi watu hawatafuti ajira bali wanatafuta kipato cha kujiendeleza
January Makamba akiwa amezungukwa na vijana wa Bodaboda akiwasikiliza shida zao.

kimaisha. Kuajiriwa ni moja tu ya njia ya kutafuta kipato. Tukiwa na
dhana ya kipato itaweza kutusaidia kupanua wigo wa mawazo na fikra
kuhusu mambo tunayoweza kuyafanya.

Sasa, nini tufanye kumaliza hili tatizo?
Kwanza, kupatikana kwa fursa za vipato kwa wananchi kuna uhusiano wa
moja kwa moja na kunawiri kwa uchumi wa taifa, kuongezeka kwa shughuli
za uzalishaji mali na uwekezaji wa sekta binafsi katika shughuli zinahusisha
watu wengi, uwekezaji wa Serikali kwenye miradi mikubwa, na kuwepo kwa
mazingira rahisi na mazuri ya kuanzisha na kufanya biashara. Kwa hiyo haya
mambo lazima tuyafanye kwa uthabiti na kwa dhamira ya dhati kabisa.

Pili, Serikali imekuwa na mipango mizuri ya kuwezesha yote haya lakini
kumekuwa na nidhamu ndogo katika utekelezaji na ufuatiliaji. Tatizo la kipato
kwa wananchi linahitaji mkakati mahsusi, mkakati mkubwa na wa haraka
– mkakati ambao utaweka nidhamu na wajibu wa kisheria kwa wahusika
kuutekeleza.

Suala la ajira linahitaji msukumo na hatua za kimapinduzi, na sio maneno
tu ya kurudia kauli kwamba ni bomu bila kutoa ufumbuzi.
Pamoja na hatua hizi nilizozitaja awali napendekeza hatua nyingine mahsusi
za kumaliza tatizo la ajira na kuweka chachu mpya ya ukuaji wa uchumi:
Bunge lipitishe Muswada Maalum, Muswada wa Matumizi kwa
Uwezeshaji Kiuchumi kwa Vijana, ambao utakuwa ni sheria maalum
ya matumizi ya shilingi trilioni 3.6 kwa ajili ya mkakati wa miaka mitatu
wa kupanua ajira kwa kuchochea shughuli za uzalishaji mali na uchumi
au Jobs Bill kwa lugha nyingine.

Mwaka 2009, ulipotokea mdororo wa uchumi na wanunuzi wa pamba kukaribia
kufilisika Rais Kikwete alionyesha ujasiri na kupeleka Bungeni Mpango
Mahsusi wa kiasi cha shilingi trilioni 1.7 kuokoa zao la pamba na mabenki
yaliyowakopesha wanunuzi wa pamba. Sasa ni wakati wa kutengeneza
Muswada na Mpango Mahsusi na wa hatua kubwa zaidi ya ile ya 2009 kwa
ajili ya kukabiliana na tatizo la ajira.
Kwa kifupi, Muswada huu, utatenga fedha na kuweka utaratibu kwa maeneo
muhimu yafuatayo:

Kwanza, kuwezesha kujengwa na kufufuliwa kwa viwanda 11 vya nguo nchini.
Huko nyuma tulishawahi kuwa na viwanda vingi vya nguo. Sasa hivi havizidi
vitano. Sekta ndogo ya viwanda vya nguo ndio inayoajiri watu wengi zaidi lakini
pia ndio itakayotoa soko la uhakika la zao la pamba. Kwa sasa, ni asilimia 30 tu
ya pamba yetu ndio inayotumika nchini. Fedha hizi zitatumika kama dhamana
kwa makampuni binafsi hapa nchini kukopa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda
vipya 11. Hatua nyingine ya kuchukua hapa ni hatua ya kikodi na kiushuru ili
kuwezesha viwanda hivi kukabiliana na ushindani wa kanga, vitenge, mitumba
na vitambaa vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.

Sera za kukuza viwanda vilivyo na uwezo wa kuajiri watu wengi – kama
vya nguo- na vyenye kuzalisha bidhaa za matumizi ya wengi ndani ya
nchi na zile za kuuza nje zitawekewa kipaumbele.

Pili, fedha hizi zitatumika kama mkopo na dhamana ya mkopo kwa yoyote
anayetaka kuanzisha kiwanda au viwanda vya kusindika au kuongeza thamni
ya mazao ya kilimo – ikiwemo zao la korosho ambalo ubanguaji wake unaajiri
watu wengi.

Mtu yoyote atakayeamua kuanzisha kiwanda cha kuongeza thamani
ya mazao ya kilimo, kitakachoajiri watu kuanzia kumi, hasa maeneo ya
vijijini, atapendelewa na Serikali na kusaidiwa kuharakisha uwekezaji
huo na atapewa nafuu ya kodi.

Tatu, shughuli za ujenzi wa nyumba zinaajiri watu wengi. Kwa hiyo sehemu ya
fedha hizi zitatumika kuwezesha uanzishwaji wa makampuni madogo na ya kati
ya ujenzi wa nyumba lakini pia kuanzisha miradi mingi na mikubwa ya ujenzi
wa nyumba bora za makazi na biashara kwa maeneo ya mijini na vijijini. Tuna
mahitaji makubwa ya nyumba na tuna mahitaji makubwa ya ajira. Tukijenga
nyumba nyingi kila siku kama wendawazimu tutamaliza matatizo mawili kwa
mpigo. Sambamba na hili, ujenzi wa viwanda vya vifaa ya ujenzi, kama vile
viwanda vya nondo, mabati, simenti, vigae, vioo, ili kupunguza gharama za
ujenzi wa nyumba pia ni muhimu.

Lakini sote tunajua kwamba ujenzi wa miundombinu mikubwa, hasa ya
usafirishaji ni njia mojawapo ya kuongeza chachu katika uchumi na kuongeza
ajira. Kwa hiyo jitihada za makusudi ni muhimu ziwepo kuongeza kasi na ukubwa
wa miradi ya miundombinu nchini ambayo itaajiri vijana wengi zaidi na kuingiza
fedha nyingi zaidi kwenye mzunguko wa uchumi, hasa pale tutakapohakikisha
kwamba wajenzi wa miradi hii ni makampuni ya ndani yatakayohifadhi na
kuwekeza fedha hizo hapa ndani.

Nne, kwa kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Muswada huu
utaanzisha mfuko mkubwa kwa ajili ya kutoa dhamana na mikopo kwa
wajasiriamali wadogo kwa masharti nafuu kuliko mabenki au mifuko
mingineyo iliyopo hapa nchini.

Wajasiriamali watakaopewa upendeleo ni wale wanaofanya shughuli za
uzalishaji mali hasa kilimo, uvuvi, mifugo na shughuli za biashara zinazotoa ajira
kwa watu wengine. Mfuko huu utaendeshwa kwa uwazi na weledi mkubwa,
ikiwemo njia ya kutoa mtaji kwa kuchukua hisa kwenye baadhi ya biashara
hizi za kati na baadaye kuzirudisha hisa hizo kwa masharti nafuu pale biashara
hizi zinapokuwa zimeinuka. Lengo ni kurahisisha na kuharakisha upatikanaji
wa mitaji.

Tano, Muswada huu utaweka sharti kwamba asilimia si chini ya 30 ya
thamani ya manunuzi Serikalini na kwenye taasisi za umma yatatengewa
kwa ajili ya makampuni yanayomilikiwa na vijana wasiozidi umri wa
miaka 40 na wanawake – ili mradi makampuni hayo yawe na uhai
usiopungua miaka miwili na yawe yameajiri pia watu wengine.

Sita, Muswada huu utarasimisha shughuli za sanaa – ikiwemo sinema, muziki
na kazi zote za ubunifu– na kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya tasnia
hii, ikiwemo kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wazalishaji, waendeshaji
na wasanii wenyewe kwenye kuendeleza ubunifu na kuzalisha, kutangaza na
kuuza kazi mpya kwa njia za kisasa.

Saba, kwa wale wanaohitaji kuajiriwa, tutaweka vituo vya kutoa mafunzo ya
namna ya kuomba na kufanya usaili wa kazi – lakini pia tunaweza kutumia
Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, yaani FDCs, kama vituo vya kupata na kujenga
maarifa mapya kwa muda mfupi kuhusu mbinu na ushauri wa kukabiliana na
soko la ajira na fursa zilizopo za kujiajiri.

Nane, kwa biashara kubwa na viwanda vilivyopo sasa, Muswada utaweka
motisha kwa yoyote ambaye ataweza kuongeza ajira mpya 50 au zaidi kwa
mwaka, sio vibarua wa muda mfupi bali ajira kamili, kwa kupunguziwa kodi za
mishahara, yaani payroll taxes; na kwa waajiri ambao ni kampuni mpya ndogo,
yaani SMEs, motisha wa kupunguziwa kodi hizi kwa kila kazi mpya tano au
zaidi kwa mwaka.

Ukweli hapa ni kwamba kunawiri kwa uchumi hakutokani na kodi
inayokusanywa na Serikali bali kunatokana na kipato na uwezo wa
manunuzi walionao wananchi na kipato cha wafanyabiashara kuweza
kukuza biashara zao na kutoa ajira nyingi zaidi.

Tisa, Muswada utatenga fedha za kuweka mazingira ya ujenzi wa vyuo vya
ufundi, kwa kushirikiana na sekta binafsi, kwenye kila wilaya hapa nchini ili
wanafunzi ambao hawajapata fursa ya kuendelea na kidato cha kwanza au
kidato cha sita au vyuo vya ualimu wapate mafunzo mbalimbali mahsusi ya
ufundi stadi na taaluma zinazohitajika kwenye soko la ajira na kwenye uchumi
kwa ujumla. Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia kubwa ya wahitimu wa
vyuo vya ufundi hujiajiri.

Tutakapokuwa na Chuo cha Ufundi kikubwa na chenye hadhi katika
kila Wilaya tutatengeneza kundi kubwa la vijana ambao watakuwa
na maarifa na stadi za kutengeneza maisha yao na watakuwa tayari
kujiajiri.

Na utaratibu unaweza kuwekwa kwamba yoyote atakayemaliza Chuo cha
Ufundi, kama alisomea ufundi-seremala basi siku ya mahafali anakabidhiwa
vifaa vya kuanzia kazi, au mkopo au vocha ya kumuwezesha kununua vifaa
hivyo. Uwezo wa kufanya hivi tunao.

Kumi, Muswada huu utatenga fedha kwa ajili ya kuweka katika kila wilaya vituo
vya mafunzo ya maarifa mapya katika shughuli zinazoajiri watu wengi – kilimo,
uvuvi na ufugaji – na maarifa ya uendeshaji biashara ili vijana wanaofanya
shughuli hizi waweze kuzifanya kwa tija na wapate manufaa. Kwa kuanzia,
tunaweza kuanza kwa kutumia vyuo vilivyopo vya Maendeleo ya Jamii (FDCs)
ambavyo havitumiki kama inavyopaswa.

Kumi na moja, Muswada huu utaweka kanuni zitakazoainisha kiwango cha
chini cha thamani ya manunuzi yanayofanywa na wawekezaji wakubwa, hasa
katika sekta za mawasiliano, madini na mafuta na gesi, kufanywa hapa nchini
na kutoka kwa makampuni ya hapa nchini.

Kumi na mbili, Muswada utaanzisha Mamlaka ya Ujasiriamali Mdogo na wa
Kati (Small and Medium Enterprises Authority). Mamlaka hii kubwa, ambayo
itaanzishwa kisheria, itachukua na kuunganisha baadhi ya majukumu ya Baraza
la Uwezeshaji la Taifa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na
itakuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu maendeleo ya kampuni changa
na biashara ndogo nchini. Kote duniani, biashara za kampuni ndogo na za kati
ndio injini ya uchumi wa nchi.

Hapa kwetu asilimia karibu 90 ya biashara zote
nchini ni biashara ndogo na za kati, ambazo zinaajiri watu wasiozidi wawili.
Wajasiriliamali Wadogo na wa Kati wana changamoto mahsusi, zikiwemo za
masuala ya kodi, urasimishaji, masuala ya vibali, leseni, mitaji, elimu ya biashara,
na uelewa wa fursa zilizopo. Changamoto hizi zikitatuliwa basi mchango wa
biashara hizi kwa uchumi na utatuzi wa ajira utakuwa mkubwa. Kwa mujibu
wa takwimu za Benki ya Dunia, asilimia 20 tu ya biashara na kampuni ndogo
zikiongeza mfanyakazi mmoja kwa mwaka, ajira 400,000 zitazalishwa. Je
asilimia 80 za biashara hizi zikiongeza watu watatu kwa mwaka? Tutakuwa
tumemaliza tatizo la ajira. Lakini, ili hili litokee, lazima tuwe na taasisi madhubuti
kama hii Mamlaka ninayopendekeza, ambayo itashughulika na ustawi wa
biashara na makampuni madogo na ya kati.

Katika kusaidia biashara na makampuni madogo na ya kati, Mamlaka ya
Ujasiriamali Mdogo na wa Kati inaweza kupewa majukumu yafuatayo: kwanza,
kusimamia utekelezaji wa sharti jipya la kisheria la asilimia 30 ya manunuzi
ya Serikali yapewe kwa kampuni ndogo na za kati zinazomilikiwa na vijana
na wanawake wenye uwezo; pili, kuyajengea uwezo wa weledi wa kibiashara
makampuni madogo na ya kati kuwania zabuni; tatu, kusimamia uharakishaji
wa malipo kutoka Serikalini kwa wazabuni wadogo na wa kati ambao biashara
zao hudhoofika na hata kampuni kufa pale Serikali inapochelewa kuwalipa;
na, nne, kujenga uwezo wa makampuni na biashara ndogo na za kati kumudu
na kuweza kutumia nyenzo za kisasa za biashara ikiwemo mifumo ya kisasa
ya mahesabu.

Mwisho, sheria hii itaweka taasisi na mifumo madhubuti ya kuhakikisha kwamba
malengo ya fedha hizi yanatimia na kila mtu anatimiza wajibu wake.

Labda nimalizie kwa kusema kwamba katika haya niliyoyasema kuna ambayo
yanafanyika kwa kiasi fulani. Msingi wa mapendekezo yangu ni kwamba,

kwanza: sasa tuyafanye kwa msukumo mkubwa zaidi na utaratibu wa dharura;
pili, tuweke rasilimali-fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya kuliko kuwa na
mipango mizuri bila kuwa na fedha; tatu, badala ya kuwa na mipango na mikakati
tu, basi kuweka sheria itakayolazimisha na kuweka wajibu wa kutekeleza
mipango na mikakati hii. Lakini mwisho, kuunganisha yale mazuri ya sasa na
haya mapya ili kuwa na mwendelezo utakaowezesha utekelezaji wa haraka
bila kufumua kila kitu.Tukifanya haya yote kwa nidhamu kubwa, tutawakomboa
watu wengi katika maisha ya mashaka kuhusu kipato na ustawi wao.


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment