Wednesday, 13 August 2014

[wanabidii] Re: Mwigamba: Wameniweka kizuizini lakini mawazo yangu yako huru

9

On Wednesday, December 21, 2011 12:46:24 PM UTC+3, Samson Mwigamba wrote:

Wameniweka kizuizini lakini mawazo yangu yako huru

"WAMENIWEKA kizuizini kwa zaidi ya wiki moja lakini mawazo yangu hayakuzuiliwa hata kwa dakika moja, wameulaza mwili wangu katika mazingira magumu kwa zaidi ya wiki moja lakini ubongo wangu haukuathirika hata chembe, kwa zaidi ya wiki moja walifanya kazi ya kuudhoofisha mwili lakini roho ya ujasiri iliyo ndani yangu imeimarika maradufu". Haya ni maneno niliyoyatamka kwa watu wa kwanza niliokutana nao baada ya kuachiwa kwa dhamana mahakamani Kisutu siku ya Alhamisi Desemba 15, 2011 na kesho yake Ijumaa Desemba 16, 2011 nikayaweka kwenye ukurasa wangu wa Facebook.

Sitaingia undani wa kesi yangu iliyo mahakamani ndugu wasomaji ambapo ninashtakiwa kwa uchochezi na imeelezwa na waendesha mashtaka wa serikali ya JK kwamba nimewashawishi askari wa majeshi yote kukataa kutii amri ya serikali halali iliyoko madarakani. Makala husika wengi mmeshaisoma na kama kweli ni ya uchochezi mahakama ya Kisutu itaamua.

Kwa sasa napenda kuwaambia wasomaji wangu kwamba safari yangu ya siku 8 iliyoanzia chumba cha mahabusu cha Kituo Kikuu cha Polisi Dar es salaam na kuishia Gereza la Mahabusu la Keko ilikuwa ya mafanikio makubwa. Fanikio la kwanza ni kwamba safari hiyo imesababisha makala ile isomwe na askari wengi zaidi na raia wengi zaidi. Wakati naandika makala ile nilikuwa na wasiwasi kwamba pengine askari wengi wa nchi hii hawasomi makala kama hizi kutokana na asili ya kazi yao. Lakini nilikuwa na wasiwasi kwamba pengine hata raia wa kawaida ni wachache watakaosoma na hivyo ujumbe wangu kuwa umewafikia watu wachache. Nashukuru ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Robert Manumba kwa kubuni mbinu ya kunikamata, kuniweka rumande na hatimaye kunifikisha mahakamani ambapo amefanya askari na raia wa kawaida wengi sana kuitafuta makala hiyo na kuisoma wengine mara mbili na wengine mara tatu na hata mara nne.

Wazo la msingi la makala ile ilikuwa kuwataka askari kufanya kazi kwa kutumia akili zao kwa kutafakari. Kama askari wanatakiwa kutii amri bila kutumia akili yao kwa nini wale walioamriwa wakawakamate na kisha kuwapeleka msitu wa Pande na kuwaua wafanyabiashara wa Mahenge hatimaye walifikishwa mahakama ya Kisutu na serikali ya JK huyo huyo na IGP huyo huyo, DCI huyo huyo na hata DPP huyo huyo? Lakini swali lingine, kama askari anatakiwa kufanya kazi ya kutii amri halali na haramu bila kutumia akili yake, kwa nini rais huyu huyu alilihutubia taifa kupitia kwa wazee wa Dar es salaam na kuwaasa wafanyakazi na umma kwa ujumla kwamba busara ya kawaida inatakiwa kufanya kazi kama mbayu mbayu? Kwamba akili ya kuambiwa changanya na yako? Si angesema pale kwamba mfano huo hauwauhusu polisi? Mimi sijui kwa nini JK ana wasiwasi sana na urais wake wa 2010 – 2015.

Nakumbuka maandamano ya kanda kwa kanda ya CHADEMA yalipoanza kule Mwanza mara moja akakimbia kwenye kulihutubia taifa na kudai eti serikali yake imechaguliwa kihalali kwa hiyo lazima CHADEMA wasubiri 2015 kuitoa madarakani. Nimeandika makala simple sana ya kuunga mkono kauli ya rais na kuwashauri askari wetu kwamba kama wafanyakazi wengine na wao "akili ya kuambiwa wachanganye na ya kwao", walinda serikali ya JK wananikamata kwamba nawaasa askari wasitii amri ya serikali halali iliyoko madarakani. Huu wimbo wa 'serikali halali iliyoko madarakani' unamaanisha nini? Je hii si dalili kwamba JK anajua kwamba safari hii aliingia madarakani kwa kuchakachua na hivyo akiona hata 'nyasi' anadhani ni 'nyoka' wa kumtoa madarakani? Mbona wakati ule alipopata ushindi wa asilimia 80.2 hatukuusikia huu wimbo? Kwa nini miaka hii? Na kwa nini Februari 5 mwaka huu akiwahutubia wana CCM wenzake kule Dodoma aliwaambia "wapinzani wametusumbua sana na hivyo huko tuendako inabidi tugangamare sana"? Je, kugangamara alikomaanisha ni kwamba aliingia madarakani isivyo halali na hivyo inabidi wagangamare ili kusalia kwenye madaraka kwa miaka 5? Na je, kugangamara kwenyewe ndo huku kwa kutumia ofisi ya DCI kunyamazisha uhuru wa maoni? Kama ndivyo napenda nirejee maneno ya mwandishi Angela Kiwia kwenye Dira la Jumatatu wiki hii kwamba wamekosea sana maana hiyo ni sawa na kuzuia mvua isinyeshe.

Fanikio la pili la safari yangu hiyo ni kwamba imeniwezesha kuishi japo kwa siku kadhaa maisha ya nusu jehanamu iitwayo mahabusu hapa Tanzania. Sasa siogopi tena kwenda huko wala siogopi tena kufungwa. Na fanikio la tatu nimefanikiwa kujua yale ambayo sikuyajua. Yako mengi yaliyonipeleka huko na ambayo ndiyo niliyoyataka na nitayaandikia ripoti kamili na kuifikisha kunakohusika. Lakini najua wengi mnataka kujua ilikuwaje huko hivyo nitawasimulia kwa kifupi ilikuwaje. Nilipigiwa simu na SSP Hiza wa ofisi ya DCI makao makuu ya jeshi la polisi Jumatatu Desemba 5. Nikaitika wito na kuripoti ofisini kwake Jumanne kesho yake ambapo nilihojiwa na Inspekta Msaidizi Nicholaus Stanslaus juu ya makala niliyoitaja hapo juu nikituhumiwa kama nilivyoeleza. Baada ya kuandika maelezo yangu nilitakiwa kuripoti tena polisi kesho yake Jumatano na nikafanya hivyo na ndipo nilipokamatwa siku hiyo hiyo na kuswekwa rumande ya kituo kikuu cha polisi Dar es salaam. Nililala humo mpaka asubuhi wakaja kunichukua na kunirejesha makao makuu ya jeshi kabla ya asubuhi hiyo hiyo ya Alhamisi Desemba 8 kupelekwa mahakama ya Kisutu na kusomewa shtaka hilo la uchochezi.

Walikuwepo madiwani wawili waliokuwa tayari kunidhamini lakini kwa maombi ya upande wa mashtaka nilitakiwa kuwa na wadhamini wawili na mmoja lazima awe na hati ya nyumba. Na kwa sababu hakuna aliyelitarajia sharti hilo hakuna aliyekuwa nayo pale mahakamani na hivyo nikaambiwa sikutimiza masharti ya dhamana na ndipo nikapelekwa kwenye gereza la mahabusu la Keko. Niliingia gerezani Keko nikiwa nimevalia vazi la kombati kitu kilichowafanya mahabusu zaidi ya 1000 walioko mle na wafungwa takribani 100 pamoja na askari magereza wote kunitambua kwamba ni mtu wa CHADEMA. Kama kuna kitu nawashukuru wapelelezi wa DCI Manumba na usalama wa taifa ambao tuligundua kwamba walikuwa wakifanya kazi kwa karibu sana katika suala hili, ni kule kutouambia uongozi wa gereza la Keko kunitenga na mahabusu wa kawaida. Kwa hiyo nilipofika nilichanganywa nao ugali na maharage, nikalala nao 'mchongoma', mpaka nikapata fursa ya kutembelea chumba cha 'gereza ndani ya gereza'.

Ugali unatolewa mara moja kwa masaa 24 na mchana wa kati ya saa 6 na saa 9. Ni ugali uliopikwa kwa unga ambao kimsingi hata mbwa anayefugwa nyumbani kwa waziri anaweza asiule kwa maharage yaliyochemshwa (si kupikwa). Baada ya kula saa 10 alasiri kengele inapigwa na wote mnalazimishwa kwenda kulala. Selo namba 5 na 6 za bwalo namba IV ambazo nililala (namba 5 siku moja na namba 6 siku 6), zote zina eneo la futi za eneo 450. Kwa kipimo cha siku hizi ni chumba cha kama mita 9 kwa tano hivi. Mpaka leo kwenye milango yako kibao kimebandikwa kwamba wanatakiwa kulala watu 15 kila selo lakini namba 5 tulilala 66 na namba 6 hadi naondoka tulikuwa tukilala watu 64. Siku ile ya kwanza nilipelekwa mnadani (mahali ambapo mahabusu wageni hujikusanya na manyapara wa kila selo kuja kuchagua idadi ya kuongeza kwenye selo zao kama wanunuzi wachaguavyo ng'ombe mnadani) na nikachukuliwa kwenda namba 5. Kule tulilala mchongoma. Mchongoma ni aina ya kulala kwa kujibananisha kupita kiasi ili watoshee watu zaidi ya 60 kwenye selo waliyopaswa kulala watu 15.

Kwanza mnajinyoosha kama maiti inyooshwavyo kisha mnalalia ubavu ambapo wa kwanza akilala kwa kuelekeza kichwa ukutani anayefuata ataelekeza miguu, anayefuata kichwa, anayefuata miguu, mpaka mwisho. Hakuna kujigeuza kwa kuwa hakuna nafasi na utakuwa unawasumbua wenzako lakini kutokana na kuchoka inabidi kila baada ya masaa mawili nyapara apige makofi na hapo ndipo mnageuka wote na kulalia ubavu mwingine.

Hayo ni machache kati ya mengi sana niliyoyagundua kule. Kama nilivyosema mwanzo, yaliyo mazito nitayafikisha kunakohusika. Lakini naomba niwashukuru sana mahabusu wa  Keko kwa jinsi walivyonipokea na ushirikiano walionipa tangu waliponipokea. Kwa kuwa niliingia nikiwa sina ndoo ya kuchotea maji nilitakiwa nisioge mpaka siku ninapokwenda mahakamani kwa mujibu wa sheria za selo kama nilivyopewa orientation na mabwana afya wa selo zote za 5 na 6. Lakini siku ya kwanza nilipolala namba 5 ratiba ilikatizwa na mahabusu wote wakatangaziwa kwamba wamwachie kiongozi aoge kwanza. Nikaenda kuoga na asubuhi nilioga pia wakati ni wale wanaomiliki ndoo 2 ndio wanaoruhusiwa kuoga mara mbili kwa siku.

Kesho yake kijana kutoka Arusha alinitambua na kuniuliza. Nilipomhakikishia kwamba mimi ndiye Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha alisikitika sana. Amekaa ndani ya gereza lile tangu 2008 na kesi yake haijaanza kusikilizwa. Yeye alinipeleka kwa askari wa selo namba 6 ambaye amekaa humo gerezani tangu 2010 Julai akiwa ni zao la siasa chafu za CCM kwa kuwa alikuwa anagombea udiwani kwenye kata moja. Yeye alinipangia mahali pa kulala kwenye kigodoro change peke yangu akisema kiongozi siwezi kulala mchongoma. Nilioga mara mbili kwa siku kwa ridhaa ya mahabusu wote na siku ya zamu yangu ya kuchota maji, tuliokuwa nao zamu walikataa katakata nisichote maji. Hata kombati ilipochafuka nikataka kufua, vijana walininyang'anya na kuifua wao.

Siku naondoka mle kwa pamoja waliniomba kwa niaba ya mahabusu wote wa Tanzania niwe msemaji wao. Nilikubali wajibu huo na nitautekeleza kwa uwezo wangu wote kwa namna tuliyokubaliana nao. Nachukua fursa hii kuwapa pole mahabusu wote Tanzania kwa jinsi ambavyo wanatendewa kinyume cha katiba ya nchi ibara ya 13 (6) (b) ambayo inasema, "ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo". Lakini ndugu hawa wamefungwa tayari bila mahakama kuthibitisha kama wana hatia. Wakati naingia nilikuta katoka siku chache tu zilizopita mahabusu ambaye aliishi ndani ya gereza hilo kwa miaka 11 halafu baadaye mahakama ikamwachia huru kwamba hakutenda kosa hilo.

Mahabusu tunaowaona ndani ya mabasi na makarandika ya polisi ni asilimia chini ya 20 ambao wametenda makosa kweli. Wengi ni wale ambao wanakamatwa na askari wakifika kituoni wanaulizana, "haroo, ile kesi ya wizi wa kutumia silaha nyumbani kwa IGP imeshapata mtu?" Akijibiwa bado, ndipo hutamka, "ripe hiri ri-Wambura". Na anamalizia kwa kumwambia si ulijifanya mjanja, utafia jela. Vivyo hivyo kwa kesi za mauaji. Matokeo yake vijana wa watu waliokamatwa kwa uzururaji wanajikuta wanafikishwa mahakamani kwa mauaji na hawatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama waliyofikishwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji na wanakwenda kukaa jela miaka mitano, sita, nane, kumi ama hata 11 bila hatia. Wanaacha kazi zao ama biashara zao, familia zao zinayumba, wanaliongezea taifa mzigo wa kuwalisha bila kufanya kazi kwa miaka yote hiyo kumbe kwa sababu ya polisi wetu kuwabambikia kesi aidha kwa chuki binafsi ama kwa sababu wamekosa rushwa ya kuwapa.

Mahabusu hawa hawaruhusiwi kupiga kura wala kuchangia mchakato wa katiba mpya. Hawana mawasiliano na yoyote na simu ndani ya gereza ni kosa la jinai II ambalo litakupeleka gerezani ndani ya gereza. Nilikwenda kuwasalimia wale waliokuwa ndani ya gereza gerezani. Ni watu wenye makosa ya kukutwa na simu, ama sigara ama wakapigana na wenzao. Hawa huwekwa kwenye selo maalum namba 6 kwenye bwalo namba 6. Ndani ya selo hiyo watakaa siku 14 mchana na usiku bila kutoka nje ya selo. Aidha katika siku zote kumi na nne wataishi uchi wa mnyama hata kama watakuwemo watano. Watashinda uchi na kulala uchi na zamani chumba kilijazwa maji na hivyo wakilala wanalala majini. Siku hizi wamepunguza kwa madai ya kuheshimu haki za binadamu. Kwa siku wanakuwa wanapewa chakula  mara moja na ni ugali robo ya ule anaokula mahabusu wa kawaida. Na hawapewi mboga isipokuwa rundo la chumvi.

Nikataka kujua hizo simu zinaingizwaje gerezani. Kwa sababu siku tunaingia tulivuliwa nguo zote na kusachiwa kwa kupitishiwa kwenye mwili scanner ya kutambua kama tumeficha kitu chochote mwilini. Na hilo hufanyika kwa kila mahabusu ama mfungwa anayeingia kutoka nje ya mlango wa gereza bila kujali kama atatoka na kuingia mara ngapi kwa siku hiyo. Nikaambiwa kwamba askari wenyewe wanachukua rushwa kwa mahabusu na kuwaletea simu halafu kisha tena wanakuja kuzikamata na kupewa rushwa na wakikosa wanakupeleka kwenye selo ya adhabu.

Ndugu zangu ukurasa huu hautatosha kueleza yote. Nawasihi tu tubadili mtazamo na kuanza kupigani haki za hawa watu pia. Ni watanzania wenzetu wanaoonewa sana bila mtetezi kwa kuwa tulio nje tunadhani ni majambazi yote, ni wauaji wote, ni wezi wote, ni wachochezi wote, na kila aina ya makosa kumbe sivyo. Jaribu kutafakari lakini kujua vizuri ni mpaka ufike kule. Kama una ubavu andika makala ya uchochezi upelekwe!       

Samson Mwigamba, Tanzania Daima, Jumatano  Desemba 21, 2011.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment