Thursday, 28 January 2016

[wanabidii] Kwa nini tusimwache Magufuli afanye kazi?

SINA tatizo la msingi na wananchi wa kawaida kuhoji na kulalamika juu ya uamuzi wa aina mbalimbali anaochukua Rais John Magufuli akiwa katika harakati za kutekeleza ahadi zake kama mgombea wa urais. Sina tatizo kabisa na watu ambao hawajawahi kuwa sehemu ya serikali au walio nje ya serikali (ambao hawakuwahi kushika nyadhifa kubwa) wakilalamika na kuhoji mambo mbalimbali na hata kupinga uamuzi wowote.

Hata hivyo, nina tatizo la msingi kabisa ninaposikia viongozi au watendaji ambao siku chache nyuma waliwahi kushika nafasi kubwa za uongozi wakianza kupinga mwelekeo na utendaji wa Serikali ya Magufuli. Tanzania ina Rais mmoja tu ambaye ndiye anadhamana ya kuliongoza taifa kwa miaka mitano ijayo. Yeye ana jukumu la kusimamia serikali yake anavyopenda.

Sasa inapotokea watu – ambao labda waliitaka nafasi hiyo hiyo ya Magufuli – wanaanza kumkosoa na kuhoji uwezo wake wa kiuongozi ni lazima watu hawa wakataliwe na kukemewa. Wakataliwe kwa sababu wao hawakuchaguliwa na mipango yao ya kuitaka nafasi ile ya Magufuli ilishindikana. Hili ni matokeo ya demokrasia tu.

Kama Magufuli ataanza kuwasikiliza hawa na kujali wanayoyasema na hivyo kutekeleza wanayoyataka ina maana nchi itakuwa na uongozi usio na mwelekeo. Chukulia kwa mfano mtu ambaye amekosoa ubomoaji wa waliojenga kiholela, au anayehoji watu kuchukuliwa hatua kali, au wakwepa kodi kubanwa; hivi huyu mtu anataka kutuambia kuwa yeye angekuwa Rais hawa wakwepa kodi angefanya nao nini?

Angeshikana nao mikono na kuimba "kioo kioo alikivunja nani?" Hivi ambaye anapinga hizi bomoabomoa ina maana yeye angewaacha watu waendelee kujenga kiholela kwa sababu kuwabomolea nyumba zao watu watalia na kupata mishtuko? Hivi si ndiko nchi ilikuwepo huko kwa miaka karibu ishirini hii?

Hivi, leo hii wakuu wa TRA wameng'olewa, wakuu wa Uhamiaji matatani, Takukuru bosi katimuliwa halafu watu wanahoji "ooh anafanya hivyo kwa sababu hawa wametuliwa na mwingine" hivi ina maana wao wangeshika nafasi ya Magufuli leo hii watu wa TRA, Uhamiaji, Takukuru wangeendelea kupeta? Au wenzetu wangefanya nao nini? Au wafanyabiashara wajanja wajanja (waliokwepesha makontena yao) wenzetu wangefanya nao nini? Ina maana wasingeenda kuangalia kinachotokea Bandari? Wasingemfukuza mtu hata mmoja? Wasingemhamisha anayetakiwa kuhama? Na kwa hakika wasingeagiza watendaji wabovu wasifikishwe mahakamani?

Kama kweli wana tatizo na Magufuli ndugu zetu hawa waseme wao wangefanya nini na kama wanataka kuwatetea hawa wakwepa kodi watoke hadharani na waseme wanawatetea kuliko kujificha kwenye pazia la kujifanya wanatoa maoni ya ushauri?
Ushauri gani wa kumshauri kiongozi mkuu wa nchi asifanye kazi aliyosema atafanya? Hivi Magufuli aliposema anataka kwenda kutumbua majipu walifikiria anasema kama utani au ngonjera ili wengine waje na beti zao nao wajibu?

Mbona – kama nilivyosema huko nyuma – Magufuli bado hajaanza kazi mwenyewe hasa hasa? Hivi walimtaka Magufuli aingie na kuendelea kana kwamba mambo yako sawa tu? Au wenzetu walikuwa hawafuatilii muda ule wa kampeni yale ambayo Magufuli aliyasema? Au walidhani alikuwa ni mwanasiasa kama wengine ambao wanasema wasiyomaanisha na wanamaanisha wasiyoyasema? Magufuli alisema alichosema na sasa anakifanyia kazi na hawa "magenius' wetu wanataka ageuke alivyosema?

Binafsi naamini kabisa kuwa hata wapinzani wanapokosoa wanakosoa kwa haki yao lakini hawawezi kukosoa na kumtaka Magufuli asifanye kazi. Sijamsikia mpinzani wa kweli ambaye anapinga Magufuli kushughulikia viongozi wabovu, wakwepa kodi, watumia madaraka vibaya na akabakia mpinzani. Mpinzani ambaye anataka Magufuli awaonee huruma, awaogope baadhi yawatu (wawe wafanyabiashara au vinginevyo) huyo si mpinzani. Na kiongozi yeyote ambaye anatoa ushauri ambao unaonekana una lengo la kupunguza kasi na makali ya kazi ya Magufuli sidhani kama analitakia taifa ahueni au anawatakia (anajitakia) yeye ahueni mahali fulani.

Binafsi kama nilivyosema huko nyuma, naunga mkono harakati za mabadiliko na ninaziunga kwa asilimia mia moja na moja. Magufuli asirudi nyuma, asisite, asitishike na asiwaangalie machoni wale ambao wanakutana na mkono wa sheria. Magufuli asirudi nyuma kwa sababu Tanzania imekuwa na muda wa kutosha wa viongozi vigeugeu, uchwara na wenye kuendekeza "uenzetu huu" kiasi kwamba wameacha alama mbovu ambazo tunatamani zifutwe kabisa.

Mapambano ya kweli dhidi ya ufisadi ndio yameanza na kwa hakika yatagusa hata wasioguswa, yatashika wasiowahi kushikwa na yatarudisha heshima ya Mtanzania popote pale alipo. Mabadiliko haya ni lazima yapate upinzani kwani ndivyo ilivyo asili ya mabadiliko yoyote yale ambayo yanalengo la kubadilisha kwa haraka na kwa kiasi kikubwa maisha ya watu. Ni lazima kuwepo kwa upingamizi (resistance) dhidi ya mabadiliko. Lakini mabadiliko ni lazima!

Wenye mawazo ya kutaka kuongoza nchi tofauti na Magufuli; na wale ambao wanataka kuona nchi iendeshwe tofauti na hivi wana muda wa kujipanga; miaka mitano si mingi. Waje na mapendekezo yao 2020 na wapiga kura wakiwakubalia watawachagua; sasa hivi hizi ni zama za Magufuli. Anaiweza shughuli.

0 comments:

Post a Comment