Na Maalim Kisisyina,
Kwa muda mrefu sasa ndugu zetu wa kisiwa cha Pemba wamekuwa wakitajwa
kwa sifa nyingi mbaya. Lakini hakuna mtu aliye na sifa mbaya zote,
ndugu zetu wa Pemba pia wana sifa nyingi nzuri ambazo siwezi
kuziorodhesha zote hapa.
Baadhi ya sifa hizo ni ukarimu, na kuamini upesi kila jambo, na umoja
kwa wanaloliamini. Hizi ndio silaha kuu na sifa za wazi za ndugu zetu
hawa. Ndugu zetu hawa ni watu wanaopenda kuwakirimu wageni na
hawapendi kukirimiwa. Pia wakishaliamini jambo hakuna malaika wa
kuwabadilisha msimamo wao. Asiyelijua hili na akawaulize CCM
watamjibu.
Katika sifa zote nilizozitaja, hii ya kuamini kila kitu imekuwa
ikiwaadhibu ndugu zetu hawa kwa kiasi cha kutisha. Na kama
nilivyokwishasema, ndugu zetu wakishaliamini jambo lao na kulikubali
hakuna malaika, kizuu, wala msukule wa kuwabadilisha imani zao hizo.
Wao huwa tayari kufa na kukosa kila kitu kusimamia na kutetea msimamo
wao huo.
Sawia na hili, ndugu zetu wakishalipenda jambo au kuliendekeza huwa
ndio utamaduni wao kwani wenyewe husema 'liingialo mjini si haramu'.
Ushahidi wa hili rudia matukio ya vifo vilivyosabaishwa na kula kasa
mwaka 1996 kule Vitongoji na Wingwi. Pia rudia matukio kama hayo kule
Tumbe tarehe mosi hadi tarehe sita Disemba mwaka 2011, ambapo zaidi ya
watu 11 walikufa kwa kula kasa.
Labda sasa nirudie katika hoja yangu isemayo kwamba tabia ya kuamini
kila kitu na kukishikilia bila kukichunguza au kukijuwa vizuri kwa
undani wake kumekuwa ndio janga kubwa la wananchi wa Pemba. Na pamoja
na kuwa tabia hii imekuwa ikileta athari lukuki ambazo baadhi
nitazitaja hapa, hakuna hata mtu mmoja aliyejali wala kuzinduka kwa
hili.
Ndugu zetu hawa wamekuwa kama wale watoto wanaocheza mchezo wa kitoto
unaoitwa 'Watoto muwangapi, wale wale Sada Mbaraka', wakati watoto hao
wakinyofoloewa mmoja mmoja na zimwi, wao huendelea kuitikia tu 'Ni
wale wale Sada Mbaraka' mpaka wakizinduka wamekwisha wote au kabakia
mmoja wa mwisho alie usoni.
Kwa mfano, wakati wa miaka ya 1970, kula Pemba ukienda kuposa ukasema
wewe ni Jeshi basi ilikuwa huulizwi tena suali, utaozeshwa tu na watu
wote watakunyenyekea. Kwa kuamini kuwa mtu mposaji huyo ni Jeshi kuna
dada zetu wakaozeshwa manyang'au na magumegume ya kutikisa jehenamu.
Hata Siku watu walipogutuka, ilikuwa tumeshakaushwa kweli kweli. Ukaja
msimu wa miaka ya 1980, ambapo ukisema wewe ni Mwalimu au wafanya kazi
Bizanje, basi mke ni wako. Tukaliwa tena. Mwanzoni mwa miaka ya 1990,
ukienda Pemba ukisema wewe ni mfanyabiashara una duka Bara, ujue una
mke hata kama ana uzuri wa Shaharizade utapewa tu. Mwishoni mwa miaka
ya 90 na 2000s, ukisema unakaa ulaya, hata ukipeleka picha inayonesha
miguu yako tu, basi utapewa mke unayetaka. Hivi ndivyo ndugu zetu
walivyo na imani zao zinavyowapeleka.
Sasa katika mfano huo hapo juu sikusudii kupinga watu kuozeshana, laa
hasha! Nakusudia kusema kuwa kuna baadhi ya ndoa za uaminifu kama huo
zilileta faida lakini ziko zilizotia hasara kupita kiasi.Kwa mfano
katika hiyo miaka ya 1980s na hadi hivi Karibuni, kulikuwa na mtindo
wa watu kuozesha watoto wao kwa watu wanaoishi Muscat, Oman. Harusi
hizi zilikuwa za aina yake hasa kwa ufahari na magharama
yaliyoyakifanywa kwa harusi zenyewe.
Mbali na hayo harusi hizi zikifanywa kwa chapu chapu kuliko mkate wa
jemi. Yaani mposaji anakuja leo anajifanya ana haraka, siku ya pili au
ya tatu anaowa. Na hutoa mahari ambayo ni thamani ya ngamia au wakati
mwengine thamani ya gari mahari hayo. Basi kwa tabia ya kuamini mno
watu kibubusa, mtu huyu huozeshwa mtoto huyo wa watu hata kama mtoto
huyo hataki, bila kuchunguzwa wala kufatilia lolote juu ya mume huyo.
Matokeo yake, wakishakuolewa ndugu zetu hawa na kuchukuliwa Muscat,
hufanywa watumwa wa daraja la kwanza. Na kwa taarifa tulizonazo, watu
hawa hupelekwa Salala huko kuchunga mifugo, kusimamia mashamba ya
mitende, au kufanya kazi za punda za utumishi wa nyumbani. Baya zaidi,
toba sikio, kuna habari kuwa msichana huyu huwa kaolewa na watu zaidi
ya nane waliochanga mahari yale mengi kuja kuoa kule Pemba. Nasema
lisemwalo liko, kama haliko laja, wako ndugu zetu yaliyowakuta haya.
Hili la kwanza.
La pili na nnalolichukia zaidi, na pia ninalotaka pia kuwafikishia
taarifa Wizara ya wanawake na watoto, ni ile tabia ya watu wanaojiita
wa mjini ama Pale Chake, Wete na Unguja mjini, kutoka kwenda Pemba,
hasa maeneo ya Micheweni kuomba watoto wadogo wa kike kwa kisingizio
cha kuwalea.
Kama nilivyokwishasema, Wapemba wanaaamini kila mtu tena Upesi, na
ndio wakampa John Okelo pa kukaa kule Vitongoji kisha akaja kupindua
Unguja. Kwa tabia hii wazazi hukubali kuwatoa watoto wao wadogo wa
kike na kuwapa watu wa mjini wanaojidai kutaka kuwalea na kuwasomesha.
Ukweli ni kwamba, na kwa kushuhudia kwa macho yangu, watoto wa aina
hii wanateswa na kunyimwa haki zao za msingi kama watoto na hata kama
binadamu. Nimwahi kushuhudia watoto waliochukuliwa kutoka maeneo ya
Micheweni walio chini ya umri wa miaka 12, wakitumwa kwa kazi za
nyumba na kutukanwa. Watoto hawa wana manyanyaso makubwa na hawapewi
elimu wala upendo wanaostahili.
Bahati nzuri au mbaya watoto hawa hujengwa kwa misingi ya nidhamu ya
woga, kiasi ambacho hata wakija wazazi wao au mtu kuwauliza huwa
wazito kusema ukweli. Lakini mateso yakijaa usoni hujionesha kama
kioo. Ukiwaona tu watoto hawa kwa jicho moja tu utajua kuwa wana hali
ngumu.
Kinachonishangaza zaidi, ndugu zetu wa Pemba (na watumbatu kwa hili
wamo), bado huamini kutoa watoto wao kwa watu wasiowajua eti kwa kila
kinachodawaiwa kupunguziwa mzigo wa ulezi. Hii si haki na naiomba
Wizara husika ifuatilie suala hili na kulipatia ufumbuzi haraka
iwezekanavyo.
La mwisho ni hivi juzi kule Ziwani Pemba. Tunaambiwa kuna kikundi
kinahamasisha Liwatwi na kuwaingiza watoto katika dini ya kishia.
Bahati nzuri au mbaya pia, sisi watu wa visiwa hivi hatuoni hasara ya
jambo hadi tupate madhara. Na kwa hapa sitatoa mfano wa meli mbovu
tunazoziamini kusafiria zikituuwa. Naliacha kama lilivyo.
Turudi kwenye ushia. Suala la kuwepo kwa watu wa aina ya ushia kule
Pemba lipo siku nyingi. Na wamekuwa wakiwachukuwa watoto wetu siku
nyingi kuwapeleka kuwasomesha shule zao kule bara kwa muda mda mrefu
sasa.
Moja ya skuli hizo ni 'Wal-ul-asri' iliyoko Kibaha mkoa wa Pwani.
Ukienda skuli hii utawakuta ndugu zetu wengi wa Kipemba wakisoma hapa
wazazi wao wakiamini wanasomeshwa dini ilhali wanasomeshwa upotofu tu
wa Ushia uliokosa dira. Lakini wapi, hakuna anaejali. Na hata
tulipoanza kushtuka juzi, tumeshachelewa sana.
Tumechelwa sana kwa sababu, mambo yote haya niliyoytaja yameshakuwa
makongwe ni ya muda mrefu sasa, na yameshaleta athari kubwa katika
jamii zetu. Nini kifanyike? Badala ya kukimbilia afisi za mufti na
kushitaki huku tukitokwa na vipovu vya midomo kwa mihasira na jazba,
naona kwamba suluhisho pekee, ni kubadilika tabia. Yaani kuna haja
iundwe timu maalum ya uamsho wa kuwabadilisha watu tabia na kuwataka
watafakari kila jambo kwa kina na kuacha kuamini bila kufanya utafiti
wa jambo lenyewe.Na kwa hili tu ndio tutafanikiwa. Tuacheni kuamini
kibubusa, tutumie akili zetu na maarifa tutaangamia!
Natoa hoja!
--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 comments:
Post a Comment