Sunday 22 December 2013

Re: [wanabidii] HOTUBA YA WAZIRI MKUU MIZENGO P. PINDA , KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 14 WA BUNGE

Wakati wanashinikiza jeshi lifanye kazi walitegemea nini? Kama wasingetaka watu wapigwe wangetuma asasi za kiraia mashehe na wachungaji kwenda kuelimisha umma madhara ya ujangili.

Sasa munatuma jeshi waliofundishwa kupiga na sio kuelimisha umma, wamepiga munawasakama mawaziri, sasa mizigo imepumua wala haitajwi tena.


----------
Sent from my Nokia phone

------Original message------
From: Abdalah Hamis <hamisznz@gmail.com>
To: <wanabidii@googlegroups.com>
Date: Sunday, December 22, 2013 12:02:58 AM GMT-0800
Subject: [wanabidii] HOTUBA YA WAZIRI MKUU MIZENGO P. PINDA , KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 14 WA BUNGE




*HOTUBA YA WAZIRI MKUU MIZENGO P. PINDA , WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA
MKUTANO WA 14 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 21, DESEMBA 2013*


*I: **UTANGULIZI *

*a) **Masuala ya Jumla *



*Mheshimiwa Spika,*

*1. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa
kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa Dodoma kwa takriban siku 15
za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi za Mkutano wa 14 wa
Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa hivi leo.*



*Mheshimiwa Spika,*

*2. Nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa
Dkt. Asha Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge
katika Bunge lako Tukufu. Wengi wetu tunafahamu uwezo mkubwa wa Dkt. Asha
Rose Migiro na bila shaka ndiyo sababu Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa
kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia sifa nzuri alizonazo. Pamoja na
kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje ya Bunge lako Tukufu.*



*Mheshimiwa Spika,*

*3. Tangu Mkutano wa 13 wa Bunge baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa
na Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia fursa hii kuwapa pole wote
waliofikwa na misiba hiyo. Lakini katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge
walipata fursa ya kujadili Azimio la Bunge kuhusu kuungana na Nchi ya
Afrika Kusini, katika kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga ubaguzi wa rangi,
Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba Mandela
kilichotokea tarehe 5 Desemba 2013. Wote tunakubaliana kwamba huu ni msiba
Mkubwa kwa Dunia nzima na hasa kwa wale wanaomfahamu Mzee Mandela na
historia yake.*



*4. Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwakilisha vyema Watanzania
wote katika msiba huu mkubwa wa Afrika na Dunia nzima. Hotuba ya Mheshimiwa
Rais aliyoitoa wakati wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela tarehe 15
Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa kuitangaza Tanzania Dunia nzima
katika ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani Afrika katika Karne
ya 20. Ninaamini kwamba hiyo ni Historia ambayo haitafutika vizazi vingi
vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga na kufuata nyayo zake.*





*b) Maswali Mheshimiwa Spika,*



*5. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kuuliza maswali ya
msingi 170 na ya nyongeza 458 ambayo yote yalijibiwa na Serikali. Aidha,
maswali 17 ya msingi na 15 ya nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali
ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa
kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa Mawaziri kutoa majibu ya maswali hayo
kwa umahiri mkubwa.*



*Mheshimiwa Spika,*

*6. **Pamoja na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako
lilikamilisha kazi kubwa *

*zifuatazo:*



*Kwanza: Bunge lilijadili na kukamilisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni
wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];*



*Pili:*

*Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge za Sekta*



*Mtambuka.*

*Tatu:*

*Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge*



*zinazosimamia Fedha za Umma; na*

*Nne:*

*Kujadili Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za Kisekta.*



*7. Aidha, Bunge lako Tukufu lilijadili kwa utaratibu wa Hati ya Dharura
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka
2013 [The Excise (Management and Tariff) (Amendment) Bill, 2013]. Mwisho
Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 ulisomwa kwa
mara ya kwanza.*



*8. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili
Taarifa hizo na kutoa maoni na ushauri kwa uwazi mkubwa na kwa kina.*

*Mapendekezo na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umepokelewa na
Serikali na utazingatiwa kwa uzito unaostahili.*



*II: **KILIMO *

*a) **Hali ya chakula Nchini Mheshimiwa Spika, *

*9. **Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa 13, hali ya
upatikanaji wa Chakula Nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha
katika maeneo mengi *



*kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika maeneo
mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi
Oktoba na Novemba, 2013 katika maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula
na lishe inaonesha kuwa jumla ya Watu 828,063 wanakabiliwa na upungufu wa
chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi
Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya Tani 16,119 za chakula cha
mgao kwa Halmashauri zenye mahitaji ya chakula cha msaada. Hadi kufikia
tarehe 16 Disemba 2013, jumla ya Tani 13,716 zilikwishachukuliwa na
Halmashauri husika. Tani 2,402 zilikuwa hazijachukuliwa na Halmashauri za
Mwanga, Babati, Igunga, *

*Mpwapwa na Manyoni.*



*10. **Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo
hazijachukua chakula hicho kufanya hivyo kabla ya tarehe 15 Januari 2014.
Ambao *

*hawatatekeleza maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria. Nitumie
nafasi hii kuwahakikishia Wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia
upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa
lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.*



*b) Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini Mheshimiwa Spika,*

*11. Kutokana na miezi hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa
ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua.
Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele
katika soko hapa Nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi kikubwa. Kwa
mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 536.86 kwa kilo
mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikia Shilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba,
2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka
Shilingi 1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10 kwa
kilo mwezi Novemba, 2013.*



*12. Pamoja na kuwepo kwa hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa
baadhi ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini
ikilinganishwa na zile za kipindi kama hiki mwaka jana. Natoa wito kwa
Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha wakulima
kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada
katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu.
Halmashauri zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela wa chakula kutoka
mashambani na majumbani mwa Wakulima kwa lengo la kujihakikishia
upatikanaji wa chakula cha kutosha.*







*c) Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa*



*Mheshimiwa Spika,*

*13. Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ilipanga
kununua Tani 250,000 za nafaka. Wakala umeendelea na kazi hiyo na hadi
kufikia tarehe 11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa umekwishanunua kiasi cha
Tani 218,499 za nafaka sawa na Asilimia 87.4 ya kiasi kilichopangwa
kununuliwa. Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Desemba, 2013, Maghala ya Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba ya jumla ya Tani 233,808
za nafaka. Kati ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi na Tani 493 ni za
Mtama.*



*14. Wakati huo huo, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unaendelea
kuhamisha chakula kutoka katika maghala yake yaliyoko katika Mikoa
iliyozalisha ziada kwenda kwenye maghala yaliyoko kwenye Mikoa yenye
upungufu wa chakula ili kukabiliana na mahitaji ya chakula cha msaada
kitakachohitajika kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe 9 Desemba,
2013, jumla ya Tani 44,129 za Mahindi zimekwishahamishwa. Serikali
inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kununua chakula katika Mikoa yenye
ziada ya chakula na kukipeleka katika Mikoa yenye upungufu wa chakula.*





*d) Hali Halisi ya Usambazaji wa Pembejeo*



*Mheshimiwa Spika,*

*15. Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali
ilichapisha jumla ya vocha 2,796,300, kwa ajili ya pembejeo za Kilimo kwa
msimu wa Kilimo wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12 Desemba, 2013, Tani
74,925 sawa na Asilimia 96 za mbolea ya kupandia na Tani 42,295 sawa na
Asilimia 91 ya mbolea ya kukuzia zilikuwa zimekwishafikishwa katika Mikoa
husika kulingana na aina ya mazao yanayohitaji mbolea hizo. Aidha, Maghala
ya Wakala wa Mbolea Jijini Dar es Salaam yana akiba ya kutosha ya mbolea
hiyo. Nirejee kutoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha kuwa vocha
zote zinatolewa kwa walengwa kwa wakati sambamba na aina ya pembejeo
inayomlenga Mkulima husika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.*



*e) Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.*



*Mheshimiwa Spika,*

*16. Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi
Bilioni 109.6 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya
kununua Tani 250,000 za nafaka. Hadi kufikia tarehe 19 Desemba, 2013 NFRA
ilikuwa imenunua jumla ya Tani 218,499 zenye thamani ya Shilingi Bilioni
109.25 na kwa ajili hiyo. Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri ya wastani
wa Shilingi 500/= kwa kilo ya mahindi, zoezi hilo lilikuwa na matokeo
mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita na liliwavuta
Wananchi wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia nafaka. Hadi sasa
Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa ajili ya zoezi hilo na
imehakikisha kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa NFRA wamelipwa
fedha zao. Aidha, natambua kuwa NFRA ilitumia baadhi ya Wakala kukusanya
nafaka hiyo kutoka kwa Wakulima na kama nilivyosema katika Mkutano wa 13 wa
Bunge, Serikali inatambua kuwa Wakala hao kutoka Mikoa ya Arusha, Dodoma,
Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga wanaidai Serikali jumla ya
Shilingi Bilioni 8.65 Niwaombe Wakala wote wanaoidai Serikali kuendelea
kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa deni hilo
kwa vile kiasi cha deni lao lipo ndani ya bajeti iliyotengwa kwa ajili
ununuzi wa nafaka katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.*





*III: **MPANGO WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA *





*Mheshimiwa Spika,*



*17. Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua Mpango wa Taifa wa Huduma
Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial Inclusion Framework).
Uzinduzi wa Mpango huu ulifanywa na Malkia wa Uholanzi Mheshimiwa Máxima
Zorreguieta*

*Cerruti ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa katika Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha na kushuhudiwa na
Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Wawakilishi wa
Taasisi za Umoja wa Mataifa.*



*Mheshimiwa Spika,*



*18. Lengo la Mpango huo ni kusimamia ukuzaji wa huduma za kifedha kwa
jamii Nchini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya
Fedha. Vilevile, Mpango unalenga kusogeza huduma karibu kwa jamii pana
zaidi ya Watanzania kwa kutumia mifumo ya Teknolojia mbalimbali katika
kufikisha huduma za kifedha kwa Wananchi na hasa Wakulima, Wafugaji na
Wavuvi waliopo Vijijini ambao wengi wao wako nje ya mfumo rasmi wa kifedha.
Teknolojia hizo ni pamoja na:*



*(a) **Huduma za Kibenki za moja kwa moja na kupitia Wakala (Agent
Banking); *



*(b) **Huduma za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali kama vile
M-PESA, TIGO *

*PESA, AIRTEL MONEY na Easy PESA.*



*(c) **Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of Sales – POS). *



*19. **Aidha, Mpango huu utaweka mazingira linganifu na yaliyo bora
kwa kutumia Sayansi na Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi,
kuimarisha Sekta ya *



*Fedha katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa ujumla. Mpango huu pia
utawezesha kuongeza kasi ya upatikanaji wa Chakula, masuala ya Lishe na *



*Maendeleo Vijijini kwa ujumla.*



*Mheshimiwa Spika,*



*20. Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika Nchi mbalimbali Barani
Afrika unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo rasmi wa Taasisi za
Kifedha ni Asilimia 24 tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi waliopo kwenye
Mfumo rasmi wa Asasi za Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na Vyama vya
Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOs) ni Asilimia 22. Asilimia 78 ya
Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na wengi wao ni kutoka Vijijini
hasa Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unalenga
kufikia Asilimia 50 ya Watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha
ifikapo mwaka 2016.*



*Mheshimiwa Spika,*

*21. **Kiwango hiki kidogo cha Wananchi walio katika Mfumo rasmi wa
huduma za *



*kifedha unatokana na changamoto zifuatazo:*



*Moja: Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha Vijijini ni hafifu
hususan barabara, mawasiliano, makazi na huduma za kiusalama;*

*Mbili:* *Wananchi wengi wa Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua*

*umuhimu na faida ya huduma za kifedha. Aidha, utamaduni wa*

*kujiwekea akiba na kukopa ni mdogo; na.*



*Tatu:* *Taasisi nyingi za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa
Vijijini*

*ambao ni Wakulima hawana fedha za kutosha kuweza kuweka akiba*

*katika Taasisi hizo na uwezo wao wa kukopa mikopo ni mdogo, hivyo*

*wakipeleka huduma zao huko hawatapata faida.*



*Mheshimiwa Spika,*



*22. Zipo faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Wananchi
wengi wa Vijijini hasa Wakulima. Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:*



*Moja:*

*Kuwezesha Wananchi kujiwekea Akiba na pia kupata mikopo ya*



*kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za*



*kijamii hivyo kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;*

*Mbili:*

*Huduma za Kifedha Vijijini zinawawezesha Wananchi wengi hasa*



*Wakulima kupata mikopo ya pembejeo na mikopo ya ununuzi wa*



*mazao;*

*Tatu:*

*Huduma za Kifedha Vijijini ni Mkombozi wa Makundi maalum kama vile*



*Vijana, Wanawake, Wazee, na Walemavu. Aidha, zinasaidia Wananchi*



*kujiongezea kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na*



*kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki;*



*na*

*Nne:*

*Kuwepo kwa Huduma za Kifedha Vijijini kunaongeza Usalama wa*

*Chakula, kulinda mazingira na kufanya Vijiji kuwa ni sehemu nzuri ya
kuishi. Mheshimiwa Spika,*

*23. Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuanzisha Huduma Jumuishi za
Kifedha Nchini kwa mfano tumeweza kuanzisha Benki nyingi Nchini. Tayari
tunazo Benki takriban 52 zenye matawi zaidi ya 609 kote Nchini. Lakini pia
tunazo huduma za Bima kwa Makampuni Binafsi zaidi ya 27 na Mawakala wa Bima
takriban 600. Ipo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Umma 5, Masoko ya Mitaji na
Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban 5,600.*



*24. Aidha tunazo huduma za Kifedha kwa kutumia Huduma za Kifedha kupitia
mtandao (PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (POINTS OF
SALES – POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo zaidi ya 55,000 ambapo
Waajiriwa wa moja kwa Moja (Direct Employment) wanakadiriwa kufika takriban
100,000.*

*Mheshimiwa Spika,*

*25. Maisha bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na kutumia Teknolojia na
kurahisisha maisha. Kwa mfano, huduma za M-PESA peke yake zinawezesha
malipo kwenye biashara mbalimbali zaidi ya aina 300 ikiwemo manunuzi kwenye
Supermarket na maduka ya kawaida. Huduma hizo ambazo zinatolewa pia kwa
njia ya TIGOPESA, AIRTEL MONEY, EASY PESA zinaweza kulipia Luku, Ada za
shule na Vyuo, Tiketi za ndege, kufanya marejesho Bodi ya Mikopo ya Elimu
ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya Makampuni haya yameunganisha huduma zao na
Benki zaidi ya 20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard Chartered,
Amana Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia huduma za
jumuishi za kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka Akaunti ya Benki
kwenda M- PESA, TIGO PESA n.k. halafu akazitoa kupitia Wakala. Kwa sasa
Watumishi walio Vijijini hawana tena sababu ya kufunga Ofisi kufuata
mishahara Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha na wanaweza kutoa pesa
kupitia Wakala, na kwa kufanya hivyo ufanisi na tija kwa Watumishi
unaongezaka. Mheshimiwa Spika,*

*26. Ni kweli kwamba tunayo kazi kubwa ya kutekeleza Dhana ya Huduma
Jumuishi za Kifedha Nchini. Lakini ni ukweli kuwa Uzinduzi wa Mpango wa
Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha una manufaa makubwa na mengi ikiwemo
kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini kwa kupeleka maendeleo
Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo ya Milenia. Ni
matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango huu utatuwezesha kusonga mbele
kwa kasi kubwa zaidi. Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za Kifedha na Vituo
vya Kifedha kupitia mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia
Wakala kuongeza jitihada katika kusambaza huduma za Kifedha Vijijini ambako
ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi wanaohitaji huduma hiyo.*



*IV:* *NISHATI NA MADINI*





*a)* *Mradi wa Gesi*



*Mheshimiwa Spika,*



*27. Kama ambavyo Wananchi wengi wanafahamu, Serikali kupitia Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi
wa mitambo ya kusafishia Gesi Asilia katika maeneo ya Madimba, Mtwara
Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa. Pia ujenzi wa Bomba la kusafirishia
Gesi hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam unaendelea
vizuri. Mradi huu utakapokamilika utaunganisha maeneo yanayozalisha Gesi
Asilia hususan Mnazi Bay-Mtwara, Songo Songo, Kisiwani, Mkuranga, Ntorya na
maeneo yaliyogunduliwa Gesi katika eneo la bahari ya kina kirefu. Lengo la
Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi Asilia mbali na matumizi mengine,
inatumika katika kuzalisha umeme ambao kwa sasa Asilimia kubwa unazalishwa
kwa kutumia nishati ya mafuta yanayoingizwa kutoka Nchi za nje na hivyo
kuligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.*

*Mheshimiwa Spika,*

*28. **Katika utekelezaji wa mradi huu, Kazi zifuatazo zimekamilika
hadi kufikia *





*tarehe 30 Novemba, 2013:*

*Moja:*

*Kukamilika kwa upakuaji wa Shehena ya Sita (6) ya Mabomba ya Mradi*



*yapatayo 4,444 ya umbali wa Kilomita 51.169 katika Bandari ya Mtwara.*

*Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013 ni 24,935 ya*





*umbali wa kilomita 295.5;*

*Pili:*

*Kusafisha Mkuza wa Mabomba, tayari Kilomita 498.5 zimekamilika;*

*Tatu:*

*Usafirishaji wa mabomba kutoka kwenye yadi za kuhifadhia na*





*kuyasambaza kwenye Mkuza tayari kwa kuyaunganisha kwa*





*kuchomelea. Hadi sasa mabomba ya Kilomita 186.9*





*yamekwishasafirishwa;*

*Nne:*

*Uchimbaji wa njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa Kilomita 27.0*





*umekamilika;*

*Tano:*

*Uwekaji wa mabomba kwenye njia yake sambamba na kuweka Mkongo*



*wa Mawasiliano (Fiber Optic Cable) umekamilika Kilomita 21.1;*

*Sita:*

*Kufukia bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano. Tayari Kilomita*



*7.30 za Bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano zimefukiwa; na*

*Saba:*

*Utafiti wa njia ya Bomba la Baharini nao umekamilika.*



*Hayo ni maeneo machache ambayo nimeona niyataje.*





*Mheshimiwa Spika,*



*29. Ni kweli kwamba kazi za mradi huu ni kubwa lakini kwa ujumla
zinaendelea vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo za mradi huu ambazo
tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi wa Mradi ambao
sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi wa Gesi na
Mafuta. Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi ni za kitaalamu
sana, malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC) ni kuajiri wafanyakazi
Wakiwemo Wazawa mapema ili waweze kushiriki na kujifunza kwa vitendo
shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi hatua kwa
hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa ujenzi. Utaratibu huu utasaidia kupata
wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania watakaoendesha (operations) na
kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi kwa kipindi
chote cha matumizi.*

*Mheshimiwa Spika,*

*30. Vilevile moja ya makubaliano katika Mkataba wa utekelezaji wa Mradi
huu, Mkandarasi anawajibika kuwapeleka Wafanyakazi kwenye mitambo na
mabomba yanayofanya kazi kwa sasa kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja ili
wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia shughuli zote za kuendesha
mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi. Malengo ya TPDC ni
kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti wakati wa kipindi
cha ujenzi ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi Wafanyakazi wote wawe
wamekwishapata uzoefu wa kutosha.*



*Mheshimiwa Spika,*

*31. Kampuni nyingi zilizopo Mtwara zinazojishughulisha na mambo ya
utafiti na uzalishaji wa Gesi na Viwanda vinavyohusiana na matumizi ya
Gesi, zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa. Kwa mfano, Mpango wa
kujenga mitambo ya kutengeneza Gesi kuwa kimiminika (LNG) wa Kampuni ya
British Gas Tanzania utakuwa na utengenezaji wa ajira nyingi za kiwango
kuanzia Kada ya Chini na Kada ya Kati ambayo itasomesha Watanzania kupitia
VETA katika fani mbalimbali. Wako watakaosomeshwa katika fani ya Vyuma,
wengine ujenzi, uhandisi wa miundombinu na ufundi wa vyuma na umeme.*



*32. Katika Kada ya Kati, Kampuni ya Gesi Tanzania wanatarajiwa kusomesha
wataalamu 16,756 waliofaulu vizuri masomo ya Kidato cha Nne. Takwimu
zinaonesha kuwa kwa Mtwara tu, kumekuwapo ajira mpya 400, na Watanzania
wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta ni sawa na
Asilimia 70 ya watoa huduma hiyo Nchini. Asilimia 30 iliyobaki ya watoa
huduma inatolewa na Wageni.*





*33. Katika Kada za Juu, Kampuni itasomesha na kuajiri Wataalamu wa
Jiolojia, Uhandisi, Kemia na Sayansi husika kwenye Gesi na Mafuta. Matokeo
yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa VETA 370 wamesomeshwa
kuhusu Gesi na Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa na Wanafunzi 12
wa Kada za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na Mafuta ndani
na nje ya Nchi.*



*Mheshimiwa Spika,*

*34. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya British Gas
Tanzania wamegundua gesi kiasi cha Futi za Ujazo Trilioni 13. Katika
kuandaa na kuendesha mradi wa uzalishaji Gesi nyingi kiasi hicho ni dhahiri
kwamba ajira zitapatikana kwa maelfu ya Watanzania. Katika hatua ya ujenzi,
mradi utatoa ajira kwa maelfu; na katika uzalishaji (operations) ajira
nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini, na katika mnyororo wa
usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii kuwapa
Watanzania matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa mengi sana,
kuanzia upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba Waheshimiwa
Wabunge tuendelee kuwaelimisha Wananchi*

*wetu kuhusu manufaa ya mradi huu katika Nchi yetu. Ni fursa ya kipekee
ambayo Wananchi wetu wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha
bora.*



*V: **MATUMIZI YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs) *



*Mheshimiwa Spika,*

*35. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Serikali ililiarifu Bunge lako
Tukufu kuhusu mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Moja
ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi ya Mashine za
Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devices- EFDs). Mashine
hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta moja kwa moja na Mamlaka ya
Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata mapato stahiki bila
udanganyifu. Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia Mtandao wa
Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye Hifadhi Kuu ya
Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.*



*Mheshimiwa Spika,*

*36. **Katika utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka huu, Serikali
imelenga kuingiza Walipa Kodi 200,000 kati ya 1,500,000 ili waweze kutumia
Mashine za *



*Kielektroniki. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye biashara
kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40.
Katika zoezi hili, Wafanyabiashara Wadogo wanaoendesha biashara zisizo
rasmi kama vile Wamachinga na wale wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama
Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata kidogo.*

*Mheshimiwa Spika,*

*37. Katika utekelezaji wa zoezi hili kumejitokeza malalamiko kutoka kwa
baadhi ya Wafanyabiashara Nchini hususan wa Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Lindi
na Dar es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na matumizi ya Mashine hizi.
Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu: Bei kubwa ya ununuzi
wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za kutolea Risiti;
Mchakato uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa wa kutumia
Mashine hizo; na Gharama za matengenezo.*



*Mheshimiwa Spika,*

*38. Kwa kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano ya
Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine za Kielektroniki
zinafanya kazi zifuatazo:*

*Moja: Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara
huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya*



*kuandikia risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;*



*Pili:* *Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za
mauzo, manunuzi*



*na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua*

*miaka mitano;*

*Tatu:*

*Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa siku,*



*kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi*



*kisichopungua miaka mitano;*

*Nne:*

*Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja*



*kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na*



*Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya*



*Taifa ya Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;*

*Tano:*

*Mashine zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka*



*kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu*



*Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;*

*Sita:*

*Kutuma na kupokea fedha kwa njia ya "Mobile Money". Utaratibu*



*huu unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na*



*huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji,*



*Simu, n.k;*

*Nane:*

*Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza*



*inayoeleweka kwa Wananchi wengi;*

*Tisa:*

*Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania*

*kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza Kodi halali.
Mheshimiwa Spika,*

*39. Msingi wa bei ya kununulia Mashine hizi za Kielektroniki umezingatia
pamoja na mambo mengine, manufaa na faida nyingi nilizozitaja kwa mtumiaji
na ubora wa mashine zenyewe. Aidha, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali Duniani unaonesha kuwa
mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo juu zinauzwa na
wasambazaji kwa kati ya Shilingi 600,000/= (Dola 375) hadi Shilingi
778,377/= (Dola 486) ikilinganishwa na bei za Mashine za Kielektroniki za
Nchi nyingine zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania ambazo zinauzwa
bei kubwa za kati ya Dola za Kimarekani 360 hadi 870. Pamoja na bei hizo,
Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana na Wasambazaji wa Mashine
hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei hizo.*



*Mheshimiwa Spika,*

*40. Kuhusu bei za karatasi za kutolea Risiti uchunguzi unaonesha kuwa
karatasi hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/= hadi Shilingi 4,500/=
kuzingatia ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo. Karatasi hizo zina
uwezo wa kutoa wastani wa risiti kati ya Risiti 200 hadi 1,000 kulingana na
urefu wa "Paper Roll"! au Bunda. Bei ya Karatasi hizi zinazojulikana kama
"Thermal Paper" umezingatia kwamba ni za kisasa na hazifutiki kwa urahisi
na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza usalama.*

*Mheshimiwa Spika,*

*41. Kuhusu utaratibu uliotumika kuwapata Watengenezaji na Wasambazaji wa
Mashine hizi za Kielektoniki na Wasambazaji wa karatasi, napenda
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa ushindani wa
Kimataifa na haukuwa na dosari yoyote.*





*Mheshimiwa Spika,*

*42. Katika kutafuta Watengenezaji na Wasambazaji, kwenye Awamu ya Kwanza
Watengenezaji Wanne (4) na Wasambazaji Sita (6) walipatikana kwa kutumia
Zabuni ya wazi ya Kimataifa (International Competitive Tendering) kama
ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni
zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi Desemba Mwaka 2009 mpaka Mei 2010
makubaliano yaliingiwa kati ya kila Mtengenezaji na Msambazaji
aliyechaguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya "Memorandum of
Understanding (MOU).*



*43. Kwenye Awamu ya Pili ya utekelezaji wa utaratibu huohuo wa Zabuni ya
Watengenezaji ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News, The African, Tovuti
ya TRA na Tovuti ya PPRA. Jumla ya Wazabuni Kumi na Nne (14) walituma
maombi ambayo yalifunguliwa mara moja baada ya saa Nne asubuhi tarehe 27
Septemba 2012. Watengenezaji wa Mashine Wanne (4) walichaguliwa kati ya
Kumi na Nne (14) waliokuwa wameomba na Wasambazaji Watano (5) walipatikana
kati ya Tisa waliotuma maombi yao ndani ya muda. Kwa kifupi, huo ndio
utaratibu uliotumika ambao ulikuwa wa wazi na ushindani.*

*Mheshimiwa Spika,*

*44. Ili kuhakikisha ubora wa Mashine hizi za Kielektroniki,
Watengenezaji wametoa "Guarantee" ya muda wa miaka mitatu kwamba Mashine
inayoharibika bila kukusudia na watawajibika kutoa mashine nyingine na pia
kutoa elimu ya matumizi ya mashine hizo. Vilevile, kwa mujibu wa Mkataba
ulioingiwa kati ya Wasambazaji na TRA, Wasambazaji wanawajibika kuzifanyia
matengenezo mashine hizo kila zinapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa
watumiaji kutafuta watengenezaji wao wenyewe. Napenda kuwahakikishia
Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za
Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia
Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na kuwawezesha
kulipa kodi stahiki Serikalini.*



*Mheshimiwa Spika,*

*45. Kwa kutambua umuhimu wa mashine hizi katika kuongeza Mapato ya Ndani;
na ili kuyashughulikia malalamiko ya baadhi ya Wafanyabiashara
yaliyojitokeza, Serikali imesogeza mbele muda wa mwisho wa kununua Mashine
za Kielektroniki hadi tarehe 31 Desemba, 2013. Lengo ni kuwawezesha
Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa kununua mashine hizi na kujifunza
namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa
Sekta Binafsi inaendelea kutoa*

*elimu kuhusu matumizi endelevu na faida za Mashine za Kielektroniki kwa*

*Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na huduma. Natoa wito kwa
Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Serikali
kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Mfumo huu wa
Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu na
kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.*



*VI:* *USHIRIKIANO WA KIMATAIFA*



*Mheshimiwa Spika,*



*46. Tarehe 16 – 25 Oktoba 2013 nilifanya ziara ya kikazi Nchini China
kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li
Keqiang.*



*Katika ziara hiyo, nilifuatana na Viongozi wa Serikali wakiwemo baadhi ya
Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa Asasi za Sekta
Binafsi Tanzania na Watendaji Wakuu wa Serikali na Mashirika ya Umma ambao
walishiriki kwenye mazungumzo na Wabia wetu kwa upande wa Jamhuri ya Watu
wa China.*



*Mheshimiwa Spika,*



*47. Dhamira kubwa ya ziara hiyo kimsingi ilihusu; kukuza mashirikiano ya
kibiashara na utalii Nchini, kufanya mazungumzo na vyombo vya fedha ili
kupata mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili marafiki, kuona Sekta
Binafsi ya Tanzania inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa China na mwisho
kutoa shukrani kwa misaada na mikopo ambayo Nchi yetu imepokea kutoka
Jamhuri ya Watu wa China.*



*Mheshimiwa Spika,*



*48. Kama mnavyojua Taifa la Jamhuri ya Watu wa China ni miongoni mwa
Nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na limepiga hatua kubwa sana
katika maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika
Taifa la China, nilitoa mwaliko wa kuwakaribisha ili kushirikiana na
Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wake katika Nyanja za kiuchumi,
utamaduni na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na
soko kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.*



*Mheshimiwa Spika,*



*49. Katika ziara hiyo nilipata fursa ya kutembelea Miji ya Beijing,
Shenzhen, Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata nafasi ya kukutana na
Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China. Kutokana na Mikutano hiyo,
baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma wameanza kuja Nchini kwa ajili ya
kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ili kuanzisha
ushirikiano wa kiuchumi.*

*Mheshimiwa Spika,*



*50. Kwa ujumla ziara hii ilikuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano, pamoja
na kuendeleza na kudumisha ushirikiano ambao umeanzishwa na Viongozi
waasisi wa Nchi hizi mbili yaani Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati
Mwenyekiti Mao Zedong wa Jamhuri ya Watu wa China, kwenye ziara hiyo,
niliweza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Bwana Li Keqiang,
pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China. Ninaamini tukijipanga
vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.*



*Mheshimiwa Spika,*



*51. Ziara yangu pia ilifanikisha kutiwa saini kwa Mikataba ya
ushirikiano wa Tanzania na China katika eneo la Sayansi na Teknolojia na
katika Utalii. Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu uuzaji wa bidhaa
za baharini za Tanzania Nchini China na kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa
Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao la Pamba Nchini. Aidha, Mikataba ya
Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na Makazi baina ya Makampuni
ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya Umeme – TANESCO,
Shirika la Taifa la Maendeleo – NDC na Shirika la Taifa la Nyumba – NHC
ilisainiwa.*



*Mheshimiwa Spika,*

*52. Mafanikio mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuyashawishi Makampuni
makubwa ya usafiri wa anga na Mawakala wa safari za kitalii kuwekeza
Tanzania. Katika jitihada hizo nilikutana na Makampuni ya China Hainan,
China Southern Air Line Holding Company na China Travel Service (Holdings)
Hong Kong Limited.*

*53. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa kiasi kikubwa Makampuni
haya ya Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha utayari wao wa kuanzisha
safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na China. Aidha, Kampuni
ya*

*China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited **ambayo inafanya
biashara ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali duniani wameonesha
nia ya kuja kuwekeza hapa Nchini katika Sekta ya Hoteli kubwa za Kitalii.
Kampuni ya China Merchants Holdings International Limited ambayo imehusika
katika ujenzi wa Bandari kubwa na Mji wa Shenzhen katika Jimbo la
Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia ubia na Serikali yetu katika
ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na Mji wa Bagamoyo
unaotarajiwa kuwa "Trade Hub" ya Afrika.*



*Mheshimiwa Spika,*

*54. Tanzania imedhamiria kuendeleza uchumi wake kwa lengo la kufikisha
Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa Kati kabla au ifikapo mwaka 2025. Viashiria
vyote vinaonesha hivyo, na ndio sababu Makampuni yote niliyozungumza nayo
wakati wa ziara hiyo yameonesha shauku kubwa ya kuja kuwekeza Tanzania
katika Sekta mbalimbali na mengine tayari yapo Nchini kutekeleza miradi
mbalimbali. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kwa upande
wake*

*tutajitahidi kupokea Uwekezaji huo na hivyo kunufaika na matokeo
tunayotarajia. Aidha, tutaendelea kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na
uwekezaji ili kuweza kuvutia Mitaji na Wawekezaji wengi zaidi pamoja na
Watalii kutoka China na maeneo mengine duniani.*



*VII:* *JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI*



*Mheshimiwa Spika,*

*55. Mtakumbuka tarehe 7 Novemba, 2013 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihutubia Bunge ambapo
pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki
na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Napenda kulijulisha Bunge
lako Tukufu kwamba katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 Kampala Nchini Uganda,
Wakuu wa Nchi hizo akiwemo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
walikutana na waliidhinisha na kuweka Saini Itifaki ya Umoja wa Fedha wa
Afrika Mashariki. Aidha, Viongozi hao walizitaka Nchi Wanachama kukamilisha
taratibu za kuridhia Itifaki hiyo ifikapo mwezi Julai, 2014.*



*Mheshimiwa Spika,*

*56. Manufaa ya Umoja wa Fedha ni pamoja na: kupunguza gharama ya kufanya
biashara katika Nchi Wanachama; kuwezesha Nchi Wanachama kuwa na kiwango
kidogo na tulivu cha Mfumuko wa Bei; kuwa na viwango vidogo vya riba ya
kukopa; na kuepusha athari za ubadilishaji wa fedha ndani ya Jumuiya kwa
kuwa na Sarafu Moja. Matarajio ni kujenga ukanda tulivu wa kifedha
(Monetary and Financial Stability Zone) utakaorahisisha na kusaidia ukuaji
wa biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya.*



*Mheshimiwa Spika,*

*57. Katika Mkutano huo wa Kampala Wakuu wa Nchi pia waliridhia Mfumo wa
kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuagiza
kuwa ifikapo mwezi Januari 2014, Nchi Wanachama ziwe zimeanza utekelezaji
wake na kuukamilisha ifikapo au kabla ya mwezi Juni 2014. Aidha, Wakuu wa
Nchi walipokea Taarifa kuhusu maendeleo ya Mpango Kazi wa kuelekea
kuanzisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Walitumia muda wa
Mkutano huo kujadili hali ya usalama iliyopo katika Nchi hizi na waliona
kuna umuhimu wa kuongeza juhudi katika kukabiliana na Ugaidi.*



*Mheshimiwa Spika,*

*58. Kwa ujumla Mkutano huo ulikuwa na mafanikio sana hasa katika
kuimarisha Umoja wa Jumuiya. Aidha Wakuu wa Nchi wote kwa pamoja walitumia
muda huo kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha kwamba mahusiano yetu kati
ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanadumu na tunaendelea kuijenga
Jumuiya na kuiimarisha kwa nguvu zetu zote.*

*X: **PROGRAMU YA KUBORESHA MIJI NCHINI (URBAN LOCAL GOVERNMENT
*

*STRENGTHENING PROGRAMME-ULGSP**)*



*Mheshimiwa Spika,*

*59. Wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge, nilieleza kuhusu
Programu ya Kuboresha Miji Nchini (Urban Local Government Strengthening
Programme-ULGSP) ya miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2013 hadi 2018. Huu ni
mwendelezo wa Programu ya Uendelezaji na Uboreshaji Miji Nchini (Tanzania
Strategic Cities Programme -TSCP); ambao kwa sasa unakaribia kumalizika
utekelezaji wake. Programu hii ya ULGSP kwa sasa inahusisha Manispaa 11 na
Miji 7. Manispaa hizo ni Tabora, Morogoro, Shinyanga, Lindi, Sumbawanga,
Musoma, Songea, Singida, Iringa, Bukoba na Moshi. Miji mingine inayohusika
ni Kibaha, Geita, Babati, Korogwe, Mpanda, Njombe na Bariadi. Halmashauri
hizi zinazojumuisha Manispaa na Miji 18 ziko tayari baada ya kukidhi vigezo
vilivyowekwa, ambavyo ni pamoja na:*



*i. **Kuongeza Bajeti ya mapato kila mwaka; *

*ii. **Kutokuwa na Hati Chafu za Hesabu za Halmashauri, *

*iii. **Kuunda Kamati za kushughulikia matatizo yanayotokana na
Programu *

*kwenye ngazi ya Halmashauri, ngazi ya Kata na Mitaa;*

*iv. **Kuhakikisha Programu hiyo imetangazwa na kueleweka na wakazi
wa *

*Halmashauri za Manispaa na Miji;*

*v. **Kuhakikisha kuna Wakuu wa Idara wa kutosha; *

*vi. **Kuhakikisha Sheria za Manunuzi zinafuatwa; *



*vii. **Kuhakikisha Watu watakaohamishwa na Programu na kulipwa
fidia *

*hawazidi nyumba 20;*



*viii. **Kuhakikisha miradi iliyotekelezwa inalingana na thamani ya
fedha *

*iliyotumika;*



*ix. **Kutekeleza miradi ya miundombinu iliyoko kwenye menu; *



*x. **Kupeleka taarifa za kila robo mwaka za miradi kwa muda
unaotakiwa; *



*xi. **Kuhakikisha kuna Master Plan ya Mji; *



*xii. **Kuhakikisha ukusanyaji wa kodi ya majengo unaongezeka kati
ya Asilimia 5 *



*hadi 30; na*



*xiii. **Kuhakikisha taarifa za Mkaguzi wa Ndani zinaenda kwenye
vikao vya *

*Halmashauri kila robo mwaka.*



*Ukikosa hapa fedha hizo hazipatikani.*



*Mheshimiwa Spika,*

*60. Nimetaja baadhi ya Vigezo kwani viko zaidi ya 200 na vinagusa kila
Sekta ya Halmashauri. Upimaji wa vigezo vyote vitafanyika mara 2 kwa mwaka;
na Halmashauri zitakazoshindwa kufikia Alama (Marks) 60 na kuendelea,
watapunguziwa fedha za miradi yao. Hivyo, Mikoa na Mabaraza ya Madiwani
lazima yahakikishe kuwa vigezo vyote vinasimamiwa na kutekelezwa
kikamilifu. Aidha, TAMISEMI wawachukulie hatua za kisheria wale wote
watakaozembea katika kutimiza vigezo hivi na kuathiri maendeleo ya
Wananchi.*



*Mheshimiwa Spika,*

*61. Programu hii ambayo ni ya kwanza Afrika itatumia Dola za Kimarekani
255, fedha ambazo zilikuwa zitolewe mwezi Julai mwaka huu, lakini kutokana
na matatizo ya ubadhirifu yaliyojitokeza kwa Wasimamiaji wa fedha
zilichelewa kutolewa. Hata hivyo, baada ya kuwapeleka wahusika wa
ubadhirifu kwenye Vyombo vya Sheria, Wafadhili waliridhika na hatua
zilizochukuliwa, hivyo tarehe 27 Novemba, 2013 Wafadhili walitoa fedha za
Awamu ya Kwanza, ambazo zilitumwa kwenye Halmashauri hizo 18. Miradi
iliyopo kwenye Programu ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na
mifereji ya mvua, uwekaji taa barabarani, ujenzi wa Stendi za Mabasi,
upimaji viwanja, utengenezaji wa madampo, kuweka miundombinu ya majitaka na
uboreshaji wa makazi. Hii ni baadhi ya Miradi ya Miji iliyoibuliwa na
Halmashauri zenyewe kufuatana na matatizo ya Miji hiyo. Hivyo, ninawaomba
TAMISEMI – wasimamie Programu hii vizuri ili Miradi husika iweze kutatua
matatizo ya Wananchi katika maeneo yao na kuhakikisha Mapato ya Halmashauri
yanaongezeka. Lengo ni kuwezesha Halmashauri hizo kujitegemea baada ya
Miradi hiyo kukamilika.*





*XI: USIMAMIZI NA UDHIBITI WA FEDHA KATIKA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA*





*Mheshimiwa Spika,*

*62. Kama ambavyo itakumbukwa, wakati wa majadiliano ya Taarifa ya Kamati
ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa za Serikali za
Mitaa, kwa mwaka 2011/2012, Waheshimiwa Wabunge walionesha masikitiko yao
kwa vitendo vya ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na baadhi ya Halmashauri
Nchini.*

*Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia mjadala huo walidai kuwa
Serikali imekuwa haichukui hatua dhidi ya Watumishi wanaofanya makosa
katika Halmashauri. Napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja
na matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye Mamlaka za Serikali za
Mitaa kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha za Umma, Serikali imejitahidi
kuimarisha usimamizi na utendaji katika eneo hili. Jitihada hizi
zimedhihirishwa na Matokeo ya Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali ambayo yanaonesha kuongezeka kwa ubora wa Hati za Ukaguzi
zinazotolewa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan kuanzia mwaka 2000
hadi sasa. Kwa mfano, mwaka 2000/2001 Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unaonesha
kuwa Halmashauri*

*zilizopata Hati safi zilikuwa 16 sawa na Asilimia 14 ya Halmashauri zote.
Aidha, Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 23, sawa
na Asilimia 20 na Halmashauri zilizopata Hati Chafu zilikuwa 75 sawa na
Asilimia 65 ya Halmashauri zote.*



*Mwaka 2005/2006 Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati Safi iliongezeka hadi
kufikia 53, sawa na Asilimia 43 na Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka
zilikuwa 67, sawa na Asilimia 54 na Halmashauri zenye Hati Chafu zilikuwa
Nne (4), sawa na Asilimia Tatu (3).*

*Mwaka 2011/2012 taarifa za Ukaguzi ziliimarika zaidi ambapo Halmashauri
zilizopata Hati Safi ziliongezeka maradufu hadi kufikia 104, sawa na
Asilimia 78 na zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 29, sawa na Asilimia 21
na hakukuwa na Halmashauri iliyopata Hati Chafu.*

*Mheshimiwa Spika,*

*63. Jitihada hizi ni kubwa. Hivyo, Serikali itaendelea kuimarisha
Usimamizi na Udhibiti na Mapato na Matumizi ya Serikali katika Sekta zote
na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi na tija katika
utendaji na kudhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za Umma. Lengo ni
kuongeza kasi ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu na Kukuza Uchumi
kwa haraka.*



*Mheshimiwa Spika,*



*64. Pamoja na jitihada hizo za Serikali zinazoonekana, napenda
kuwahakikishia kwamba Watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha
za Umma wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi,
kushushwa vyeo, na kufikishwa mahakamani. Aidha, kesi za Watumishi hao ziko
katika Mahakamani na katika Vyombo vya nidhamu vya Halmashauri na Tume ya
Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao kuhakikisha kwamba tunajenga
nidhamu. Kutokana na hatua hizo kati ya mwaka 2011/2012 hadi Septemba, 2013
jumla ya Wakurugenzi 52, Wakuu wa Idara 65 na Watumishi wengine 749
wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika
Halmashauri mbalimbali Nchini. Hatua hizo za kinidhamu ni kama ifuatavyo:*

*i) **Waliofukuzwa kazi ni 232, *

*ii) **Waliosimamishwa kazi ni 186, *

*iii) **Waliovuliwa Madaraka ni 33, *

*iv) **Waliopunguziwa Mshahara ni 1, *

*v) **Walioshushwa Cheo ni 32, *

*vi) **Walipewa ONYO ni 113, *

*vii) **Waliofikishwa Mahakamani ni 233, *

*viii) **Waliofikishwa Polisi na TAKUKURU ni 36. *

*Serikali itaendelea kusimamie eneo hili kuhakikisha fedha za Umma
zinatumika vizuri.*



*Mheshimiwa Spika,*

*65. Pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa Watumishi hao mmoja
mmoja, Serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana
na tatizo la ubadhirifu wa mali za Umma katika Halmashauri. Juhudi hizo ni
pamoja na kuongeza uwezo kwa kuajiri Wahasibu wa kutosha katika Halmashauri
zetu; kuanzisha Kamati za Mapato na Matumizi katika ngazi zote za
Halmashauri na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Kamati za Mapato na
Matumizi za Halmashauri zote. Mbinu nyingine zinazotumika ni kufanya
Ukaguzi Maalum kubaini ufisadi na ubadhirifu wowote uliojitokeza. Kwa
mfano, Katika mwaka wa fedha 2011/12 kumefanyika Kaguzi maalumu kwenye
Mamlaka za Serikali za Mitaa kumi na nne (14), ambazo ni Kilindi, Kiteto,
Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro,
Dodoma, Mbarali na Bunda. Kaguzi hizo zimesaidia sana katika kujenga
nidhamu ya Watumishi katika Halmashauri hizo.*



*Mheshimiwa Spika,*

*66. Serikali pia imeweza kubadili na kuweka Mfumo wa 'Lawson' katika
kila Halmashauri ili kumaliza tatizo la Mishahara kwa Watumishi
waliofariki, walioacha kazi, wastaafu, n.k. Vilevile kuna Mfumo wa Epicor
9.05 ambao zinasaidia kudhibiti Bajeti za Mapato na Matumizi katika
Halmashauri Nchini. Mafunzo kuhusu matumizi ya Mifumo hii mipya yanaendelea
kutolewa ili kuweza kutumia mifumo hii kwa ufanisi. Vilevile, Wakuu wa
Mikoa walikwishaagizwa kuhudhuria Vikao vya Baraza za Halmashauri; katika
kujadili Hoja za Ukaguzi ili Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
aweze kufuta zile zilizojibiwa kikamilifu. Hoja ambazo hazikupata majibu
kikamilifu, Sheria zifuatwe na wenye kuhusika na ubadhirifu wowote
wachukuliwe hatua zinazostahili. Aidha, Maafisa Masuuli (Wakurugenzi)
wanaohusika na Hoja mbalimbali za Ukaguzi wanapaswa kuitwa kwenye
Halmashauri walizotoka ili kujibu hoja zinazowahusu bila kujali
wamehamishiwa wapi.*



*XI:* *HITIMISHO*



*Mheshimiwa Spika,*

*67. Tumekuwa na muda mzuri wa kujadili masuala muhimu yanayohusu
maendeleo ya Nchi yetu hapa Bungeni kwa kipindi chetu tulichokuwa katika
Mkutano huu. Napenda niwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu.
Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa
kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya
kuongoza Vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa
Wabunge kwa michango yao wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu wa Bunge
na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake
ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma
mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari
kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na
maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru
Madereva kwa kazi nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa
Wabunge,*

*Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika
Mkutano huu.*



*68. Niwashukuru Wabunge wote kwa kujadili vizuri hoja za zilizojitokeza
hapa Bungeni. Lakini kipekee niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri Wanne
waliokubali kubeba jukumu ka kuwajibika kwa yote yaliyotokea. Tunawashukuru
kwa uzalendo wao kwa Nchi yetu na tunawatakia kila la kheri katika maisha
yao. Mheshimiwa Spika,*

*69. Tunahitimisha shughuli za Bunge hili tukiwa tumebakiza siku chache
kabla ya kufika Mwisho wa Mwaka huu 2013. Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye
wingi wa Rehema atujalie katika siku hizi chache tuweze kusherehekea
Sikukuu njema ya Krismas na tuvuke salama mwisho wa mwaka na kuingia Mwaka
Mpya 2014 kwa Amani na Furaha!.*



*Mheshimiwa Spika,*

*70. Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wote tunavyofahamu, tutakuwa na
Bunge la Katiba litakalofanyika mapema mwakani na kwa tarehe
itakavyopangwa. Kutokana na utaratibu huo ni dhahiri kwamba wengi wetu
tutakutana wakati wa Bunge la Katiba. Nitumie fursa hii kuwatakia safari
njema mnaporejea kwenye maeneo yenu na wengi wenu niwatakie mapumziko mema
ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya hadi tutakapokutana wakati wa Bunge la
Katiba.*



*Mheshimiwa Spika,*

*71. Baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi
litakapokutana kwa Mkutano maalum wa Kumi na Tano wa Bunge la Bajeti tarehe
06 Mei, 2014 saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu hapa Dodoma.*



*Mheshimiwa Spika,*

*72. **Naomba kutoa hoja. *

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment