Thursday 10 October 2013

[wanabidii] WASOMI KAENI PEMBENI, WANYONGE SHIKENI HATAMU!

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Katika makala yangu ya juma lililopita, nilifafanua chimbuko la itikadi ya Umajumui wa Afrika na kubainisha kuwa ndiyo inayopaswa kuongoza mapambano ya wanyonge. Makala yaliishia kwa kuwahamasisha wanyonge wote wa Afrika kuungana na kupambana kwa pamoja bila kujali dini zao au makabila yao, vyama vyao au kazi zao, maeneo yao au nchi zao, jinsia zao au umri wao. Kwa kufanya hivyo hawatakuwa na cha kupoteza isipokuwa minyororo yao, minyororo inayowafanya waendelee kuwa mafukara huku jasho lao na rasilimali zao zikiwatajirisha mabeberu wa nje pamoja na mawakala wao wa humu ndani.

Lakini je, wanyonge wataungana vipi? Na ni nani wa kuchukua jukumu hilo la kuwaunganisha wanyonge ili wapambane na mfumo dhalimu wa ubepari, ambao kwa sasa umechukua sura ya uliberali mambo-leo? Makala ya juma hili yamelenga kujibu maswali hayo.

Ni jukumu la wasomi
Kama nilivyoelezea juma lililopita, kati ya silaha za thamani ambazo wanyonge waliporwa mara baada ya uhuru ni itikadi ya Umajumui wa Afrika. Itikadi hii iliondolewa mikononi mwa wanyonge na kuwekwa mikononi mwa watawala. Na watawala wengi hawakuwa tayari kusalimisha mamlaka ya nchi zao ili kuunda dola la Muungano la Afrika kwa sababu mamlaka ya kidola ndiyo yaliyowapa fursa za kuishi katika anasa za kitajiri pamoja na kuwatumikia mabeberu.

Kwa hiyo, si ajabu kwamba viongozi wenye mtazamo wa kimajumui waligeukia makundi mbadala katika jamii zao na kuwapatia jukumu la kuongoza harakati za kujenga umajumui wa Afrika. Kwa upande wa Nkrumah, pamoja na kuendelea kuwashawishi viongozi walioingia madarakani, alivigeukia pia vyama vya wafanyakazi na taasisi nyingine zilizowaunganisha wananchi, na kuvihamasisha kuongoza juhudi za kuiunganisha Afrika.

Nyerere pia, hasa baada ya mwaka 1965, aliona kuwa kundi pekee lenye uwezo wa kuongoza juhudi za kuubadili uzalendo/utaifa (nationalism) kuwa Umajumui wa Afrika (pan-Africanism) ni kundi la wanazuoni, na hasa wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu. Hii ni kwa sababu wao wana muda wa kutosha kufanya uchambuzi kwani hawabanwi na shughuli za uzalishajimali ama utawala.

Lakini pia ni kwa sababu vyuo vikuu, kwa tafsiri ya Nyerere, ni vitovu vya mijadala, tafiti na maandiko, ambayo huwafanya wasomi "wasimame katika kweli kama wanavyoiona, bila kujali yale yatakayowatokea wao binafsi". Ndio maana pia Mwalimu alikipenda sana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani), ambapo alikwenda mara kwa mara kushiriki katika mijadala na wasomi.

Lakini wasomi ni sehemu ya unyonyaji
Mwalimu aliwakabidhi wasomi mikoba ya kuongoza mapambano ya Kimajumui tarehe 13 Julai 1966 alipotoa hotuba katika uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Zambia. Lakini mwezi Oktoba 1966, Mwalimu alikumbana na maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakipinga kulazimishwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa miaka miwili, huku wakipokea asilimia 40 tu ya mishahara yao. Asilimia 60 zingekuwa ni mchango wao katika ujenzi wa taifa.
Katika tukio hilo, Mwalimu aliukata mshahara wake kwa asilimia 20 na kisha kuwaambia wanafunzi:

 "Mamishahara ya anasa haya ndiyo yaliyojenga kasumba hii kwa wasomi, wote! Mimi na ninyi. Sote tumo katika tabaka la juu la wanyonyaji… Kila mmoja katika nchi hii anadai hisa yake. Kila mmoja isipokuwa mkulima maskini. Atadaije? Hajui lugha hiyo… Ni nchi ya aina gani hii tunayoijenga?"

Katika kutafakari nukuu hiyo ya Mwalimu, tunaweza kujiuliza swali moja: kama Mwalimu alijua kuwa wasomi, kama walivyo watawala, ni sehemu ya wanyonyaji, je, kwa nini aliwakabidhi jukumu adhimu la kupigania Umajumui wa Afrika na kuongoza mapambano ya wanyonge?

Ndipo likaja Azimio
Ifahamike kwamba maandamano yale ya wanafunzi yalimfanya Mwalimu autafakari mfumo mzima wa nchi yetu, kitu kilichomfanya agundue jinsi wanyonge (wakulima na wafanyakazi wa ngazi za chini) walivyokuwa wamesahaulika katika nchi hii. Ili kurejesha matumaini ya wanyonge ndipo Mwalimu akaja na Azimio la Arusha ambalo ndilo lingekuwa silaha ya wanyonge dhidi ya wanyonyaji na waporaji wa ndani na nje ya nchi. Lakini Azimio lenyewe pia, kama ilivyotokea katika itikadi ya Umajumui wa Afrika, lilikabidhiwa kwa watawala ili walitekeleze. Hawa, kwa kushirikiana na mabeberu, walitumia kila mbinu kulihujumu na hatimaye kulizika. Pengine nikipata wasaa huko mbeleni nitaandika kwa kirefu juu ya Azimio na jinsi lilivyohujumiwa na hatimaye kuuawa.

Hebu turejee kwa Mwalimu na wasomi. Mwalimu alichukua hatua madhubuti ya kuubadili mfumo wa elimu ili uendane na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Aliwahimiza wasomi kuutumikia umma bila kudai malipo ya ziada. Fedha za kuwasomesha zililipwa na wanyonge, hivyo wasomi walipaswa kuwatumikia wanyonge kwa uadilifu mkubwa na kupigania maslahi ya wanyonge.

Kwa upande wa walimu, wao walikuwa na nafasi ya pekee ya kuleta mapinduzi katika nchi hii. Akihutubia mkutano wa walimu toka nchi nzima mwaka 1969, Mwalimu aliwasihi walimu kuzalisha wanamapinduzi na sio vimashine. Kipimo cha utumishi wao kingekuwa ni vijana wenye kujiamini, wanaokataa unyonyaji, dhuluma na ukandamizwaji; vijana wapigania usawa na wanaofanya kazi kwa bidii na maarifa ili kukabiliana na changamoto zinazowakumba wao na jamii nzima. Mwalimu aliwataka walimu kuachana na kasumba ya kikoloni ambayo ilikuwa ikipima usomi wa mtu kwa kutumia karatasi (vyeti), kiasi kwamba mtu asipopata cheti hajioni kama amesoma.

"Wasomi mmetusaliti"
Je, wasomi wametimiza jukumu hilo la kuongoza mapambano ya wanyonge? Katika makala yangu ya wiki jana, wasomaji walionitumia maoni walilalamika kuwa sisi wasomi tumewasaliti wanyonge kama ilivyo kwa wanasiasa. Nitanukuu ujumbe kutoka kwa mmoja wa wasomaji hawa aliyejitambulisha kwa jina la Alawi Ugama wa Tandika, Dar es Salaam:

"Hatuna cha kupoteza isipokuwa minyororo yetu, ni kweli mwalimu. Je, ni nani wa kutuunganisha ikiwa nyie wenye dhamana hiyo tayari ni mabepari? Ndio. Maana wasomi wenye pesa na wanasiasa mpo kwenye fungate! Maskini mnyonge aende wapi?"

Hicho ndicho kilio cha wanyonge, kwamba wasomi tumewasaliti. Ni kilio cha haki, na ni cha kweli tupu. Sisi walimu wa vyuo vikuu (hatupendi kuitwa walimu, tunataka tuitwe wahadhiri) tumesaliti jukumu letu la msingi. Wengi wetu tumekuwa makahaba wa kitaaluma (academic prostitutes) kwa kuwa tumeamua kuuza usomi wetu sokoni ili kujiongezea kipato. Wengi hatufanyi tafiti za mambo yanayowahusu wanyonge mpaka kuwe na malipo, na tumejikita kutoa ushauri-elekezi (consultancies) kwa makampuni ya kibepari, serikali (zinazotawaliwa na vibaraka na waporaji) au asasi za kiraia ambazo nyingi pia hutegemea ufadhili wa mabeberu na kujidai zikiwapigania wanyonge huku zikiwarudisha utumwani. Haiyumkiniki kuwa wahadhiri wa vyuo vikuu wakiteuliwa katika vyeo vya serikalini hujiingiza katika uozo na upuuzi ule ule ufanywao na watawala. Mfumo unaowafukarisha wanyonge, ndio unaotufaidisha sisi wasomi.

Wanafunzi tunaowazalisha pia ni sehemu ya tatizo. Wengi wao hawana ari ya kuwatumikia wanyonge bali kutajirika. Shida yao kubwa wawapo vyuoni ni kupata vyeti ili waingie sokoni kujiuza. Soko halihitaji watu wanaofikiri na kupinga unyonyaji, bali "vimashine", yaani watu wafanyao kazi kama mashine bila kuhoji anaefaidika na jitihada zao.

Ikitokea wanafunzi wetu wanadai mikopo ndipo hujiita watoto wa wakulima. Fedha ziingiapo kwenye akaunti basi husahau kabisa kuhusu huyo mkulima. Wengi wao hawajishughulishi kuandaa mijadala au tafiti kuhusu mustakabali na ukombozi wa wanyonge. Ni nani anayejitanabaisha kinadharia na kwa vitendo na kundi la wanyonge, na kulikana tabaka lake ili akapambane pamoja na hao wanyonge?
Hata wajiitao "wanaharakati" katika vyuo, huwatumia wanyonge kama mtaji wa kisiasa ili baadae wakagombee ubunge au kuteuliwa katika nafasi za ulaji. Ni nani anayedadisi chanzo cha madhila ya wanyonge? Japo wanafunzi wetu wanapaswa kubeba lawama za kukubali kuwa sehemu ya tatizo, lakini zigo kubwa la lawama tunapaswa kulibeba sisi walimu kwa kushindwa kuzalisha wanafunzi wanamapinduzi, wapingao ubepari na kupigania maslahi ya wanyonge kwa nadharia na vitendo.

"Hivyo kaeni pembeni"
Sina hakika kama wasomaji walionitumia ujumbe walikuwa wamesoma maoni yaliyotolewa na Jumuiya za Wanataaluma wa Vyuo vya Umma nchini juu ya rasimu ya katiba mpya. Kati ya moja ya mapungufu makubwa ambayo wahadhiri wameyaona katika rasimu ni kwamba haikutaja itikadi tunayopaswa kufuata. Kisha wakatoa pendekezo kuwa rasimu ijayo itamke kuwa itikadi yetu ni "ubepari", na kwamba serikali sharti ichukue hatua madhubuti za kuitimiza itikadi hiyo. Hao ndio wasomi ambao Mwalimu aliwakabidhi jukumu la kuongoza mapambano ya wanyonge.

Mwalimu alishatuonya wasomi kuwa "kama ninyi walimu msipowaongoza wanyonge wa Afrika, ikitokea siku akawepo mtu wa kuwaondoa katika umaskini na mateso mtapaswa kukubali kukaa pembeni na mkubali kuongozwa na jeshi la wanyonge wa Afrika. Na nitafurahi nikiwaona mkidharauliwa kwa sababu mlikuwa viongozi wasiofaa".

Wanyonge shikeni hatamu
Uzoefu wa miaka 5o ya Uhuru umetuonyesha kuwa kati ya kosa kubwa ambalo wanyonge wanaweza kulifanya ni kuwakabidhi wasomi na watawala haki ya kuwaongoza na kuwatawala. Kitabaka, wasomi na watawala hawana ugomvi kwani wana maslahi yanayofanana. Wote ni watumishi wa mabepari, na kazi yao huwa ni kuwapa wanyonge matumaini hewa huku wakiwauza kwa mabepari.

Ninapozungumzia wasomi hapa nawagusa hata wale ambao wanaongoza asasi za kiraia, makampuni ya kibepari (yawe ya serikali au binafsi), vyama vya siasa au hata vyama vya wafanyakazi. Ukichukua mishahara yao, magari yao, nyumba zao, makampuni yao, hapo hujazungumzia safari za ndani na nje  ambazo zina posho za kujikimu achilia mbali watoto wao katika shule za binafsi (ndani na nje ya nchi), utapata jeshi la watu wenye maslahi ya kuuendeleza mfumo wa kibepari na hata kufikia hatua ya kutamka kuwa "katiba itamke kuwa itikadi yetu ni ubepari"! Kundi hili haliwezi kuongoza mapambano ya wanyonge. Hivyo, wanyonge sharti wajiongoze wenyewe.

Nitakapopata wasaa katika siku za usoni, nitafafanua kwa kina namna ambavyo wanyonge wanapaswa kushika hatamu katika mapambano kwa kujenga mshikamano wa kitabaka na kuongozwa na itikadi sahihi!

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment