Monday 7 October 2013

[wanabidii] UMUHIMU WA MAWASILIANO KATIKA KUZUIA UHALIFU

"UMUHIMU WA MAWASILIANO KATIKA KUZUIA UHALIFU"


"Mawasiliano ni kitu/nyenzo muhimu katika uhai wa chombo chochote kile" Katika karne ya 21 ya  maendeleo ya sayansi na teknolojia suala la mawasiliano limeshika kasi kubwa kwa kila Mwananchi na Hata wadau wake. Kwa namna hii, mawasiliano limekuwa ni jambo muhimu sana ambalo huwezesha mtu na mtu kupashana habari, wizara kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi kuhusu matukio, na hata malengo na mikakati iliyojiwekea.

Kwa hapa kwetu  nchini, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Tanzania Communication Regulatory Authority – TCRA ) ndicho chombo kinachosimamia biashara ya mawasiliano kwa njia ya simu, matangazo ya redio na televisheni, utoaji wa huduma za
posta, ugawaji na usimamizi wa masafa ya matangazo ya redio pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano. Chombo hiki kina majukumu ya kulinda na kusimamia maslahi ya watumiaji wake na kusambaza taarifa mbalimbali za kiushauri na kiulinzi kwa watumiaji wa mawasiliano na kwa Wizara mbalimbali za serikali.

Katika kufanikisha shughuli mbalimbali za kiutendaji, Jeshi la Polisi nchi limejitahidi katika kuhakikisha suala la mawasiliano na upashanaji habari kwa umma linazingatiwa. Hii ni kwa nia ya kutoa fursa kwa wananchi kutumia nyenzo hii ya mawasiliano kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusiana na matukio ya uhalifu,wahalifu,majanga, ajali, na hata kutoa taarifa pindi waonapo kuna jambo au kitu wanachokitilia mashaka. Je,ni mara ngapi mimi na wewe tunatumia nyenzo hii ya mawasiliano katika kudhibiti na kuzuia vitendo vya uhalifu?au ni mara ngapi mimi na wewe tunasaidia kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kufanikisha utendaji wake?

Miaka ya hivi karibuni Jeshi la Polisi Tanzania limezidi kuimarisha shughuli zake za kiutendaji na kutoa fursa kwa wananchi kushirikiana na Jeshi hili ili kudhibiti na kuzuia vitendo vya uhalifu kwa njia/dhana ya Polisi Jamii na Polisi Rafiki pale wananchi wanapo shiriki kikamilifu katika ulinzi wa mali zao na maisha yao kwa kushirikiana zaidi na Jeshi la Polisi. Dhana hii pia imetoa fursa kwa wananchi kuwa huru kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa Jeshi la Polisi zinazo husiana na uhalifa, wahalifu au, matukio mbalimbali kama vile ajali za barabarani, majanga  na nyingine za kiusalama.

Katika kuhakikisha Wananchi wana shiriki katika utoaji wa taarifa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ndipo lilipoanzisha Miradi mbalimbali ambayo inafanya kazi sambamba  na kwa ukaribu zaidi na wananchi ili kuweza kusaidia katika mawasiliano na utoaji wa taarifa. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na; Usalama wetu kwanza, mradi wa safiri salama, mradi wa ukamataji salama,klabu marafiki shuleni (Polisi Rafiki), huduma bora kwa mteja (customer care), utii wa sheria bila shuruti, kuzuia ukatili wa kijinsia (TPF-Net), kuzuia na kupambana na wahamiaji haramu, mazingira salama na mingine mingi.

Kupitia miradi hii ya Polisi Jamii, Jeshi limeweka wasimamizi na watendaji kwa kushirikiana na wananchi na pia kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kufanikisha utendaji wake. Uwepo wa miradi hii ni fursa pekee kwa wananchi kuwasiliana na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kudhibiti uhalifu. Kwa kutekeleza hili Jeshi la Polisi limeamua kutoa namba za simu za Makamanda wa Mikoa , wakuu wa polisi wa wilaya na Wakuu wa Vikosi kama vile Kikosi cha Usalama Barabarani ili Wananchi wawe huru muda na wakati wowote hata kama wapo safarini kutoa taarifa za kiusalama ili kudhibiti matukio ya uhalifu na ajali zinazoweza kuepukika.

Matumizi ya nyenzo hii ya mawasiliano imekuwa na nguvu sana katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika Jeshi la Polisi na kuongeza ufanisi. Kwani Jeshi limekuwa likipokea taarifa, maoni, na changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi na wadau. Njia hizi za mawasiliano zimeonekana kuwa zikitumiwa vizuri zitafanikisha malengo yetu ya kudhibiti,kuzuia, na kupambana na uhalifu. Matumizi sahihi ya usambazaji taarifa kwa kutumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii, kwa sasa ni sehemu pekee inayotoa fursa kwa wananchi kutoa taarifa, maoni na hata changamoto ambazo Jeshi huzibadilisha kuwa ni fursa katika kuongeza ufanisi wa kiutendaji.

Jeshi la Polisi linazidi kutoa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa Jeshi hili, kazi na majukumu yake. Kwa njia ya mikutano ya Polisi Jamii na Polisi Rafiki, elimu imeweza kutolewa na kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali. Pia elimu ya utoaji salama wa taarifa imeendelea kutolewa katika Shule za Msingi na Sekondari ili wanafunzi wajue wajibu wao na umuhimu wao katika Jeshi kwa njia ya kutoa taarifa sahihi kwa lengo la kudhibiti uhalifu na vitendo vya uvamizi katika Shule.

Wizara imeona umuhimu wa chombo hiki na kuongeza wigo wa mawasiliano baina yake na wananchi. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saidi Mwema akifungua mkutano wa siku mbili wa Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa shirikisho la Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) alisema, "Watanzania wote wakitoa taarifa na kuzipeleka katika mamlaka husika, kwa mujibu wa sheria za mwenendo wa jinai kifungu namba 7, hatimaye watuhumiwa wataweza kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria".

Ni wazi kuwa kila mmoja wetu akishiriki katika utoaji wa habari, basi tunauwezo mkubwa wa kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali na kudhibiti vitendo vya uhalifu. Pia tutakuwa na uwezo mkubwa wa kulinda maisha yetu, mali zetu pamoja na kuokoa mali zilizo katika mazingira ya kuibwa au kuporwa. Bila kushirikiana na wananchi Jeshi bado litakuwa na kazi kubwa kwani wahalifu wamo ndani ya jamii na wanaishi miongoni mwetu. Sote tuone tunayo sababu ya kushiriki katika ulinzi kwa njia ya utoaji taarifa kwa mamlaka husika tukiamini kuwa "mawasiliano ni nyenzo yenye nguvu" [communication is power].


Imetolewa na:
[DIWANI ATHUMANI – ACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment